Prime
SPOTI DOKTA: Bondia kufia ulingoni sababu ni hii

Muktasari:
- Ulimwengu wa masumbwi hasa barani Afrika uliingia katika majonzi kutokana na kifo hicho cha ghafla cha bingwa wa zamani wa uzito wa Light Heavy wa taifa hilo na Afrika Magharibi.
KUELEKEA Sikukuu ya Eid Fitr jijini Nigeria, iligeuka huzuni katika mchezo wa masumbwi baada ya bondia Gabriel Olanrewaju kufariki dunia wakati wa pambano baada ya kudondoka katika raundi ya 10.
Ulimwengu wa masumbwi hasa barani Afrika uliingia katika majonzi kutokana na kifo hicho cha ghafla cha bingwa wa zamani wa uzito wa Light Heavy wa taifa hilo na Afrika Magharibi.
Bondia huyo kijana mahiri, alifariki dunia akiwa ulingoni wakati akipambana na bondia kutoka nchini Ghana usiku wa Jumamosi katika Uwanja wa Bukom Arena, Ghana. Pambano hilo la kusisimua na kuvutia lilianza kwa mabondia hao kurushiana makonde mazito jambo lililoibua msisimko kwa mashabiki uwanjani.

Wababe hao walionyesha umakini, ukakamavu na ustadi wa wa kipekee, lakini katika raundi za baadaye, Olanrewaju alionekana kuhangaika akionyesha dalili za kuchoka ikiwamo kuyumbayumba. Katika raundi ya 10 baada ya kupokea mfululizo wa vipigo vya makonde mazito bondia huyo aliangukia kwenye kamba za ulingo akiwa na viashiria vya kupoteza fahamu.
Wahudumu wa huduma ya kwanza walibaini hali hiyo, hivyo waliingia haraka kumhudumia, huku umati wa watazamaji ukiwa unatazama kwa mshangao na kustua. Pamoja na juhudi kubwa za watoa huduma ya kwanza kuokoa maisha ya bondia huyo, lakini baadaye alitangazwa kuwa amefariki dunia katika hospitali iliyo karibu na uwanja huo.
Spoti Dokta ilifuatilia tukio hilo ambalo limesambaa sana katika mitandao ya kijamii na kuwasikitisha wapenzi wa michezo huku wakijiuliza nini sababu ya kifo hicho.
SABABU AINA HII YA MAJERAHA
Kitabibu sababu ya kifo hicho ni kuvuja kwa damu katika ubongo kulikosababishwa jeraha aina ya tatu la ubongo ambalo linahusisha mchubuko au mchaniko wa ubongo. Aina hiyo ya jeraha husababisha kifo cha ghafla kwa sababu ubongo ndio mdhibiti mkuu wa matukio nyeti ya mwili yanayotufanya kuwa hai ikiwamo mapigo ya moyo na upumuaji.

Hivyo ubongo unapopata majeraha makubwa na damu kuvunja ina maana kuwa tishu za ubongo zitakosa lishe ya damu yenye hewa safi ya oksijeni hatimaye tishu hizi zitakufa. Aina hiyo la jeraha hujulikana kitabibu kama Cerebral Lacerations, ni jeraha lenye matokeo mabaya linaloweza kusababisha kifo cha mapema au ulemavu wa kudumu.
Aina hiyo ya jeraha linatokana na kitu kizito kutua kichwani na kusukuma mfupa wa kichwa yaani fuvu kisha kujeruhi ubongo. Vilevile fuvu linaweza kuvunjika au kupasuka hatimaye kujeruhi ubongo. Kazi kubwa ya fuvu ni kulinda ubongo usipate madhara na vitu kutoka nje ya mwili.
Madhara ya awali ya jeraha la aina hiyo ni kuvuja damu kulikotokana na shinikizo kubwa la kitu kilichogonga kichwani, hivyo kusababisha majeraha ya vijinyuzi vya mishipa ya fahamu. Hali hiyo ikitokea husababisha mlipuko katika tishu, mabadiliko ya shughuli za ndani ya tishu na ubongo kuvimba.
Hapa madhara ya muda mfupi yanayojitokeza ni kama vile kupoteza fahamu, kuweweseka au kuchanganyikiwa, kushindwa kuwezesha mihemko na mawasiliano ya mwili pamoja na kupatwa na degedege. Madhara mengine ni pamoja na ubongo kujaa maji, ute wa mfumo wa ubongo na uti wa mgongo kuvuja, majaraha katika mishipa ya damu na fahamu kwenye ubongo na ogani kuu kusitisha utendaji.
Ubongo ni ogani nyeti iliyosheheni tishu za mfumo wa fahamu ambazo zimo ndani ya pango na hulindwa na tishu ngumu sana yaani fuvu la kichwa. Ubongo huwa na kazi kama vile kutafsiri taarifa za misisimko mbalimbali, kudhibiti mapigo ya moyo, upumuaji na kuamrisha kutoka kwa vichochezi.

