Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tshabalala hakustahili kuondoka hivi Simba

TSHABA Pict


Kama kuna kizazi cha dhahabu cha wachezaji wazawa katika miaka ya karibuni kilichoifanya Simba ing’are katika soka la ndani na Afrika, basi ni kilichoondokana na unyonge wa kukosa ubingwa miaka mitano mfululizo na kugeuza kibao na kuwa ubabe wa miaka minne mfululizo, kikimjumuisha beki wa kushoto Mohamed “Tshabalala” Hussein Zimbwe.


Nahodha huyo aliungana na wazawa wengine kama Shomari Kapombe, John Bocco, Mzamiru Yassin na Aishi Manula pamoja na wageni waliokuwa wakiingia na kutoka, kutikisa soka la ndani kwa kutwaa ubingwa mara nne mfululizo, huku ikifika hatua ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho.


Kati ya wote hao, Tchabalala na Kapombe walitamba kwa muda mrefu bila ya kushuka kiwango, huku Kapombe akikosekana wakati fulani kutokana na majeraha wakati ilikuwa ni nadra kwa Zimbwe kukosekana uwanjani.

Kapombe, Manula na Bocco walikuwa ni baadhi ya wachezaji waliotokea Azam FC ambako waliiwezesha kutwaa ubingwa wa soka wa Bara, lakini wakati klabu hiyo ilipoweka sera mpya ya mishahara, hawakukubaliana nayo na kusogea Mtaa wa Msimbazi ambako Simba ilikosa ubingwa kwa misimu mitano mfululizo na wakati mwingine kukaa nje kabisa ya michuano ya kimataifa.

TSHA 01

Simba ilikuwa na nia ya dhati ya kurejesha ubabe wake na mara moja dhamira hiyo ikatimia na wababe hao wa Kariakoo wakaanza kutawala soka la ndani na baadaye kuendeleza utamaduni wake wa kung’aa kimataifa.

Kwa kawaida kundi la wachezaji kama hawa walioiwezesha timu kusimika chapa yake kimataifa, hupewa heshima kubwa na wale waliokuwa mstari wa mbele hupewa hadhi ya ugwiji au ulejendari. Yaani wachezaji wa mfano kwa klabu hiyo na ambao majina yao ni taswira kwa klabu.

Wengine hupewa majukumu ya uwakilishi katika baadhi ya mambo na wengine hutumiwa kudumisha utamaduni wa klabu na ndio maana unaona wachezaji kama Luis Figo, hutumia timu ya wachezaji wastaafu wa Real Madrid katika hafla maalum, au Andy Cole aliletwa na Airtel wakati wa mashindano ya Airtel Rising Star kutangaza sera na utamaduni wa Manchester United.

Wapo ambao hujiendeleza kwa fani nyingine na kurudi kuitumikia klabu katika majukumu mengine kama ilivyokuwa kwa akina Franz Backenbeur walivyorejea Bayern Munich katika majukumu ya uongozi.

Wachezaji wa aina hii huwa na matunzo maalum wanapoelekea kustaafu au kuchoka na kwa kuiheshimu klabu huamua kutoenda klabu pinzani na badala yake kuchagua kwenda kumalizia soka lake sehemu nyingine, kama ilivyo kwa gwiji wa Real Madrid, Luca Modric ambaye ameamua kuhamia AC Milan baada ya kuishi Madrid kwa muda mrefu.

TSHA 02

Huyu atakaribishwa wakati wowote jijini Madrid akirejea kwa shughuli yoyote. Hata kama AC  Milan itajikuta imepangwa na Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa miaka ijayo, mashabiki watasimama kumpigia makofi wakati atakapokuwa anaingia Uwanja wa Santiago Bernabeu kuonyesha heshima kwa mchango wake kwa klabu.

Hadhi ya ugwiji haitokani pekee na mchezaji kuiwezesha klabu kutwaa mataji, bali pia kuichezea klabu kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Bocco, Manula, Mkude na sasa Tchabalala huku hatima ya Mzamiru bado haijawekwa bayana.

Manula ameripotiwa kurejea Azam, wakati Bocco alienda kumalizia soka lake JKT Tanzania. Mkude na Tchabalala wamehamia Yanga, ambao ni wapinzani wakubwa wa Simba.

Uamuzi wa wawili hao unamaanisha kuwa wanapoteza hadhi na heshima ya ugwiji wa klabu ya Simba kutokana na uamuzi wao wa kuvukia ng’ambo ya pili, kama ilivyokuwa kwa Figo alipoamua kuondoka Barcelona na kujiunga na Real Madrid au Luis Enrique alipoondoka Real Madrid na kutua Barcelona.

