SOMOE NG’ITU: Ndoto ilianzia kuwa rubani hadi ubosi soka la wanawake
Muktasari:
- Mafanikio hayaji kwa bahati, hujengwa kwa jasho, uamuzi mgumu na moyo wa kutokata tamaa. Na ili kufikia mafanikio hayo, lazima mtu upitie milima na mabonde, uanguke na kuinuka ili kuweza kufikia malengo.
KUNA wanawake wanaosubiri bahati na kuna wanaoijenga kwa mikono yao kwa kuthubutu kuandika hatima zao upya pale ndoto zinapobadili mwelekeo.
Mafanikio hayaji kwa bahati, hujengwa kwa jasho, uamuzi mgumu na moyo wa kutokata tamaa. Na ili kufikia mafanikio hayo, lazima mtu upitie milima na mabonde, uanguke na kuinuka ili kuweza kufikia malengo.
Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza Mwenyekiti wa Soka ya Wanawake Tanzania (TWFA), Somoe Ng’itu ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ambavyo ndoto yake ya kuwa rubani ilipofifia, lakini hakuruhusu maisha yazime, kwani ndoto nyingine iliibuka upya katika tasnia ya habari na baadaye kwenye uongozi wa soka la wanawake.
Somoe anasema, alitamani kuwa rubani, akaishia kuwa mwandishi akaingia katika ushindani mkali wa tasnia ya habari, akajijengea jina na leo anasimama kama kiongozi wa soka la wanawake na Kamishna wa Mechi wa Kimataifa.
URUBANI HADI KUANDIKA
Sio kila mwanadamu anafanya kazi ya ndoto yake hasa ambao wamepata bahati ya kuajiriwa ni wachache sana ambao wanafanya kile walichokuwa wanatamani kukifanya tangu wakiwa shule kama ambavyo anathibitisha Somoe.
“Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa rubani (kuongoza ndege) lakini mambo yangu haya kwenda kama nilivyokuwa natarajia kutokana na matokeo niliyoyapata baada ya kuhitimu elimu yangu matokeo yangu hayakukidhi nilichokuwa nakitamani,” anasema Somoe na kuongeza;
“Tangu nikiwa na umri mdogo nilikuwa napenda sana kusafiri, hivyo nilipanda ndege muda mwingi nilikuwa natumia kumtazama muongozaji na kujikuta nikipenda kazi hiyo na kupambana katika elimu yangu ili nitimize ndoto yangu, lakini mambo yalienda tofauti.”
Somoe anasema hadi sasa bado anafurahia safari na kuvutiwa na kile kinachofanywa na marubani, lakini haoni tena nafasi ya kutimiza ndoto ya kuwa rubani zaidi ya kufurahia safari na hajawahi kuchoka kila anapopata nafasi ya kusafiri kwa ndege kwa sababu ni kitu anachokipenda.
SUZAN MUNGI ALIVYOMVUTA
Licha ya kushindwa kufikia malengo ya kufanya kile alikuwa anatamani kukifanya tangu akiwa mdogo, Somoe anasema alijikuta anaingiwa na tamaa ya kuwa mwanahabari baada ya kuvutiwa na mtangazaji wa ITV, Suzan Mungi miaka hiyo.
Anasema alipenda kuangalia taarifa ya habari kila siku na kuvutiwa na aina ya usomaji wa taarifa wa mwanadada huyo ambaye alimfanya aingie darasani kusomea uandishi wa habari.
“Nilikuwa navutiwa na aina ya utangazaji wa habari aliokuwa anaufanya Zainab na ndipo nilipofanya uamuzi wa kujiunga na Chuo cha Dar es Salaam School Journalism (DSJ) mwaka 1998,”
“Nikiwa chuo nilipata bahati ya kufanya majaribio katika gazeti la Nipashe. Nilianza na habari za mahakamani chini ya bosi Hamis Kibari baada ya muda bosi wa dawati la michezo, Angetile Osiah aliniona na kuomba nihamie upande wa michezo hapo ndio safari yangu ya uandishi wa habari za michezo ilipoanzia.”
Anasema baada ya kuwa chini ya Angetile alikuwa anaandika habari za michezo na burudani na kwa upande wa michezo alikuwa mdau zaidi wa soka la wanaume.
