Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya Osimhen inavyowapa moyo vijana choka mbaya

OSIMHEN Pict

Muktasari:

  • Hadithi ya “kutoka kwenye umasikini hadi utajiri” ni kitu kinachobainisha simulizi nzuri ya kuvutia kuhusu maisha ya mshambuliaji wa Kinigeria, Victor Osimhen.

LAGOS, NIGERIA: WANASEMA kuzaliwa masikini ni jambo moja, lakini kufa ukiwa masikini ni jambo jingine.

Hii ni kauli inayohamanisha mapambano katika kujikwamua kimapato na kiuchumi.

Hadithi ya “kutoka kwenye umasikini hadi utajiri” ni kitu kinachobainisha simulizi nzuri ya kuvutia kuhusu maisha ya mshambuliaji wa Kinigeria, Victor Osimhen.

Washambuliaji wa kiwango chake, miongoni mwa bora zaidi duniani, mara nyingi hujua mapema mafanikio yao ya kitaaluma ni jambo lisiloepukika.

Lakini kwa Osimhen, mwenye miaka 27, ilionekana kana kwamba dunia nzima ilikuwa dhidi yake alipokuwa akijaribu kugeuza kipaji chake kuwa taaluma.

Pauni 250,000 kwa wiki anazolipwa sasa katika klabu kubwa ya Uturuki, Galatasaray S.K., ni jambo ambalo nafsi yake ya utotoni isingeweza hata kulifikiria.

Osimhen na ndugu zake sita waliishi katika chumba kimoja huko Olusosun, mtaa wa mabanda uliopo Lagos, Nigeria, karibu na dampo kubwa zaidi la taka barani Afrika.

Maisha yake magumu yalianza mapema alipompoteza mama yake akiwa bado mtoto mdogo. Baba yake alikuwa dereva aliyepoteza kazi, kisha akapata ajira ya kuosha vyombo katika jiko la kituo cha polisi.

Kwa kuwa kipato hicho hakikutosha kulipa kodi, Osimhen alilazimika kwenda katika dampo la taka kutafuta viatu vya mpira vilivyotupwa ili aweze kucheza soka.

Katika mahojiano na jarida la The Players' Tribune, aliwahi kusema: “Nakumbuka usiku mmoja nilipokuwa na takriban miaka 12, mwenye nyumba alichoka. Akakata umeme katika nyumba yetu.

“Tulikuwa tumekaa gizani katika chumba kimoja sisi saba, hakuna televisheni, hakuna chochote.

OSIM 07

“Nilitoka nje nikakaa karibu na mtaro wa maji taka, halisi kabisa mtaro, nikaanza kulia. Nikatazama juu angani nikamuuliza Mungu, ‘Maisha ya aina hii ni ya mtoto kweli?’”

Hali ilikuwa mbaya kiasi Osimhen alilazimika kuacha kucheza soka kwa muda ili kusaidia familia yake kujikimu.

Anajieleza kama mpambanaji aliyekuwa akiuza chupa za maji kwenye taa za barabarani kwa madereva, kufanya kazi ndogondogo kwa mchungaji maarufu huko Lagos, kushuka kwenye visima kufanya kazi hatarishi na hata kushiriki katika kipindi cha maswali na majibu Nigeria na alishinda kiasi kinacholingana na Pauni 5 moja kwa moja kwenye runinga.

Osimhen alikumbuka: “Hiyo ndiyo ilikuwa pesa nyingi zaidi kuwahi kushika mikononi mwangu wakati huo. Kama kulikuwa na pesa za kupatikana, nilikuwa hapo.

“Kila nilichopata nilikabidhi kwa ndugu zangu ili wanunue chakula na kulipa kodi.

“Usiku mwingi nililala kanisani. Nyumba yetu haikuwa hata na paa la kutosha. Ilikuwa inaanza kubomoka.”

OSIM 02

Hivyo ndivyo safari yake ya maumivu ilivyoanza, safari iliyomgeuza kutoka kijana wa mitaani hadi kuwa nyota wa kimataifa.

Soka lilianza kurejea polepole katika maisha ya Osimhen, ingawa hadi alipofikisha umri wa ujana wa kati, alikuwa akicheza tu katika timu ya kanisa la mtaani kwao.

Baada ya kushindwa kuwavutia makocha wa timu ya vijana chini ya miaka 17 ya Nigeria kwenye majaribio ya kwanza na kulia njiani wakati anarudi nyumbani, alijiamini kujaribu tena mara ya pili kwa msaada wa rafiki wa mtaani aliyekodisha gari kwa safari ya saa tisa.

