SPOTI DOKTA: Madhara kucheza kandanda na maumivu iko hivi

Muktasari:
- Mchezaji huyo anapokuwa ndio tegemeo katika mafanikio ya timu husika hudiriki kushawishiwa au kutaka mwenyewe kucheza na maumivu yake ikiwa bado kupona vizuri.
KATIKA mapito ya mwanasoka kuna nyakati za furaha na nyakati ngumu. Moja ya nyakati ngumu ni pale mchezaji anapopata majeraha yanayoambatana maumivu na huku anahitajika na timu.
Mchezaji huyo anapokuwa ndio tegemeo katika mafanikio ya timu husika hudiriki kushawishiwa au kutaka mwenyewe kucheza na maumivu yake ikiwa bado kupona vizuri.
Kwa kawaida kuna maumivu ya wastani, ya kati na yale makali. Uwepo wa maumivu yatokanayo na michezo huwa ni ishara kuwa jeraha halijapona na kinga ya mwili inawajibika kukarabati jeraha.
Wachezaji kandanda hukabiliwa na majeraha kutokana na mambo kadhaa ikiwamo mchezo huo kuhusisha shughuli nyingi za kimwili kama vile kukimbia kwa kasi, kusimama ghafla na mabadiliko ya mwelekeo.

Matendo haya yote ndio ambayo huweka mkazo kwenye misuli, mifupa, maungio na mishipa. Hali hii ndio inamfanya mchezaji kandanda kuwa na maumivu katika mwili wake.
Kwa kawaida mara kwa mara majeraha mengi ya soka hutokea kwenye goti, kifundo na misuli ya paja na kigimbi cha mguu.
Wachezaji wengi hutegemea dawa za maumivu ambazo nyingine zinauzwa katika maduka ya dawa kudhibiti maumivu ili kuweza kucheza mechi muhimu kwa kulazimisha au kulazimishwa.
Kwa kawaida njia rahisi inayokubalika kukabiliana na maumivu kwanza ni kupumzika kucheza, kutumia dawa za maumivu na uvimbe na pia kufanya mazoezi lainishi na ya kuimarisha misuli.
Vile vile maumivu ya awali ya miguu huweza kukabiliwa kwa mchezaji kutumia barafu, kufunga bandeji ya kunepa na kuunyanyua mguu kuzidi kifua.
MAUMIVU NI ISHARA MUHIMU
Maumivu ya papo hapo hutuonya juu ya madhara ya baadaye na pia hutuzuia kuharibu miili yetu. Ndio maana mchezaji anapokwatuliwa huweza kukaa dakika kadhaa hatimaye hustahimili na kuendelea kucheza.

Hiyo maana yake taarifa hiyo imetafsiriwa na ubongo kuwa jeraha hilo si kubwa mwili unaweza kustahimili kuendelea.
Lakini pia ni kawaida unaweza kuendelea kucheza na maumivu kuzidi kuwa makali kiasi kushindwa kuendelea. Hiyo maana yake aidha jeraha liliongezeka hivyo kuleta maumivu zaidi.
Tunapata maumivu kama yasiyopendeza ambayo kwa ujumla inatuashiria tuondoke kwenye hali ya hatari ikiwamo kutofanya matendo yanayoongeza ukubwa wa jeraha.
Maumivu makali mara nyingi hupotea haraka tunapokuwa salama, lakini katika utulivu hapo baadaye huweza kujirudia na kuwa makali yasiyovumilika hivyo kumlazimu mwanasoka kutoendelea kucheza.
WALIOCHEZA NA MAUMIVU WALIKIONA
Moja ya makala ya gazeti la Januari 03, 2021 la michezo la Uholanzi liliongelea wanasoka wakubwa wa nchi hiyo ambao walicheza wakiwa na maumivu kwa kulazimishwa.
Mwandishi Richmond aliweka wazi katika taarifa yake hiyo akionyesha kukosekana kwa utu kwa mwanasoka mwenye maumivu.
Marco Van Basten alikuwa akicheza akiwa na maumivu na ambayo ilimletea madhara baadaye, taarifa hiyo ilinukuliwa katika kitabu chake na mahojiano katika The Observer na Donald McRae.
Anaeleza kuwa kuna alikuwa ameumia kifundo cha mguu na akawa na maumivu makali ambayo yalikuwa yanampa wakati mgumu hata kutembea tu kwenda chooni ambako ilikuwa ikimlazimu kushika ukuta na vizingiti ili tu asiukanyagie mguu ulioumia ambao ukigusa chini alikuwa anapata maumivu makali yaliyomlazima kufumba mdomo kuzuia miguno.
Anasema alikutana na hali hiyo mara baada ya kulazimika kutumia dawa ya maumivu alizoshauriwa na daktari wa timu ili kukabiliana na maumivu ya jeraha alilokuwa nalo hatimaye aweze kucheza mechi muhimu za Ulaya.
Van Basten alisema; “Ilikuwa ngumu sana kwa sababu nilitoka kiwango cha juu zaidi katika soka hadi kiwango cha chini kabisa cha kutokuwa na furaha binafsi.
“Baada ya matatizo mengi ya upasuaji nilikuwa nikichechemea. Sikuweza kufanya chochote bila maumivu. Nilikuwa mlemavu na madaktari hawakuweza kunisaidia. Ilikuwa anguko kubwa sana na wakati wa giza hasa.

