UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Bwalya na Kambole mahakamani?

Bwalya atimka Simba

MZEE wa Kaliua nimekabidhiwa rungu la hakimu, mezani nina kesi mbili za kuzihukumu. Kesi kati ya raia wawili wa Zambia na klabu mbili kubwa nchini Tanzania.

Kesi ya kwanza, mshitakiwa ni Simba, anashtakiwa na wadau wa soka Tanzania kwa kumruhusu mchezaji wao kipenzi Rally Bwalya kuondoka kipindi ambacho bado walikuwa wanamhitaji.

Kesi ya pili, mshtakiwa Yanga, anashtakiwa na wadau wa soka kwa kumsajili ‘mshambuliaji wa kawaida’, Lazarous Kambole.

Baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote, upande wa mshtaki na mshitakiwa nadhani nianze kutoa hukumu ya kesi ya pili!

Upande wa mshitaki wanadai mshitakiwa amewalaghai kwa kumsajili mshambuliaji wa kawaida wanayeamini uwezo haumtoshi kucheza klabu kubwa kama Yanga.

Kisa? Katika michezo zaidi ya arobaini na tano ambayo Kambole ameichezea timu yake ya zamani Kazier Chiefs, hajafanikiwa kufikisha hata mabao matatu! Ni takwimu mbovu kwa mchezaji wa eneo la ushambuliaji.

Ni hoja nzito inayofikirisha kutoka kwa wadau wa soka nchini. Lakini, kabla ya yote tukumbuke amefeli katika ligi ya Afrika Kusini. Kusanya vidole vyako, hesabu wachezaji wote waliowahi kufeli katika ligi bora zaidi kuliko ya Tanzania kisha watazame walipotua nchini. Nini kilitokea? Labda walifeli lakini si kwa ukubwa ule wa Afrika Kusini.

Ninaweza nikakuhesabia wachache kwa haraka. Luis Miquissone ambaye mpaka sasa hivi ‚Simba wanamuota‚ aliwahi kusajiliwa na Pitso Mosimane pale Mamelodi Sundowns, alifeli vibaya na walimzungusha kwa mkopo kabla ya kufika Simba.

Wote tunafahamu Miquisone alikuwa mchezaji wa aina gani alipokuwa nchini, wote tunafahamu jinsi anavoteseka sasa hivi kule Misri.

Kuna mchezaji bado anaitwa Bernard Morrison, wote tumeshuhudia mabalaa yake akiwa ndani ya uzi wa Yanga na Simba. Pia tunafahamu vyema aliwahi kufeli vibaya kule Afrika Kusini.

Kesi kama hiyo imemtokea Mzimbabwe anayeoongoza safu ya ushambuliaji ya Azam FC, Prince Dube. Dube aliwahi kufeli vibaya kule Super Sport lakini wote tunaona anachokifanya Ligi Kuu Bara.

Unaweza ukaendelea kutaja wachezaji wengine waliofeli katika ligi imara zaidi lakini wakafanikiwa nchini na usimalize orodha yako.

Unaweza ukawataja kina Clatous Chama na wenzake. Kwa hiyo kufeli kwa Kambole huko Afrika Kusini bado hakutoi jibu la moja kwa moja atafeli nchini.

Bado tunabaki na ukweli tuna ligi nyepesi ambayo mchezaji wa kawaida katika ligi ngumu kama ya Afrika Kusini ana nafasi ya kuibuka staa. Naweza kumwekea Kambole dhamana, pia tuna ukweli mwingine tunaopaswa kuukubali usajili wowote ni kamari.

Unaweza ukamsajili mchezaji mzuri kisha akapotea vibaya, ningewaulumu Yanga kama wangemsajili mchezaji kama Yikpe ambaye alifeli hadi ligi ya Kenya lakini kwa Afrika Kusini bado naweza kuwakingia kifua.

Tuhamie kwenye kesi ya Rally Bwalya. Kwamba Bwalya alikuwa mchezaji muhimu sana kwa Simba na hawakupaswa kumruhusu aondoke? Sikubali sana!

Nadhani Bwalya ni mchezaji anayegawa pande mbili unapomweka mezani kumjadili. Kuna nyakati unaona kama ni muhimu sana kwa Simba lakini zipo nyakati unahisi kama Simba wanamuhitaji kiungo mzuri Zaidi yake.

Hata Simba wenyewe walikuwa hawaelewi kama bado wanahitaji kuendelea nae au wamuoneshe mlango wa ‚‘Exit’. Walikuwa katikati wakihofia juu ya uamuzi wowote watakaoufanya juu ya Bwalya.

Amazulu wamekuja kuwarahisishia kazi ya kufikia maamuzi ambayo yalikuwa yanawatesa. Kwa mtazamo wangu, Simba kufanikiwa kumpunguza Bwalya ni kitu kizuri kwasababu watapata nafasi ya kumsajili kiungo mwingine imara zaidi.

Kumbuka Simba wanaweza kusajili wachezaji 12 tu wa kigeni hivyo lazima wazitumie vema nafasi zao kupata wachezaji ambao hawawezi kuwapata nchini.

Ningemtetea Bwalya kama angekuwa mzawa. Lakini hapo hapo kumbuka kwamba Bwalya anaondoka kwenda katika ligi kubwa zaidi, anazidi kupandisha wasifu wake zaidi.

Katika umri wa miaka 28 anazidi kujiongeza muda wa kucheza zaidi kwenye klabu imara zaidi. Anaweza kufeli Amazulu akarejea nchini tena akacheza Simba, Yanga au Azam kisha akazidi kuporomoka kuelekea Namungo na kwingineko.

Kwahiyo kwake ni faida kwamba atazidi kukamata pesa za soka zaidi, hivyo Simba na Bwalya wote wamepiga bao! Wazungu wanasema ‘win-win situation’.