SIO ZENGWE: Wachambuzi wana lugha za mazingaombwe

NAIKUMBUKA katuni moja ilitoka zamani inaonyesha jinsi wanasiasa walivyo na lugha za mazingaombwe. Katuni hiyo inamwonyesha mwanasiasa mmoja akiwa jukwaani na mkononi ameshikilia chupa.

Hata hivyo, akawashangaza watu pale alipouambia umati uliofurika mkononi mwake ameshika glasi. Watu hawakuamini alichosema na picha ya pili inaonyesha watu wakiguna kwamba; "Haiwezekani tuone chupa halafu tuambiwe ni glasi!"

Picha ya tatu inaonyesha yule mwanasiasa ameshatambua kuwa ule umati haukubaliani na alichosema na hivyo kuungana nao, huku akiendelea kushikilia msimamo wake wa awali.

Alisema; “Ndio, hii ni chupa, lakini unaweza kuitumia kama glasi!”

Aliwaacha watu hoi maana amekubaliana na msimamo wao kuwa alishokishika mkononi ni chupa lakini akaendelea kushikilia uongo wake wake, ni glasi.

Ndiyo mwelekeo ambao wachambuzi wetu wameamua kuuchukua.

Kwanza kabisa hakuna anayewalazimisha kutabiri matokeo ya mechi za klabu zetu kwa kuwa utamaduni wa soka unajulikana duniani kote. Soka ndiyo unaoongoza kwa kutotabirika duniani.

Ndiyo maana mchezo huu umevutia kampuni nyingi za ubashiri wa matokeo na vikorombwezo vingine vilivyoko ndani, yaani kama timu itakayotangulia kufunga, timu zote kufunga, sare au vitu vingine kibao.

Hata hivyo, utabiri wa matokeo ya mechi ni sehemu ndogo sana ya uchambuzi na ndiyo maana wale manguli wa uchambuzi hujiepusha sana na kutabiri matokeo, hasa zinapocheza timu ambazo hawakuzichezea enzi za ujana wao au hawazishabikii.

Uchambuzi wa mechi ambayo itachezwa huzingatia mambo mengi muhimu, kama umuhimu wa mchezo huo kwa pande zote, matokeo ya mechi za karibuni, uwezo wa wachezaji binafsi, mbinu za kocha, hali ya wachezaji kama ni majeruhi au wana kadi pamoja na watakaoziba nafasi zao na sehemu ambayo mechi inachezwa kutokana na umuhimu wa mashabiki.

Kwa mchambuzi ambaye atazingatia hayo na mengine muhimu kwa mechi, hatakuwa na haja ya kusema timu gani itashinda kwa sababu uchambuzi wake utatoa picha ya hali ya mchezo utakavyoisha na hivyo msikilizaji au mtazamaji kubakia na jibu lake mwenyewe.

Mara nyingi, mtu anapochambua kwa kuangalia vitu hivyo nilivyovitaja hapo juu na vingine muhimu, huweka tahadhari na jambo fulani likienda hivi, basi uwezekano mkubwa jingine likaenda hivi. Yaani hajipi uhakika mechi itakwenda hivi na itaisha hivi kwa sababu mambo mengi yanaweza kubadili mazingira na matokeo kuwa tofauti kabisa na matarajio ya wengi.

Hakuna aliyetarajia Mamelodi Sundowns angeondolewa kwa kuruhusu mabao mawili nyumbani baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini, ikiwa imepoteza wachezaji wawili kwa kadi nyekundu.

Ukifuatilia mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, huwezi kujua nini kilitokea. Lakini ndio hivyo, beki akajikuta akiutumbukiza mpira golini wakati Mamelodi ikihitaji sana kulinda uongozi wa mabao 2-1.

Ndivyo mchezo wa soka usivyo na adabu. Ikitokea mchambuzi akaapa timu fulani itashinda, hawezi tena kutumia mazingira yaliyobadilika kama hoja ya kutetea utabiri wake pale matokeo yatakavyokuwa tofauti na alivyotabiri.

Mwenendo huu wa kutabiri umezidi kukua nchini. Kila mtu aliye kwenye redio anadhani kutabiri ndio kuwa mchambuzi mzuri. La hasha! Kuna wanaoamini kwa sababu redio sasa zinazingatia zaidi hadhira iliyopo mtandaoni, You Tube, wachambuzi wengi wameamua kujitoa ufahamu kwa ajili ya kutengeneza views nyingi ama kujipatia umaarufu.