USHINDANI KWA WENGINE
Katika kila kazi iliyo na mafanikio ushindani haukosekani kama anavyothibitisha Somoe kuwa alipokuwa anapambania ulaji wake alikutana na ushindani wa waandishi mahiri ambao hata hivyo aliweza kuwaacha mbali kwa kuandika stori nzuri na bora.
“Kipindi hicho uandishi ulikuwa na ushindani mkubwa na stori nyingi zilikuwa ni ‘exclusive’ tofauti na miaka ya sasa ambapo waandishi wanakuwa na stori aina moja. Sijisifu ila nilikuwa Mwandishi mzuri ambaye nilikuwa naandika stori zenye upekee.
“Kipindi hicho kulikuwa na ushindani mkubwa, tulikuwa na mchuano na stori zetu hazikuwa za kupiga simu au kusubiri mmoja atafute na mwingine achukue kama ilivyo sasa.”
Somoe anasema walikuwa wanapishana kwenye viwanja vya mazoezi mmoja akienda leo mwingine anapanga kwenda kesho kila mmoja anakuwa na stori ya tofauti kulingana na aina ya mazoezi waliyokutana nayo siku husika kwa kugawana viwanja vya timu mbalimbali.
“Kipindi cha usajili ndio ilikuwa inakuwa gombania goli kusaka exclusive, kila mmoja anaibuka na stori yake. Vita ilikuwa inakuwa kubwa, najivunia nilikuwa bora sana nyakati zote stori zangu zilikuwa za tofauti na bora.”
KIDAU ALIVYOMBEBA HADI FIFA
“Nakumbuka 2019 TFF lilitoka tangazo la nafasi za kusaka makamishna wa michezo, nilimpigia aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau kumuuliza kama naweza kuwania nafasi hiyo aliniambia ndio naweza inanifaa ndipo nilipochukua fomu ya kujiandikisha,” anasema na kuongeza:
“Nilifanya usaili na kufanikiwa kuipata nafasi hiyo. Baada ya kufanikiwa nilisimamia mechi moja ya Daraja la Kwanza (Championship) na moja Daraja la Pili. Baada ya hapo nilipandishwa kusimamia mechi za Ligi Kuu Bara.”
Somoe anasema mwaka uliofuata Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilitoa nafasi ya wakufunzi kutoka Tanzania kwenda kujiunga kupata mafunzo na TFF ilimchagua kuwa mwakilishi kwa kwenda kupata mafunzo ya awali huko.
“2021/22 CAF iliniteua kuwa kamishina wa soka la Afrika, nikapata nafasi ya kusimamia baadhi ya mechi kama ilivyo kwa baadhi ya waamuzi wetu ambao wanapata nafasi ya kwenda kuchezesha mechi za kimataifa,
“Haikuishia hapo, niliendelea kupata mafunzo mbalimbali ya ukamishna ambapo sasa natambulika kama Kamishna wa mechi wa FIFA na CAF. Najivunia mafanikio haya yametokana na kujitoa. Mimi naamini katika kupambania ninachokiamini.”
Anasema majukumu yake kama kamishina ni kusimamia mechi za kufuzu na mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya soka ya kimataifa na ya Afrika (FIFA/CAF).
MIAKA 20 NEWSROOM MOJA
Haikuwa rahisi, lakini Somoe ameipambania kazi yake kwa zaidi ya miaka 20 huku akidumu katika kampuni moja kwa miaka 20 hadi sasa na hapa anafunguka sababu.
“Niliajiriwa IPP ambayo inachapa magazeti ya Nipashe na The Guardian tangu Septemba Mosi, 2006 kwa hiyo mwaka huu tarehe na mwezi kama huo natimiza miaka 20 ndani ya kampuni hii, lakini nje ya hapa nimefanyia kazi ya uandishi kwa zaidi ya miaka hiyo.
“Sababu za kudumu kwa muda mrefu ni kutokana na waajiri wangu kunipandishia mshahara kila ambapo nilipokuwa napata ofa ya kutaka kutoka Nipashe kwani nilishawahi kupata nafasi ya kwenda kufanya kazi Habari Leo na kufikia makubaliano.”
Anasema mara baada ya kwenda kufanya mazungumzo na Habari Leo na kupewa mkataba kwa ajili ya kuusaini, aliporudi Nipashe kwa ajili ya kuaga alihojiwa dau analopewa na waajiri wake wapya na ndipo uongozi wa kampuni ulipombakiza na kumpa kiasi kama ambacho ameahidiwa na washindani wao.
