Simu moja tu, unanasa saini zao fasta

Muktasari:

  • Hata hivyo, wachezaji ambao hawana timu yoyote kwa sasa, bado wana nafasi ya kujiunga na klabu hizo licha ya dirisha kufungwa.

LONDON, ENGLAND: USIKU wa Ijumaa, Agosti 30 ulishuhudia dirisha la usajili wa wachezaji la majira ya kiangazi likifungwa kwa timu za England.

Hata hivyo, wachezaji ambao hawana timu yoyote kwa sasa, bado wana nafasi ya kujiunga na klabu hizo licha ya dirisha kufungwa.

Na hakika kuna mastaa kibao wenye vipaji vya hali ya juu kabisa wanaweza kupatikana bure kabisa kwenye kipindi hiki ambacho dirisha la uhamisho wa mastaa limeshafungwa.

Baadhi ya mastaa hao wanaopatikana bure, yamo majina makubwa kabisa yatakayokonga nyoyo za mashabiki wa Ligi Kuu England kwa kwenda kujiunga na timu zao.

Kuna mastaa wa maana kabisa na wenye vipaji vikubwa kwa sasa hawana timu, wakishindwa kunaswa na timu nyingine hadi dirisha limefungwa. Kwenye orodha hiyo ya mastaa, wapo kwenye thamani kubwa kabisa inayokaribia Pauni 80 milioni.

Mastaa wakubwa kabisa waliotamba kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, akiwamo winga wa zamani wa Fulham, Chelsea na Arsenal, Willian na beki kisiki wa zamani wa Liverpool, Joel Matip ni miongoni tu mwa wachezaji ambao hawana timu kwa sasa na unaweza kuwapata bure.

Straika wa zamani wa Manchester United, Anthony Martial naye hana timu na kuungana na wachezaji wengine matata kabisa, akiwamo mchezaji mwenzake wa zamani huko Old Trafford, Memphis Depay, ambaye amekuwa akihusishwa na klabu ya Rayo Vallecano.

Wakali wa zamani wa Nottingham Forest, Serge Aurier na Keylor Navas nao kwa sasa hawana timu, sambamba na beki wa kati, Sergio Ramos, naye yupo sokoni kutafuta timu mpya na anapatikana bure. Simu moja tu.

Beki mwingine makini kabisa, Mats Hummels naye anatafuta timu mpya ya kuichezea msimu huu baada ya kuachana na Borussia Dortmund mwishoni mwa msimu uliopita.

Staa wa Euro 2024, Adrien Rabiot, mwenye thamani ya Pauni 30 milioni sokoni, lakini kiungo huyo hana timu kwa sasa baada ya kuachana na Paris Saint-Germain. Kwenye kikosi cha kwanza kinachoweza kuundwa na wachezaji waliohuru kwa sasa, Rabiot kwenye sehemu ya kiungo anaweza kucheza pacha na Dele Alli.

Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa England kwa sasa anafanya mazoezi kwenye kikosi cha Everton kujiweka fiti, lakini hana timu baada ya mkataba wake kwenye timu hiyo ya Goodison Park kufika ukomo mwishoni kwa msimu uliopita.

Kwenye fowadi ya kikosi hiki, kuna huduma ya straika wa zamani wa Sevilla, Wissam Ben Yedder. Hakika, thamani ya kikosi cha kwanza cha mastaa wanaoweza kupatikana bure, thamani yake sokoni inakaribia Pauni 80 milioni.

Idadi ya wachezaji wanaoweza kupatikana bure hata kwenye kipindi hiki ambacho madirisha ya usajili yamefungwa huko kwenye Ligi Kuu za Ulaya, inafanya uwezekano wa kutengeneza kikosi kingine matata kabisa. Kikosi kingine, kinaweza kuwa na kipa wa zamani wa Liverpool na Newcastle United, Loris Karius.

Sambamba na kipa huyo, kikosi hicho pia kinaweza kuwa na wakali wengine wenye majina makubwa kabisa kama John Egan, Cheikhou Kouyate na Patrick van Aanholt kwenye safu ya ulinzi, wakati Brandom Williams na Victor Moses watacheza kwenye wing-back.

Kiungo wa zamani wa Arsenal, Francis Coquelin atajiunga na Etienne Capoue na Steven Alzate kwenye eneo hilo la katikati ya uwanja.

Kwenye eneo la ushambuliaji kutakuwa na huduma ya Andre Ayew na Eric-Maxim Choupo-Moting, ambaye ameachwa na Bayern Munich mwishoni mwa msimu uliopita. Mastaa wote hao wa maana kabisa bado wanaweza kusajiliwa na klabu za Ligi Kuu England kwa sasa licha ya dirisha la usajili kufungwa tangu Ijumaa iliyopita ya Agosti 30. Simu moja tu, inatosha kuwanasa.