Soka la Mbeya lawashtua wadau, wakuna vichwa

Muktasari:
- Kwa miaka takribani mitano nyuma, Mbeya ilikuwa kitovu cha soka huku ukiwa Mkoa wa pili baada ya Dar es Salaam kuwa na timu nyingi za Ligi Kuu na kuufanya Mkoa huo kuwa tishio katika medani za soka.
MWENENDO wa soka la Mbeya kwa miaka ya karibuni imeonekana kuwashtua wadau na mashabiki mkoani humo, huku wengine wakitahadharisha yasitokee ya jijini Tanga, Mwanza na Arusha.
Kwa miaka takribani mitano nyuma, Mbeya ilikuwa kitovu cha soka huku ukiwa Mkoa wa pili baada ya Dar es Salaam kuwa na timu nyingi za Ligi Kuu na kuufanya Mkoa huo kuwa tishio katika medani za soka.
Mwaka 2020/21 ilishuhudiwa timu nne zikiwa Ligi Kuu, ikiwa ni Mbeya Kwanza, Mbeya City, Tanzania Prisons na Ihefu, lakini pia ziliwahi kuwapo Tukuyu Stars na Boma FC ambazo zilitamba kwa muda wake.
Kwa sasa Mbeya imeonekana kuporomoka zaidi kwenye soka, hali inayoibua minong’ono na sintofahamua tatizo linaloimaliza kwenye medani za kandanda huku wengine wakihofia kutokea ya Tanga, Mwanza na Arusha.
Pamoja na idadi kubwa iliyokuwapo, Mbeya imebakiwa na timu mbili Ligi Kuu ikiwa ni Tanzania Prisons na Ken Gold, ambazo zinakatisha tamaa kutokana na matokeo yao hivi sasa.
Ikumbukwe Tanga iliwahi kupata pigo la kushusha timu tatu kwa mpigo, ikiwa ni Mgambo Shooting, African Sports na Coastal Union zilizoshuka daraja msimu wa 2016/17.
Baadaye Coastal Union ndio waliweza kurejea tena Ligi Kuu, huku African Sports wakionekana kuchechemea ambapo kwa sasa wapo championship, huku Mgambo Shooting wakipotea mazima.
Kwa upande wa Mwanza, iliwahi kuwa kwenye rekodi ya timu nyingi za Ligi Kuu, ikiwa ni Toto Africans, Mbao FC, Gwambina na Alliance, ambapo kwa sasa ni tia maji tia maji.
Mwanza macho yote yapo kwa Pamba Jiji ambayo nayo mwenendo wake Ligi Kuu si wa kurudhisha sana, ambapo lolote linaweza kuwakuta iwapo hawatashtuka mapema.
Toto Africans kwa sasa haijulikani ligi gani inashiriki sawa na Mbao FC, huku Gwambina ikipotezwa moja kwa moja tangu iliposhuka daraja misimu mitatu nyuma, huku Alliance ikiwa First League kwa kujikongoja.
Arusha jiji la kitalii, lilitamba kwa muda wake ikiwa na timu za JKT Oljoro, Arusha FC na Madini FC, ambapo kwa sasa hawaijui tena Ligi Kuu baada ya timu hizo kupotea.
Macho ya wadau na mashabiki wa Mkoa huo usioishiwa hekaheka, yamebaki kwa Mbuni FC na TMA zinazoshiriki Championship, wakiamini moja wapo inaweza kukata kiu.
Kilichozikuta Mikoa hiyo, kinaonekana kutokea Mbeya baada ya timu zake kuporomoka kwenye soka la ushindani huku nyingine zikipoteana, hali inayowaamsha wadau kutahadharisha.
TUKUYU STARS
Hakuna asiyekumbuka historian a rekodi kali za wakongwe hao, ambapo moja ya heshima iliyoweka ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1986, ambapo kwa sasa ipo ligi daraja la tatu Mkoa.
Timu hiyo ilikuwa tishio kwa wababe wa soka nchini, Yanga na Simba lakini kwa sasa imebaki stori na kuamka kwake haijulikani kutokana na kutokuwa na mwelekeo wowote.
BOMA FC
Ilikuwa na mwelekeo mzuri licha ya kutofika Ligi Kuu, ambapo kwa sasa haieleweki msimamo wake kutokana na kutoshiriki ligi yoyote, huku uliokuwa uongozi wake kusambaratika.
Timu hiyo ilionesha ushindani zaidi msimu wa 2018/19 kwenye daraja la kwanza (kwa sasa championship), ambapo ilikuwa kwenye uelekeo wa kuweza kupanda Ligi Kuu, lakini haikufanikiwa.
MBEYA KWANZA
Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2021/22 ilionekana kuweza kuleta mabadiliko kutokana uongozi wake kutokuwa kwenye makundi, lakini yaliyowakuta ilibaki historia.
Mbeya Kwanza ilishiriki ligi hiyo msimu mmoja na kushuka daraja, ambapo baadaye mabosi waliamua kuhama viwanja wakianza Mabatini, Morogoro, Songea na sasa wapo Mtwara.
Hadi sasa timu hiyo inacheza Championship ambapo haioneshi dalili za moja kwa moja kama ina nia ya kurejea tena Ligi Kuu kutokana na matokeo iliyonayo kwenye ligi hiyo.
