SPOTI DOKTA: Majeraha ya maungio yako hivi

Muktasari:
- Ulikuwa ni mchezo wa funga nikufunge, mabao saba yalishuhudiwa katika mechi hiyo ambayo Inter Milan ilitinga fainali mara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.
USIKU wa Jumanne katika nusu fainal ya pili Ligi ya Mabingwa Ulaya Ulaya ilishuhudiwa mechi kali kati ya Inter Milan na Barcelona iliyochezwa kwenye Uwanja wa San Siro, Italia.
Ulikuwa ni mchezo wa funga nikufunge, mabao saba yalishuhudiwa katika mechi hiyo ambayo Inter Milan ilitinga fainali mara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.
Katika jicho la kitabibu mchezaji ambaye ni hana utimamu, legelege mvivu wa mazoezi ni vigumu kuweza kucheza mchezo ule na kudumu kwa muda mrefu awanjani akiwa na kasi ile ile.
Huwa ni vigumu katika mechi kama ile pamoja na ya jana ya PSG na Arsenal kukosa wachezaji wenye majeraha ya wastani katika maungio. Hii kwa sababu maeneo hayo ya mwili ndio msingi wa mwili kujongea.
Wapo wachezaji katika mechi hiyo walikuwa hoi wakichechemea kutokana na mchezo huo kuwa na kasi muda wote uliochezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kutotoa mshindi.
Majeraha maungio huwa ni kawaida kuwapata wanasoka wakiwa katika mechi kali, hii ni kutokana na kila timu kuhitaji kushinda ili kutinga fainali.
MAUNGIO, TENDONI NA LIGAMENTI
Ungio kwa kitabibu hujulikana kama joint ambayo huundwa na misuli, mifupa, miishilio ya misuli ambayo ni kama vile mkia inayojulikana kama Tendoni na nyuzi ngumu ambazo hujulikana kama ligaments.
Ligamenti na Tendoni zimeundwa na tishu plastiki zenye uwezo wa kunepa au kuvutika kama mkanda wa malighafi yenye asili ya mpira.
Ni maeneo ambayo ndiyo yamebeba mijongeo mbalimbali kama vile kunyooka, kujikunja, kueleka pembeni au kati, au kuelekea juu au chini, kujizungusha katika mhimili wake. Kuna takribani maungio 350 katika mwili wa binadamu, lakini kwa mwanasoka ungio la paja na kiuno, goti, kifundo cha mguu, kiwiko, bega na kiganja ndio yanayojulikana zaidi.
Wachezaji wa soka wote wanacheza mchezo huo wakitumia viungo vya mwili ambavyo ni misuli, mifupa na nyuzi za ligamenti na tendoni ambavyo vinaunda maungio mbalimbali ya mwili.
Mijongeo hii inayofanyika ndio inamwezesha mchezaji kuweza kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kwa kucheza soka kunyumbulika, kupiga chenga na kupiga mashuti.
Wakati kwa mabeki na mawinga wa pembeni ndio wakimbiaji sana uwanjani, maungio ndio humwezesha kukimbia kasi kwa wale wa mbio fupi au wale wa mbio ndefu kukimbia kidogo kidogo kwa muda mrefu.
Lakini yote haya yanapofanyika huwa hapakosekani majeraha ambayo yanaweza kumweka nje ya uwanja mchezaji na hatimaye kushindwa kutimiza majukumu yake.
KINACHOJERUHI MAUNGIO
Ungio linaundwa na misuli, mifupa, ligamenti na tendoni na huku pia kuwepo na uteute ambao ndio kama vile kilainishi na vijiplastiki katika maungio ili kuzuia mifupa kusagika wakati wa kujongea.
Kujeruhiwa kwa maungio ni kutokana na kujeruhiwa moja kwa moja au kujijeruhi au ni matokeo ya kiungo kutumika sana mara kwa mara ikiwamo kwa kuvutika sana au kulika kutokana na kutumika sana.
Mfano mzuri ni wanasoka ambao hupata mara kwa mara majeraha ya kuchanika nyuzi za misuli ya paja, goti na kifundo cha mguu kwasababu maeneo haya ndio yanatumika sana wakati wa kucheza soka.
Vitu ambavyo mara kwa ndivyo vinajeruhiwa huwa ni majeraha ya tishu laini za katika ungio.
Moja ni vijeraha vya misuli au vimichubuko kitabibu hujulikana kama strain. Aina ya jeraha hili la ungio huwa na dalili kama maumivu, kuvimba, kukakamaa kwa misuli na kushindwa kujongesha ungio hilo.
Mbili ni vijeraha vya nyuzi ngumu za ligamenti au tendoni kutokana na kuvutika kupita kiwango cha uvutikaji. Aina hii ya majeraha ya ungio hujulikana kama Sprain.
Huambatana na dalili kama vile maumivu, kuvimba, vimchubuko na kushindwa kufanya matendo kadhaa ya kimjongeo ya ungio na inawezekana pia kuwepo kwa mlio wakati wa jeraha lilipotokea. Mlio huo kitabibu hujulikana kama popping sound.
Aina ya tatu ya jeraha la ungio hujulikana kama mvunjiko, kitabibu Fracture. Inaweza kutokea kwa mifupa migumu na ile mifupa plastiki yenye kazi ya kunyonya mawimbi ya shinikizo la uzito.
Dalili zake ni kuvimba, kushindwa kufanya kazi, maumivu makali ambayo huwa makali sana mara baada ya kutaka kutembea au kujongesha ungio au pale unapominya.
Kwa lile jeraha la mvunjiko wa wazi mfupa huweza kuonekana ukiwa umetoka nje huku pia kuweza kuambatana na mchaniko wenye kuvujisha damu.
Aina ya nne ya jeraha la ungio ni kuteguka, kitabibu hujulikana kama dislocation au subluxation. Dalili ni pamoja na kuona kuhama kwa mfupa na umbile lisilo la kawaida katika ungio, maumivu, kuvimba na kupishana kwa mifupa ya ungio na kushindwa kujongea kabisa.
HUDUMA RAHISI MATIBABU
Huduma ya haraka ya awali ni pamoja na mchezaji kupumzishwa au kutolewa, jeraha kulindwa kwa vifaa tiba vya huduma ya kwanza ili lisijijeruhi zaidi, uwekaji wa barafu eneo lililojeruhiwa.
Vile vile kufungwa bandeji mvutiko ili kubana kiasi na kama ni mguu hunyanyuliwa kidogo kuzidi kifua na kama ni mkono basi hunyanyulia kidogo na kuegeshwa katika mto au tandiko lililokunjwa.
Majeraha ya maungio yanaweza kuepukwa endapo mwanamichezo atafanya mazoezi ya viungo na kupasha mwili moto angalau kwa dk5-10 kabla ya kuanza mechi.