SPOTI DOKTA: Mvunjiko wa pua wa Mbappe uko hivi

Muktasari:

  • Yalikuwa ni matoke mabaya kwa timu hiyo ambayo ndio walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu, lakini baadaye kibao kiligeuka wakajikuta wakichapwa mabao 2-1.

KATIKA mchezo wa nusu fainali ya Euro 2024, juzi Jumanne nchini Ujerumani, miamba ya soka barani Ulaya Ufaransa ilitupwa nje ya mashindano ikiwa na staa wake mwenye mvunjiko wa pua, Kylian Mbappe.

Yalikuwa ni matoke mabaya kwa timu hiyo ambayo ndio walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu, lakini baadaye kibao kiligeuka wakajikuta wakichapwa mabao 2-1.

Siku moja kabla ya mechi ya nusu fainali ilielezwa kuwa afya ya mchezaji huyo ilitia shaka kutokana na jeraha hilo ambalo alilipata katika mchezo dhidi ya Australia katika ngazi ya makundi.

Itakumbukwa kuwa mshambuliaji huyo ambaye pia ni nahodha alitolewa nje kabla ya dakika 15 za mwisho kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Ureno kutokana na kutoneswa kwa jeraha hilo.

Alitoneshwa jeraha hilo wakati aliporuka kuwania mpira wa juu na mchezaji wa Ureno, Bernardo Silva ambaye alipopiga mpira wa kichwa ukatua usoni na kulitonesa jeraha hilo.

Alipatiwa matibabu haraka pale uwanjani, lakini hali yake haikuwa sawa, hivyo ilimlazimisha kocha wa timu hiyo, Didier Deschamps kumtoa haraka na nafasi yake kuchukuliwa na Bradley Barcola.

Mchezaji huyo amekuwa akicheza mashindano hayo tangu mwanzo akiwa na mvunjiko wa mfupa wa pua, jeraha ambalo alilipata katika mchezo kwa kugongana na beki Kevin Danso wa Autralia.

Tangu kipindi hicho amekuwa akivaa kifaa maalumu cha kukinga jeraha ambalo halikuwa tishio kwake kucheza. Lakini ikawa bahati mbaya katika mchezo wa robo hakuweza kuendelea.

Katika mchezo wa nusu fainali hapo juzi, mshambuliaji huyo ilielezwa awali kuwa asingejumuishwa katika mchezo huo kutokana na sintomfahamu ya jeraha.

Pamoja na kupata jeraha hilo, lakini bado haikuonekana kama linaweza kumzuia kucheza kwani halikuwa tishio kiafya.

Mojawapo wa madaktari bingwa wa upasuaji wa urembeshaji wa maumbile ya mwili, Mark Mikhail nchini Uingereza aliliambia gazeti la Mailonline wiki iliyopita kuwa Mbappe baadaye atahitaji kufanyiwa upasuaji wa pua.

Alisema kuwa jeraha hilo linaweza kumfanya kuwa na mwonekano mbaya kama hatafanyiwa upasuaji wa urembeshaji. Ingawa aliweka wazi upasuaji huo siyo wa dharura, bali ni wa kupanga hapo baadaye.

Alisema kuwa kwa sasa kikubwa ni kuwa anaweza kupumua bila kikwazo chochote ndio maana aliruhusiwa kucheza akiwa na kikinga jeraha cha uso maarufu kama kinywago cha usoni.

Lakini taarifa ya madaktari inasema kuwa staa huyo mwenye miaka 25 ambaye sasa ni mchezaji wa Real Madrid atahitajika kufanyiwa upasuaji ili tu kudumisha mwonekano wake.

Ingawa timu ya madaktari wa timu walisema kuwa jeraha hilo siyo lazima ahitaji upasuaji kwa sasa. Walisema hivyo baada ya kumfanyia vipimo na tathimini ya kina.

Ndio maana bado waliridhia acheze katika mchezo wa robo fainali na hatimaye nusu fainali bila hata kikinga jeraha cha uso kwa kucheza dakika zote 90.

Katika mchezo huo staa huyo hakuweza kuonyesha makali kama ilivyozoeleka na bahati mbaya timu yake ilitolewa katika mashindano hayo ikiwa na mastaa lukuki.


MAJERAHA YA PUA

Majeraha ya pua yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati na makubwa ambapo yanaweza kuhusisha mvunjiko au majeraha ya tishu laini. Kwa Jeraha alilopata Mbappe ni la kati la mvunjiko wa pua.

Mvunjiko wa pua unahusisha kuvunjika kwa mifupa ya juu ya ukingo wa pua. Mara nyingi hutokana na jeraha butu baada ya kugongwa na kitu kizito kama ilivyotokea kwa Mbappe alivyongana na Kelvin wa Australia.

Mojawapo wa huduma alizopata ni palepale uwanjani kurudisha mfupa katika sehemu yake. Ndio maana ilielezwa kuwa inaweza isihitaji upasuaji kama ilivyo kwa mivunjiko mingine inayotokea mwilini.

Na katika mchezo wa robo fainali alipotonesha jeraha hilo alipewa huduma maalumu ili kukabiliana na hali ya maumivu aliyopata.

Pua ni moja ya eneo la usoni ambapo huwa na mifupa migumu na mifupa laini iliyo kama plastiki inayojulikana kitaalamu kama cartilage. Mifupa hiyo huwa laini ukilinganisha na ya kawaida.

Hatari ya jeraha la pua linaweza kuwa hatari endapo kutakuwa na mvunjiko mkubwa na kuvuja damu nyingi ambayo inaweza kuziba njia ya hewa. Hii inapotokea ni jambo la dharura linalohitaji huduma ya haraka.

Katika Kombe la Dunia 2014 mchezaji wa timu ya taifa ya Marekani, Clint Dempsey alipata mvunjiko wa pua.  Alishauriwa kuvaa kifaa maalumu cha kukinga pua katika mechi zinazofuata.

Hata hivyo, alikataa ushauri huo, hivyo mwenyewe alijiweka katika hatari ya kupata majeraha zaidi. Siku ya mchezo aliyopata jeraha aliamua kuendelea kucheza, lakini baadaye alieleza kuwa alipata shida ya kupumua na kizunguzungu.

Hapo alihatarisha afya yake kwani jeraha lilikuwa kubwa na njia ya hewa ilivimba na alivuja damu. Lakini wataalamu wa afya walimtibu na kuwa na afya njema.

Kwa Mbappe imekuwa bahati hakupata mvunjiko ambao ungeweza kumfanya azuiwe kucheza mchezo wa robo na nusu fainali, lakini hakuweza kuwa katika ubora wake.


Chukua hii

Mchezaji anapokuwa ni staa, huku akitegemewa na timu ni jambo la kawaida kwa timu kupambana kila njia ili kuhakikisha anapona na kucheza au hata kama hajapona.

Inawezekana pamoja na jeraha alilopata Mbappe akawa alipewa dawa za maumivu ili kumfanya asihisi maumivu yoyote na kuweza kucheza akiwa na jeraha.