Tusikubali Ligi ya mechi ya 364 ‘Hat Trick’ moja
Muktasari:
Hat Trick yake amefunga katika mechi ya nne tu ya ligi na haionekani kama itakuwa hat trick yake ya mwisho. Lakini vilevile haionekani kama itakuwa hat trick pekee katika ligi.
LIGI inaanza Jumamosi na wachezaji wetu wana madeni mengi kwelikweli. Kule England, Diego Costa anaoongoza katika wachezaji wanaolipa madeni. Sio kwa kufunga mabao saba katika mechi tatu, bali tayari ameshapiga ‘Hat Trick’.
Hat Trick yake amefunga katika mechi ya nne tu ya ligi na haionekani kama itakuwa hat trick yake ya mwisho. Lakini vilevile haionekani kama itakuwa hat trick pekee katika ligi.
Kuna watu wengi ambao watamjibu. Sio msimu unaoweza kuisha vipi bila ya Robin van Persie kumjibu Costa.
Kuna mambo ambayo unaweza kuyaona ni kama ya kawaida katika macho yetu, lakini kumbe tunayatazama zaidi katika Ligi Kuu za Ulaya na kudhani yanatokea katika ligi yetu kumbe sio kweli.
Misimu mitatu iliyopita ilichezwa ligi yenye mechi zaidi ya 300 Tanzania nzima lakini kulikuwa na Hat Trick moja tu kutoka kwa mshambuliaji wa Polisi Dodoma, Juma Semsue. Walau msimu uliopita, Amiss Tambwe aliwaongoza wachezaji watatu kupiga Hat Trick.
Bado inabakia kuwa aibu kubwa kwa washambuliaji na wachezaji wa nafasi nyingine kucheza mechi 364 za msimu huku kukiwa na Hat Trick tatu tu msimu mzima. Inaonyesha kiasi gani wachezaji wetu hawako katika daraja la kucheza Ligi Kuu.
Lakini ni mara ngapi umekwenda katika uwanja wowote ule unaochezwa Ligi Kuu na kushuhudia mabao murua ya mipira ya adhabu. Hapana. Mchezaji anakwenda kujaribu tu jinsi ya kupiga kama vile yuko mazoezini. Akikosa anarudi katika nafasi yake kujipanga.
Katika mechi 364 za msimu uliopita, hakuna mchezaji aliyefunga mabao walau manne ya mpira wa adhabu na hivyo kuwatia hofu mashabiki au wachezaji wa timu pinzani.
Akina Abeid Mziba pia hawapo tena katika timu zetu. Katika mechi 364 za Ligi yetu, ni nani ambaye msimu uliopita ameashiria kwamba yeye ni hatari sana kwa mipira ya vichwa? Hakuna.
Changamoto ya watu maalumu (specialists) katika maeneo fulani ya uwanja nayo imetoweka. Hakuna mtaalamu wa vichwa, hakuna mtaalamu wa mipira ya faulo, hakuna mtaalamu wa mashuti ya mbali.
Katika hili la mashuti ya mbali, Jonas Mkude alifunga bao maridadi katika pambano dhidi ya Prisons msimu uliopita. Baada ya hapo hakuweza kurudia tena. Lakini kwa wenzetu ndio tunaona akina Frank Lampard wakirudia tena na tena kila wakati.
Tuna mtaalamu wa mipira ya kurusha tu, Mbuyu Twite au wakati mwingine Oscar Joshua. Kila Twite akirusha mpira inaonekana kuwa hatari. Lakini tulipaswa kuwa na wachezaji wa namna hii katika kila idara na katika kila timu.
Kwa nini hatuna watalaamu hawa tena? Jibu ni rahisi tu. Wachezaji wetu wanacheza soka kitimu zaidi na hawana mazoezi binafsi. Hakuna mchezaji aliyeamua kufa na ubora wake na kuachana na mapungufu yake mengine.
Tunawaona wachezaji wetu wakishuka katika basi la timu, wakifanya mazoezi yao, wakimaliza, wanakunywa maji wanaondoka. Ni nadra kukuta wachezaji wakibaki uwanjani na kutoka jasho kwa ajili ya kufanya mazoezi yao binafsi.
David Beckham alikuwa anatumia zaidi ya saa zima peke yake kufanya mazoezi ya kupiga faulo (free kicks). Baadaye ujuzi wake aliuhamishia katika mechi. Mpaka leo ndiye mchezaji anayeongoza kwa kufunga mipira mingi zaidi ya faulo katika Ligi Kuu ya England.
Ni wakati wa wachezaji kuzitendea haki kamera za Azam TV. Ligi inahitaji wachezaji maalumu katika kila eneo. Tuzitendee haki takwimu ambazo tunaziona kila mara kwa wenzetu. Tuko katika dunia mpya ambayo hakuna kinachoweza kusahaulika kwa urahisi mbele ya televisheni zetu.
Bao la mshambuliaji wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ katika pambano la ufunguzi wa Ligi dhidi ya Azam lilitenda haki katika televisheni za Azam TV. Lilitenda haki binafsi kwake na kumtambulisha kama mshambualiji anayejua kufunga pengine kuliko kuuchezea mpira katika maeneo mengine ya uwanja.