Sh10.6 bilioni zimefanya Uwanja wa Gombani uwe hivi!
Muktasari:
- Hiyo ilikuwa sehemu ya hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, akizungumza Januari 13, 2026 kwenye uzinduzi wa Uwanja wa Gombani uliopo Wilaya ya Chake Chake iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
"NAPENDA kuipongeza Serikali kwa juhudi zake katika ujenzi wa viwanja iwe vya wilaya au mkoa. Baada ya kusema hayo, sasa nitamke rasmi kwamba uwanja mpya wa Gombani nimeufungua rasmi. Asanteni sana."
Hiyo ilikuwa sehemu ya hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, akizungumza Januari 13, 2026 kwenye uzinduzi wa Uwanja wa Gombani uliopo Wilaya ya Chake Chake iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais Mwinyi alizindua uwanja huo siku ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 na kushuhudia Yanga ikibeba ubingwa kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 matokeo kuwa 0-0.
Uzinduzi huo umefanyika baada ya Januari 8, 2025, Rais Mwinyi kuweka jiwe la msingi la ukarabati wa uwanja wa Gombani na viwanja vingine katika Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba na Gombani umefanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwemo uwekaji wa paa jipya, ujenzi wa kuta, vyumba vya wachezaji, eneo la watu mashuhuri, maegesho, uwekaji wa minara ya taa, mifumo ya maji na umeme, pamoja na ujenzi wa uwanja wa mazoezi pembezoni.
Kwa mujibu wa taarifa za ukarabati huo wa awamu ya pili, umegharimu kiasi cha Dola za Marekani 4,250,000 (zaidi ya Sh 10.6 bilioni) na umefanywa na Kampuni ya REFORM SPORTS kutoka Uturuki.
Januari 13, 2026 zikiwa zimepita takribani siku 370, uwanja huo umezinduliwa rasmi huku kukiwa na viwanja vingine vimejengwa na vinavyoendelea kujengwa kisiwani Pemba.
MSIKIE MENEJA WA GOMBANI
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Meneja wa Uwanja wa Gombani, Nassor Salim, amesema kuwa, uwezo wa mashabiki kuingia uwanjani hapo ni 15,000, huku nyasi bandia zilizowekwa kwa sasa zina mpango wa kubadilishwa hapo baadaye na kuwekwa hybrid kama New Amaan Complex.
Kwa lugha ya Kiswahili, Hybrid ni mchangayiko wa nyasi asili na bandia zinazotumika kuwekwa sehemu ya kuchezea katika viwanja vya michezo kama mpira wa miguu zilizoruhusiwa na FIFA na CAF tofauti na viwanja vyenye nyasi bandia pekee ambavyo kwa sasa FIFA na CAF hawaviruhusu kuchezewa mashindano yaliyo chini yao.
"Hadi sasa uwanja huu una nyasi bandia, lakini baadaye watabadilisha na kuweka kama zile za New Amaan Complex.
"Kule nyuma kuna viwanja viwili, mmoja ni wa mpira wa miguu na mwingine wanaita four in one, yaani kiwanja kimoja kinatumika kwa michezo minne tofauti. Kuna mpira wa kikapu, volleybal, mpira wa mikono na netiboli.
"Cha kuwaambia wakazi wa Pemba ni kwamba uwanja huu huku kwetu tumepata tunu ndani yake, kwa hiyo ni kitu adimu kwetu kimekuja Pemba, hivyo tunatakiwa tukitunze na tukihifadhi kwa kizazi chetu na vijavyo," anasema.
KLABU ZA BARA ZAKARIBISHWA PEMBA
Hivi sasa Yanga, Azam na Singida Black Stars zimehamishia mechi zao za CAF kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kwa mechi za nyumbani, hatua hiyo imemfanya Salim kuzikaribisha pia kuutumia Uwanja wa Gombani kwa mashindano mbalimbali.
Salim anasema: "Tunazikaribisha timu zote iwe kutoka Tanzania Bara au Unguja zije Pemba kwenye Uwanja wa Gombani ambao ni wa kisasa, tunaruhusu timu zije kuutumia kama zinavyokwenda Amaan."
MANDHARI YA UWANJA
Ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 15,000 waliokaa kwenye viti kwa utulivu mkubwa, imewekwa milango minane ya mashabiki kuitumua wakati wa kuingia ambayo inarahisisha waingie kwa wingi bila ya usumbufu.
Majukwaani, kuna viti na V.I.P ni tofauti na maeneo mengine kwani upande huo viti vyake ukiinua tu, vinajikunja. Upande mwingine ni vile sio vya kujikunja.
Hii ni tofauti na New Amaan Complex na viti vyake upande wote ni vya kawaida, havijikunji. Kasoro tu pale kwa wageni maalum.
"Uwanja una milango minane ya mashabiki kuingia hali inayotoa urahisi kwao na utaratibu mzuri wa kuja kushuhudia mechi," anasema.
ENEO LA WAANDISHI WA HABARI
Siku hizi viwanja vingi vimeboreshwa eneo la waandishi wa habari wanapokaa na Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na New Amaan Complex pale Unguja wameweka mfumo wa umeme unaomruhusu mwandishi wa habari kuchaji vifaa vyake vya umeme.
