Twenzetu robo fainali

HAKUNA kitu kinachosubiriwa kwa hamu na mashabiki Simba na Yanga wikiendi hii kama kuziona timu hizo zikiandika historia ya kufuzu kwa pamoja kwenda hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF. Haijawahi kutokea tangu ziundwe. Hata Afrika Mashariki inasubiri kwa hamu wasaa huu.

Simba ipo Kundi C la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikicheza leo Jijini Dar es Salaam dhidi Horoya AC ya Guinea, kisha watani wao Yanga kumalizia kazi kesho Jumapili kwa kuvaana na US Monastir ya Tunisia.

Mechi zote zitapigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kama timu hizo zitautumia vyema uwanja wa nyumbani, maana yake zitajihakikisha kwenda robo fainali ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kufuzu hatua hiyo kwa pamoja ndani ya msimu mmoja.

Haijawahi kutokea kwa timu mbili za Tanzania kwa ngazi ya klabu kufika robo fainali ya michuano ya Afrika kwa msimu mmoja, lakini raundi hii nuru imeonekana kwani Simba na Yanga zina nafasi ya kufanya hivyo na kuweka rekodi hiyo tamu inayoliheshimisha taifa.
Kufuzu huko kwenye hatua hiyo mbali na kuwa ni heshima kwa Tanzania, lakini pia itaziweka karibu timu hizo katika kuogelea mamilioni ya fedha zinazotolewa na wadhamini wa michuano hiyo inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).


SIMBA
Simba hadi sasa ipo nafasi ya pili kwenye kundi D baada ya kucheza mechi nne ikipoteza mbili za mwanzo na kushinda mbili zilizofuata ikivuna alama sita nyuma ya vinara Raja Casablanca ya Morocco ambao tayari wamefuzu baada ya kushinda mechi zote nne za mwanzo na kufikisha pointi 12 kileleni.
Nyuma ya Raja na Simba, zipo Horoya yenye alama nne ilizovuna kwa kushinda mechi moja na kutoa sare moja kati ya nne ilizocheza na mkiani ipo Vipers ya Uganda yenye pointi moja katika mechi nne zake.

Hivyo Simba ikishinda leo katika mechi itakayopigwa kwa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku itaungana na Raja kutinga robo fainali kwani itafikisha alama tisa ambazo sio Horoya wala Vipers inayoweza kuzifikisha katika mechi zilizobaki.
Simba ikiichapa Horoya itakuwa imebakiza mechi moja ugenini dhidi ya Raja ambayo hata hivyo sio ya muhimu kwani tayari itakuwa imefuzu na Horoya itakuwa imebakiza mechi nyumbani na Vipes ambayo hata ikishinda itaishia alama saba tu.
Hiyo ndiyo inaifanya Simba kutakiwa kujitoa kwa nguvu zote kwenye mechi ya leo ili kushinda kwani kama itatoa sare itafikisha alama saba na Horoya kufikisha tano na kusubiri mechi za mwisho kuamua nani afuzu na kutokana na Raja kuonekana kuwe kwenye ubora mkubwa nafasi ya Simba itakuwa finyu kuliko ya Horoya ambayo itakutana na vibonde Vipers.
Na kama Simba ikipoteza hali itakuwa hivyo hivyo kusubiri mechi  ya mwisho kwani Ushindi kwa Horoya utaifanya kufikisha pointi saba na kukaa nafasi ya pili na hapo Simba itakuwa imebakiza dua mbaya tu kwa Horoya ili ifungwe na Vipers mechi ya mwisho na yenyewe ishinde mbele ya Raja ugenini jambo ambalo linawezekana lakini ni gumu.

Hata hivyo matokeo ya mechi zilizopita yanaipa nguvu Simba kuliko Horoya kwenye mechi hiyo kwani Simba imeshinda mechi mbili za mwisho za CAF dhidi ya Vipers nyumbani na ugenini lakini Horoya imechapwa mili za mwisho na Raja.
Licha ya kwamba Horoya siyo timu ya kubeza lakini Simba pia ina uwezo wa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kushinda kama ilivyofanya Horoya kwake ikishinda 1-0.
Eneo ambalo linaweza kuamua mechi hiyo kwa Simba ni lile la ushambuliaji ambalo halijawa na namba nzuri kwenye michuano hii likiwa limefunga bao moja tu la Clatous Chama kwenye mechi iliyopita dhidi ya Vipers kwa Mkapa kwani katika mchezo wa kwanza bao lilifungwa na beki Henock Inonga.

Safu ya mbele ya Simba imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi za kupata mabao lakini umaliziaji wake umekuwa butu jambo ambalo katika mechi ya leo wanahitaji kuhakikisha makosa hayo hayajirudii na kutumia kila nafasi wanayopata kupata bao.
Hata hivyo Wekundu wa Msimbazi hao wanatakiwa kuwa makini na eneo lao la mabeki wa Pembeni ambapo Mohamed Hussein na Shomari Kapombe wamekuwa wakipanda kushambulia na kuchelewa ckurudi jambo ambalo kama watazembea linaweza kuwa tatizo kwao kutokana na ubora na kasi ya mawinga wa Horoya.

