SIO ZENGWE: Tusisubiri kukejeli, La Liga wanawatoa wengi

WAKATI huu kila mmoja anasubiri kwa hamu kushuhudia maendeleo ya makubaliano ya Yanga na Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, kuhusu mageuzi ya kiuendeshaji wa klabu hiyo ya Dar es Salaam.

Yanga inataka iondokane na mfumo wa sasa wa uendeshaji ambao ni wa kiridhaa sana na kuingia mfumo wa kisasa utakaoiwezesha klabu hiyo kujiendeleza kwa kutumia fursa nyingi zinazoizunguka na hivyo kuacha utegemezi wa uwezo binafsi wa mtu mmoja mmoja au wafadhili.

Hamu hiyo ya kushuhudia mageuzi hayo imegawanyika; wako wanaosubiri kwa hamu kuona mpango huo ukikwama ili wakejeli, kudhihaki na kutumia nafasi hiyo kuonyesha ubovu wa viongozi wa Yanga na wako wanaosubiri kuona mafanikio ili yaiwezeshe klabu kuanza kujiendeleza kwa njia za kisayansi tofauti na hali ya sasa ambayo ni ya kubahatisha.

Hali kama hiyo iko kwa watani wao wa jadi, Simba ambako wapinzani wa mageuzi tayari wanakebehi mabadiliko wakitumia kutoingizwa kwa Sh20 bilioni kama hoja ya kudhihirisha hakuna kinachofanyika, huku upande mwingine ukitumia mafanikio ya uwanjani kama hoja ya kuonyesha mageuzi yanasaidia.

Ndivyo tulivyojijengea utamaduni wa kufurahi kufeli au kutumia mafanikio kukera wanaopinga au kuhoji badala ya kuyatumia kuwaelewesha ili wote wawe kwenye mtumbwi mmoja.

Hiyo ni katika ngazi ya klabu. Mageuzi kama hayo yanatakiwa yawe yanafanyika katika ngazi za vyama, yaani Ligi Kuu ya Vodacom kwa ngazi ya kitaifa na vyama vya mikoa hadi wilaya.

Ni kwamba huwezi kuwa na klabu ambazo zimepiga hatua katika kuweka maendeleo ya kisasa, wakati unayezisimamia uko nyuma kiuendeshaji.

Hivi sasa La Liga imeingia makubaliano na Ligi Kuu ya Ukraine kufanya kazi pamoja kuendeleza soka.

Makubaliano hayo yalisainiwa mwanzoni mwa mwaka huu, Ukraine ikiwakilishwa na Ievgen Dykyi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ligi Kuu na La Liga ikiwakilishwa na Oscar Mayo, ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo kimataifa.

Makubaliano yataanzisha mawasiliano baina ya ligi hizo mbili ya kubadilishana ujuzi wa uongozi, uendeshaji taasisi kubwa (corporate governance), uongozi wa michezo, masuala ya televisheni na ya masoko.

Makubaliano hayo yanaitaka La Liga kutoa mwongozo wa jinsi ya kuendeleza mashindano ya Ligi Kuu ya Ukraine, uanzishaji wa maudhui mapya na mikakati ya kidigitali kwa ajili ya kutangaza soka la kulipwa la Ukraine duniani.

Pia pande hizo mbili zitashirikiana katika harakati nyingine kama kubadilishana ujuzi kwa kuendesha makongamano na mikutano kwa ajili ya kuzipa klabu za Ukraine ufahamu kuhusu mbinu zinazotumiwa na La Liga, mafunzo na semina zinazolenga majukumu tofauti kwa klabu za Hispania na Ukraine ili kuhamasisha zibadilishane taarifa zitakazoziwezesha kukabili changamoto tofauti katika soka.

Pia zitaziwezesha klabu kukabiliana na mambo kama uharamia wa chapa za klabu na kupambana na ubaguzi wa rangi na kuimarisha soka la watoto.

La Liga imewezesha hayo kutokana na kumtumia mwakilishi wao aliye Ukraine, Jesus Pizarro, kama ilivyo na mwakilishi wake hapa Tanzania ambaye anafanya kazi kubwa ya kuitangaza chapa hiyo.

Maeneo yaliyotajwa katika makubaliano ya Ukraine na La Liga ni yale ambayo bado yanatusumbua sana hapa Tanzania. Bado akili yetu iko viwanjani kusaka mafanikio, lakini hatuangalii timu zinafikaje huko viwanjani ambako tunasubiria mafanikio.

Hatufikirii hao wachezaji tunaowaona uwanjani wameishije hadi kufikia siku ya kwenda uwanjani. Hatufikirii hao wachezaji wamewezaje kuvaa jezi wanazotumia kwenye hizo mechi, na kikubwa zaidi hatufikirii walisajiliwaje na wanawezaje kumudu maisha yao hadi mechi zinafika wanaenda uwanjani na baada ya mechi wanarudi nyumbani.

Haya yote yanahitaji uwezo wa kisayansi wa kuyashughulikia. Na kwa kuwa wapo wenzetu ambao walishafanya uchunguzi na kupata dawa, hakuna haja ya kupoteza muda kufanya uchunguzi. Kinachotakiwa ni kuchukua yale yanayotufaa katika matokeo ya uchunguzi wao na kuyaweka katika mazingira yetu.

Ndivyo inavyofanya Ligi Kuu ya Ukraine na ligi nyingine zote katika dunia yetu, kuendeleza uendeshaji wa mashindano yake.

Sidhani kama Tanzania tunaweza kuepuka kufuata nyayo hizo. Bodi ya Ligi inatakiwa iamke sasa na kuangalia washirika wanaoweza kuisaidia kuendesha mashindano yake, ambayo ni Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Wapangaji wa mipango ya maendeleo ya ligi hizo wanahitaji stadi za kisayansi na kisasa kufanikisha mipango yao, wanahitaji stadi za kusimamia, stadi za kutathmini na stadi za kutangaza mashindano.

Haya mambo hayawezi kuja kwa kubahatisha, bali kutafuta kutoka kwa wale waliotutangulia.

Anaweza kujitokeza mjinga mmoja akauliza, “wewe ulifanya nini wakati ukiwa pale (TFF)?” Ndio ujinga wetu.

Tukiachana na ujinga huo, La Liga na wengine wana mengi ya kutusaidia tukiwatafuta.