Si kosa la Singano bali wanaomwita Messi

Muktasari:

Nilizungumzia uwezo wa wachezaji wa Yanga na Azam kwa kukiri kuwa wana wachezaji wazoefu, ingawa mashabiki hasa wale wa Simba walikuwa wakiwadhihaki wale wa Yanga kuwa ni wazee! Wakati uzoefu na ukomavu wa mchezaji unaanzia miaka 24,25 na kuendelea na wala hakuna mchezaji mzee anayeweza kucheza mpira wa ushindani.

WAKATI Ligi Kuu Bara ilipokuwa inakaribia kuanza niliulizwa na mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti, Oliver Albert akitaka kujua timu gani zinaweza kufanya vizuri katika ligi inayoelekea ukingoni sasa.

Sikusita kumweleza kubwa nafasi kubwa ipo kwa Azam na Yanga na wakati huo huo sikuwa na mawazo kabisa ya ujio mzuri wa Mbeya City, sikuipa nafasi Simba hasa kutokana na aina ya usajili walioufanya huku wakilenga kukitengeneza kikosi chao ili kiweze kuja fanya vizuri misimu miwili ijayo. Nilizungumzia usajili wa wachezaji wa Yanga na Azam kuwa umelenga kuimarisha zaidi vikosi vyao na hata maandalizi waliyoyafanya Azam mwanzoni mwa msimu yalilenga kuitengeneza timu vile vile kwa Yanga hali ni hiyo hiyo.

Simba wao waliongeza baadhi ya watu wachache wazoefu ingawa hawakuwa kwenye viwango vizuri sana huku wakijivunia mseto mzuri wa vijana waliowapandisha toka kikosi chao cha pili, waliamua kwa dhati kabisa kumchukua kocha Abdallah Kibadeni ambaye huko nyuma aliwahi kuwa mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho hivyo alikuwa akiwajua vizuri wachezaji hao vijana waliokuwa na hamu sana ya kucheza ligi na damu yao ilikuwa ndiyo kwanza inachemka hivyo kila kitu walichofundishwa walikifanya kwa usahihi uwanjani, vijana hawa walikuwa na kasi na wasumbufu kwa mabeki wa timu nyingine zikiwemo Yanga na Azam,hawa vijana bado ni wachezaji wa mechi chache kuanzia 10 kushuka chini, si wachezaji wanaoweza kucheza michezo mingi fululizo na kibaya zaidi michezo yenyewe inafululiza kila baada ya siku tatu au sita, hawa si wachezaji wanaocheza michezo mingi sana wakiwa kama timu, ukitaka wacheze michezo mingi basi vijana kwenye kikosi cha kwanza wasiwe wanazidi watatu, kwao inakuwa rahisi kuchanganya damu yao na ya wachezaji wazoefu,ndiyo maana mchezaji kama Frank Domayo, Simon Msuva na Juma Abdul ambao walicheza timu moja ya vijana wa miaka chini ya 20 pamoja na akina Ramadhani Singano maarufu kama Messi, Said Ndemla, Shomari Kapombe, Thabit na wengineo wao hao wa Yanga wanaonekana kutochoka mapema na wanazidi kuimarika kila siku.

Nilizungumzia uwezo wa wachezaji wa Yanga na Azam kwa kukiri kuwa wana wachezaji wazoefu, ingawa mashabiki hasa wale wa Simba walikuwa wakiwadhihaki wale wa Yanga kuwa ni wazee! Wakati uzoefu na ukomavu wa mchezaji unaanzia miaka 24,25 na kuendelea na wala hakuna mchezaji mzee anayeweza kucheza mpira wa ushindani.

Ndani ya kikosi hicho cha Simba alijitokeza kijana mmoja mwenye kipaji kizuri sana na akionekana kuja kunyang’anya namba za wachezaji wakongwe, watu wa mpira hasa wa kizazi hiki wakampachika jina la ‘Messi’ na tatizo hata viongozi wa timu ya Simba kipindi kile na makocha wakaendelea kulikuza jina la Messi bila kujua kwamba jina hili linammeza mchezaji na kwa bahati mbaya mwenye jina halisi bado anacheza kwa kiwango cha juu sana duniani! Uwezo wake ni mkubwa mno kulinganisha na jitihada za kijana wetu, niliwahi kuzungumza kuwa Singano litukuze jina lako usikubali kuitwa Messi maana kila mtu atakayekuja uwanjani atataka kukuona ukifanya kazi sawa na anazofanya Lionel Messi wa Barcelona, ukikosea watu wanashangaa. Haya ndiyo mambo ya mashabiki wa leo wa soka, walimdanganya kijana huyu na kidogo naye alisahau akidhani kweli ana U-Messi, mashabiki hawa leo wanadiriki kusema kuwa kiwango chake kimeshuka! Toka lini Singano alicheza kwa kiwango cha wachezaji wa Ulaya? Huyu kijana ndiyo kwanza anapigana kupata uwezo na awe mzoefu, bado hata kwenye timu ya Taifa hana namba ya kudumu, leo hii watu wanataka afanye maajabu, anajazwa sifa nyingi za kufikirika kwa nini sasa asipate hasira pale anapolaumiwa!

Hebu endeleeni kumpa ushirikiano kijana huyu aje kuwa faida kwa nchi, waandishi wa habari za michezo, punguzeni kumuandika kwa jina la Messi, wale watangazaji wa mpira kwenye radio mbalimbali mwiteni Singano yeye mwenyewe alishasema hataki mumuite Messi lakini bado tumeng’ang’ania Messi Messi, kijana anahitaji kupumua ili apate utulivu wa akili bado yu mbichi.