SPOTI DOKTA: Bila uzito mwepesi vigumu kunyumbulika

New Content Item (1)
New Content Item (1)

WAKATI  Kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola anatua katika klabu hiyo akitokea Bayern Munich alionekana ni muumini wa wachezaji ambao ni wepesi kunyumbulika uwanjani.
Aina ya wachezaji anaopenda kuwasajili na hata alionao sasa wengi wao ni wale ambao wana maumbile madogo ambao ni wepesi kunyumbulika na huku wakitumia akili kwa wakati.
Hata katika mechi ya juzi ya usiku wa ligi ya UEFA uliocheza juzi usiku wa Jumanne ambayo walitoa kipigo cha kipekee chao mabao 7-0 dhidi ya RB Leipzig ilionyesha dhahiri kuwa aina ya wachezaji alionao ni wepesi.

Wepesi wa mwanasoka ina maana mchezaji anaweza kufanya matendo ya kimchezo kwa haraka huku akiweza kuumudu vyema uzito wake wa mwili.
Wengi wa wanasoka wakulipwa wenye kiwango cha juu na wenye kunyumbulika duniani wanaonekana kuwa sio wavivu na huku miili yao ikionyesha haina chembe ya ukibonge.
Tazama miili kama Ilkay Gundogan, Luka Modric, Lionel Messi na Thiago Alcantara, ambao ni kielelezo cha wachezaji wepesi wenye uwezo wa kunyumbulika wanapocheza mchezo wa soka.

Wengi wa wachezaji wa aina hii ni kama vile alivyo Chama kwa hapa nchini, Feisal Salum 'Fei Toto' nao ni aina ya wachezaji ambao ni wepesi kunyumbulika.
Siri kubwa ya wachezaji wa aina hii kuweza kunyumbulika ni mazoezi na huku wakidhibiti vyema uzito wao wa mwili ambao unaangukia katika wastani wa kilo 65-70.
Wakati Pep Guardiola anamwacha Yaya Toure wengi walimnyooshea kidole kwa kudhani kuwa ni mbaguzi lakini kiufundi ilionekana yeye ni muumini wa soka la kuvutia akipendelea kutumia viungo wepesi.
Wepesi na unyumbulikaji kwa mwanasoka hauji hivi hivi, ni lazima awe mwenye nidhamu ya mazoezi na ulaji wa vyakula kwa kuzingatia maelekezo ya mtaalam wa lishe ya wanasoka na benchi la ufundi.

Bila kuwa na uzito mwepesi ni vigumu kwa mchezaji kuweza kunyumbulika hasa kwa eneo la kiungo ambalo ndio nguzo ya mafanikio kwa timu yoyote.
Jicho la tatu la kitabibu linatazama soka la nchi za dunia ya tatu ambapo bado kuna changamoto ya klabu za soka kutokuwa na kipato cha kuweza kuwa na wataalam wa lishe ya wanasoka.
Vile vile Benchi ukosefu wa benchi bora la mazoezi ya viungo ambalo ndio huleta matokeo makubwa katika utimamu wa mwanasoka ambao ndani yake kuna wepesi hivyo kuweza kunyumbulika.
Udhibiti wa uzito wa mwili na kuzingatia maelekezo ya programu ya mazoezi ndio chanzo cha wachezaji wa kimataifa kama Luka Modric kuweza kuhudumu kwa muda mrefu akiwa na uzito wa mwili ule ule.
Ili kulipa mkazo jambo hili kwa soka letu la kibongo ni vizuri angalau leo wachezaji na wasomaji mkapata ufahamu kuhusu namna ya kuweza kutathimini uzito wako wa mwili.