Osimhen alikuwa miongoni mwa mamia ya vijana waliokuwa wakitafuta nafasi, lakini alitumia vyema dakika 15 alizopewa kwa kufunga mabao mawili.

OSIM 03

Ilikuwa ni baada ya daktari wa timu kumwambia kocha kijana aliyekuwa anarudi polepole kwenye gari lake akidhani amekataliwa tena, ndiye aliyefunga mabao hayo mawili, ndipo aliporejeshwa kambini.

Alisema: “Kama daktari wa timu asingefanya hivyo, leo nisingekuwa mchezaji wa soka. Labda ningekuwa nafanya kazi kwenye visima.”

Osimhen aling’ara kwa kufunga mabao 10 katika mechi saba wakati Nigeria ilipotwaa Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 mwaka 2015, mafanikio yaliyomletea zawadi ya maelfu machache ya pesa, kiasi kidogo, lakini kilichobadilisha maisha yake.

Aliongeza: “Maisha yangu yalibadilika haraka sana. Niliwapigia simu dada zangu na kuwaambia, ‘Nawahamisha kutoka nyumba ya chumba kimoja kwenda ya vyumba viwili. Kila kitu kimeshughulikiwa. Ninachowaomba tu ni kuniweka kwenye maombi yenu.”

Maelfu hayo yaligeuka kuwa mamilioni pale aliposajiliwa na VfL Wolfsburg mwaka 2017.

OSIM 04

Alisema “alirukaruka na kupagawa kwa furaha” pesa zilipoingia kwenye akaunti yake ya benki, alipiga magoti na kumshukuru Mungu.

Osimhen alicheza mechi 16 bila kufunga bao kwa upande wa klabu hiyo ya Ujerumani, lakini alivutia macho ya Lille OSC baada ya kufunga mabao 20 akiwa kwa mkopo katika klabu ya Ubelgiji, Royal Charleroi S.C., msimu wa 2018-19.

Msimu wake wa mabao 13 katika Ligue 1 akiwa katika miaka yake ya mapema ya ishirini uliishawishi SSC Napoli kulipa ada ya uhamisho iliyovunja rekodi ya klabu mwaka 2020.

Hata hivyo, kabla tu ya uhamisho huo kukamilika, alikumbwa na pigo jingine la maumivu baada ya kumpoteza baba yake na kutokana na hali yake ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa klabu yake, hakuweza kurudi nyumbani kwa wakati kumuaga.

OSIM 05

Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Mnigeria huyo, ambaye alikata tamaa kabisa kuhusu namna soka linavyoendeshwa.

Anasema: “Nakumbuka nilitupa simu na nikachanganyikiwa kabisa. Niliharibu vitu vyote ndani ya nyumba. Nilivunja kila kitu. Nilikuwa nje ya akili yangu. Kelele ziliwafanya majirani waje kuniangalia.

“Nilijiuliza, ‘Kama huu ndiyo mpira wa miguu, basi kuna maana gani? Nataka tu kuwa na familia yangu."

“Niliporudi nyumbani, nilihisi huenda nisicheze tena soka. Nilichukizwa sana na kila kitu.”

Kocha wa wakati huo wa Napoli, Luciano Spalletti, alimchukua chini ya uangalizi wake na kumsaidia kurejea kwenye mstari sahihi.

OSIM 06

Na Osimhen akalipuka kwa kufunga mabao 26 ya ligi na kuivunja laana ya miaka 33 ya Napoli kutoshinda taji la Serie A katika msimu wa 2022-23.

Baadaye uhusiano kati yake na klabu uliharibika, lakini Osimhen ameendelea kufumania nyavu Uturuki, ambako anaendeleza hadithi yake ya mafanikio isiyotarajiwa na kuthibitisha kwa vijana wanaokulia katika mazingira magumu kila kitu kinawezekana.

Osimhen alieleza: “Nataka kuwa chanzo cha hamasa kwa watoto waliokulia mazingira kama yangu. Tuko mamilioni.

“Watoto wanaopaswa kufanya kazi ili kupata mlo wao unaofuata. Kuuza maji barabarani. Kuchimba kwenye dampo kutafuta kitu cha kuuza. Kupambana. Kuota ndoto. Kuomba. Kwa neema ya Mungu, niliweza kufanikiwa.”