Kwamba, kama kuna mechi kubwa ambayo inafuatiliwa na wengi, kitu pekee kinachoweza kumpa umaarufu ni kujihusisha na mchezo huo kwa kutabiri matokeo ambayo hayafikiriwi na wengi. Kwa hiyo anaamua kusema “hapo ndio mwisho wao”. Au anatabiri timu fulani itashindwa na haitasonga mbele.

Lugha za mazingaombwe huja pale utabiri wao unapokwenda tofauti na matokeo. Wapo wawili waliosema ‘eti’  walitoa utabiri huo ili kuihamasisha timu icheze vizuri zaidi na kushinda. Kweli?

Hivi hizi timu zinahitaji wachambuzi kuhamasishwa ili zicheze vizuri? Hivi kazi ya wachambuzi ni kuhamasisha? Kwa hiyo uchambuzi wao huwa ni wa uongo? Au basi wamegeuka kuwa vitengo vya uhamasishaji vya timu?

Najua yapo maswali mengi kuhusu tabia hiyo ya utabiri inayozidi kukua.

Wapo ambao wanatetea utabiri wao kwa kugeuzageuza maneno. Lakini hakuna aliyewalazimisha kutabiri na hivyo hakuna sababu ya kusumbuka hadi kuanza kutumia lugha za mazingaombwe.

Sheikh Yahya Hussein alikuwa akitabiri mambo mengi ya kitaifa na kidunia na sehemu kubwa ya utabiri wake haikuwa kama alivyofanya. Lakini hakuna aliyemlaumu wala kumzongazonga kwa kuwa watu walijua Sheikh Yahya hakuwa mchambuzi bali mtabiri wa mambo yanayoweza kutokea. Utabiri wake haukutokana na kuchambua hali ya kiafya ya viongozi na baadaye kuibuka na utabiri kiongozi mmoja mkubwa atafariki mwaka huu. Kwa sababu kifo hakitokani na magonjwa pekee, bali hata ajali ambazo ni ngumu kuchambua na kuibuka na majumuisho hizo ajali zitaua kiongozi mmoja mkubwa nchini au duniani.

Kwa hiyo hawa wachambuzi wangekuwa ni watabiri kama Sheikh Yahya, hakuna ambaye angewalaumu kwa kuwa wangekuwa wanazungumzia kitu chenye uwezekano wa kutokea au kutotokea.

Lakini mtu ambaye anatumia stadi za kisayansi kuchambua hali ya timu na kuibuka na majumuisho yanayoonyesha timu moja itashindwa, huyo hana budi kulaumiwa au kusakamwa pale mambo yanapokwenda tofauti.

Hali ni tofauti kwa watabiri wa hali ya hewa. Hawa hutumia sayansi kuchambua mienendo mbalimbali ya hali ya hewa duniani na kutabiri uwezekano wa kimbunga kikubwa, mvua kubwa au za rasharasha. Lakini kwa sababu mazingira hubadilika kila baada ya muda, watu hawa hutoa taarifa zinazoonyesha mabadiliko hayo na hivyo uwezekano wa kuwepo mvua kubwa au za rasharasha kutoweka.

Hawa wenzetu, hawakai na wachezaji wakati wote, hawaendi mazoezini kufuatilia mwenendo wa maandalizi na wala hawana viashiria vyovyote vinavyoonyesha mabadiliko katika maandalizi na hivyo hali inaweza isiwe kama walivyotabiri.

Lakini bado wanashikilia msimamo wao hadi baada ya mechi. Eti wanaangalia rekodi za nyuma pekee, timu moja haijawahi kukubali kipigo nyumbani au si rahisi kwa timu kutoka eneo moja la bara kuitoa timu ya eneo la Arabuni.

Mpira hauko hivyo. Mpira unachezwa na binadamu ambaye wakati wote anafikiria afanye nini zaidi kuboresha alichokifanya jana. Mpira hutegemea mambo mengi kiasi kwamba si rahisi kutabiri kesho utakuwaje.

Cha muhimu zaidi; kwani kuna ulazima wa kutabiri?

Wachambuzi wakiendelea hivi, basi hizi lugha za mazingaombwe hazitaisha. Watabaki kusema walitabiri ili kuihamasisha timu au kufafanua kimiujiza kile walichokisema wakati wa kutabiri.

Kama wanadhani kutabiri ni muhimu na utabiri wao umekwenda kinyume mara kadhaa, basi wamekuwa bidhaa adimu kwa kampuni za michezo ya kubahatisha ambazo watu wengi wakikosea kubeti, kwao ni faida kubwa. Kwa nini wasichukue ajira huko?