Yapo maneno mengi yakiwemo ya msemaji wa klabu ya Simba, Ahmed Ali, uongozi umeachana na Tshabalala wakati sahihi, huku wengine wakisema ameondoka wakati kiwango chake kikielekea ukingoni.

TSHA 03

Lakini nanusa kasoro moja katika kushughulika na wachezaji wenye mchango mkubwa klabuni na wanaojitolea miaka yao mingi Mtaa wa Msimbazi.

Isingekuwa rahisi kwa Bocco kukataa kustaafu ghafla na kwenda kufundisha timu ya vijana wakati alikuwa anaamini bado ana nguvu za kutosha kupambana kwenye ligi ya Tanzania, akilinganisha kiwango cha juu cha Simba na klabu nyingine, ukiachana na Yanga na Azam.

Ni lazima uamuzi huo wa kutaka kumstaafisha ghafla hakuufurahia na pengine haukufanywa baada ya mazungumzo ya kina na mchezaji kujua ambalo angependelea kulifanya katika kipindi ambacho klabu iliona hakuwepo kwenye mipango yake ya baadaye.

Hali ilikuwa hivyo kwa Mkude, ambaye kibaya zaidi aliamua kuvuka mstari na kwenda makutano ya Mtaa wa Jangwani na Twiga. Ingawa alionekana alikuwa mwishoni mwa uchezaji wake, bado alikuwa anastahili heshima na staha ya mchezaji aliyefanya kila kitu kuhakikisha Simba inapata kile ilichotaka.

TSHA 04

Ingawa katikati ya safari kulikuwa na matatizo ya kinidhamu yaliyosababisha aonekana ana tatizo la afya ya akili (kama kweli kulikuwa na uchunguzi wa kisayansi), bado alistahili heshima ya kipekee katika kuzungumzia hatua ambayo ingefuata baada ya Simba kumwona hahitajiki tena.

Kwa muda mrefu kiungo Muzamiru amekuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha, lakini kumeibuka tetesi kwamba huenda akaachwa katika usajili ujao.

Kumuacha Mzamiru si dhambi wala si kosa la jinai, bali jinsi ya kuachana ndio kitu muhimu na ambacho kinaweza kujenga picha mbaya hadi wachezaji wengine waone hawataweza kupata heshima kubwa hata wakijitolea vipi kuitumikia klabu.

Na sasa limeibuka sakata la Tshabalala, nahodha wa Simba aliyerithi mikoba ya Bocco. Ni kama ni rasmi beki huyo wa kushoto ameshajiunga na Yanga, kitu cha nadra sana kwa nahodha wa moja ya timu pinzani za Kariakoo kutoka moja na timu hizo na kujiunga na nyingine.

Kama alishawishiwa kuondoka, ni lazima uongozi wa Yanga uliona tatizo katika kushughulika na masuala ya mchezaji wa umri wake na ndio wakalitumia kumshawishi ajiunge kwao wakimhakikishia kuwa hatakutana nalo upande wa pili.

Na kama mwenyewe aliamua kuondoka, basi kuna udhaifu katika kushughulika na wachezaji wanaostahili kupewa heshima ya ugwiji kwenye klabu hiyo.

TSHA 05

Ni lazima uongozi utambue, kumuacha mchezaji nyota aliyeitumikia klabu kwa muda mrefu si dhambi na wala si kosa la jinai, bali cha msingi ni jinsi ya kuongea naye ili aondoke akiacha chapa ya klabu ikiwa imara na akiwa balozi mzuri wa klabu kwa wachezaji wengine.

Ni lazima Simba ijichunguze katika masuala ya wachezaji hao wachache waliosimama kidete kwa takriban miaka minane kuhakikisha Simba inatamba katika soka la Tanzania na Afrika. Hawa ndiyo mabalozi wa klabu na ndiyo watakuwa marejeo kwa wachezaji wengine wanaotaka kujiunga na Simba au wanaotaka kusaini mikataba mipya ya kuongeza muda wa kuitumikia klabu.

Yaani wengi watawaangalia na kufuatilia habari zao kabla ya kuchukua uamuzi wa kusaini mkataba au kuongeza muda.

Na pale itakapowezekana watawatafuta kwa njia yoyote kuulizia ushauri wao kabla ya kuchukua hatua yoyote.

Klabu hazina budi kuheshimu magwiji wao hata pale zinapokuwa hazina uwezo wa kiuchumi wa kuwagharimia ili waendelee kuchezea klabu zao.

Hili hutengeneza chapa nzuri ya klabu ndani nan je ya nchi.