Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Kimbia, fanya mazoezi ya viungo

Muktasari:

Zoezi la ukimbiaji litakuwa bora zaidi endapo pia utafanya pamoja mazoezi ya viungo kabla na baada ya ukimbiaji.

WIKI iliyopita tuliukaribisha mwaka 2025 kwa kusisitiza kuwekeza katika zoezi la ukimbiaji ili kujenga mwili wenye afya njema.

Zoezi la ukimbiaji litakuwa bora zaidi endapo pia utafanya pamoja mazoezi ya viungo kabla na baada ya ukimbiaji.

Bila mazoezi ya viungo kungekuwa na idadi kubwa ya majeruhi katika michezo. Vilevile kwa wale wanaofanya kazi ofisini wangeweza kupata hisia pengine ni wagonjwa.

Ingawa siyo lazima uwe ni mfanya mazoezi pekee ili ufanye mazoezi ya viungo, hata wale wanaofanya shughuli zinazoushughulisha mwili kama makuli, wakulima, mafundi ujenzi na wafanyakazi wa ndani nao wanahitaji mazoezi hayo.

Mazoezi haya ndio yanayoufanya mwili ujione ni mpya usio na uchovu wala maumivu ya viungo. Zoezi la ukimbiaji linahusisha viungo vingi vya mwili, hivyo ni kawaida kupata uchovu.

Kabla ya kuingia katika mazoezi hayo na baada ya mazoezi ni kawaida wakufunzi wa mazoezi ya viungo kutumia muda wa angalau dakika tano.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa mazoezi hayo ndio nyenzo kuu ya kuandaa mwili kufanya majukumu ikiwamo mazoezi ya ukimbiaji.

Kabla ya kuianza siku wataalamu wa sayansi ya mazoezi ya mwili wanashauri unapoamka tu kitandani ufanye mazoezi ya viungo angalau hata kwa dakika tatu hadi tano. Hapa tunapata picha kuwa mazoezi ya viungo yana faida kubwa kuandaa mwili kufanya mazoezi ikiwamo kabla na baada ya ukimbiaji. Hii ni kwa sababu yanauponya mwili na uchovu hasa baada ya viungo kufanya kazi sana.

Kunyoosha viungo vya mwili huwa ni kwenye maeneo ya misuli, maungio, ngozi, nyuzi ngumu za tendoni na ligamenti na vifupa plastiki ambavyo ndivyo huwa na kazi ya kuujongesha mwili kutoka pointi moja kwenda nyingine.

Unyooshaji huanzia miguuni na mikononi, kiwiliwili, kichwani na shingoni na huhitajika kufanyika taratibu kwa muda wa dakika tano hadi 10 ili kupata faida zifuatazo:

- Faida kubwa ya kwanza ni kuondokana na uchovu, hivyo kukufanya kupata utulivu wa kimwili na kiakili na hatimaye kuwa na hamasa na ari ya zoezi la ukimbiaji.

- Kurundikana kwa shinikizo katika misuli huifanya ijikunyate, hivyo kuleta hali ya hisia ya kukakamaa na kutohisi wepesi. Hali hii huleta madhara hasi kiakili pamoja na kimwili.

- Unyooshaji viungo vya mwili husaidia kuondoa shinikizo lililopo katika misuli, hatimaye kuuwezesha mwili kuianza siku vizuri kwa ufanisi, hivyo baadaye kukupa hamu ya kufanya zoezi la ukimbiaji.

- Ndiyo maana wanamichezo wote hupasha miili moto kwa mazoezi ya viungo kabla ya kuingia kufanya mazoezi au kucheza mechi lengo likiwa ni kuvifanya viungo kupata wepesi na kuweza kunyumbulika.

- Ikumbukwe pale unapokuwa umetulia muda mrefu kabla ya ukimbiaji unaweza kuhisi uchovu au kuumwa viungo hatimaye kukupa hofu pengine ya unaumwa.