“Mshahara wangu ndani ya kampuni ya Nipashe ulikuwa unapanda kila ninapopokea ofa kutoka kampuni nyingine tofauti, hivyo thamani yangu ilikuwa inapanda kama ilivyo kwa wachezaji wakitakiwa na timu mbili pinzani na hii ndio sababu ya mimi kukaa kwa miaka mingi bila kuondoka hapa.”
U-MISS ALIKWAMA HAPA
Ukiacha uandishi wa habari, mwonekano wake kipindi hicho akiwa na umri mdogo alivyokuwa na mwili wa ki-miss na urefu, ulimvuta aliyekuwa mratibu wa zamani wa mashindano ya Miss Tanzania, marehemu Hashim Lundenga kumshawishi ashiriki shindano la urembo.
“Nakumbuka marehemu Lundenga alifanikiwa kunishawishi niingie kwenye shindano la kuwania taji la miss, nilikubali na nilihudhuria mazoezi mara moja tu nikaacha kutokana na maneno mengi yaliyokuwa yanazungumzwa nyuma ya ushindi ambayo siwezi kuweka wazi kila mmoja aliyekuwa anafuatilia kipindi hicho anafahamu,” anasema Somoe na kuongeza;
“Baada ya mazoezi ya siku moja sikurudi tena na kuamua kujikita katika tasnia ya uandishi ambayo nimedumu nayo hadi sasa sijawahi kujuta kuichagua licha ya changamoto chache nilizokutana nazo.”
Somoe anasema katika upambanaji waje hajawahi kuichukia kazi hiyo wala kukutana na changamoto iliyomkatisha tamaa akatamani kuiacha huku akikiri kupitia nyakati ngumu kupindi ambacho kampuni nyingi za media ziliyumba kiuchumi hadi kufikia wakati kushindwa kulipa mishahara kwa wakati.
“Changamoto ngumu ni miaka ya hivi karibuni, kampuni nyingi za habari zikawa zinapitia ugumu wa kutokulipwa mishahara kwa wakati, nashukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kazi ninayofanya huko ilifukia mashimo kwa kujipatia kipato nje ya tasnia yangu ya uandishi ambacho kilikuwa kinaendesha maisha yangu.”
LIUNDA ALITAKA AWE MWAMUZI
Katika harakati zake za utendaji kazi ya soka akiwa ni mwandishi wa habari, Somoe anasema alishawahi kufuatwa na Mkufunzi wa Waamuzi, Leslie Liunda akimshawishi aingie katika nafasi ya kusomea uamuzi.
“Nakumbuka kipindi hicho nikiwa katika majukumu yangu, Liunda alijaribu kunishawishi niiingie kwenye kozi ya uamuzi nilishindwa kutokana na shida ya kifua ambayo niko nayo,” anasema na kuongeza:
“Ushawishi huo ulitokana na namna walivyokuwa wananiamini katika utendaji kazi wangu hasa kwenye uandishi kipindi hicho waamuzi wengi walikuwa wanashindwa kuandika ripoti, hivyo waliamini nitaweza kusaidia kama nitasoma kozi hiyo.
“Liunda alitamani sana niwe mwamuzi, aliamini ntaweza kuandika ripoti vizuri kutokana na changamoto kubwa iliyokuwapo ya kukosekana kwa waamuzi wengi wazuri wa kuandika ripoti,m lakini hilo lilishindikana kutokana kwa changamoto yangu ya tatizo la kifua.”
UONGOZI ILIKUWA NI NDOTO
Kuna kauli inasema uongozi ni wito na imethibitishwa na Somoe ambaye amebainisha kuwa kuwa kiongozi kwa upande wake ilikuwa ni ndoto yake na anashukuru ameweza kutimiza lengo hilo akiwa kiongozi wa mchezo anaoupenda.
“Tangu mwaka 2008 ambapo nilikuwa mjumbe kwenye kamati katika ya soka la wanawake nilikuwa nianze kuongoza, lakini nilijiona sitoshi kutokana na umri niliokuwa nao kipindi hicho,
“Kwenye uongozi nilianza kwa kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa Soka ya Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya Amina Karuma hadi sasa nimepata nafasi ya kuwa Mwenyekiti,”
Somoe anasema haikuwa rahisi kwake kuaminiwa kupewa nafasi hiyo, lakini kwa kusimamia misingi na kulipambania soka la wanawake kumemfanya kuwapa kazi nyepesi wajumbe kumpigia kura za ndio kwenye uchaguzi uliopita.
