Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashine hizi namba zinazibeba sokoni

Muktasari:

  • Kutokana na hayo, wapo wachezaji kutoka Ligi Kuu Bara na Championship ambao wamefanya vizuri na huenda wakatafuta changamoto katika timu zingine kutokana na namna walivyoupiga mwingi kwenye vikosi wanavyochezea kwa sasa huku wengine kutoongeza mikataba mipya.

LIGI Kuu Bara msimu huu inakwenda kumalizika hivi karibuni, huku ushindani ukizidi kuonekana kuanzia malengo ya ubingwa, vita ya ufungaji na mengineyo jambo linaloonyesha kuimarisha mashindano hayo na klabu kwa ujumla.

Kutokana na hayo, wapo wachezaji kutoka Ligi Kuu Bara na Championship ambao wamefanya vizuri na huenda wakatafuta changamoto katika timu zingine kutokana na namna walivyoupiga mwingi kwenye vikosi wanavyochezea kwa sasa huku wengine kutoongeza mikataba mipya.

Lakini, nyuma ya hilo kuna msukumo pia wa namna walivyoonyesha soka la ushindani katika timu walizocheza na hivyo namba zao zitakuwa ushawishi katika safari yao ya soka. Twende pamoja...!


FEISAL SALUM 'FEI TOTO' (AZAM FC)

Feisal ni mmoja wa viungo wenye vipaji vikubwa na sasa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika 2026, ingawa tayari timu kibao ikiwemo Yanga aliyoichezea kabla ya Azam FC, Simba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zinamtaka.

Nyota huyo ni mchezaji aliyefanya vizuri zaidi 2024 akichangia mabao 27 katika Ligi Kuu baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimfunika Stephane Aziz KI wa Yanga aliyetua Wydad Casabalanca ya Morocco hivi karibuni aliyefunga 12 na asisti tisa. Mwaka huo Fei aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi akifuatiwa na Aziz KI aliyechangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa huku Gibril Sillah wa Azam FC pia akihusika na mabao 13 akifunga manane na kuasisti matano.

Kiwango bora cha Fei kilimfanya kumaliza na mabao 19 Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi nyuma ya Aziz KI aliyekuwa Yanga aliyeibuka kinara akifunga 21.

Fei hadi sasa katika ligi akiwa na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam amehusika katika mabao 17 baada ya kufunga manne na kuasisti 13 akiwa ndiye mchezaji anayeongoza kwa asisti nyingi zaidi.


SELEMENI BWENZI (KENGOLD)

Licha ya KenGold kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship, lakini miongoni mwa washambuliaji wa kikosi hicho waliofanya vizuri ni pamoja na Selemani Bwenzi, jambo linaloweza kuzivutia timu nyingine kuitaka saini yake.

Nyota huyo alijiunga na KenGold katika dirisha dogo la Januari 2025 akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, na tangu atue amechangia mabao sita Ligi Kuu kati ya 22 ya KenGold baada ya kufunga matano na kuasisti moja. Lakini akiwa na Mbeya Kwanza, Bwenzi alichangia matatu baada ya kufunga moja na kuasisti mawili. Bwenzi anadai alisaini mkataba wa miezi sita KenGold, jambo linalompa nafasi ya kuamua hatima ya sehemu atakayocheza msimu ujao.


PETER LWASA (KAGERA SUGAR)

Kiungo huyo mshambuliaji anacheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza akiwa na kikosi hicho baada ya kuonyesha kiwango bora kilichowavutia mabosi wa Kagera Sugar walioingia vitani kumsajili Agosti 15, 2024 akitoka KCCA ya kwao Uganda. Licha ya Kagera Sugar kushuka daraja, Lwasa aliyewahi pia kuicheza URA ya Uganda, Sofapaka, Kariobangi Sharks na Gor Mahia zote za Kenya ndiye mchezaji wa Kagera Sugar aliyeifungia mabao mengi Ligi Kuu baada ya kutupia nyavuni mara nane.


JOSHUA IBRAHIM (KENGOLD)

Nyota huyo alijiunga na KenGold msimu huu akitokea Tusker ya Kenya akisaini mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho kilichoshuka daraja, jambo linalofanya huenda asicheze Championship msimu ujao akatafuta changamoto sehemu nyingine.

Akiwa na KenGold msimu huu ameifungia mabao manne ya Ligi Kuu Bara na kuonyesha kiwango kizuri kilichowavutia mabosi wa Namungo FC 'Wauaji wa Kusini' kuinasa saini yake kwa mkopo wakati dirisha dogo la Januari na hadi sasa ameifungia bao moja.


ANDREW SIMCHIMBA (GEITA GOLD)

Unapotaja miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri Ligi ya Championship msimu huu hutaacha kumtaja mshambuliaji nyota wa Geita Gold, Andrew Simchimba kutokana na kiwango bora alichoonyesha. Nyota huyo wa zamani wa Coastal Union, Azam na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars.

