Skudu akoshwa na Doumbia Yanga, awataja Maema, De Reuck
Muktasari:
- Kama hufahamu ni kwamba jina Skudu ni ufupisho wa jina la ukoo wake kutoka jina la Makudubela ambalo alilikatisha na kuamua kujiita Skudu.
UKITAJIWA majina yake halisi kwamba Mahlatsi Makudubela pengine itakuwa ngumu kufahamu nani anazungumziwa lakini ukisikia Skudu haraka unajua hapa anazungumziwa winga mmoja mwenye mwili mdogo lakini fundi wa kuuchezea mpira.
Kama hufahamu ni kwamba jina Skudu ni ufupisho wa jina la ukoo wake kutoka jina la Makudubela ambalo alilikatisha na kuamua kujiita Skudu.
Skudu ni raia wa kwanza kutoka Afrika Kusini kucheza soka la Tanzania na baadaye akafungua milango kwa wengine, akipita pale Yanga aliyoitumikia kwa msimu mmoja.
Winga huyu mcheshi alirudi nchini hivi karibuni tena akitakiwa kuisaidia timu yake ya sasa Wiliete kuitoa timu yake ya zamani Yanga katika vita ambayo ilikuwa kubwa kwao na kuishia kutupwa nje kwa jumla ya mabao 5-0 kwenye mechi ya raundi ya awali ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kurejea kwa Skudu nchini Mwanaspoti likapata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalum kujua mambo mbalimbali ya safari yake ya soka akiwa hapa nchini na baadaye kuondoka.
KUONDOKA YANGA
Skudu anaanza kuelezea namna alivyokabiliana na uamuzi wa kuondoka Yanga akisema haikuwa rahisi huku akifafanua zaidi.
“Kusema kweli haikuwa rahisi, unajua kulihitajika baadhi ya mambo kufanyika hasa kuhusu familia yangu ambayo nilikuwa nayo hapa Tanzania, ndio katika soka wachezaji wanakuja na kuondoka, lakini jambo moja la uhakika ni kwamba Yanga na Tanzania siku zote zitakuwa karibu na moyo wangu,” anaeleza Skudu huku akiendelea kufafanua zaidi.
AWAFUNGULIA MILANGO WENGINE
“Ilikuwa heshima kubwa kwangu kuiwakilisha Afrika Kusini kuja hapa Tanzania, nilikuwa mtu wa kwanza kutoka nyumbani kuja hapa kama mchezaji na baada ya muda nikaona wengine wakija kama makocha Fadlu Davids na wenzake, lakini sasa pia kuna Neo Maema, Rushine De Reuck, kwangu nachukulia kama Mungu alinituma kuja hapa kuwawashia mwanga wengine waje. Ni kama nilisikia sauti ikiniambia kuna maisha unaweza kupiga hatua hata kama ni nje ya Afrika Kusini.”
DILI LA MAEMA, RUSHINE
“Wakati Simba inawataka Rushine (De Reuck) na Neo Maema kwanza hawa lazima ufahamu ni rafiki zangu sana, wote walinitafuta baada ya kupata ofa ya kutakiwa na Simba waliniuliza mengi juu ya Simba, maisha ya Tanzania, ligi ya hapa na nikawaambia ninayoyafahamu, niliwaambia kwamba unapokwenda kucheza klabu kama Simba au Yanga hizo ni timu ambazo zinahitaji sana matokeo mazuri wakati wote.
“Nina furaha na Rushine nimeona ameanza kufunga mabao na pia akiingia kikosi cha kwanza, kuhusu Maema kwa kuwa ametoka kwenye majukumu ya timu ya taifa kwenye mashindano ya CHAN nadhani bado ana uchovu kidogo, atakuja kufanya makubwa kwa kuwa ana ubora mkubwa.”
MAISHA YA YANGA
“Angalia kabla ya yote Tanzania nilikaribishwa vizuri sana ndio maana nikasema itakuwa na nafasi maalum kwenye moyo wangu, Tanzania ni kama nyumbani kwangu kwingine, siku zote nikiwa najisikia kwenda sehemu kutulia, akili yangu inaniambia nenda Tanzania, wakaufanya uwepo wangu hapa uwe wa amani sana, nilifurahia sana muda wote niliokuwa na Yanga.”
WAKATI MGUMU UWANJANI
Skudu hakuwa mchezaji ambaye alipata muda mwingi wa kucheza akiwa na Yanga ndani ya mwaka mmoja aliocheza hapa, anaeleza ilivyokuwa.
“Kama utakumbuka, nilipofika Tanzania mchezo wangu wa kwanza wa mashindano ilikuwa ni mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Yanga dhidi ya Azam pale Tanga. Kwenye mchezo ule niliumia vibaya kipindi cha kwanza tu, nikapata jeraha ambalo liliniweka nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu. Nilivyopona sawasawa na kurudi uwanjani timu ikawa inafanya vizuri, unapata jeraha na kurudi unakuta timu ipo kwenye kiwango bora.
“Haikuwa rahisi kwa kocha kubadilisha kikosi chake cha ushindi kwa haraka, akawa ananipa muda wa kucheza taratibu, lakini kadiri muda ulivyokuwa unasogea ratiba ya mechi ngumu ikawadia, usisahu wakati huo tulikuwa chini ya kocha Miguel Gamondi ambaye mpira aliokuwa anautaka, ulikuwa hauendani sana na namna mimi nacheza, kocha alikuwa anataka winga ambaye anaupunguza uwanja lakini mimi nilikuwa napenda kucheza pembeni zaidi.
“Nilijifunza mengi kufanya kazi naye. Gamondi alikuwa ni kocha ambaye alikuwa anatambua umuhimu wangu bila kujali changamoto nilizopitia. Unajua kuna wakati vitu vinatokea kama mchezaji unavichukua unajifunza na unaendelea na maisha.
“Haikuwa ishu wanayosema kwamba nilikuwa sina nguvu ya mwili kunisaidia kupambana, hapana, ilikuwa ni suala la majeraha na niliporudi haikuwa rahisi, unajua huwezi kubadilisha timu inayoshinda, Yanga ilikuwa inashinda kila mchezo, ilikuwa ngumu kidogo, tulikuwa wengi tuliokumbana na hali hiyo akiwamo Denis Nkane, hatukupata muda wa kutosha.
HATUA YA KUONDOKA
“Nilikutana na wasimamizi wangu kwa kuwa nilishaanza kuona kama sitaweza kuendelea, nilikaa kikao na kocha pia tukazungumza juu ya mustakabali wa baadaye, nikaona ni muda wa kutafuta changamoto nyingine.
NNE ZILIMHITAJI
“Ukafika wakati nikaanza kutafuta changamoto mpya, nikapokea ofa za kutakiwa kurudi tena Tanzania, Singida ilikuwa ya kwanza na baadaye Coastal Union, lakini nikasema acha nikapate muda wa kupumzika nyumbani, ilikuwa muhimu kurudi kwanza nyumbani kuweka sawa mambo ya familia.
“Baada ya muda nakumbuka ndio ulikuwa wakati kocha Fadlu anakuja Simba, nikazungumza naye, lakini pia Simba wenyewe walinipigia hatukufikia muafaka, baadaye Azam nao wakaja tukazungumza nadhani utakumbuka kuna picha zilitembea nilipokuwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo (Abdulkarim Amin), tulikutana Johannesburg.
MAISHA NJE YA UWANJA
“Kama nilivyosema nilikuwa na wakati mzuri sana hapa Tanzania, maisha ya nje ya uwanja sikukutana na changamoto yoyote, sijutii kitu chochote kwa kuja kwangu ndio maana unaona nimekuja hapa na nina furaha.
“Mimi ni mtu wa familia muda wote kama sipo uwanjani nitakuwa na familia yangu, napenda kutumia muda mwingi kufurahi na familia, nitapika na mke wangu, huwa napenda tupike pamoja, lakini pia tutatoka pamoja, mimi ni mtu wa kupenda kuabudu Mungu, natenga muda wa kwenda sana kanisani, hayo ndio maisha yangu, sijawahi kunywa pombe wala kuvuta sigara.
AZAM FC ILIMPELEKA AS VITA
Baada ya kuondoka Yanga, Skudu akatua pale AS Vita ya DR Congo hapa anaeleza safari ya kufikia huko kumbe ilianzia Azam FC.
“Uamuzi wa kwenda DR Congo naweza kusema ulianzia Azam FC, nilikwambia kabla kwamba nilikuwa nahitajika Azam sasa kocha wao wakati huo alikuwa Youssouf Dabo ambaye baadaye aliondoka Azam na kwenda Vita.
Alipofika kule tuliongea na akanipa mazingira ya anachotaka, ilikuwa heshima kutakiwa na kocha mkubwa kama Dabo ilikuwa ngumu kusema hapana na baadaye tukakubaliana na kwenda huko, nikakutana pia na kocha Bruno Ferry ambao wote walikuwa Azam, kwahiyo mradi ule wa Vita ulinivutia na nikaenda kuungana nao, nilisaini mkataba mfupi tu wa miezi sita ili kila mmoja apate nafasi ya kuridhika na huduma ya upande mwingine.
“Nikiwa pale Vita miezi ya mwisho ya mkataba wangu Wiliete wakaanza kuzungumza na mimi tukaendelea mpaka nilipoachana na Vita na kurudi nyumbani, nilipofika nyumbani Wiliete walikuja na tukamalizana, nilivutiwa nao kwa kuwa ilikuwa ni klabu ambayo inakwenda kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
YANGA HAWA HAPA, ASHTUKA
“Wakati huo sikuwa najua kama tutakutana na Yanga lakini droo ilipofanyika nikashtuka kuona tumeangukia kwa Yanga, nilishtuka sana lakini wachezaji wenzangu hawakuonyesha kushtuka.
“Mimi ndio nikaanza kuwaambia aina ya timu ambayo tutakutana nao, wakaanza kuitafuta kwenye mitandao, nilikuwa na picha nyingi kichwani itakuwaje nakwenda kukutana na timu yangu ya zamani tena.
BRUNO FERRY TENA
“Wakati tunaanza maandalizi ya msimu mpya ghafla nikapokea sapraizi nyingine ya kukutana na kocha Ferry, ambaye kwangu ni kocha wa mbinu sana, tukakutana Wiliete ikawa nafasi nyingine ya kufanya kazi kwa pamoja.
MAISHA YA CONGO
“Maisha ya Congo yalikuwa magumu sana, kwenye mataifa yote ambayo nimeingia na kutoka nadhani Congo nimekutana na ugumu mkubwa wa maisha, sio tu kuhusu miundombinu kiujumla lakini hata maisha ya kijamii, watu wa kule wanakabiliana na changamoto nyingi sana za kimaisha, uchumi wao pia ni changamoto, kitu kilichonishangaza hii ndio nchi inayomiliki madini ya kipekee sana Afrika, lakini uchumi wao na maisha yao hayako sawa, pia vita imechangia sana kuharibu ile nchi, nilifika kule wakati ambao kumetokea machafuko muda mfupi uliopita
“Unaweza kufikiri kwamba mchezaji unafanya mazoezi makali kwa miezi mitatu bila kujua ligi itaanza lini, ilikuwa inasumbua sana lakini nilitumia maisha yale kujifunza kwamba unaweza kwenda sehemu na ukakutana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
VIPI USALAMA WA WACHEZAJI
“Kusema ukweli hakuna mchezaji ambaye niliona amekumbana na vurugu zozote, machafuko mengi yalikuwa yanatokea kwenye mji mwingine ambao uko mbali na Kinshasa ambao tulikuwa tunaishi sisi, baada ya muda mkataba wangu kumalizika niliwaaga, ilikuwa ni uamuzi wangu niliwaambia inatosha, kocha Dabo alitangulia kuniacha kule baada ya kupata nafasi ya kukuza taaluma yake alipokwenda kujiunga na Libya, lakini nikabaki na Ferry.
ISHU YA MGUNDA
“Kama nilivyokwambia haikuwa rahisi kukabiliana na maisha ya Congo, mambo mengi yalikuwa na changamoto, ilikuwa unatakiwa ujiandae sawasawa kiakili, unafanya kazi sehemu ambayo mishahara inachelewa sana, namuelewa (Ismail) Mgunda nadhani aliona arudi sehemu ambayo ana amani nayo.
KUTOLEWA NA YANGA
“Unajua kwamba huwezi kununua uzoefu, Yanga ilituzidi sana kwenye mechi mbili, ilicheza kwa uzoefu mkubwa hii ni timu ambayo asilimia 90 ya wachezaji wake ndio walikuwa wanashiriki mashindano kwa mara yao ya kwanza, angalia namna Pacome (Zouzoua) alichotufanya yaani kosa moja tu likamaliza kila kitu, tulijitahidi kufanya kitu mchezo wa pili lakini bado haikuwa rahisi, tunakubaliana na uhalisia.
DOUMBIA HUYU NI BALAA
“Kuna huyu Doumbia ni mchezaji hatari sana ni fundi kwelikweli, akiwa na mpira ni hatari sana, ana mbinu, anajua sana kupiga pasi, ana uwezo wa kuutengeneza mchezo kama anaangalia kwenye kioo.
YANGA AMEIONAJE
“Nafikiri wamepata wachezaji bora ambao wamewasajili, Doumbia, Andabwile (Aziz), Chikola (Offen) hawa ni wachezaji wazuri sana nimewaona, hata kocha wao naye Romain Folz ni kocha mzuri, namfahamu nimefanya naye kazi Afrika Kusini, naye ananifahamu, najua falsafa zake na kitu ambacho kimenivutia wamefanya usajili huo mzuri ndani ya muda mfupi, ni kama timu mpya kidogo inahitaji kujengwa.
“Unaona kama huu mwanzo timu inacheza namna hii, muda utakavyosogea itakuwa hatari sana haitaweza kuzuilika kirahisi bado hawajafika kucheza kwenye ubora wao wa juu, wakifika huko itakuwa balaa.”
Akizungumzia hatua ya mashabiki kutokukubali kiwango cha timu yao sambamba na kocha wao Folz, Skudu anapingana na hoja hiyo akisema: “Hapana. Kama nilivyosema ndio kwanza timu zinatoka kwenye maandalizi ya msimu. Kuna mtitiriko wa ukuaji, kuna muda utafika utatakiwa kucheza kwa kiwango cha juu na huo muda sio Yanga pekee timu nyingi bado hazijafikia, huwezi kufikia kucheza kwa kiwango cha juu ukiwa ndani ya mechi 10 za kwanza.
“Yanga ambayo tumekutana nayo ina kikosi cha ushindani sana na kwa ratiba ambayo wanayo na ‘rotesheni’ wanayofanya kuanzia kwenye mechi za ligi mpaka Ligi ya Mabingwa nadhani kocha ana kikosi kipana ambacho anaweza kukiunganisha, nadhani wana nafasi kubwa ya kupasua na kufika mpaka makundi, sina wasiwasi na hilo kabisa.
