SIO ZENGWE: Prof. Nasreddine Nabi ameweza

KATIKA mechi mbili zilizopita kabla ya Jumamosi, kipa anayeonekana kudhihbirisha kuwa namba moja katika kikosi cha Yanga, Djigui Diarra, hakuwepo kikosini kutokana na majukumu ya kitaifa ya nchini kwao, Mali.

Akiwa katika majukumu ya kimataifa, Abdallah Mshery alishika nafasi yake na aliruhusu bao moja tu.

Si Diarra peke yake, kiungo Stephane Aziz Ki, beki wa kulia, Djouma Shaaban walikosa mechi takriban tatu kila mmoja, huku nahodha Bakari Mwamnyeto akiingia na kutoka kikosini, na Feisal Salum akikosa mechi ya Jumamosi kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Waliosalia, baadhi walikuwa kama Mwamnyeto. Yaani Tuisila Kisinda, Gael Bigirimana, Dennis Nkane, Dickson Ambundo, Ibrahim Bacca, Farid Mussa na Herritier Makambo, huku baadhi wakianza katika baadhi ya mechi na wengine kupewa dakika chache za mwishoni.

Ndivyo ambavyo Kocha Mtunisia, Nasreddine Nabi amekuwa akipanga na kupangua kikosi chake tangu alipokabidhiwa mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Na si kuwatumia na kutowatumia tu, bali hata kuwabadilisha nafasi baadhi ya wachezaji pale kunapokuwa na umuhimu huo. Wakati ameingia tu kuifundisha Yanga, Nabi alikumbana na tatizo la beki wa kushoto. Mustafa Yassin alikuwa amepata majeraha. Jibu lilikuwa rahisi tu; nafasi ya Mustafa ingeshikwa na David Bryson, ambaye pia anatumia guu la kushoto. Lakini jibu hilo halikuwa kichwani mwa Nabi. Badala yake akamchukua Kibwana Shomari kutoka benchi na kuanza kumchezesha kushoto.

Wengi hawakutarajia, lakini Kibwana alicheza kwa kujiamini na ikaonekana ni kama abakie hukohuko hata Yassin akipona. Kibwana alipoumia, jibu likawa rahisi tena kwa kuwa Yassin alishapona majeraha.

Nabi hakutaka jibu hilo. Alimrudisha Farid Mussa kucheza beki ya kushoto na mhitimu huyo wa soka la vijana akalipa fadhila kwa kocha wake. Akaonekana mtamu zaidi kwa kuwa mbali na kuzuia, alikuwa akiongeza idadi ya watu wakati wa kushambulia.

Msimu mpya ulipoanza, Joyce Lomalisa alishapatikana na hivyo kuonekana kuwa tatizo la beki wa kushoto limeshaisha. Lakini Nabi aliona dawa kamili bado haijapatikana. Ni kama alimtaka afanye jitihada za kuingia kikosi cha kwanza na si kuingia kwa sababu alitafutwa kwa udi na uvumba. Inaonekana sasa ameshamwamini, lakini kwa utamaduni ambao Mtunisia huyo ameuonyesha, hilo halitamhakikishia Lomalisa namba ya kudumu.

Upande wa kulia pia amekuwa akizungusha wachezaji. Mara kadhaa Dickson Job amekuwa akipewa jukumu la kucheza kulia pale kunapoonekana kuna matatizo kwa mabeki tegemeo wa upande huo.

Kwa kutazama kwa juujuu unaweza kusema bado Nabi hajapata mabeki pacha wa kati. Kuna wakati ilionekana kama Mwamnyeto na Job wameshajihakikishia namba katika nafasi hiyo. Lakini, mara kadhaa Mwamnyeto ameshaanzia benchi huku Yannick Bangala akiungana na Job kucheza nafasi hizo mbili. Na siku hizi, taratibu ameanza kumchezesha Bacca huku nahodha akianzia nje.

Kubadilika mara kwa mara kwa mabeki wa kati pia hugusa sehemu ya kiungo mkabaji. Bangala hulazimika kuacha kucheza mbele ya mabeki na kwenda kuongoza safu ya ulinzi na hivyo Khalid Aucho kurejea au Biigirimana na Zawadi Mauya kushika nafasi hiyo au hata Fei Toto kurudi nyuma kucheza mbele ya mabeki. Mara nyingine unakuwa hata huelewi nafasi hiyo itajazwa na nani.