Kocha Mbrazil wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' ameliambia Mwanaspoti kuwa ataingia kwenye mechi hii akiwa na lengo moja tu la kushinda huku mshambuliaji Jean Baleke akisema hawataki kurudia makosa kwenye kufunga.
"Kila mmoja wetu anajua mechi hii tunataka kusdhinda tu, tunatambua ugumu wa Horoya na tunawaheshimu lakini nafasi yetu ni sasa tunaenda kushinda ili kuingia robo fainali na kila mmoja yupo tayari kutimiza lengo hilo," alisema Robertinho.
"Sina bao hadi sasa kwenye michuano ya CAF, lakini ni kweli pia ulivyosema hatujapata mabao ya kutosha kama safu ya ushambuliaji, lakini tumejifunza kutokana na makosa na sasa kwa yeyote atakayepata nafasi naamini atafanya vyema na kufunga ili kuhakikisha tunashinda mechi," alisema Baleke.
Kwa namna Mwanaspoti lilivyofuatilia kwa ukaribu mazoezi ya Simba, huenda leo ikaanza na kikosi hiki;
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Saidi Ntibanzokiza na Clatous Chama.


YANGA
Wananchi msimu huu wamekuja kwa hasira na sasa lengo lao ni kutoboa hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini hesabu ya sasa ni kushinda kesho Jumapili dhidi ya Monastir na kufuzu robo fainali.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na alama saba baada ya kucheza mechi nne kushinda mbili, sare moja na kupoteza moja nyuma ya Monastir ya Tunisia ambayo imefuzu tayari ikiwa na pointi 10 ilizovuna baada ya kushinda mechi zake tatu na kutoa sare moja kati ya nne ilizocheza.

Nyuma ya Monastir na Yanga, zipo TP Mazembe ya DR Congo yenye alama tatu baada ya kushinda mechi moja na kupoteza tatu katika nne ilizocheza na mkiani ipo Real Bamako ya Mali yenye pointi mbili ilizovuna kwenye sare mbili ilizopata na kupoteza mechi mbili kati ya nne ilizocheza.
Hata hivyo katika kundi hili, Yanga inanafasi kubwa ya kufuzu robo fainali licha ya kwamba Mazembe na Bamako nazo zinaweza kufuzu.

Yanga ikishinda mechi ya kesho dhidi ya Monastir itafuzu moja kwa moja robo fainali kwani itafikisha alama 10 ambazo sio Mazembe wala Bamako wanaweza kuzifikia hata wakishinda mechi zo zilizobaki.
Licha ya kufungwa 2-0 na hao hao Monastir ugenini katika mechi ya kwanza, Yanga bado inanafasi ya kupindua meza na kuwafunga watunisia hao kwa Mkapa.
Kama Yanga itapata sare kwenye mechi hiyo bado itakuwa na nafasi ya kusonga kwani itafikisha alama tisa na sare au unshindi katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya TP Mazembe itaipeleka robo fainali.
Moja ya faida ilizo nazo Yanga kwenye mechi hiyo ni kutokuwepo kwa kipa namba moja wa Monastir mwenye kadi tatu za njano pia moja ya mawinga wake hatari atakosekana kutoka na majeraha aliyopata mazoezini.

Yanga inapaswa kutumia vyema nafasi hizo lakini pia inapaswa kuongeza umakini katika kukaba mipira ya kutenga (Faulo na Kona) ambayo imekuwa Silaha kubwa kwa Monastir na katika mechi ya kwanza ugenini mabao yote yalifungwa kwa njia hiyo.
Lakini pia Yanga inafaida ya kuwa na safu imara ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao sita hadi sasa kwenye hatua hiyo hivyo ikijipanga vizuri inaweza kutumia nafasi zinazotengenezwa na kupata ushindi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Yanga, Mtunisia Nassredine Nabi alisema anawajua vyema Monastir na amekaa na wataalamu wa Yanga kuwasoma na hadi sasa wanajua wataingiaje kesho.
"Tunawafahamu Monastir na tumetumia muda mwingi kuwasoma, ni timu nzuri lakini sehemu kubwa ya ubora na udhaifu wake tunaijua na tumekwisha pata namna ya kuwakabili na kushinda kwani ndio lengo letu," alisema Nabi.
Beki wa Yanga Dickson Job alisema wapo tayari kwa mechi hiyo na kila kitu kinaendelea vizuri.

"Tupo tayari kupambana, kama wachezaji tumejiandaa kuhakikisha timu inashinda na sasa tunasubiri muda wa mechi ufike tukapambanie alama tatu muhimu," alisema Job aliyecheza mechi zote za hatua ya makundi.
Kwa namna Yanga ilivyofanya mazoezi, huenda kesho ikaanza na kikosi hiki; Djigui Diarra, Joyce Lomalisa, Djuma Shaban, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala, Jesus Moloko, Kharid Aucho, Fiston Mayele, Mudathir Yahya na Keneddy Musonda.


KUOGA MINOTI
Achana na yale mamilioni ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye kila bao, Simba na Yanga zikitinga robo fainali zitapata mkwanja mrefu ikiwa kama Bonasi ya kufika hapo.
Kama Simba itafika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itapata Dola 650,000 ambazo ni zaidi ya sh 1.4 Bilioni za Kitanzania.
Kwa upande wa Yanga kama itafika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itavuna mkwanja wa Dola 350,000 ambazo ni zaidi na Sh 800 milioni za Kitanzanaia.
Lakini pia kama zitashindwa kufuzu basi zitapata fedha za kumaliza nafasi ya tatu na nne kwenye kundi ambapo kwa Yanga itakuja Dola 275,000 zaidi ya sh 600 milioni za Kibongo na Simba itavuta Dola 550,000 ambazo ni kama sh 1.2 bilioni hivi.