Katika Championship Simchimba amekuwa mfungaji bora sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame wa TMA FC waliofunga mabao 18 kila mmoja, huku akiiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya nne. Kama utakuwa umesahau pia Simchimba ni miongoni wa nyota waliowahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2022-2023 alipofunga mabao saba akiwa na Ihefu.


EDGAR WILLIAM (FOUNTAIN GATE)

Mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka na hadi sasa akifunga mabao sita na kuasisti moja katika Ligi Kuu Bara, japokuwa amekuwa muhimili licha ya mwenendo mbovu wa kikosi kilichopo nafasi ya 14.

Edgar alijiunga na kikosi hicho akitokea KenGold aliyoipandisha Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya kuonyesha kiwango bora kilichomfanya kuibuka mfungaji bora wa Championship kufuatia kuweka rekodi ya kufunga mabao 21.

Mabao hayo yanamfanya kushikilia rekodi ya mshambuliaji aliyefunga mengi zaidi katika Championship, kwani tangu msimu wa 2017-2018 hakuna aliyefunga idadi hiyo, huku mkataba wake na Fountain Gate ukiwa wa msimu mmoja, hivyo lolote linaweza kutokea.


MISHAMO MICHAEL (KENGOLD)

Mishamo ni miongoni mwa wachezaji waliochangia timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu uliopita, ingawa msimu huu pia ameshuka nayo. Licha ya hayo uwezo aliouonyesha unamfanya kumuweka sokoni kutokana na takwimu bora alizokuwa nazo. Msimu uliopita wa Ligi ya Championship alifunga mabao 10 na hadi sasa amefunga matano na kuasisti mawili katika Ligi Kuu huku akitengeneza pacha bora ya ushambuliaji na nyota mwenzake, Edgar William aliyetua Fountain Gate msimu huu.


ABDULAZIZ SHAHAME 'HAALAND' (TMA FC)

Huu ni msimu wa pili kwa Shahame kuitumikia TMA ya Arusha tangu alipojiunga nayo 2022-2023 akitokea Pan Africans baada ya kuachana na Mbeya Kwanza, huku akiwa miongoni mwa mshambuliaji tegemeo. Msimu uliopita nyota huyo anayefananishwa na mshambuliaji wa Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, alifunga mabao 10 katika Ligi ya Championship, ingawa msimu huu ameonyesha kiwango bora zaidi baada ya kumaliza na mabao 18. Idadi hiyo ya mabao ni sawa na iliyofungwa na nyota wenzake Andrew Simchimba wa Geita Gold na Raizin Hafidh (Mtibwa Sugar) na kuiwezesha TMA kumaliza msimu huu ikiwa nafasi ya tano na pointi 53.


GIBRIL SILLAH (AZAM FC)

Tangu Sillah ajiunge na Azam FC, Julai 1, 2023 akitokea Raja Casablanca ya Morocco amekuwa miongoni mwa mawinga bora katika Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili aliyoichezea, jambo linalozifanya timu mbalimbali kuanza kuiwinda saini yake.

Raia huyo wa Gambia inaelezwa bado hajasaini mkataba mpya na kikosi hicho, huku kukiwa kuna taarifa za kuhusishwa na Yanga ambapo msimu wake wa kwanza alifunga mabao manane na huu ameshafunga tisa katika Ligi Kuu Bara.


OFFEN CHIKOLA (TABORA UNITED)

Chikola amekuwa akihusishwa na Yanga ingawa uongozi wa Tabora United ulijitokeza na kueleza bado ana mkataba zaidi na kikosi hicho, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuelezwa yuko mbioni kutua KMC katika dirisha dogo la Januari 2025.

Chikola alijiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Geita Gold inayoshiriki Championship, ambapo kwa sasa ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi ya kikosi hicho Ligi Kuu akiwa amefunga saba na kutoa asisti mbili.


JONATHAN SOWAH (SINGIDA BLACK STARS)

Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu amefunga mabao 11 Ligi Kuu akionyesha kiwango bora na kuzifanya timu mbalimbali kuanza kuiwinda saini yake ikiwemo Yanga.

Nyota huyo aliyejiunga na Singida akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya aliyoitumikia kwa miezi sita, alionyesha kiwango bora pia kwani alihusika na mabao saba baada ya kufunga matano na kuasisti mawili kwenye mechi tisa.

Sowah alijiunga na Al-Nasr Benghazi Januari 27, 2024 akitokea Medeama ya kwao Ghana ambako pia alionyesha kiwango bora na kuzivutia timu mbalimbali ikiwemo Yanga baada ya kuisumbua kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Akiwa na Medeama aliyojiunga nayo Januari 11, 2023 akitokea Danbort alicheza mechi 20 za Ligi Kuu Ghana, ambapo alifunga mabao 16, huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika alifunga matatu kwenye mechi saba alizochezea kikosi hicho.