Pia kuna viti vinavyohamishika, huku juu wakiweka kama benchi linalisaidia unapoandika uwe kwenye utulivu.
Pale Gombani ni tofauti kidogo. Kuna hiyo mifumo ya umeme, lakini wameweka kiti na meza yake vikiachiana nafasi vikiwa havihamishiki.
VYOO
Katika Uwanja wa Gombani, kumetengwa sehemu nane na ndani yake kuna jumla ya vyoo 120 vinavyotumiwa na mashabiki kujisaidia haja kubwa na ndogo.
"Vyoo jumla vipo 120 vinavyotumika kwa haja kubwa na ndogo. Hili ni jambo zuri kwani kwa wingi wa mashabiki wakijitokeza inawapa wakati mzuri wa kwenda kujisadia bila ya usumbufu," anabainisha Salim.
KUMBE SIO GOMBANI TU
Salim ameliambia Mwanaspoti, ukiachana na Gombani unaopatikana umbali wa kilomita 34.3 kutoka Wilayani ilipo bandari ya Pemba, ikiwa ni mwendo wa saa moja kwa gari binafsi, kuna viwanja vingine vipo mikoa ya Kaskazini Pemba na Kusini Pemba vikiwa na madaraja tofauti ya wilayani na mkoani.
Kuna daraja la kwanza wakivipa jina la type one na daraja la pili ni type two. Hivi vina hadhi kama Gombani. Pia kuna vya wilaya ambavyo vinafanana na kile kilichopo pembeni ya Gombani au vile vya kule New Amaan Complex kwa pembeni.
"Ukiachana na Gombani, kuna viwanja vingine vinajengwa hapa Pemba, kuna cha type one, type two na viwanja vya wilaya. Kwa Pemba tuna mikoa miwili, kuna mkoa wa Kusini na mkoa wa Kaskazini.
"Mkoa wa Kusini kuna viwanja viwili vya wilaya na kimoja cha mkoa. Hiki cha mkoa ni type one kipo Kangani, kimewekwa viti vya mashabiki, ni wa kisasa kabisa.
"Kwa upande wa wilaya ni viwanja viwili ambapo kimoja ni kile cha Gombani pembeni ya uwanja mkubwa, kingine kipo sehemu moja inaitwa Chambani ambacho kuna cha mpira wa miguu na four in one kama Gombani.
"Tukienda upande wa Kaskazini kwa maana ya Wete na Micheweni, kuna kiwanja cha type one cha mkoa, na viwili vya wilaya.
"Hiki kiwanja cha mkoa kipo sehemu moja inaitwa Kinyikani, ukifika Chamanangwe sehemu ya maonyesho mbele kidogo kuna kituo cha polisi ndio kuna kijiji kinaitwa Kinyikani, hapo kinajengwa kiwanja kikubwa ambacho ni type one, kina sifa na vigezo vyote vinavyofaa kutumika kwa mechi za mpira wa miguu levo ya kimataifa.
"Halafu tuna viwanja vya wilaya, kimoja kikubwa kipo Micheweni, kingine Wete sehemu moja kuna kijiji kinaitwa Pandani, huko kiwanja kimejengwa kikubwa kina sifa zote na tayari kimekamilika.
"Uwepo wa viwanja hivi ni fursa kubwa sana hapa Pemba na watu wana hamasa sasa hivi hususani katika mpira wa miguu.
"Kwa Pemba hivi sasa mpira wa miguu ni mchezo maarufu sana kwani Dokta Mwinyi ametuwezesha katika sekta ya michezo na tunajivunia kuwepo kwake."
NENO LA ZFF
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga amezungumzia maboresho yaliyofanywa kwenye Uwanja wa Gombani akisema: "Mwaka jana ilichezwa fainali ya Kombe la Mapinduzi hapa Gombani lakini ilikuwa katika mazingira ambayo uwanja haujakamilika, baada ya kumaliza fainali ile tukapisha ujenzi uendelee ndiyo maana hata Ligi Kuu ya Zanzibar haikuwa ikichezwa humu ndani.
"Ukiangalia paa limepigwa la kisasa tofauti na ilivyokuwa mwaka jana, viti vimefungwa tena kwa utaratibu mwingine. Kati ya kiti kimoja na kingine kuna nafasi ambayo inakufanya ukikaa huchoki. Kuna tofauti kubwa sana na mwanzo.
"Niseme tu hongera kwa Dokta Mwinyi kwa kazi kubwa kutokana na wakandarasi waliopewa hii tenda kufanya hapa, wamefanya kwa ukamilifu wake.
"Huu ni wetu sote, kama una timu yako inahitaji kuutumia uwanja huu ifuate utaratibu. CAF Champions League inachezwa hapa, hata CAF Confederation, hata michezo mingine, kuna AFCON inakuja.
"Ukarabati wa viwanja hivi unakuja kutokana na kwamba tuna jambo letu. Zanzibar tuna AFCON 2027 inakuja huku. Tuna Gombani, Amaan na kuna balaa lingine Fumba, huko ndiyo usiseme."