Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba SC wana kazi si mchezo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wamekuwa na mwenendo wa kusuasua msimu huu kutokana na aina ya matokeo wanayopata kulingana na misimu minne iliyopita.

Simba wapo nafasi ya pili wakiwa wamecheza mechi 12, wameshinda saba, sare nne, kufungwa mmoja, wakifunga mabao 14, kufungwa matano wana pointi 25. Wapo nyuma pointi 10 dhidi ya watani zao, Yanga.

Kutokana na mwenendo wa matokeo mabaya kuna mambo kwenye maeneo mbalimbali yanachangia hilo.


WAHUSIKA

Mwenendo mbaya wa mastraika wa Simba kina Meddie Kagere, Chriss Mugalu na John Bocco unachangia.

Simba wamecheza mizunguko 12 na Kagere ndiye kinara wa ufungaji wa mabao katika kikosi hicho akiwa na manne - wastani wa bao moja kila baada ya michezo minne.

Jambo baya zaidi kwenye mizunguko 12, Mugalu na Bocco licha ya ubora na uwezo mkubwa waliona kufunga hakuna aliyefunga hata bao moja.


MECHI YA PILI

Kikosi hicho licha ya kutengeneza nafasi za kufunga kwenye michezo miwili iliyopita na kutumia mastraika watatu na wachezaji wengine wenye uwezo wameshindwa kupata hata bao moja.

Simba imecheza mechi mbili sawa na dakika 180, dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar lakini imeshindwa kuzifunga. Sio jambo la kawaida timu iliyo na wachezaji bora eneo la ushambuliaji kushindwa kufunga hata bao moja.


MECHI 12

Katika misimu minne iliyopita iliyopita Simba ilichukua ubingwa mfululizo hakuna hata mmoja walifikisha mizunguko 12 ya ligi wakiwa wametoka sare nne.

Msimu uliopita hadi kumaliza mizunguko 34 walikuwa wametoka sare tano, jambo ambalo msimu huu linaweza kuvunjwa kama Simba wasipobadilika.


SILAHA ZAO

Simba msimu uliopita mastaa wao walikuwa moto na muda wote unawaona katika viwango bora uwanjani jambo ambalo kwa sasa halipo.

Ukiachana na Luis Miquissone aliyeweza kuamua mechi mwenyewe kutokana na uwezo wake wa kufunga, kutengeneza nafasi na kuhusika kwenye mabao muhimu ambaye kwa sasa hayupo na Clatous Chama aliyerejea dirisha dogo la usajili, mastaa wengine wapo. Sio kama Simba walitakiwa kubaki na Luis aliyetimkia Al Ahly, bali walitakiwa kupata mbadala sahihi. Msimu uliopita wachezaji wa timu pinzani pindi walipokutana na Simba walikuwa na wakati mgumu kuzuia silaha za Msimbazi wakati huo akiwemo Luis mwenyewe, Chama, Rally Bwalya, Mugalu, Bocco, Kagere na wengineo.

Kutokana na wachezaji wengi wa Simba kushindwa kuonyesha ubora msimu huu wapinzani wao wamekuwa wakiamini wanacheza na timu ambayo lolote linaweza kutokea.


UBORA WA YANGA

Wakati Simba walipokuwa wanapitia wakati mgumu na kusuasua kupata matokeo mazuri msimu uliopita kikosi cha Yanga hakikuwa kwenye ubora kama ilivyo msimu huu.

Hata hivyo, ilikuwa rahisi Simba kufanya vibaya na kurejea mchezoni ikiwemo kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi kutokana na Yanga kutokuwa na kikosi cha kutisha kama ilicho nacho msimu huu.

Yanga ya wakati huo ilikuwa na wachezaji wa kawaida kama Yikpe Gnamien, David Molinga, Sadney Urikhob na wengineo wengi wa namna hiyo.

Msimu huu Simba wana mlima mkubwa wa kupanda ili kutetea ubingwa kutokana na kuimarika kwa Yanga yenye wachezaji wengi bora kama Fiston Mayele, Khalid Aucho, Djuma Sha-bani, Djugui Diarra na wengineo.


USAJILI WAO

Simba kwenye dirisha kubwa la usajili walisajili mastaa 12 na walionekana kufanya vizuri ni watatu kama si wanne ambao ni Henock Inonga, Kibu Denis, Saido Kanoute na Pape Sakho.

Wengine wamekuwa na viwango vya kawaida na hata kushindwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kiasi cha kuamua kuachana nao dirisha dogo.

Kushindwa kufanya vizuri kwao kuliwafanya mabosi wa Simba kutumia nguvu nyingi kumrudisha Chama kikosini kutoka RS Berkane ya Morroco.

Wakati Simba wakiendelea kusota kwa usajili walioufanya na kushindwa kufanya vizuri, Yanga ni tofauti kwani nyota wao wengi wapya wapo moto.


BENCHI LA UFUNDI

Mabadiliko matatu yaliyofanyika katika benchi la ufundi Simba yamechangia kikosi hicho kutokuwa na mwenendo unaoridhisha. Simba walianza msimu na Didier Gomes aliyeondoka na kikosi kilibaki chini ya Hitimana Thierry aliyefanya vizuri kwenye mechi alizokuwa kaimu kocha mkuu.

Baada ya muda mfupi, Pablo Franco akapewa mikoba akifanya kazi na wasaidizi wake Hitimana na Selemani Matola, lakini ndani ya muda mfupi Simba waliachana na Hitimana.

Wakati Simba wakisuasua kwenye eneo hilo Yanga kuna Nesreddine Nabi aliyepewa usaidizi wa kutosha kutoka kwa kocha mwenye uelewa wa soka la Tanzania, Cedrick Kaze na kama haitoshi wamemleta aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Milton Nienov ambaye alimtengeneza Aishi Manula kuwa bora zaidi.


BWALYA, MORRISON BADO

Wakati msimu unaanza Simba miongoni mwa wachezaji waliobaki wakitegemewa kufanya makubwa wapo ni Rally Bwalya na Benard Morrison.

Bwalya alitegemewa kuziba pengo la Chama kutokana na aina yake ya uchezaji wakati Morrison alionekana kuwa mbadala wa Luis. Wote wawili wameshindwa kufanya ambacho wengi walifikiria licha ya kupata nafasi ya kucheza michezo mingi.


KOCHA SIMBA

Aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma anasema kikosi hicho kimepoteza ari ya kujiamini kutokana na aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakiyapata.

Djuma anasema kuna Simba alikutana na hali kama hiyo na alichofanya ni kuwajenga kiakili wachezaji ili kujiamini.

Anasema Simba waliondoka wachezaji wawili muhimu Luis na Chama ambaye amerejea na bado kikosi chao kina wachezaji wenye uwezo ambao wakirudisha morali ya kushindana watafanikiwa.