Hali ni kama hiyo kwa washambuliaji wa pembeni; Bernard Morrison, Kisinda, Jesus Moloko, Ambundo na Nkane ambao wamekuwa wakiingia na kutoka, ingawa Morrison amekuwa akipata nafasi zaidi, akifuatiwa na Moloko.

Mchezaji pekee ambaye hajabadilishiwa majukumu wala nafasi ni Fiston Mayele, ambaye siku zote amekuwa akicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, na anapohitajika kupumzika, basi Makambo hupewa hizo dakika 10 au 15 za mwisho, au mechi ambazo Mcongo huyo hawezi kucheza kabisa au siku ambayo Nabi ameamua kumpumzisha kutokana na uchovu au majukumu ya mechi zinazofuata.

Hivi karibuni ameanza kumpa nafasi, Clement Mzize kama mshambuliaji wa kati na tayari mchezaji huyo amelipa fadhila kwa kufunga bao dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa, pengine ni kutokana na mazingira au staili yake, Nabi ametumia misimu miwili aliyokuwa nchini kujenga kikosi kipana ili kunapotokea upungufu wa wachezaji wa nafasi fulani, tayari awe na mtu ambaye atamudu hata kama nafasi hiyo si aliyoizoea.

Sasa Nabi anaonekana ana kikosi kipana, lakini ukiangalia kwa makini na ukifuatilia vikosi vinavyoanza katika mechi tofauti, unaona dhahiri upana huo ameutengeneza. Upana haujatokana na kundi kubwa la wachezaji ambao unaweza kusema ni bora, bali wenye ubora uliotengenezwa kulingana na mahitaji yake na aina ya mchezo anayoitaka.

Wapo wanaosema Yanga bila ya Mayele si lolote katika ufungaji, lakini Mzize aliwashtua watu kwa kiwango chake dhidi ya Kagera na hakuna shaka kuna ushindani mkali sasa kati ya Makambo na Mzize, ambaye anaonekana kuwa na kasi ya kuingia kikosi cha kwanza akitumia vyema urefu na kasi yake.

Ukosefu wa kikosi kipana ndio uliomgharimu Zinedine Zidane kutwaa ubingwa wa La Liga katika msimu wake wa mwisho. Alikuwa na mtihani mkubwa wakati nyota wake tegemeo, Luca Modric, Toni Kroos, Carvajal, Sergio Ramos na Karim Benzema wakiwa majeruhi na wengine wakizidiwa na uchovu; awatumie katika mechi muhimu za mwisho za La Liga au awahifadhi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Mwishoni alilazimika kuwapumzisha na hivyo kuchukua baadhi ya wahitimu wa Castilla washike nafasi hizo. Alipoteza ubingwa wa Hispania lakini akafanikiwa Ulaya. Hakuwa na kikosi kipana licha ya kuwa na rundo la washambuliaji kama Rodrigo, Mariano Diaz, Fede Velvede, ambao alikuwa hajamwaamini. Hakuwa ametengeneza kikosi kipana, ambacho leo Carlo Anceloti amekijenga kwa kutumia wachezaji walewale akiongoza wachache sana. Kwa hiyo, katika soka la kisasa ule mtindo wa kupumzisha wachezaji (rotation) pekee hautoshi kujenga kikosi kipana, bali pia kubadilisha majukumu au nafasi kwa baadhi ya wachezaji ndiko hufanya timu kuwa tayari kila wakati.

Ipo mifano mingi duniani ya kuwabadilishia wachezaji majukumu ili kocha anufaike na uzoefu na ustadi wa mchezaji. Kwa hiyo, Nabi ana nafasi na heshima yake katika kujenga kikosi kipana. Nina uhakika kuna wachezaji wengi ambao aliwataka lakini haikuwezekana, hivyo njia pekee ambayo ingeweza kumfanya awe na matokeo mazuri ni kujenga kikosi kipana.

Leo hii Yanga inashangilia mechi ya 49 –sawa na Arsenal—bila ya kupoteza, lakini huenda hawajui hiyo unbeaten imetengenezwa na asilimia karibu 70 ya kikosi kizima kilichosajiliwa. Ni wachache ambao hawaoni nafasi.ha kwanza. Kwa kuwa wengi wanaonja, tena baadhi kwa nafasi tofauti na zile zao za asili, hali ya kujiamini inakuwa kubwa na kocha anazidi kupata matokeo anayohitaji.

Kikosi kipana si kuwa na wachezaji wengi bora, bali kuwafanya wawe bora na tayari kulingana na wakati.