“Hali ilibadilika kutoka mbaya hadi kuwa mbaya zaidi. Baada ya kufanyiwa upasuaji mara kadhaa, na kuonana na madaktari sehemu mbalimbali duniani, nilikuwa nimejaribu kila kitu, lakini hatukuweza kupata suluhisho.”
Alielezea hayo Van Basten ambaye mwaka 1993 alicheza mechi yake ya mwisho na kuamua kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 28 kutokana na majeraha ya kujirudia ya kifundo cha mguu.
Nguli mwingine kutoka nchini Uholanzi ambaye aliwahi kuwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1971, 1973 na 1974, Johan Cruyff katika kitabu chake ameeleza kuwa mara kadhaa amewahi kuchezeshwa akiwa na maumivu ili tu kuisaidia timu.
Anasema kuwa alijeruhiwa kwa mara ya kwanza Desemba 1986 na hakupata nafuu kwa njia zote.
Alikuwa na majadiliano na daktari ambaye alisema, ana tatizo lakini haitakuwa mbaya na anaweza kucheza hivyo hivyo. Johan anasema hii ilikuwa mbaya kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Daktari alimwambia kuwa wanafanya makubaliano kuwa hatacheza mashindano yote na baadhi ya mafunzo anaweza kuruka.
“Lakini lazima ucheze Ulaya. Haidhuru kitakachotokea, lazima ucheze fainali. Hilo ndilo jambo tulilofanya.”
Wachezaji hawa waliweka wazi kuwa walipata madhara makubwa kucheza kandanda na maumivu kwani majeraha hayo yaliongezeka ukubwa na kuwapa maumivu zaidi na huku yakawa shida kutibika.
MUHIMU KUMJALI MCHEZAJI KWA HIVI
Hapa kuna baadhi ya njia za kuchukua, ambazo zinahusiana uzingatiaji wa haki za mgonjwa na maadili kwa daktari.
Maumivu na jeraha vinahusiana moja kwa moja, ambavyo ina maana kwamba tunahitaji kuchunguza na kutathmini mtu na si mchezaji.
Pat Wall, mmoja wa baba wa sayansi ya kisasa ya maumivu, alikuwa akizungumza na kuandika kuhusu hili katika miaka ya 70. Wall alisema; ‘Maumivu yanaainishwa vyema kuwa ni ufahamu wa hali ya uhitaji kuliko hisia.’
Nguli huyu anashauri kutopuuza maumivu na kushauri kuchukua hatua muhimu za awali za kuondoa maumivu yaliyojitokeza papo kwa hapo.

Anasema kuwa wanasoka ni watu wanaocheza mpira, sio tu ni hilo pekee bali kuna zaidi ya hayo kwao. Anashauri wanasoka wasikilizwe wanaposhitakia maumivu yao, na sio kufikiria timu pekee.
Muhimu kuwapa nafasi na muda wa kuzungumzia jinsi inavyowafanya wahisi na kuelezea hali ya maumivu yao ya mwili.
Muhimu kuhimiza uwezeshaji wa matibabu tangu mwanzo ili mtu ahisi udhibiti bora wa maumivu aliyonayo. Hii inampa hamasa mchezaji.
Kuunda hali za kupona na kupata hali bora katika mawazo, hisia, uhusiano, mazingira, hali ya uhuru na kujistahi.
Kufanya mchezo kuwa bora kwa kufikiria juu ya wachezaji na kile wanachochangia kwa jamii kupitia miguu yao, na zaidi haswa mioyo yao. Mfano ni kile anachofanya Marcus Rashford kutoa chakula kwa wanafunzi bila malipo.
Ni muhimu wakati wa maumivu, majeruhi kusikilizwa, kuthaminiwa kama binadamu, kutunzwa, kuongozwa na kutiwa moyo.