Simba, Yanga waliogopana kwa Mkapa

Kiungo wa Simba Jonas Mkude, katikati ya Khalid Aucho na Feisal Salum wa Yanga akitoa pasi katika mchezo wa Kariakoo Derby iliyochezwa jana katika Uwanjan wa Benjamini Mkapa.
WALE jamaa wa Kariakoo wakamaliza mechi hakuna mbabe. Kama nilivvoandika Jumatano iliyopita katika safu ya ‘Ubishi wa Mzee wa Kaliua’ haiji mechi kubwa nchini kuizidi mechi ya Simba na Yanga.
Ipo ipi nyingine? Haipo. Hata wakija Al Ahly kucheza na Simba au Yanga bado haipewi ukubwa sawa na wanapokutana Simba na Yanga. Mechi ya Simba na Yanga ikiisha sare kelele zinapungua mtaani. Kwa kiasi fulani utulivu unapatikana wakitoshana nguvu.
Hii iliisha kwa sare mbaya zaidi kwa washambuliaji - sare tasa. Sare tasa huwapa sifa walinzi zaidi kuliko washambuliaji.
Ndiyo maana haishangazi sana kuwaona watu wakiyataja majina ya mabeki kama wachezaji bora zaidi wa mchezo. Joash Onyango, Henock Inonga, Bakari Mwamnyeto na Shomari Kibwana ni kati ya wachezaji kadhaa walioibuka kuwa nyota wa dabi ya taifa.
Hili lilitokana na woga uliojaa katika vifua vya wachezaji wa timu zote mbili hasa viungo. Viungo ambao kwa kawaida wanategemewa wahusike zaidi katika kupika mashambulizi. Walichagua kutumia nguvu kubwa zaidi kulinda kuliko kushambulia.
Hakukuwa na sababu yoyote ya msingi kufanya hivi zaidi ya woga wa kutotaka kuruhusu bao. Huu woga ulififisha mashambulizi. Mpira mwingi ulichezwa kwa usalama katikati ya uwanja. Ni hii sababu iliwapa mabeki nafasi ya kujidai kwasababu hawakuwekwa katika nyakati ngumu na viungo waliokuwa wakipika mashambulizi.
Ndipo hapo Onyango na Inonga walifanikiwa kumuweka ‘gerezani’ Fiston Mayele. Upande wa pili wa uwanja Mwamnyeto na pacha wake Dickson Job walifanikiwa ‘kumpiga pingu’ Meddie Kagere.
Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Bernard Morrison ambao walipaswa kuwa karibu zaidi na washambuliaji wao walijikuta wakicheza mechi ya peke yao isiyohusisha washambuliaji wao. Hapa ndipo sifa ya Shomari Kibwana ilipoibuka baada ya kutembea na kufanikiwa kumsimamisha Morrison.
Hii ikiwa ni mara ya pili anafanya hivyo baada ya kufanikiwa kummeza katika pambano lililopita la ligi ambalo Zawadi Mauya aliwapa Yanga ushindi mwembamba wa bao moja.
Ushahidi mwingine wa ukosefu wa mashambulizi ya kutosha ni kutazama kazi waliyoifanya makipa wote wawili. Lango la Aishi Maunula lilikuwa matatani mara moja tu muda wote wa mchezo kama ambavyo ilikuwa kwa Djigui Diarra.
Shuti la Sadio Kanoute alilolifuta vyema Diarra na mpira wa Saido Ntibazonkiza uliogonga mwamba wa pembeni kisha ukamrudia Mayele aliyekuwa eneo la kuotea. Hakukuwa na nafasi zingine za wazi zilizotengenezwa ambazo zingeweza kuwa mabao.
Labda kosa alilolifanya Manula la kukosea kutoka langoni kisha mpira ukamvuka na kunaswa na Mayele aliyezuiwa na Onyango kuupasia mpira wavuni linaweza kuhesabika kama nafasi ambayo ingestahili kuwa bao. Vinginevyo hakukuwa na nafasi nyingine.
Zaidi tunaweza tukawa tumeushuhudia mwisho wa Pascal Wawa na Simba. kwa muda mrefu Simba wamekuwa hawamtazami kwa jicho zuri sana Wawa. Mwisho wa msimu uliopita jina lake liliwekwa kwenye kilengeo kwamba lazima aondoke na hawakuwa tayari kumuongezea mkataba, lakini kocha aliyekuwepo Didier Gomes alisisitiza kwamba bado anamhitaji. Simba walimuongezea mkataba kwa shingo upande.
Katika mechi hiyo mabeki wa katikati wa Simba waliibuka mashujaa wa mchezo kwa sababu nilizozieleza awali. Hicho kinaweza kuwa kitasa cha ‘exit’ kwa Wawa ndani ya Msimbazi na mara nyingi mechi za Simba na Yanga zinatumika kutoa hukumu za ajabu. Ni mechi hii ambayo iliwaaminisha Yanga kwamba wanaweza kumuacha Kelvin Yondani na kucheza na Said Makapu kwa sababu kama hiyo Simba wanaweza kumpa talaka Wawa.
Mtu mwingine anayepitia wakati mgumu kama Wawa ni kiungo wa DR Congo, Tonombe Mukoko. Eneo la kati la Yanga bado linaonekana kuwa salama chini ya daktari wa mpira kutoka Uganda, Khalid Aucho na Mkongomani Yanick Bangala. Ni mechi ya pili ya dabi Yanga wanacheza bila Mukoko. Bahati mbaya ni kwamba hadi mashabiki wao hawamkumbuki kwa sababu wanaocheza nafasi yake wanafanya vizuri. Ndiyo maana haishtui kuona viongozi wa Yanga hawaumizi kichwa kuufikiria mkataba wake unaoelekea mwisho kwasababu wanafahamu hata akiondoka bado watakuwa salama.