TFF, Azam TV zinapowadhulumu mashabiki
Muktasari:
Ikumbukwe kuwa Azam TV ndiyo waliopewa haki pekee ya kurusha mechi hizo kwa miaka mitatu.
WIKI iliyopita, Edo Kumwembe, alitembelea Azam TV na kutuhabarisha maandalizi ya runinga hiyo kurusha ‘laivu’ mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Ikumbukwe kuwa Azam TV ndiyo waliopewa haki pekee ya kurusha mechi hizo kwa miaka mitatu.
Wakati wa kuingia mkataba wa kuonyesha mechi hizo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Azam TV walipaswa kuhakikisha kuwa wadau wote wanatendewa haki ili upande mmoja usibaki ukilalamika.
Wadau ninaowazungumzia hapa ni klabu shiriki, Azam TV wenyewe, TFF pamoja na mashabiki.
Ukiondoa Yanga ambao ni kama bado wameisusa Azam TV, klabu 13 za Ligi Kuu zimeipokea runinga hii kwa mikono miwili na wameshalamba fungu kiasi.
Hali kadhalika kwa Azam TV ambao ndiyo waliotoa ofa ya kutaka kuonyesha michuano hii kwa dau walilotangaza nao pia wamekubali kuwa wametendewa haki.
TFF kwa upande wao, na hapa naunganisha na Bodi ya Ligi Kuu, ndiyo walioufanyia kazi mkataba wa udhamini na hivyo wameridhika na kiwango kilichotolewa.
Hapa anabaki mdau mmoja muhimu sana, naye ni shabiki ama mpenzi wa soka.
Baada ya yote kufanyika, wapenzi wa soka walikaa wakisubiri jambo moja tu; kuona mechi za Ligi Kuu zikionyeshwa laivu runingani Azam TV! Hilo likifanyika ndipo haki ya mtazamaji ama mpenzi wa soka inakuwa imetimizwa.
Hadi sasa, hakuna shabiki aliyeshuhudia ‘laivu’ mechi yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Hii ni kwa sababu Azam TV haiko hewani hadi sasa na haijulikani lini itaanza matangazo, huku Ligi Kuu ikiingia raundi ya tatu wikiendi hii.
Wakati ligi inaanza, uongozi wa TFF ulieleza kuwa mechi zitaanza kuonekana ‘laivu’ kuanzia raundi ya nne ya mzunguko huu wa kwanza. Hii ina maana kuwa mechi za wiki ijayo (kwa mujibu wa TFF) zitakuwa laivu.
Lakini kwa uzoefu wangu katika runinga, nina uhakika wa asilimia 99 kuwa mechi za raundi ya nne hazitakuwa laivu Azam TV hata kama malaika atashuka kutoka mbinguni, labda kwenye runinga nyingine!
Na hapo ndipo mtazamaji ama mpenzi wa soka anapokuwa hatendewi haki katika suala hili la haki za kuonyesha mechi za Ligi Kuu msimu huu. Wapenzi wa Simba, Azam FC, Rhino Rangers na Mbeya City walioko mikoani, tunaweza kusema hadi sasa wameachwa solemba.
Sasa kuna ubishi kuwa lipi goli bora (hadi sasa) kati ya lile alilofunga Haruna Chanongo wa Simba katika mechi dhidi ya JKT Oljoro ama lile la Chrispine Odulla wa Coastal Union alilofunga pia katika mechi dhidi ya JKT Oljoro.
Ni Azam TV peke yake ndiyo ingetuonyesha na kukata mzizi wa fitina lakini nina hakika wao na TFF pia hawana si tu kumbukumbu za magoli hayo bali pia picha za mechi hizo mbili.
Nilishauri wiki kadhaa zilizopita katika safu hii na nirudie kushauri tena. Azam TV ni wageni sana katika ulimwengu huu wa mawasiliano na wanahitaji muda kujiandaa.
Isingekuwa dhambi kama TFF wangeipatia Azam msaidizi kwa maana ya TV yenye uzoefu na iliyo hewani sasa hata kwa kupewa mechi chache ili wapenzi wa soka wasidhulumiwe haki yao kama ilivyo sasa ambapo hakika hawatendewi haki.
TFF haijachelewa bado na iwape haki yao mashabiki wa soka wenye kiu ya kuziona ‘laivu’ timu zao runingani.