UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni kweli Simba haimuhitaji Kagere?

UKITEMBELEA mtandao wa Google na kuandika jina la Meddie Kagere, utaambiwa amezaliwa Oktoba 10 mwaka 1986. Kimahesabu hapo, Meddie ana miaka 34.

Kama unajua mwaka mwingine wowote aliyezaliwa mshambuliaji huyu tishio, nijuze kupitia namba zangu za simu hapo juu. Mchezaji wa soka ni mchezo wa wazi, mchezo wa soka ni mchezo wa matokeo, bila chembe yoyote ya mashaka, Kagere ana sifa zote za kuendelea kuitumikia Simba .

Kagere ana sifa zote za kuendelea kutamba ndani ya Ligi Kuu Bara hata kama atakuwa nje ya Simba, katika msimu yake miwili ya kwanza, hakuna mchezaji yeyote wa ligi yetu aliyewahi kufikia idadi ya mabao 45 aliyofunga Kagere, sikumbuki kama Tanzania imewahi kuwa na mchezaji kama Kagere msimu yake miwili ya kwanza.

Ni kweli watu kama kina Mohammed Hussein Mmachinga walikuwa habari nyingine, fundi kweli kweli, ni kweli watu kama Zamoyoni Mogella walikuwa habari nyingine, rafiki mkubwa wa nyavu, ni kweli mshambuliaji kama Madaraka Suleimani alikuwa mwiba sana.

Mtu wa kutupia nyavuni kwenye kila engo lakini, sikumbuki kama kuna hata mmoja aliwahi kufunga mabao 45 ya ligi kuu ndani ya misimu yake miwili ya kwanza, ni kweli hawa wazee walikuwa moto wa kuotea mbali lakini, mabao ya Kagere kwenye misimu yake miwili ya kwanza ni habari nyingine.

Wakala wa Kagere amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya Habari akisema mteja wake huyo anaelekea ukingoni mwa mkataba wake na Simba ni kama hawana dalili za kuendelea na mshambuliaji huyo raia wa Rwanda ambaye mpaka sasa anakamata nafasi ya pili ndani ya Simba kwenye orodha ya wafungaji wa klabu hiyo ndani ya ligi kuu.

Ni kweli Kagere hana ufundi wa kina Mmachinga, ni kweli Kagere hawezi kufikia ubora wa kina Mogella hata kidogo lakini, jamaa anajua sana kufunga, labda Kagere ana umri mkubwa, labda ni zaidi ya miaka 34 tunayoiona mitandaoni.

Cha msingi hapa sidhani kama inapaswa kuwa umri, nadhani apitwe kwa mchango wake uwanjani, ni kweli kila mtu ana mawazo yake, kila mtu ana namna tofauti ya kumtazama mchezaji, kwa namna ambavyo unamtazama MK 14, ni kweli Simba haimuhitaji tena kuelekea msimu ujao?

Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu, mabao 11 aliyofunga Kagere msimu huu, yanamfanya awe na jumla ya mabao 56 katika misimu yake mitatu na msimu bado haujamalizika, akifunga mabao mengine manne, atakuwa na wastani wa kufunga mabao 20 kwenye kila msimu. Hizi namba sio za kubeza, mchezaji wa aina hii huwa hawapatikani kila siku, ni wachezaji wachache sana wenye muendelezo huu, ni kweli kila siku umri unasogea lakini bado anafunga.

Kagere siku hizi amekuwa sio chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Simba, John Bocco na Chris Mugalu wamekuwa kwa nyakati tofauti wakiwa chaguo la kwanza mbele ya Kagere lakini, haiondoi ukweli kuwa bado Kagere ana ubora wa kucheza ligi yetu.

Bado namwona ni mchezaji wa bao 15 mpaka 20 kwa msimu, timu zetu nyingi zimekosa wachezaji aina yake, bado Simba wanaweza kumbakisha na atawasaidia lakini, wangepunguza tu urefu wa mkataba.

Siamini kama Kagere anaweza kukupa chini ya mabao 15 kwa msimu, hana mambo mengi sana lakini, bado nadhani anaweza kufunga, kwa kuitazama Simba na aina ya wachezaji iliyonao, unadhani ni sawa endapo Simba wataamua kuachana na MK 14? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Pale kwenye ushambuliaji ni kama Bocco amezaliwa upya kwa sasa, katika mechi nne zolizopita, amefunga mabao saba, ni moto wa hali ya juu sana, hata yeye kabla ya mwezi uliopita alipokuwa nje kwa majeraha, ni kama watu waliamini amekwisha.

Ni kama watu waliamini hawezi kurudi tena kwenye ubora wao, lakini, kwa sasa amewaziba watu wote mdomo, ameupiga mwingi, amekuwa rafiki mkubwa wa nyavu.

Namtazama Mugalu ambaye hakuwa na wakati mzuri sana kwenye Ligi ya Mabingwa, ukimtazama mechi za hivi karibuni, na yeye ni kama ameamka, ni kama amechangamka, ni kama amerudisha urafiki na nyavu .

Naona picha hiyo hiyo ikijirudia kwa Kagere, namuona akiamka tena, namuona akiendelea kufumba jicho lake, unadhani Simba watakuwa sawa wakimuacha Kagere? Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kwenye miaka 20 ya hivi karibuni, huwezi kutaja washambuliaji watatu mahiri ukaacha jina la Kagere, amefunga sana, siku akiacha kufunga, nitaunga mkono suala la kumuacha lakini kwa sasa, bado. Kama Simba wanauwezo wa kumpata mshambuliaji mwingine kijana mwenye uwezo wa kuwapa mabao 20 kwa msimu, naweza kushawishika.

Lakini tofauti na hapo, sidhani kama maamuzi ya kumuacha Kagere yatakuwa sawa. Namkumbuka Amissi Tambwe, namkumbuka Kipre Tchetche, namkumbuka Bocco, hawa wanaume wamekuwa moto sana ndani ya ligi, Tchetche aliamua tu kuondoka mwenyewe pale Azam FC, angetaka kubaki naamini bado angekuwa anafunga tu.

Bocco bado anapasia nyavu kama juzi na jana, hata Kagere bado ana uwezo wa kufunga, najua Simba ni klabu kubwa na imejaa watalaamu, bila shaka watafanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya pande zote mbili, kama unadhani Kagere amekwisha, amezeeka, nijuze na mimi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.


IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR