Siri ya timu zikipanda kutodumu Ligi Kuu

New Content Item (3)
New Content Item (3)

MBEYA. JANA katika mfululizo wa makala haya ya Ripoti Maalumu ya Ligi ya Championship tuliona namna klabu nyingi zinavyopata tabu kwenye ishu za usafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Ilieleza pia jinsi bajeti ndogo inavyoziangusha timu hizo na leo katika kuhitimisha tunaangalia mkwamo unaozikuta baadhi ya timu zinapopanda Ligi Kuu Bara...Ebu tiririka nayo...!


PANDA SHUKA
Kwa kuangalia misimu saba kuanzia mwaka 2015 timu nane zimepanda na kushuka daraja huku sababu zikionekana ni uwepo wa maandalizi mabovu kwa timu na kuwepo kwa viongozi wasiojua soka.
Msimu wa mwaka 2015/16 African Sports ilipanda na msimu uliofuata ikashuka, msimu wa mwaka 2017/18 Majimaji FC na Njombe Mji zikapanda na msimu uliofuata zikashuka, African Lyon ilipanda msimu wa mwaka 2018/19 na ikashuka msimu uliofuata.
Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2018/19 msimu uliofuata ikashuka daraja, Ihefu FC zilizopanda msimu wa mwaka 2020/21 msimu uliofuata zikashuka daraja na Mbeya Kwanza ilipanda msimu uliopita na msimu huu ipo Championship.


TATIZO NINI?
Aliyekuwa Katibu wa Njombe Mji, Baraka Ambakisye anasema sababu kubwa iliyowafanya wapotee kwenye ramani ni maandalizi mabovu ambayo yaliifanya timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2017/18 na kushuka msimu wa mwaka 2018/19.
"Timu ilikuwa na wachezaji wazuri lakini mwisho wa siku hatukuweza kutekereza vyema maslahi ya wachezaji ambao mwisho wa siku hawawezi kufanya vyema kazi yao.
"Soka ni ajira ambayo watu huendesha maisha yao kupitia mishahara yao lakini unapoanza kuweka maneno mengi bila vitendo ndipo tulipoanza kushindwa kuiendesha timu," anasema Ambakisye.
Anasema timu nyingi zinakuwa hazijajiandaa kwaajili ya kucheza Ligi Kuu hasa kwa kuwepo na viongozi ambao hawana msingi wa uongozi wa soka na mwisho wa siku timu inaumia.
Ambakisye anasema haamini kwenye suala la uzoefu sababu kama timu imepanda Ligi Kuu inakuwa imejiandaa na wanatakiwa kuwa na 'pre season' nzuri lakini mwisho wa siku unakuwa na wachezaji ambao hawapo kiushindani.
"Unajua kuna kuupenda mpira na kuuongoza mpira lakini pale kwetu tulikuwa na viongozi ambao hawana maadili na kuwabagua baadhi ya wachezji hivyo na kujenga matabaka yaliyochangia kuiangusha timu.
Timu haikuwa na wadhamini wa kutosha kujiendesha ndio maana Njombe Mji ilifika wakati walishindwa kuwalipa wachzaji mishahara na fedha zao za usajili wengi hawakumaliziwa.
"Mwamko ulikua mdogo kwa watu katika kuisapoti timu yao sababu ya baadhi ya viongozi walitumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe kuliko timu na mwisho wa siku wadau wakajiondoa."
Mwenyekiti wa Mbeya Kwanza, Mohamed Mashango anasema kilichowaangusha wao hadi kushuka daraja hawakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto ambazo zingewafanya kumudu kwenye ligi.
"Tulikuwa na wachezaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) lakini hawakuwa bora kwa Ligi Kuu hivyo hawakuweza kuhimili changamoto za ligi.
Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila anasema Ihefu haikujiandaa vyema kwenye ndio maana hawakufanya vizuri na mwisho wa siku wakajikuta wanarudi walikotoka.
"Ligi Kuu kunahitaji uvumilivu mkubwa wa wachezaji unaokuwa nao lakini hilo kwetu halikuwa hivyo na tulipokuja kushtuka tayari tumeshachelewa na ligi ipo ukingoni."


USIMBA, UYANGA
Ambakisye anasema sababu nyingine iliyoiangusha Njombe Mji ni kuwepo kwa viongozi ambao ndani yake walikuwa wanazitazama zaidi timu zao za Simba na Yanga kuliko Njombe Mji.
"Inakuja timu hapa lakini unaona Njombe Mji inakwenda kucheza na kikosi cha kawaida sana, mfano tulienda kucheza Shinyanga FA halafu wachezaji wengine walibaki Njombe na bado viongozi wanaona sawa.
"Inakuja Yanga unaona viongozi wa Njombe Mji wapo 'bize' na Yanga kuliko Njombe Mji yenyewe. Uzalendo haukuwepo sababu maadili ya kazi lazima utumikie sehemu unapofanyia kazi.
Ambakisye anasema ndani ya timu hiyo walikuwa na watu kutoka mikoa mbalimbali lakini mwisho wa siku mtu anajionyesha wazi yupo Simba au Yanga kuliko Njombe Miji na ukifuatilia ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa kwenye timu.


BENCHI LA UFUNDI
"Mfano unaweza ukawa na daktari ambaye hana utaalamu wa kutosha wa kuhudumia timu, kocha wa viungo ambaye hayupo sawa katika kuiandaa timu na kuna makocha nao sio wazuri katika suala la kuwaweka sawa wachezaji kwenye mambo ya saikolojia.
"Kuna wakati tulikuwa na kocha Ali Bushiri ambaye enzi zake alikuwa kipa, lakini kwetu akawa kocha wa timu na mara nyingi yeye alikuwa anatazama zaidi semu ya 'goal keeping' kuliko timu nzima." anasema Ambakisye.
Mashango anasema wengi wanashindwa kutofautisha ubora wa madaraja ya ligi hivyo timu inapopanda Ligi Kuu na kujiona ilikuwa bora ilikotoka basi wanamawazo hayo na huko iendako itakuwa bora bila kuwa na maandalizi ya kutosha.
"Benchi la ufundi lazima liwe bora zaidi ya kule ulikotoka hivyo Mbeya Kwanza kikubwa kilituangusha ni uzoefu mdogo na mbaya zaidi tulibaki na wachezaji wengi tuliokuwa nao FDL tukijenga matumaini kwamba uzoefu waliokuwa nao chini hata juu watakuwa bora kumbe sivyo maana tunacheza vizuri lakini hatupati matokeo na unakuja kushtuka tayari ligi inakwisha."
Daniel Kirai aliyekuwa katibu wa Gwambina anasema wao moja ya vitu vilivyowaangusha ni pamoja na suala la benchi la ufundi katika kutimiza majukumu yake.
"Unajua haya mambo kila mmoja mwacheza acheze katika nafasi yake, kocha, kiongozi na mchezaji kila mmoja akifanya jambo lake kwa usahihi timu inakuwa bora lakini kwetu kuna mahali tuliyumba.
Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila anasema kama uongozi baada ya kupanda msimu huu na kuanza ligi vibaya wakaona kuna dalili mbaya ambayo ingewarejesha Championship hivyo wakatumia nguvu kubwa kuboresha kikosi kwenye dirisha dogo la usajili.