AMPA MAUA HERSI
“Ukiangalia hii timu imepoteza wachezaji wake bora ambao wameondoka, sijamuona Khalid Aucho, Clatous Chama, Aziz KI, Kennedy Musonda, lakini unaona bado kuna ubora mkubwa kama vile hajaondoka mtu, kwanza kwenye hili lazima nimpongeze rais wa Yanga injinia Hersi Said, yeye ni zaidi ya kiongozi. Akili yake itaendelea sana kusumbua timu nyingine, ukiona namna anavyoweza kuongea na wachezaji unagundua kuna akili kubwa inatumika. Mimi nimeishi Yanga najua namna akili ya huyu mtu anapofikiria juu ya ubora wa wachezaji. Yanga kuwa juu ni akili yake kubwa namna analikabili jambo juu ya klabu hii.
“Angalia namna wachezaji walioingia, unajua huwezi kumpata Aucho mpya, huwezi kupata Aziz KI mpya wala Skudu, lakini unachoweza kupata ni mtu wa daraja lilelile kwa mtindo tofauti, wameongeza ubora ili timu iendelee kuwa bora kwahiyo huu usajili umefanyika kwa ubora sana.
LIGI YA TANZANIA
“ Ligi ya Tanzania kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, naipongeza sana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwa juhudi zao za kuifanya ligi ya Tanzania kuwa ligi kubwa Afrika, kuna ushindani mkubwa pia ndani ya ligi utaona klabu kama Simba, Yanga, Singida, Azam zinafanya vizuri sana kwenye mashindano ya Afrika, ubora wa timu hizo peke yake unajieleza kwenye mengi juu ya ubora wa ligi ya hapa.
FADLU KAMSHTUA
“Kocha Fadlu namfahamu lakini sikuwahi kufanya kazi naye, nakumbuka alikuwa Raja Athletic akiwa kama kocha msaidizi akachukua ubingwa kisha akaja kujiunga na Simba, alianza kubadilisha mambo mengi ndani ya timu hiyo na kufika hata fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na hayo yote yalitokea ndani ya mwaka mmoja.
“Niliposikia ameondoka Simba, nilishtuka kwa kuwa sikuona labda anapitia wakati mgumu, baada ya siku chache nikamuona amerudi Raja, unajua maisha ya soka yako hivyo lakini kitu cha msingi hapa nadhani ameiacha Simba ikiwa kwenye eneo salama kuendeleza pale alipoishia, kuna mbegu amepanda ambazo zikiendelea kutunzwa zitazalisha mambo mazuri kwa Simba.”
ASOMEA UKOCHA
Ukitazama mwili wa Skudu unaweza kusema labda ana miaka 27 lakini jamaa ameshafikisha miaka 35 na bado haonekani kuzeeka na bado anasema anataka kuendelea kucheza huku akifichua kwamba ameshaanza kusomea ukocha.
“Bado nataka kuendelea kucheza kwa kuwa bado miguu yangu inaubeba mwili wangu vizuri, kuna wakati huwa najikuta nafurahi, kila sehemu ninayokwenda watu wananiuliza una umri gani, nawajibu “35”, halafu wanashangaa wananiambia naonekana kijana sana.
“Yanga walivyokuja Angola, nilikutana na Makamu wa Rais, Arafat (Haji) akaniambia kila akiniona anaona kama narudi kuwa kijana, kwahiyo bado nitaendelea kucheza. Lakini pia nimeshaanza kusomea ukocha, nimeshamaliza kupata leseni ya Daraja C la Uefa na sasa naanza kupambana na daraja B, najiandaa mwenyewe kwa maisha ya baadaye, nasomea hatua ya pili ya kuwa video analyst pia.
SWAHIBA WAKE YANGA
“Nilipokuwa Yanga rafiki yangu mkubwa alikuwa Maxi Nzengeli lakini pia nilikuwa karibu pia na Farid Mussa na Denis Nkane, kuna Bakari (Mwamnyeto) nisiwasahau Aucho (Khalid) na Kennedy (Musonda).
UJUMBE WAKE
“Tanzania kuna vipaji, tatizo kubwa hawataki kucheza soka nje ya Tanzania, nawashauri waongeze juhudi kusaka timu za nje ya Tanzania kama wageni wanavyokuja Bongo.”