“Nimeibuka na ushindi wa kishindo kuchukua nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa TWFA baada ya kushinda kwa kura 37 dhidi ya 14 alizopata mpinzani wangu,” anasema Somoe.
“Nilikuwa niongeze soka la wanawake muda mrefu lakini nakumbuka kuna kipindi niliikataa hiyo nafasi kwani niliona sitoshi kuwa kiongozi hadi hapo nilipojiridhisha kuwa ni muda sahihi wa mimi kuongoza soka ambalo nilijitoa mara nyingi kuhakikisha linasimama na kuwa bora.”
MAFANIKIO AJIVUNIAYO
Tanzania ni mfano wa mataifa ya kuigwa yanayopiga hatua kwenye soka la wanawake.
“Najivunia kuwa kiongozi wa soka la wanawake licha ya changamoto nyingi zilizopo tukikosa udhamini, bado tumekuwa na mafanikio makubwa chini ya uongozi wangu, nina mengi ya kujivunia,” anasema na kuongeza;
“Chini ya uongozi wangu timu imefanikiwa kushiriki Kombe la Dunia kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 17 nchini India mwaka 2022 na kufanikiwa kufika robo fainali kwa Afrika;
“Nchi imetwaa makombe ya Kanda ya Mashariki na Kati (Cecafa) na Kanda ya Kusini (Cosafa), kwa timu za umri kuanzia chini ya miaka 17, U-20 na Twiga Stars na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya Wanawake.”
Anasema pia klabu za wanawake zimeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika nusu fainali ambayo ni kati ya timu nne za juu ikianza Simba Queens na JKT Queens ambayo ilishiriki mashindano nchini Ivory Coast katika miji ya Korhogo na San Pedro yakishirikisha timu nane.
Somoe anasema chini ya uongozi wake timu za wanawake zimebeba makombe zaidi ya matano lakini pia ni Mabingwa wa Afrika na mwaka huu wanatetea ubingwa wa Cecafa.
“Ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa soka la wanawake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ukanda wa Afrika Tanzania tunaongoza kutwaa mataji mara nyingi tukichukua mara tatu, Ethiopia mara moja sawa na Kenya, haya ni mafanikio makubwa najivunia,
“Licha ya changamoto ya kukosa uwekezaji bado tumefanikiwa kupata mafanikio makubwa, wito wangu kwa wadau wa soka ni kuomba kuwekeza kwenye ligi ya wanawake kwani kuna mafanikio na matokeo mazuri.”
Somoe anasema endapo watapata udhamini mzuri kwenye ligi hiyo ya wanawake matarajio yatakuwa ni makubwa na watakuwa kati ya timu bora zitakazotoa ushindani mkubwa kwa timu za Ulaya katika soka la wanawake.
MKWASA, SIMBA STORI BORA
Somoe anasema katika miaka 20 ya uanahabari ameandika stori nyingi sana lakini za usajaili ni kati ya stori zake bora.
“Nilishawahi kuandika stori ya usajili mchezaji ambaye siwezi kutaja jina lake hadi sasa hiyo stori iliitingisha hadi klabu ya Simba ambayo ilimsajili kwani hakuna aliyetarajia kama kuna mwandishi anaweza kuipata,” anasema Somoe na kuongeza;
“Usajili kipindi hicho ni kificho nilifanikiwa kuipata mwenyewe na kuzipiga bao media nyingi viongozi wa Simba walipambana sana kufahamu nilipata wapi stori ilikuwa ngumu kwani chanzo changu hakikutarajiwa na wengi.”
Somoe pia alizungumzia stori ya madai ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa ambapo alipata taarifa za ndani kuwa kocha huyo ana malimbikizo ya madai ya mshahara wake akatoka na stori hiyo ambayo pia ilizua taharuki kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo liliamua kumlipa.
“Stori ya Mkwasa niliandika kwa kuzingatia maaadili, lakini ilikuwa imekamilika haina maswali iliwachanganya viongozi wa shirikisho ambao waliijibu kwa kulipa deni la kocha huyo mzawa. Makocha wa kigeni walilipwa kwa wakati tofauti na wazawa.”