SIO ZENGWE: Simba isitafute suluhisho la tatizo hewa

Tuesday May 10 2022
Simba PIC
By Angetile Osiah

BAADA ya Simba kuondolewa kwa mara nyingine katika hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu ya Afrika, kumekuwepo na maneno, kejeli, dhihaka na ushauri kuhusu nini kifanyike.

Wengi wanasema Simba inapaswa kusajili wachezaji wenye hadhi ya kushinda mechi za ushindani mkubwa barani Afrika, eti kwa sababu kikosi cha msimu huu hakikuwa na wachezaji wenye uwezo wa kuifikisha mbali.

Wako wanaoamini kuwa ilitolewa kwa bahati mbaya na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mechi za robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Hao pia waliamini hivyo ilipotolewa na Kaizer Chiefs kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Wako wanaodhani kuwa uamuzi mbovu ndio uliosababisha Simba iondolewe mwaka jana na mwaka huu. Na wapo wengine wengi wenye mitazamo tofauti.

Unaweza kuamini kuwa baadhi wako sahihi na wengine hawako sahihi. Lakini inabidi kufanya tathmini ya kina.

Wakati fulani kiongozi mmoja wa vigogo wa soka Afrika alisema haoni Simba ikifika mbali Afrika, licha ya uzuri wa timu kwa kuwa ‘kwa sasa ndio wako katika hatua ya kuandika historia’ na si kuweka historia.

Advertisement

Hakuwa mbali na ukweli. Ili timu iingie katika orodha ya vigogo Afrika ni lazima ipitie hatua kadhaa ambazo kila moja ionaongeza ujuzi fulani wa jinsi ya kupambana.

Hivyo ni jukumu la viongozi kuyaona mafundisho hayo na kufanya marekebisho kulingana na mahitaji ya wakati huo.

Sioni Simba ilikosa nini kwa aina ya wachezaji iliokuwa nao, kocha, benchi la ufundi, fedha na uongozi, lakini naona uzoefu, utamaduni na ujuzi wa ushiriki wa michuano hiyo katika ngazi za juu ndio uliokosekana.

Uzoefu haujengwi kwa kutafuta wachezaji wazoefu, bali kujifunza katika kila hatua na urithishaji wa uzoefu kutoka kizazi kimoja hadi kingine au kundi moja hadi jingine. Kuna timu ambazo mtunza vifaa amekaa klabuni kwa zaidi ya miaka 15.

Huyu anaweza kuonekana si muhimu, lakini anakuwa ana uzoefu wa nini huwa kinafanyika wakati wa mechi kubwa kwa upande wa maandalizi ya nje ya uwanja. Mazungumzo yake ni muhimu katika kuwapa viongozi picha ya nini kinatakiwa kufanyika kwa wakati huo na mazingira hayo kulingana na yaliyotokea huko nyuma.

Wapo wengi wa aina hiyo wanaoweza kuchangia mawazo ya nini kifanyike.

Kuna ule utamaduni wa kutaka timu iahirishiwe mechi za nyumbani eti kwa kuwa inatetea taifa. Hii ni Imani ya hovyo ambayo inatakiwa iachwe mara moja. Cha muhimu ni kuomba tofauti ya siku angalau tatu kati ya mechi ya Afrika na ndani.

Hii humkunisha kichwa kocha; kwamba apumzishe nani na amjaribu nani katika mechi za ndani. Sioni tofauti kubwa katika vikosi vya Simba vinavyocheza mechi za Ligi Kuu, Kombe la Azam wala michuano ya Afrika. Unategemea nini kwa wachezaji hao kama si uchovu? Wakipumzika muda mrefu wataweza kupambana kwa kiwango cha juu cha utimamu wa kimwili kwa mechi?

Kwa nini timu ishinde mechi za nyumbani tu na ishindwe ugenini tena wakati mwingine kwa idadi kubwa ya mabao? Hili linaonekana kujengeka akilini mwa wachezaji kwamba kufungwa ugenini si tatizo.

Lakini yale mambo yha moto Afrika Kusini, ni tatizo ambalo huenda ni kubwa sirini ila lilikuwa halionekani. Mambo yale huvuruga saikolojia ya wachezaji kiasi cha kudhani kuwa dawa itafanya kazi hata kama hawatajituma ipasavyo.

Najua yapo mengi tofauti na yale ya aina ya wachezaji, lakini wacha niishie hapo leo. Cha msingi ni kwamba kuna matatizo halisi yanayotakiwa kushughulikiwa kuliko hayo hewa yanayozungumzwa kwa nguvu zote.

Advertisement