IHEFU
Baada ya kupanda Ligi Kuu, msimu wa 2020/21, haikudumu badala yake ilijikuta ikishuka daraja, kabla ya kurejea tena msimu uliofuata huku ikionesha ushindani mkali.
Timu kubwa hususani Yanga ndio ilijikuta ikihenyeshwa kwa misimu miwili mfululizo walipokutana uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali kabla ya kupigwa mnada.
Pamoja na heshima iliyoweka, timu hiyo iliwekwa sokoni na kuuzwa na sasa inafahamika kwa Singida Black Stars na kuwaacha mashabiki na wadau wake wakikosa uhondo wa Ligi Kuu.
MBEYA CITY
Iliitwa nembo ya Jiji kwa maana ya kutambulisha Jiji la Mbeya ambapo kwa namna fulani ilifanikiwa kuweka historia ya kudumu Ligi Kuu miaka 10, tangu ilipopanda daraja.
Hata hivyo kwa sasa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya jiji hilo, inashiriki championship kwa msimu wa pili sasa, ambapo inaonesha matumaini kuweza kurejea.
Katika michezo 11 iliyocheza, imevuna alama 22 na kuwa nafasi ya tatu kwenye msimamo, huku wengi mashabiki wake wakiihesabu kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kurejea Ligi Kuu.
MTIHANI HUU HAPA
Wakati macho yote yakiwa kwa Prisons na Ken Gold, lakini mwelekeo wa timu hizo umeonekana kupoteana kutokana na wawili hao kuwa nafasi mbili za mkiani.
Ken Gold inayocheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza, ndio inaburuza mkia kwa pointi sita, ambapo leo Jumatano itakuwa kibaruani dhidi ya Simba, kumaliza mzunguko wa kwanza.
Matokeo yoyote katika mchezo huo yatawabakiza palepale mkiani na kuweka presha kubwa kwa mashabiki wakihofia huenda ikashuka daraja kutokana na hesabu zilivyo.
Pointi sita ilizonazo inahitaji nguvu kubwa na ya ziada kwa timu hiyo kuweza kuinusuru, vinginevyo inaweza kurudi ilipotoka Championship kuanza safari upya kuitafuta Ligi Kuu.
Wakati Ken Gold ikiparuana na Wekundu leo, ndugu zao Prisons watakuwa na mtiti dhidi ya Yanga, Desemba 22 katika mchezo wa kuhitimisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa Maafande hao.
MAKOCHA WATOA NENO
Kocha Mkuu wa Ken Gold, Omary Kapilima amesema pamoja na matokeo hayo, lakini hawajakata tamaa na kwakuwa ligi haijaisha mashabiki wawe na uvumilivu.
Amesema upungufu ulioonekana ndani ya uwanja, wanaenda kusahihisha dirisha dogo kwa kuongeza nguvu ili kusaka matokeo mazuri raundi ya pili ili timu ibaki salama msimu ujao.
“Dirisha dogo litatusaidia kumaliza tatizo, tunajua presha na ugumu uliopo lakini tutapambana kadri ya uwezo kuinusuru timu kutoshuka daraja” amesema Kapilima.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata amesema hawafurahishwi na matokeo waliyonayo, lakini hatma yao ni dirisha dogo kwa kuongeza nguvu kwenye maeneo yenye upungufu.
“Tutaongeza nguvu eneo la ushambuliaji na kiungo, matokeo si mazuri na benchi la ufundi tunaendelea kupambana kusahihisha makosa ili kurejesha ari na morali ndani na nje ya uwanja” anasema Makata.
MREFA NAO
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Chama cha Soka Mkoa huo, (Mrefa), Mohamed Mashango anasema wamekuwa na vikao vya mara kwa mara na timu hizo kujadiliana mustakabali wa kubaki salama.
Anasema moja ya mapendekezo na ushauri ni kujipanga dirisha dogo kuhakikisha wanafanya maboresho ya katika timu zao ili mzunguko wa pili wafanye vizuri.
“Bila hizi timu, hatutaziona Simba wala Yanga, Mrefa tumekuwa na vikao vya mara kwa mara kujadiliana na kupeana ushauri na mapendekezo nini cha kufanya ili kubaki salama Ligi Kuu”
“Matarajio yetu ni kwamba dirisha dogo litaleta mabadiliko chanya na timu zetu zitafanya vizuri mzunguko wa pili na hatimaye kumaliza ligi katika nafasi nzuri” alisema Mashango.
WADAU NA MASHABIKI
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha soka mkoani humo, Elias Mwanjala anasema anaumizwa na mwenendo wa soka kwa Mkoa huo akieleza kuwa inahitaji nguvu ya ziada.
“Nikibahatika kurejea kwenye uongozi ni kutengeneza umoja na ushirikiano kama nilivyowahi kufanya, ni aibu kwa sasa kuona soka linaporomoka, Mbeya haikuwa hivi” anasema Mwanjala.
Naye Festo John shabiki wa soka jijini hapa, anasema kuporomoka kwa soka la Mkoa huo ni pamoja na uongozi wa timu na viongozi wenye mamlaka kutokuwa na mipango.
“Timu nyingi hazina ushirikiano na wadau wakati wa mafanikio, zinapokutwa na wakati mgumu ndipo zinawaangukia, lakini hata hizi mamlaka hazina mipango bali kutegemea mpira uwalipe” anasema John.