Prime
Simba CAFCC na maajabu ya 1993

Muktasari:
- Timu hiyo imetinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Al Masry katika mchezo wa robo fainali ulioisha kwa ushindi wa mabao 2-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2, kwani ilipoteza ugenini pia kwa kufungwa 2-0.
SIMBA imekata mzizi wa fitina. Imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kusota kwa muda mrefu.
Timu hiyo imetinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Al Masry katika mchezo wa robo fainali ulioisha kwa ushindi wa mabao 2-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2, kwani ilipoteza ugenini pia kwa kufungwa 2-0.
Mabao ya Ellie Mpanzu na jingine la Steven Mukwala yaliiweka Simba katika nafasi nzuri ya kufuta gundu lililodumu kwa misimu sita ikikwamia hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF kuanzia Ligi ya Mabingwa hadi hiyo ya Shirikisho tangu 2018-2019. Kama hujui kabla ya mechi hiyo dhidi ya Al Masry, Simba ilishacheza robo fainali nne za Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 sambamba na moja ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2021-2022, huku 2019-2020 ikitolewa mapema.
Matokeo iliyopata Simba imeiweka katika nafasi nzuri ya kurejea tukio ililowahi kulifanya mwaka 1993, ilipofika fainali ya Kombe la CAF (haipo kwa sasa) na kupoteza mbele y Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0 ikiwa nyumbani baada ya suluhu ya ugenini
Kwa sasa Simba imepangwa kukutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo iliing’oa na kuivua taji waliokuwa watetezi wa taji hilo, Zamalek pia ya Misri, Wekundu hao wakianzia nyumbani kisha kumaliza mchezo wa mwisho ugenini.

Mshindi wa jumla ya pambano hilo atatinga fainali na kukukutana ama na RS Berkane ya Morocco au CS Constantine ya Algeria waliomaliza kama vinara wa Kundi A, iliitangulia Simba iliyoshika nafasi ya pili.
MAAJABU YA 1993
Unaweza kudhani ni utani, ila yale maajabu ya yaliyotokea 1993 wakati Simba ikitinga nusu fainali ya Kombe la CAF (michuano iliyokuja kuunganishwa na Kombe la Washidi Afrika mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika) yametokea tena.
Ndio, kama hujui ni kwamba katika michuano hiyo iliyotokana na Kombe lililotolewa na aliyekuwa Mwanasiasa na Mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Cheif Moshoodi Abiola (sasa marehemu) mwaka 1992 na Simba ilitinga nusu fainali kwa kuing’oa klabu kutoka Afrika Kaskazini kama ilivyotokea msimu huu kwa Al Masry.
Simba iliitungua USM El Harrach ya Algeria kwa kuifunga jumla ya mabao 3-2, ikianza na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), kisha kwenda kulala ugenini 2-0 na kuwashangaza Waalgeria.
Kilitokea mwaka huo wa 1993 ni kama tu ilivyotokea msimu huu kwa Simba kuwaduwaza Wamisri ambao waliambulia penalti moja tu kati ya tatu ilizopiga baada ya kipa Moussa Camara wa Simba kupangua mikwaju miwili ya Al Masry kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kazi aliyoifanya Camara ni kama tu ilivyokuwa kwa 1993, wakati kipa Mohammed Mwameja alipofanya kazi kubwa kuikatili Al Harrach akiivusha Simba hadi nusu fainali.
Katika mechi ya kwanza nyumbani iliyopigwa Septemba 5, mabao mawili yalifungwa na Edward Chumila na jingine la Abdul Ramadhan ‘Mashine’ na kuihakikishia Simba tiketi ya nusu, licha ya kulala 2-0 ugenini iliporudiana na Al Harrach Septemba 18, 1993.
YATUPWA COSAFA
Ushindi huo wa 3-2 ulioivusha Simba hadi nusu fainali, uliifanya ipangwe kukutana na timu ya Atletico Sport Aviacao (ASA) ya Angola ambayo ni klabu kutoka Ukanda wa Soka wa Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Kumbuka tu, msimu huo Aviacao ilikuwa ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya CAF iliyokuwa ndio kwanza ina msimu wa pili tangu ilipoasisiwa 1992 na iliitoa Gor Mahia ya Kenya kwenye robo kwa penalti 4-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa 0-0.
Haitofautiani kabisa na msimu huu, kwani Simba sasa imepangwa kukutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambao ni klabu kutoka Ukanda wa Cosafa pia, lakini ikiwa imeshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza. Stellenbosch iliiduwaza waliokuwa watetezi, Zamalek kwa kuitungua kwa bao 1-0 ziliporudiana majuzi jijini Cairo, baada ya awali kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza. Kama ilivyokuwa mwaka 1993 kwa Simba kuanzia nyumbani dhidi ya Aviacao, ndivyo ambavyo hata safari hii itakavyokuwa, ikipangwa kuikribisha Stellenbosch Aprili 20 nchini kisha kwenda kurudiana nao wiki moja baadae ugenini.

