UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Filamu ya Bernard Morrison

Thursday May 19 2022
Morrison PIC
By Oscar Oscar

LABDA inaweza kuja kushindana na ile Isidingo ya Wasauzi kwa urefu. Baada ya kutazamwa katika nchi 103 dunia nzima Isidingo ilifika mwisho wa Machi ya 2020 ikiwa ni miaka 22 tangu ianze kutazamwa.

Wakati Isidingo inaanza kuonyeshwa katika televisheni Julai 1998 mchezaji wa Simba na raia wa Ghana, Bernard Morrison alikuwa na umri wa miaka mitano. Sijui kama ni sahihi kumuita mchezaji wa Simba kwa sasa.

Hata Simba wenyewe hawafahamu kama ni mchezaji wao. Ndiyo. Hawafahamu ndiyo maana wametoa taarifa tata kuhusu uwepo wake klabuni. Waraka uliotolewa na Simba hauelezi vema kama wameachana na Morrison au wamempa likizo kama walivyodai.

Huu ni mwendelezo wa filamu ambazo zimekuwa zikiratibiwa na Morrison tangu atue nchini kuitumikia Yanga miaka mitatu iliyopita.

Filamu yenyewe ilianza alipoondoka Afrika Kusini. Baada ya kuachana na Orlando Pirates alipitisha muda wa kukaa Afrika Kusini, mamlaka ya uhamiaji wakamfungia kuingia nchini humo.

Mchezaji wa kulipwa karne ya 21 unaishi vipi kihuni? Makosa yake yalikuja kuigharimu Simba mara mbili katika mechi za kimataifa dhidi ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates mechi ambazo Simba walimhitaji zaidi.

Advertisement

Alipofika nchini aliendelea kuachia mwendelezo wa filamu zake. Alikubali kusaini mkataba wa miezi sita kwasababu ana amini kipaji chake.

Aliaza kwa utulivu lakini baadae aligundua soka la Tanzania linaendeshwa kisela ukishapendwa basi unaishi utakavyo.

Kabla hata hajamaliza miezi sita yake akachomoa kucha zake - alipotea Yanga kwa muda kisha akarejea katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Simba. Mechi ambayo aliondoka uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko. Hakuwahi kurejea Yanga tena hadi alipoachia mwendelezo wa filamu yake miezi michache mbele.

Alisaini Simba huku akiwa na mkataba wa Yanga. Mkataba ambao baadaye ulionekana kuwa na udhaifu na baadaye kuruhusiwa kujiunga na Simba.

Kumbuka sio kwamba hakuwa na mkataba na Yanga, bali ni kwa sababu Yanga wenyewe walifanya uzembe kutozingatia baadhi ya vipengele ambavyo vingeweza kumbana. Ni hii filamu iliyompa jina la wakili msomi.

Alipojiunga na Simba aliahidi kwamba atabadili tabia zake. Simba wakaamini inawezekana. Walisahau Morrison hayupo katika umri wa kubadilika tena. Ni kama walijaribu kumfuga kunguru wakiamini anaweza kuwa njiwa.

Baada ya muda Morrison halisi alirejea na mwendelezo wa matukio ya utovu wa nidhamu ambayo sitayamaliza nikayaeleza hapa. Ni mpaka juzi ilipokuja filamu yake ya kuachana na Simba kwa kisingizio cha mapumziko.

Kama wamempa likizo kwanini wamshukuru kwa yote aliowafanyia? Huwezi kumtakia kila la heri katika maisha yake ya soka mchezaji anayekwenda kutatua matatizo ya familia. Hizo ni kauli za kiungwana za kumuaga mchezaji wako, lakini Simba wametoa taarifa kama wamemuaga na kama vile bado ni mchezaji wao.

Kwanini Simba wamefanya hivi? Majibu wanayo uongozi wa Simba.

Nilisikia mahali kwamba Simba wamechoshwa na mfululizo wa tabia zake mbovu na wameamua kuachana naye moja kwa moja. Inaweza ikawa kweli kwa kutazama historia ya mchezaji mwenyewe. Lakini swali linakuja, Simba wanahofia kitu gani kutangaza ukweli kwamba wameachana na Morrison kwa sababu za utovu wa nidhamu?

Nilipouliza mtu mmoja aliniambia kwamba wanahofia kuzungumzwa na kuchambuliwa kwamba wanapoteza utulivu wanapozungumzwa sana.

Unakaa chini unawaza hadi leo timu inayojinadi kwa ukubwa bado inahofia kupasuliwa na kalamu za waandishi wa habari?

Sasa tunasubiri mwelekeo wa Morrison, Simba wanaweza kumrudisha kundini? Sidhani. Morrison anaweza kwenda nje ya nchi? Sidhani pia. Kama atasalia nchini ataenda wapi? Sijui lakini nina uhakika hawezi kwenda Namungo au timu inayofanana na Namungo. Azam? Inawezekana lakini hatazungumzwa sana.

Sehemu pekee nje ya Simba ambayo itamfaa Morrison ni Yanga. Je anaweza kurejea Yanga? Inawezekana.

Tabu ni maisha ya Morrison baada ya kurejea Yanga. Atabadili mienendo yake?

Sidhani kama limao linaweza kuwa chungwa. Nachodhani ni kwamba popote pale atakapokuwa Morrison ndani ya hili taifa ataendelea kutuletea filamu za kutisha na kusisimua.

Nipe maoni yako kwa simu hiyo hapo juu. Tuwasiliane

Advertisement