Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWALYANZI: Hebu sikia vita hii ya Yanga na Simba

Muktasari:

  • Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na winga huyo wa zamani wa Mgambo JKT, Simba na Kagera Sugar na amefunguka mambo mengi ikiwamo kushindwa kuisahau Simba aliyojiunga nayo baada ya vita kubwa ya kugombewa Yanga sambamba na Deus Kaseke kisha kila mmoja kutua kwake.

UTASEMA nini kuhusu Peter Mwalyanzi? Winga huyu wa zamani wa Mbeya City ile iliyotetemesha vigogo wa soka chini ya kocha Juma Mwambusi amerejea katika Ligi Kuu Bara. Amepanda daraja kwa mara nyingine na Mbeya City, iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Championship.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na winga huyo wa zamani wa Mgambo JKT, Simba na Kagera Sugar na amefunguka mambo mengi ikiwamo kushindwa kuisahau Simba aliyojiunga nayo baada ya vita kubwa ya kugombewa Yanga sambamba na Deus Kaseke kisha kila mmoja kutua kwake.

Winga huyo ameanza kwa kukumbuka namna alivyoingia Simba kabla ya kutoka tofauti na kiu aliyokuwa nayo awali kabla ya kutua katika klabu hiyo ya Msimbazi.

“Simba ni timu ambayo ipo kwa ajili ya kutwaa mataji, ukiingia unatakiwa kujituma zaidi na kuamini kuwa hii nafasi niliyonayo sasa kesho kuna mwingine ataipata. Nakumbuka kuna kipindi sikuwa vizuri, nilishuka kiwango, Simba ikafanya usajili na kunitoa kwa mkopo,” anasema na kuongeza;

“Uwezo wangu ulipungua akapatikana mbadala na mimi nikatolewa kwa mkopo, mbadala wangu alikuwa ni Kichuya (Shiza) lakini pia alisajiliwa ‘Mo Ibra’ hivyo nakiri kuwa kipindi hicho natolewa kwa mkopo uwezo wangu ulitetereka kiuchezaji.”


WAGENI WAPEWE URAIA

“Ukishaona mchezaji wa nje anatamani kuendelea kucheza soka la Tanzania na kuomba uraia kabisa basi kuna kitu kakiona kwa upande wangu sioni shida ikiwezekana waongezwe wanaotamani kufanya hivyo,” anasema na kuongeza;

“Kupewa kwao uraia kunaongeza motisha kwa wachezaji wa ndani kuongeza jitihada za kupambana zaidi ili kuendana na kasi ya nyota walioamua kubaki Tanzania.’’

Mwalyanzi anasema inawafanya wachezaji wa ndani kuongeza nguvu ya kupambana zaidi hivyo wanaongeza morali ya kufanya vizuri ili kuwe na wigo mpana timu ya taifa inapotaka kuitwa.

“Wigo mpana nikiwa na maana kwamba inaamsha ari ya wachezaji hata ambao hawajawahi kuitwa katika timu ya taifa kupambania nafasi kwa kutoa changamoto kwa nyota wa kigeni ambao wameomba uraia na kutaka kunyang’anya nafasi zao.”

Anasema nafasi zinazotolewa kwa wachezaji wa kigeni wanaoomba uraia zizingatie ubora ili kutoa chachu ya ushindani kwa wachezaji wa ndani ambao wao pia wana uwezo ili kuongeza ushindani kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Mwalyanzi amefunguka hayo baada ya wachezaji wa Singida Black Stars, Emmanuel Kwame Keyekeh, Josephat Arthur Bada na Mohamed Damaro kupewa uraia.

Keyekeh raia wa Ghana, Bada wa Ivory Coast na Damaro, akitokea Guinea, kwa sasa ni raia wa Tanzania baada ya wao wenyewe kuomba kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji.


TOFAUTI YA CHAMA NA AZIZ KI

“(Clatous) Chama na (Stephane) Aziz Ki ni wachezaji wawili tofauti kila mmoja ana aina yake ya uchezaji japo kuna maeneo machache wanaingiliana lakini ukiwa kocha unaweza ukawatumia wote na wakakupa matokeo.”

“Mfano Chama ni mchezaji ambaye anapenda sana au ni mzuri zaidi kutengeneza nafasi ni kiungo ambaye anaufanya mchezo wa soka kuwa mwepesi zaidi japo pia akiwa kwenye nafasi nzuri anaweza akafunga,” anasema.

Akimzungumzia Aziz Ki aliyeuzwa na Yanga kwenda Wydad Casablanca ya Morocco, Mwalyanzi anasema ni kiungo mwenye akili ya mpira na mzuri kwenye kutumia zaidi nafasi, pia anaweza kutengeneza huku pia akisisitiza kuwa ni mkamilifu zaidi kwa kufunga na alisumbua sana alipokuwa nchini akiichezea Yanga.

“Aziz Ki ni bora kwenye kufunga lakini pia anaweza kutengeneza ukimpa mpira ndani ya 18 anakufunga, hata nje ya boksi pia anakufunga, ana jicho la kuona goli.”


MBEYA CITY YAMBEBA

Amerudi kwa mara ya pili baada ya kuichezea kwa mafanikio msimu wa 2013-14 na kuvitetemesha vigogo vya soka zikiwamo Yanga, Simba, na Azam FC. Amefunguka sababu za kuendelea kuitumikia timu hiyo akirudi msimu huu na kuipandisha kutoka Championship ikirejea kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Nimeanza kucheza soka kwenye klabu ya Mgambo lakini Mbeya City ndio timu iliyonitambulisha kwenye maisha ya soka kwani ilinipeleka Simba ambako nilienda kucheza soka la ushindani,” anasema na kuongeza;

“Mbeya City ndio timu yangu ya mafanikio imeniweka kwenye soka la ushindani, najivunia na ndio maana nimerudi kuanza upya, nafurahia kuwa sehemu ya kuipandisha tena baada ya kushuka daraja.”