- Kufanya mazoezi hayo ndiyo kunaondoa hali hiyo na hatimaye kukufanya unapoingia katika ukimbiaji kujiona umepona kwani tayari viungo vimenyooka na kuwa na utayari wa kufanya kazi.

- Mazoezi hayo yanaifanya misuli ya mwili isibane na kuipa utulivu hivyo kutoa nafasi kwa damu kutiririka kirahisi.

- Kemikali zijulikanazo kama Endorphins zinaufanya mwili kupata hisia ya furaha huku pia ikikupa usingizi mzuri na baadaye hutiririshwa wakati wa zoezi la viungo.

- Husaidia kuweka ulalo sahihi wa mwili kwa kunyoosha misuli ya mwili iliyokakamaa kwa kuivuta na kuirudisha mahali pake kiasili.

- Kunyoosha misuli kama ya eneo la chini mgongoni, kifuani na mabegani husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio sahihi, hivyo kuepusha uchovu na maumivu.

- Kukupa wepesi wa mwili au unyimbulikaji  hivyo kuufanya mwili kuwa na utayari wa mabadiliko wakati wowote ikiwamo kwenye mijongeo kama kutembea, kuruka au kukimbia.

- Kuongeza uwezo hivyo huifanya misuli na tendoni kuwa myepesi na laini, hatimaye kuondokana na kukakamaa na uchovu.

- Kadri misuli inavyofanya kazi, ndivyo pia huchoma kiasi kikubwa cha sukari. Kunyoosha viungo husaidia kuchelewesha kujijenga kwa uchovu wa mwili kwa kusaidia damu kuingia kwa wingi misulini.

- Kupunguza majeraha yatokanayo na shughuli za siku ikiwamo ukimbiaji. Hii ni kwa sababu huifanya misuli kupokea damu na virutubisho kwa wingi, hatimaye husaidia kupunguza vijidonda vya misuli na huku pia kuponesha haraka vijeraha vya misuli.

- Hukupa hisia nzuri na kujiamini kwani mazoezi hayo yanakupa burudani na hatimaye kuiboresha siku yako katika mazingira ya kazi au masomo.

- Hukujenga kinidhamu kwani kunyoosha viungo kabla ya ukimbiaji mara kwa mara huzoeleka na kuwa sehemu ya maisha yako, hivyo kuzipata faida zote kirahisi.

Habari nzuri kuhusu mazoezi ya viungo yanaboresha misuli ya eneo la kiungo ikiwamo ile ya kitako cha kiungo ambayo ni muhimu katika ufanisi wa tendo la ndoa kwa jinsia zote.

- Zoezi la viungo kabla ya ukimbiaji linapofanywa katika makundi makubwa ya wakimbiaji kama vile kabla na baada ya marathoni huongeza mshikamano hatimaye kukupa hamasa kupenda mazoezi.

Ni muhimu kushikamana na mazoezi hayo yote ili kudumisha afya ya mwili na akili, na hatimaye kulifanya zoezi la ukimbiaji kuwa bora, hivyo kukukinga na kihatarishi cha magonjwa yasiyoambukiza yaani unene.

Usiache kujiongezea maarifa kuhusu mazoezi ukimbiaji na viungo kila mara kwani yanasaidia kupata taatifa mpya zenye faida kubwa kiafya.

Kumbuka pia simu janja yako uliyonunua kwa pesa nyingi ni hazina kubwa ya mafunzo na maarifa mbalimbali ikiwamo aina ya mazoezi ya viungo, kutunza kumbukumbu za muda na umbali.

Vilevile simu janja hukupa burudani ya muziki wakati wa mazoezi ya viungo na ukimbiaji, hivyo kukupa hamasa zaidi.

Kimbia na ufanye mazoezi ya viungo kabla na baada ya ukimbiaji ili kuongeza faida nyingi zaidi za kiafya kwa urahisi.