UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni kweli Feisal alimzidi Nado msimu uliopita?

Muktasari:

KILA mara ninapenda kusema, linapokuja suala la ubora katika michezo ni suala la maoni, hakuna vigezo vilivyowekwa popote duniani vya kupima ubora wa mchezaji, kila mmoja ana vigezo vyake anavyotumia kusema kwanini anaamini mchezaji mmoja ni bora kuliko mwingine.

KILA mara ninapenda kusema, linapokuja suala la ubora katika michezo ni suala la maoni, hakuna vigezo vilivyowekwa popote duniani vya kupima ubora wa mchezaji, kila mmoja ana vigezo vyake anavyotumia kusema kwanini anaamini mchezaji mmoja ni bora kuliko mwingine.

Kila mmoja ana maoni yake kwasababu kila mtu ana mtazamo wake. Kutofautiana ni kawaida. Ndiyo maana hadi leo wewe na mshikaji wako bado hamjaafikiana nani ni bora zaidi kati ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Kila mmoja ana maoni yake.

Majuzi Shirikisho la Soka nchini (TFF) wakatuletea mada nyingine mezani, TFF walitangaza orodha ya tuzo na wahusika watakaoziwania katika vipengele tofauti.

Kabla ya kujadili vipengele na wahusika wanaowaniwa tuzo hizo, nadhani ni busara kuwapongeza TFF kwa kuelewa umuhimu wa kutoa tuzo kwa wachezaji na wadau wake tofauti, ni kweli kwamba zipo tuzo zinapaswa kutolewa kwa mujibu wa kanuni, lakini wao wameamua kwenda mbali na kutoa tuzo binafsi zaidi ya 50 ambazo hazijatajwa katika kanuni. Kwa hili wanastahili pongezi.

Baada ya pongezi nitoe maoni yangu kuhusu baadhi ya wahusika katika vipengele tofauti, kumbuka pale mwanzo nilisema linapokuja suala la maoni tunaruhusiwa kutofautiana kama hutakubaliana na mimi naomba uniandikie kupitia namba zangu hapo juu.

Tuanzie wapi? Tuanzie hapa katika tuzo kubwa zaidi ya zote, mchezaji bora wa msimu, kwa mujibu wa TFF wachezaji watatu bora wa msimu uliopita ni John Bocco, Clatous Chama na Tonombe Mukoko. Sina maswali juu ya Chama, kwa miguu yake miwili, aliamua matokeo ya Simba na hata mara kadhaa Simba walipomkosa waliteseka kiasi. Simuoni mchezaji aliyemfunika Chama ndani ya kikosi cha Simba.

Kama ilivokuwa kwa Chama, sina maswali sana juu ya Mukoko, alikuwa ‘trekta la masika na kiangazi’ kwa Yanga. Nguvu kubwa ya Yanga msimu uliopita ilikuwa katika ulinzi, ukuta wao ulikuwa salama chini ya miguu ya Mukoko, sikushangaa kuliona jina lake katika kuwania tuzo ya mchezaji bora wa msimu.

Kama sina maswali juu ya hao hapo juu, je nina maswali juu ya Bocco? Hapana! Bocco ndiye mfungaji bora wa ligi, ubingwa wa Simba umechagizwa na mabao yake ipo hoja ninayokubaliana nayo kwamba Aishi Manula alistahili kuingia katika tuzo ya mchezaji bora wa msimu, ila napata shida kila ninapojiuliza nani ampishe Manula katika ya hawa watatu Mukoko au Bocco? Niandikie kupitia namba zangu hapo chini.

Kipengele kingine kilichoibua mjadala mkubwa ni kile cha beki bora na kiungo bora wa msimu. Tuanzie hapa kwa kiungo bora wa msimu. Kama sikuwa na shida na Chama na Mukoko katika kipengele cha mchezaji bora wa msimu, lazima sitakuwa na shida nao hapa kwa kiungo bora wa msimu.

Mtu mmoja nitakayekuwa na shida naye hapa ni Feisal Salum ‘Fei Toto’. Kama kiungo mshambuliaji alipaswa kuhusika katika mabao mengi zaidi kuliko viungo wengine ili tuamini ni bora kuliko wao.

Idd Nado na Luis Miquissone ni viungo wawili waliohusika katika mabao mengi zaidi ya Fei Toto. Fei alimaliza msimu akiwa amehusika katika mabao matano pekee, Nado alihusika katika mabao 18, nafikiri Nado alipaswa kuchukua nafasi ya Fei Toto.

Niliguna kidogo nilipoona majina ya tuzo ya beki bora wa msimu kwa mujibu wa TFF, Joash Onyango hakuwa kati ya mabeki watatu bora wa msimu uliopita.

Mabeki watatu bora wa msimu uliopita ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na Dickson Job hapa nafikiri TFF waliamua tu kuweka mzani sawa kwa kuogopa kuwa na wachezaji wengi wa Simba kwenye orodha ya tuzo, Dickson alifanya kazi lakini sioni kama aliikuta kazi ya Onyango.

Mwisho kabisa nimalize kwa kutoa ushauri, ipo haja ya kuwahi kutoa tuzo kabla ya msimu mpya kuanza. Vipi kama leo Chama atakuwa mchezaji bora wa msimu? Itabidi atume mwakilishi kupokea tuzo yake. Vipi kuhusu Haji Manara? Atapokea vipi tuzo ya mhamasishaji bora wa msimu wa Simba wakati sasa yupo Yanga?