Anasema kwa sababu ndiyo timu iliyomtambulisha kwenye ramani ya mpira na imempa mafanikio anaiheshimu na yupo tayari kuvuja jasho kwa ajili ya timu hiyo ambayo anakiri kuwa imerudi vizuri na hamasa iko juu.

“Mbeya City ilikuwa Championship lakini mashabiki wameitika na wanaipenda timu yao, ukiiona inacheza mashabiki wanavyojitokeza wengi utasema inacheza Ligi Kuu. Kwa hamasa hiyo naamini Mbeya kutakuwa na timu bora na shindani.”


CHAMIONSHIP SI MCHEZO

“Championiship nguvu inatumika. Mtu hakuruhusu ucheze kwa kujiandaa sana yaani huku ni nguvu sana maarifa kidogo tofauti na Ligi Kuu ambako ni mchezo wa nafasi. Ila asikwambie mtu Championship ni kugumu.”

“Kuna raha yake kucheza Ligi Kuu kwa sababu ni mchezo wa nafasi lakini Championship mambo ni magumu sana. Ili uweze kuwa bora na kuisaidia timu kupanda daraja ni lazima uwe timamu, ujiandae hasa kwa mikimikiki iliyopo.”

Mwalyanzi anasema kupandisha timu daraja inahitaji mipango sahihi kama uongozi wa Mbeya City ulivyofanya kwa kuiweka timu pamoja kuanzia viongozi, mashabiki na benchi la ufundi kitu alichokitaja kuwa ndio siri ya mafanikio ya timu hiyo kupanda daraja.

Baada ya kuiwezesha Mbeya City kupanda daraja  na kusubiri kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, Mwalyanzi anasema hata akipewa mamilioni kiasi gani, hawezi kukubali kurudi kucheza ngazi hiyo kwa msimu wa 2025-26.


DILUNGA, MUDA NA FEI TOTO

Licha ya nyota wengi wa kigeni hasa eneo la kiungo kutajwa kwa ubora huku nyota wa ndani wakisahaulika, Mwalyanzi hajasita kuwapa maua yao baadhi ya mastaa wanaocheza eneo hilo.

“Ni kweli wageni wamekuja kuleta mageuzi kwa kufanya vizuri lakini kuna nyota wa ndani wapo vizuri na wana nafasi kubwa ya kutoa ushindani kwa wageni ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele mfano Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya na Hassan Dilunga,” anasema na kuongeza:

“Nawaheshimu viungo wote wazawa ambao wanacheza nafasi yangu, nawaomba waendelee kupambania kombe ili kujiweka katika ushindani. Hakuna mchezaji ambaye anacheza ili kupoteza muda wote tunatafuta fedha, tukiwa bora tutatengeneza nafasi ya kujiweka sokoni kwa dau kubwa.”

Mwalyanzi anasema kiwango cha wachezaji wa kizawa kinakua na kuongezeka kama ambavyo wachezaji wa kigeni wanavyozidi kuongezeka na wao wanapambana kuongeza ushindani huku akiweka wazi kuwa ndio sababu ya ligi ya Tanzania kupanda kwenye viwango ya ubora.


MAXI, PACOME NA DUBE

“Kwa miaka ya hivi karibuni kuna nyota wengi wa kigeni wamekuja kuongeza chachu ya ushindani. Nikisema nitaje kwa majina sitamaliza leo lakini Chama, Aziz Ki ambaye sasa ameondoka nchini, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube, na wengine wengi,” anasema na kuongeza;

“Uwepo wa nyota hao umeongeza chachu ya ubora wa ligi yetu lakini pia wamekuwa chachu ya ushindani kwenye soka la ndani na kimataifa. Hakuna mtu alitarajia nchi yetu ingekuwa nafasi ya nne au ya tano kwa ubora. Ukiondoa hilo pia inavuta wachezaji kutoka mataifa makubwa kuja kucheza Tanzania.”

Mwalyanzi anasema timu ambazo zinapata nafasi ya kusajili nyota kutoka mataifa mbalimbali zinatakiwa kuzingatia ubora ili kuleta nyota ambao watakuwa chachu ya kuongeza ushindani na kukuza viwango vya wachezaji wa ndani.


KASEKE ALIMTIBULIA YANGA

“Kabla ya msimu 2014-2025 haujaisha nikiwa Mbeya City nilikuwa nawasiliana na viongozi wa Yanga ambao walikuwa wanasubiri msimu uishe ili tukae meza moja kwa mazungumzo ya kusaini mkataba,” anasema na kuongeza;

“Wakati naendelea kuwasiliana nao Simba wakawa wanamtaka Deus Kaseke lakini Yanga wakamuwahi Deus na Simba baada ya kuona hivyo wakawahi kuja kunisajili, nakumbuka Yanga tulikuwa bado hatujafikia kwenye ofa, watani zao walikuja moja kwa moja na kumalizana na mimi.”

Mwalyanzi anasema dili la Kaseke lilikwamisha yeye kutua Yanga na kujikuta anacheza Simba kwa sababu viongozi wa timu hiyo hawakutaka kusubiri msimu kuisha walimalizana naye haraka ili kukwepa kuzidiwa tena na watani zao Yanga kama ilivyotokea kwa Kaseke.

“Yanga walitaka mimi nije Dar es Salaam ili tumalizane lakini Simba wao tulimaliza mazungumzo kwa simu na kufanikisha dili la mimi kutua klabuni kwao,” anasema.