Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubilionea wa Ronaldo kielelezo cha hadithi tamu ya soka

PAZIA Pict


MCHEZO wa wahuni umetupa bilionea wake wa kwanza. Soka. Na bilionea mwenyewe ni Cristiano Ronaldo kutoka visiwa vya Madeira pale Ureno. Ukitaka kuandika kila kitu kuhusu Ronaldo unaweza kujaza gazeti zima, lakini bado halitatosha.


Juzi mtandao wa Bloomberg umemtangaza Ronaldo kuwa bilionea. Ametukomboa sisi masela wa maskani, hasa wa vijiwe vya Afrika ambao maisha yetu ni ubishi mbalimbali kuhusu soka. Walau amekuwa alama yetu katika masuala ya pesa.


Kwanini? Kule katika fani nyingine wamewahi kutokea mabilionea, lakini huku katika soka ilikuwa bado. Kwa mfano, kule katika muziki tayari Shawn Carter maarufu kama Jay Z alitangazwa kuwa msanii wa kwanza wa Hip Pop kuwa bilionea. Ilikuwa mnamo mwaka 2019. Na kwa sasa anatajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 2.6 bilioni.

Wakati fulani, msanii mwingine Dr Dre ambaye pia ni mtayarishaji maarufu wa muziki nchini Marekani alishawahi kutangazwa kuwa bilionea. Hata hivyo, ubilionea wake umeshuka kwa sababu mbalimbali na sasa sio bilionea tena.

PAZI 01

Katika mchezo wa kikapu, Michael Jordan, Magic Johnson na LeBron James kwa nyakati tofauti waliwahi kutangazwa kuwa mabilionea. Katika mchezo wa gofu, Tiger Woods aliwahi kutangazwa kuwa bilionea na imebaka kuwa hivyo mpaka sasa.

Katika mchezo wa tenisi, Mswisi Roger Federer aliwahi kutangazwa kuwa bilionea. Na sasa kwa mara ya kwanza katika mchezo wa soka, Cristiano Ronaldo ametangazwa kuwa mwanasoka wa kwanza katika historia kuwa bilionea.

Tumetoka mbali hadi Ronaldo kuwa bilionea. Namna ambavyo mchezo wa soka ulikuwa ukichukuliwa. Mchezo wa kihuni. Lakini zaidi kama utachunguza hapo, basi wanamichezo wengi mabilionea wametokea Marekani kasoro Federer.

PAZI 02

Kwanini Ronaldo amekuwa bilionea? Amejitengeneza kuwa hivyo. Ni kazi ngumu kuwa bilionea katika soka na Ronaldo amekuwa bilionea huku akiendelea kucheza mchezo wenyewe. Pesa zilizoongezeka katika akaunti yake kiasi cha kuwa bilionea zimetokea Saudi Arabia ambako anacheza soka kwa sasa.

Katika umri wa miaka 40, Ronaldo ameendelea kulipwa vyema pale Saudia, lakini zaidi ni kwamba ameendelea kushikilia mikataba yake binafsi kutoka katika kampuni mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumia taswira yake kumtangaza.

Kwanini Ronaldo? Achilia mbali kwamba katika soka amekuwa na mafanikio makubwa, lakini Ronaldo ameweza kujitengeneza vyema kuwa supastaa kwa mwonekane wake na maisha yake binafsi. Ni tofauti na hasimu wake Lionel Messi ambaye licha ya kuwa na pesa nyingi, lakini hajajitengeneza kimvuto zaidi nje ya uwanja.

PAZI 03

Huku uswahilini asilimia kubwa tunaamini kwamba Messi ni zaidi ya Ronaldo katika mchezo wenyewe uwanjani, lakini linapokuja suala la kujitengeneza kimvuto Ronaldo amekwenda mbali zaidi. Haishangazi kuona anaingiza pesa nyingine zaidi ya Messi. Haishangazi kuona ndiye mwanadamu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mitandao ya kijamii kwa sasa. Amejua kujitengeneza kiasi kwamba hata watu wasiofuatilia sana mpira wamekuwa wakimfahamu Ronaldo. Hili limeongeza pesa zake kiasi cha kufikia kuwa bilionea.

Huku kwetu mtaani halikuwa jambo rahisi kwa mwanasoka kuwa bilionea. Kabla ya Ronaldo kuwa mwanasoka mwenye mvuto tuliwahi kuwa na David Beckham. Waingereza walimtengeneza haswa Beckham na mkewe, Posh Spice. Waingereza walimtengeneza Beckham kuwa mchezaji mwenye mvuto, lakini pia wakatuaminisha kwamba uwanjani alikuwa bora kuliko Zinedine Zidane, Luis Figo, Rivaldo na wachezaji wengine wa kizazi chake. Hata hivyo, Beckham hakuweza kuwa bilionea.

PAZI 04

Kabla yake, miaka hiyo ya zamani kabla ya ubilionea haujafikiwa na wanamichezo, watu kama kina Sir George Best wangeweza kuwa mamilionea. Staa wa Manchester United huyu kutoka Ireland Kaskazini ambaye alifahamika kwa jina la utani la Belfast Boy. Best alikuwa mchezaji mwenye mvuto katika miaka yake na alikuwa na kipaji maridhawa. hata hivyo, aliishia kuwa mlevi na ‘kuonea’ wanawake warembo. Inasadikika kwamba akiwa katika ubora wake aliwahi kutembea na washindi wanne wa taji la Miss World.

Na unaporudi kwa Ronaldo, hauwezi kuacha kutafakari kuhusu maisha yake binafsi. Namna alivyoibuka kuwa bilionea baada ya kutokea katika umaskini uliotopea pale Madeira. Historia yake ni tofauti kidogo na hawa kina Federer ambao walau wazazi wao walijimudu katika maisha.

Ronaldo alilelewa na baba mlevi ambaye baadaye alikufa kwa pombe na kuacha mzigo mkubwa katika familia. Ronaldo aliwahi kulazimika kulala chumba kimoja na watoto wa kike nyumbani kwao kwa sababu nyumba ilikuwa ndogo. Wakati ule akiibukia katika soka la watoto anakiri kwamba yeye na watoto wengine maskini hawakumudu maisha kiasi kwamba walilazimika kwenda kuomba makombo ya chakula katika migahawa maarufu ya McDonald kule Lisbon.

PAZI 05

Leo, Ronaldo ni bilionea ambaye anamiliki ndege yake binafsi. Achana na ushabiki wa nani zaidi kati yake na Messi, Ronaldo ni mchezaji wa kuigwa kwa staili ya maisha yake. Amepambana kujitengeneza kufika ambako amefika. Inawezekana hana kipaji cha maajabu kama Messi, lakini amepambana ndani na nje ya uwanja kuufikia ubilionea. Ametoa kafara ya vitu vingi katika maisha yake kwa ajili ya kuwa staa mkubwa ambaye ni bilionea. Wakati wa ujana wake pale Manchester United alianza kuishi maisha ya ovyo, lakini ghafla akabadilika.

Alikuwa akitembea na warembo wengi maarufu wa Marekani na kwingineko, lakini ghafla akabadilika na kuanza kuishi maisha ya kifamilia zaidi. Mpaka sasa Ronaldo hanywi pombe na ameachana na maisha yote ya anasa. Hatimaye amefanikiwa kuwa bilionea na sisi huku mtaani tunaweza kuwatambia watu wa fani nyingine kwamba mchezo wetu nao umetoa bilionea.