KINACHOSUBIRIWA
Katika mechi ya kwanza nyumbani iliyochezwa Oktoba 17, 1993, Simba ilipata ushindi wa mabao 3-1, mawili kupitia tena Chumila na jingine lililokuwa la pili la kujifunga, huku bao la kujifuta machozi la Aviaco likifungwa na Nello.
Timu hizo zilipoenda kurudiana Oktoba 31, Simba ikiwa ugenini ililazimisha suluhu na kutinga fainali. Katika mechi zote mbili, kazi kubwa ilifanywa na kipa Mwameja aliyeokoa michomo mikali ya kina Otis Mongaa Libengue ‘Libengue’, Keleki wa Keleki, Lolo, Maneco, Manuel Domingos Martin ‘Manuel’, Mariano, Miramba, Nzinga Lubusa, Nello na Yanda, huku kipa Kanka Vemba akijaribu kuipigania timu bila mafanikio kuwazuia Wekundu isivuke.Mwameja aliwakatisha tamaa Waangola wakiwa kwao, kiasi mashabiki wa timu hiyo kufikia hatua ya kumrushia mawe na takataka nyingine zilizosababisha mara kadhaa pambano hilo kusimmishwa, na dakika 90 ziliiisha kwa Aviacao iking’oka kwa mabao 3-1.
Kwa sasa mashabiki wa Simba wanaipigia hesabu ya kutaka kuiona timu hiyo ikitinga fainali na hata ikiwezekana kubeba ubingwa, ili kumaliza gundu lililozindama timu za Tanzania katika michuano ya CAF tangu ilipoanza kushikiriki mwaka 1968. Kama Simba itavuka mbele ya Stellenbosch na kutinga fainali itakuwa imefikia rekodi ya Yanga ambao msimu wa 2021-2022 walifika hatua hiyo kwa kuvaana na USM Alger ya Algeria na kulikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini. Yanga ilipoteza nyumbani mabao 2-1, lakini ikaenda kushinda ugenini jijini Algiers kwa bao 1-0 lililotokana na na penalti ya aliyekuwa beki wa timu hiyo, Djuma Shaban na kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2 na wenyeji kutawazwa mabingwa wapya. Simba itaendeleza maajabu hayo ya 1993 kwa kuing’oa Stellenbosch ya Afrika Kusini?

KIKOSI KILIVYOKUWA
Simba iliyotinga fainali za Kombe la CAF 1993 kilikuwa chini ya Kocha Abdallah ‘King Mputa’ Kibadeni na Etenne Eshente raia wa Ethiopia aliyekuwa kocha msaidizi, huku meneja wa timu akiwa ni Abdulrahman Muchacho.
Nyota wa kikosi hicho walikuwa ni pamoja na makipa Mohammed Mwameja, Mackezie Ramadhan na Offen Martin, Kassongo Athuman, Razack Yusuf ‘Careca’, George Masatu, Seleman Pembe, Fikiri Magosso, Idd Seleman ‘Meya’ a.k.a Nyigu na George Lucas ‘Gazza’. Wengine ni Abdul Ramadhan ‘Mashine’, Damian Kimti, Ramadhan Maufi ‘Lenny’, Edward Chumila, Dua Said, Malota Soma ‘Ball Juggler’, Twaha Hamidu ‘Noriega’ , Deo Mkuki, Godwin Aswile ‘Scania’, Hussein Masha ‘Smart Boy’, Abuu Omar, Joachim Masumbuko, Nico Kiondo, Bakar Idd ‘Beka Jo’, David Mihambo, Mbuyu Yondani, Michael Paul ‘Nylon’, Thomas Kipese ‘Uncle Tom’, Feruzi Teru na Rashid Abdallah.