Ubongo una sehemu kuu tatu ikiwamo eneo la mbele, katikati na nyuma. Ingawa sehemu hizo nazo zimegawanyika kuendana na utendaji. Hivyo kupata majeraha makubwa ya ubongo ina maana mambo mengi mwilini yatasimama ikiwamo upumuaji, mapigo ya moyo na hisia za mihemko mbalimbali.
Hali hii ikitokea kifo cha mapema kinaweza kutokea au ulemavu wa kudumu ikiwamo kupooza viungo vya mwili.
HISTORIA YA MAJERAHA YA UBONGO MICHEZONI
Tukio kama hilo la Nigeria siyo la kwanza kwa bondia kufia ulingoni Afrika. Mtakumbuka pia nchini Afrika Kusini mwaka jana bondia alifariki ulingoni baada ya kupigwa ngumi mfululizo. Majeraha mengi yanayowapata mabondia huwa ni maumivu na uvimbe, michaniko hasa maeneo ya usoni, mtikisiko au kuvimba kwa ubongo ambayo hayana madhara makubwa.
Hili lakupata aina hii ya majeraha ya ubongo daraja la tatu hutokea mara chache, ndiyo maana mchezo huo haujaweza kuitwa tishio kwa afya za washiriki.
JINSI YA KUPUNGUZA MAJERAHA HAYO
Ni muhimu kuzingatia miongozo ya Shirikisho la Ngumi Duniani ambalo linawaelekeza mabondia kupima afya kabla ya mapambano. Pia kutoshiriki mapambano makubwa mfululizo kwa kipindi cha miezi sita. Majeraha ya aina hiyo yanaweza kuzuiwa kwa kuvaa kofia maalumu kukinga kichwa katika mchezo wa masumbwi. Ingawa katika ndondi za kulipwa kanuni zao haziruhusu kuvaa.
Kuendelea kuzingatia mbinu za mchezo wa masumbwi kwa kujikinga na kukwepa ngumi zinazoelekea kichwani na kuzingatia matumizi ya glovu zenye kiwango ambazo zinakubalika katika mchezo wa ngumi ili kupunguza makali ya ngumi.
Vilevile wasaidizi kuwa makini na viashiria vya majeraha ya ndani ya kichwa. Mfano ilitosha wasaidizi kutupa taulo mapema pale walipoona kuwa bodia yule anaweweseka na kuonekana mchovu.

KWANINI WANAZIMIA
Kudondoka au kuyumbayumba na kukosa balansi ni kutokana na ngumi eneo ilipopiga kuwa kuna mshipa mkubwa wa damu unaopeleka damu katika ubongo.
Upigwaji wa eneo hilo unaweza kusababisha mtikisiko na kusababisha damu na oksijeni inayokwenda katika ubongo kubadili mwelekeo. Hii inaweza kusababisha mtu kukosa damu katika ubongo na hatimaye kupoteza fahamu au kufariki dunia kama itadumu kwa zaidi ya dakika sita.
Ieleweke kuwa ngumi yoyote katika eneo la kichwa ni hatari kwa afya ya ubongo. Bondia anapopigwa eneo hilo na kudondoka ni muhimu wasaidizi wakakubaliana na hali ikiwamo kuzuia kuendelea kwa pambano.