Prime
Sikiliza hadithi ya Eddie Nketiah na Bwana Saddick
WAKATI mwingine inaanza kwa ujanja wa mbali ambao hauwezi kuuelewa kiurahisi. Inaanzia kwenye mazungumzo ya kijanja yaliyopangwa baa au hotelini katika chakula cha usiku. Huwa inachekesha kidogo katika nyakati kama hizi.
Mwandishi wa michezo kutoka Afrika, Saddick Adams ameripoti kwamba mshambuliaji wa England mwenye asili ya Ghana, Eddie Nketiah yupo tayari kuiwakilisha Ghana katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika mwakani kule Marekani, Canada na Ghana.
Adams kaandika mahala, “Nketiah kwa sasa ametulia, ana miaka 26 na amepevuka vya kutosha na yuko tayari kutoa kila alichonacho kama Ghana ikimpigia simu sasa hivi. Amesema ana damu ya Ghana ipo katika mwili wake na hauwezi kuhoji kuhusu asili yake.”.
Niliishia kucheka. Vitu vingine havitokei bahati mbaya. Ni usela wa mjini. Mipango tu. Unakuta Nketiah amemsaka Saddick na kumualika kwa chakula cha usiku katika mmoja kati ya migahawa maarufu London. Inaweza kuwa mgahawa wa Bocconcino Mayfair, Tattu, Scarlett au mwingine wowote ule.
Mpango ni namna gani anaweza kuweka historia ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia kupitia taifa la asili yake, Ghana. Nketiah ana asili ya Ghana. Wamekaa wakapika mpango wao. Kwamba ionekane yalikuwa mazungumzo ya kawaida tu kati ya Nketiah na Saddick.
Baadaye Saddick akapewa mlungula aipeleke habari katika gazeti la The Sun la hapohapo Uingereza. Lengo ni kujaribu kuamsha hisia za Waghana kuanza kuvutika na hisia za Nketiah kuwa mshambuliaji wao katika michuano ya Kombe la Dunia wakati huu wakisheherea Ghana kutinga Kombe la Dunia.
Haya ni maisha ya nyuma ya pazia ambayo shabiki wa kawaida hawezi kuyafahamu. Na sasa limeanza kuwa jambo la kawaida kwa wanasoka wenye asili ya Afrika ambao wamezaliwa Ulaya. Likikaribia Kombe la Dunia wanataka kurudi nyumbani kwa sababu hawana ubora wa kutosha wa kuchezea timu za mataifa ya Wazungu.
Kombe la Dunia lina maana kubwa kwa kila mcheza soka. Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza Kombe la Dunia. Linapokaribia wanasoka wengi wanapata mshawasha wa kushiriki michuano yenyewe bila kujali wapi wamekulia. Nketiah sio wa kwanza na wala hatakuwa wa mwisho. Kama Ghana isingeshiriki Kombe la Dunia mwakani wala usingeisikia habari hii kutoka kwa Bwana Saddick. Kwanini hakuonyesha hamu ya kucheza michuano ya Afcon Desemba mwaka huu pale Morroco? Ni kwa sababu ni michuano ambayo haina hadhi kama Kombe la Dunia au Euro.
Baada ya Ghana kufuzu ndio tumepata habari hii kutoka kwa Bwana Saddick. Ni kweli kabisa kwamba Nketiah anafuzu kuichezea Ghana katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia licha ya kwamba amezaliwa Uingereza na ameshaichezea timu ya taifa ya England mechi moja. Kwa mujibu wa sheria zinazohusu mambo haya, mchezaji ambaye ameichezea timu yake ya taifa mechi moja ya ushindani au tatu ambazo sio za ushindani anaruhusiwa kwenda kucheza taifa jingine. Nketiah ameichezea England mara moja tu. Ilikuwa Oktoba 2023.
Wachezaji wa aina ya Nketiah wapo wengine. Mifano mizuri zaidi ni wale ambao wametoka katika familia moja. Kwa mfano, Kevin-Prince Boateng aliamua kuichezea timu ya taifa ya Ghana katika michuano ya Kombe la Dunia 2006 huku kaka yake, Jerome Boateng akiichezea timu ya taifa ya Ujerumani katika michuano hiyohiyo.
