SPOTI DOKTA: Sababu kifo cha Dokta wa Barcelona ni hizi

Muktasari:
- Kifo chake kilibainika mchana saa chache kabla ya timu hiyo kwenda uwanjani Estadi Olimpic Lluis Companys ambako Barcelona walikuwa wacheze dhidi ya Osasuna katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga)
KLABU ya Barcelona ya Hispania, wikiendi iliyopita ilipata pigo baada ya kutokea kifo cha ghafla cha daktari wa kikosi cha kwanza ajulikanaye kama Dk. Carles Garcia Minarro mwenye umri wa miaka 50.
Kifo chake kilibainika mchana saa chache kabla ya timu hiyo kwenda uwanjani Estadi Olimpic Lluis Companys ambako Barcelona walikuwa wacheze dhidi ya Osasuna katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), miamba hao wa Catalunya wakiwa wenyeji kwenye uwanja huo wanaoutumia kwa kipindi cha mpito wakati uwanja wao nyumbani wa Santiago Bernabeu ukiwa katika ukarabati mkubwa.
Kifo hicho kilitokea katika chumba alicholala katika hoteli ya Melina Gran Mel ambayo klabu hiyo walifikia na ipo jirani na uwanja huo. Alifariki akiwa amejipumzisha mara baada ya kumaliza majukumu yake ya maandalizi ya mchezo huo.
Tukio hilo la kusikitisha la kumpoteza mkongwe huyo wa tiba za majeraha ya michezo ndio kulisababisha kuahirishwa kwa mchezo huo.
Gazeti maarufu la michezo la Hispania lijulikanalo kama Marca katika toleo lake la Machi 8, 2025 lilieleza sababu ya kifo hicho cha ghafla ni shambulizi la moyo la ghafla. Kitabibu hujulikana kama sudden heart attack. Hili ni tatizo linalosababishwa na kuharibika kwa mishipa ya damu ya ateri inayopeleka damu katika misuli ya moyo.

Kupitia tukio hili leo jicho la kitabibu litatoa ufahamu sababu zinazochangia aina hiyo ya kifo cha ghafla.
TATIZO LA MOYO NA KIFO CHA GHAFLA USINGIZINI
Shambulizi la ghafla la moyo ni wakati moyo unapoacha kupiga ghafla na bila kutarajia hatimaye damu haiwezi kuzunguka vizuri mwilini na kuathiri mtiririko wa damu kwenye ubongo na viungo vingine.
Moyo ndiyo ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na ndiyo yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani.
Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.
Kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayosababisha matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.
Mishipa ya damu ya moyo ya Ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.
Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.
Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo ya kupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.
Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valve za moyo na pia kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.
Vile vile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.
Walio katika hatari ni wenye shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha lehemu, unene, kisukari, uvutaji tumbaku na kutofanya mazoezi, umri mkubwa 45+ na historia ya familia ya tatizo hili.

KUOKOA MWENYE TATIZO HILO
Shambulizi la ghafla la moyo ni tatizo la kiafya ambalo linahitaji huduma za dharura haraka hii ni kwasababu tatizo hili ni tishio na linaweza kusababisha kifo cha mapema.
Kitabibu hujulikana kama Cardiopulmonale resuscitation yaani CPR utomasaji wa kifua. Huduma hii itolewe ikiwa tu shambulizi la moyo limesababisha moyo kusimama.
Endapo mtu aliye na tatizo la kusimama kwa moyo atapokea CPR, inaweza kusaidia kuweka sawa damu yake kuzunguka hadi huduma za dharura au msaada wa kumpeleka kituo cha jirani kufika.
Anzisha huduma ya CPR ikiwa mgonjwa hana mapigo ya moyo au hapumui. Ikiwa huna mafunzo ya CPR, fanya CPR ya kutumia mikono pekee.
Sukuma kwa nguvu na haraka kwenye kifua cha mtu huyo. Fanya hivi mara 100 hadi 120 kwa dakika. Iwapo umefunzwa katika CPR na unajiamini katika uwezo wako, anza kwa kukandamiza kifua mara 30 kabla ya kutoa pumzi mbili za kuokoa.
Huduma ya kwanza ambayo mtu aliyejirani na aliyepata shambulizi na baadaye moyo kusimama anachotakiwa kufanya ni ifuatavyo;

1. Tambua dalili, mara nyingi viashiria vya shambulizi ni mgonjwa kuanza kushika kifuani na kuanguka ghafla, ukiona hivyo omba msaada kwa wengine, au wapige simu ya dharula kuomba huduma za dharula, na huku pia mkimweka mgonjwa mahala salama na kwenye hewa. Jaribu kumwita, ili kuona mwitiko wake.
2. Mkague kama ana dawa zozote ila usimpe kama wewe si mtoa huduma za afya.
3. Chunguza haraka viashiria nyeti vya uhai ikiwamo upumuaji, njia ya hewa na unepaji wa mishipa ya damu kama moyo unadunda.
4. Kama hali ikiendelea kuwa mbaya na kupoteza fahamu au kama mapigo ya moyo hayapo na hapumui, fungua njia ya hewa, tizama kama anapumua vema na uanze kufanya CPR ili kuokoa maisha yake.
5. Huduma ya CPR ni moja ya huduma ya kwanza muhimu kwa mtu aliyepata shambulizi la moyo hatimaye kusimama. FANYA CPR endapo una ujuzi huku omba wengine waite huduma ya dharula;
CPR INAFANYIKA HIVI
A. Mtu mzima akizimia ghafla na akiwa hapumui haraka angalia na sikiliza kifua chake kuona kifua hakichezi au hatoi sauti ya haki. Endapo ana dalili hizi mwambie mtu mwingine apige namba ya dharula kwa ajili ya ambulance kuja wakati wewe unafanya CPR.
B. Weka kisigino cha mkono wako kwenye kifua cha mtu unayemfanyia CPR kati ya chuchu moja na nyingine (katikati ya kifua)
C. Weka mkono mwingine juu ya mkono wako wa kwanza na uingilianishe vidole vyako
D. Kwa kutumia uzito wako wa mwili (si mikono yako), kandamiza kifua kwenda chini kwa umbali wa umbali 5 hadi 6.
E. Baada ya kukandamiza, mikono ikiwa kwenye kifua ruhusu kifua kijirudie kwenye hali yake ya kawaida.
F. Rudia kugandamiza kwa kiwango cha mara 100 hadi 120 kwa dakika moja hadi msaada wa mtaalamu wa afya ufike au umechoka.
G. Kwa namna nyingine kandamiza hadi mara mbili kwa sekunde moja.

Huduma hiyo inaweza kufanyika kwa kupokezana ikiwa mfanyaji wa kwanza atakua amechoka.