UZITO WA MWILI UNATHAMINIWA HIVI
Inawezekana mwanasoka au mtu wa kawaida kila siku unafanya mazoezi mbalimbali lakini hafahamu kama uzito ulionao upo katika ainisho gani la uzito.
Kama mchezaji anahitaji kuwa na wepesi wa mwili ili kukuwezesha kunyumbulika unapokuwa unacheza soka basi anahitaji kujua njia rahisi ya kutathimini uzito wake.
Ipo njia rahisi inayoweza kukokotoa na kuweza kupata ainisha la uzito wako wa mwili hivyo kuweza kuchukua hatua kwa kuboresha mazoezi unayofanya ili kukabiliana na uzito mkubwa au unene uliokithiri.
Kitaalam zipo njia kadhaa ambazo mara nyingi hutumika kubaini uzito uliokithiri au kujua mtawanyiko wa mafuta yaliyorundikana mwilini.

Njia hizo na njia za kimahesabu kwa upimaji wa mzunguko wa kiriba tumbo na kugawa kwa urefu wa mwili hujulikana kama waist circumference ratio.
Njia ya pili ni waist-hip ratio yaani uwiano wa mzunguko wa kiriba tumbo na mzunguko wa paja na ya tatu ni Body Mass Index (BMI) ambayo ni ulinganishaji wa uzito na urefu wa mwili.
Njia ya BMI ndio inatumika zaidi kutathimini uzito wa mwili kwa watu wazima, siku ya leo nitaelenga zaidi njia hii kwani ndiyo inatupa taswira ya unene mwilini.
Kwa kawaida hutumia fomula ya kimehasibu kwa kugawa wa uzito katika kilogramu na urefu katika mita kipeuo cha pili. Mfano mtu mwenye Kilo 65 na urefu mita 1.5, BMI ni 70 gawa kwa 1.5 mara 1.5.
Kwa kutumia fomula vipimo vya uzito na urefu zao linalopatikana baada ya kukokotoa ndiyo hujulikana kama BMI, njia hii inatuwezesha kubaini kama ni unene uliokithiri au ni uzito mdogo sana.

Kwa mujibu wa shirika la Afya duniani-WHO BMI inatuwezesha kuanisha uzito wa mtu katika makundi matano. Jibu linalopatikana baada ya kukokotoa ndilo linatoa ainisho la uzito.
Kwa watu wazima BMI ya 18.5-24.9 kitabibu ni uzito salama kiafya, 25.0-29.9 hapa ni uzito mkubwa, 30.0-39.9 hapa huesabika kama ni unene na 40.0 kuendelea ni unene uliokithiri.
Wengi wa wachezaji wepesi na wanaonyumbulika kwa ufanisi wana BMI ya 18.5-24.9.
Endapo BMI itakuwa chini ya 18.5 maana yake ni kuwa mtu huyo ana uzito mdogo sana. Hata katika soka mchezaji akiwa chini ya hapa hutakiwa kuongeza uzito.
Katika BMI hapa tunaweza kutofautisha uzito uliokithiri, unene na unene uliokithiri hivyo wataalam wa afya huitumia njia hii kutathimini hatari za kiafya wanazoweza kuzipata watu baada ya matokeo ya BMI.
Njia hiii ya BMI ni rahisi na haina gharama, ni njia ambayo inawezesha kubaini mrundikano wa mafuta mwilini na uzito uliokithiri kirahisi.

Makampuni ya simu za smart wana mfumo laini ndani ya simu wenye kikokotozi cha BMI unachokifanya ni kujaza tu uzito (Kg) wako na urefu wako kisha inakupa majibu (m).
Baada ya kupata bainisha mfanya mazoezi mchezaji au mtu yoyote anaweza kujijua yuko katika kundi gani hivyo kuweza kujikita katika programu ya mazoezi akijua nini anachokifanya mazoezini.


USHAURI
Siri kubwa ya mchezaji kuwa mwepesi na kunyumbulika kwa ufanisi ni kutokula kiholela, kula vyakula kwa kuzingatia lishe ya mtaalam wa lishe, kushikamana na mazoezi na kulala  usiku kwa masaa 8-10.