Ukweli ni kwamba Kevin-Prince hakuwa na uwezo wa kuichezea Ujerumani. Eneo la kiungo lilikuwa limejaa mastaa wakubwa wakiongozwa na Michael Ballack. Akaona mambo yasiwe mengi. Akatimkia Afrika. Jerome alikuwa na uwezo mkubwa na alianza kupangwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kwa muda mrefu. Kama yeye asingekuwa na uwezo basi angekimbilia Afrika kama ilivyokuwa kwa kaka yake.
Mfano mwingine ni Nico Williams na kaka yake, Inaki Williams. Wote hawa wana asili ya Ghana na wanacheza timu moja pale Ligi Kuu Hispania, Athletic Bilbao. Wahispania ni wajanja. Walipomuona Nico ana kipaji maalumu walimfunga mapema acheze timu yao ya taifa. Inaki ambaye hana kipaji kikubwa kama mdogo wake akakimbilia kucheza Ghana miaka ya karibuni tu baada ya kugundua kwamba asingeweza kuitwa mara kwa mara katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania.
Kwa sasa kilichobaki huwa ni uamuzi wa benchi ya ufundi pamoja na shirikisho la soka katika nchi husika kukubali kuingiza wachezaji kama Nketiah. Kocha wa Ghana, Otto Ado ameripotiwa kwamba hatakubali kuona wachezaji wa aina ya Nketiah ambao waliwahi kuombwa kuchezea mataifa Afrika halafu wakakataa na sasa wanataka kurudi kwa sababu ya Kombe la Dunia.
Inasemekana kwamba Nketiah aliwahi kuombwa, lakini alikataa. Nadhani aliamini kwamba angeweza kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha timu ya taifa ya England. Baada ya kugundua kwamba yuko mbali sana kufikia ubora wa kina Harry Kane, Marcus Rashford na wengineo sasa ndio ameikumbuka Ghana hasa wakati huu inapokwenda Kombe la Dunia.
Hata hawa kina Bukayo Saka mida hii wangekuwa wanafikiria kuchezea timu za Afrika kama wasingekuwa na vipaji vikubwa. Matokeo yake Afrika imeendelea kupokea makapi kutoka Ulaya na wakati mwingine unajiuliza wachezaji kama kina Nketiah wataenda kutusaidia nini katika Kombe la Dunia kama wameshindwa kupata namba katika vikosi vya Wazungu.
Wachezaji ambao hawana sana unafiki ni wale wa Afrika Kaskazini. Kina Riyad Mahrez, Achraf Hakimi, Hakimi Ziyech, Soufiane Amrabat na wengineo. Wale wamezaliwa Ulaya na wamekulia Ulaya. Licha ya ubora wao ambao ungewawezesha kucheza katika timu za taifa za huko, lakini waliamua kuwakilisha timu za asili zao mapema tu.
Kuna wachache wengine kutoka katika mataifa ya sisi weusi ambao wamezaliwa Ulaya na wangeweza kucheza timu za taifa za kule, lakini waliamua mapema kuwakilisha mataifa ya huku. Mastaa kama Pierre-Emerick Aubameyang, Kalidou Koulibaly, Edouardo Mendy na wengineo. Tusubiri na kuona. Kuanzia sasa kuna wachezaji wengi watataka kututumia kwa ajili ya kutimiza ndoto zao za kucheza Kombe la Dunia. Hii sio kwa Afrika tu. Kuna mataifa mengi madogo ambayo yamefuzu kucheza Kombe la Dunia kwa kutumia mfumo huu mpya.
Kuna nchi kama Jordan hatujawahi kusikia kama kuna wachezaji mahiri wametoka taifa hilo, lakini ghafla tunaweza kusikia kuna wachezaji fulani tunaowafahamu wanataka kuichezea Jordan kwa sababu bibi yake mzaa baba ana asili ya huko.