Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SCORPION STYLE: Zao la mbwembwe za Higuita uwanjani

Muktasari:

  • Mchezo huo ungesahaulika kirahisi kama isingekuwa kipa wa Colombia aliyekuwa na mbwembwe nyingi uwanjani, Rene Higuita, kututambulishia kile kinachoitwa ‘scorpion kick’.

SEPTEMBA 6, 1995 England ilitoka suluhu (0-0) na Colombia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa kwenye Uwanja wa Wembley.

Mchezo huo ungesahaulika kirahisi kama isingekuwa kipa wa Colombia aliyekuwa na mbwembwe nyingi uwanjani, Rene Higuita, kututambulishia kile kinachoitwa ‘scorpion kick’.


MTINDO WA UCHEZAJI

Uwanjani, Higuita aliyezaliwa Agosti 27, 1966, Medellín, Colombia, alijulikana kwa mbwembwe zake za kuvutia, utulivu akiwa chini ya presha na mtindo wa kipekee wa kucheza, mara nyingi akifanya hatari zisizo za lazima na kutoka nje ya eneo lake ili kuwatangulia wapinzani kuanzisha mipira kwa mabeki, kufanya mbio binafsi za kudribo na hata kujaribu kufunga mabao.

Hali hiyo ilisababisha aitwe “mlinda lango anayesafisha” (sweeper-keeper); hivyo, alikuwa miongoni mwa waanzilishi waliowahamasisha makipa wengine kuchukua majukumu makubwa zaidi mbali na lango.

Ingawa alikuwa kipa, Higuita pia alijulikana kwa kufunga mabao moja kwa moja kupitia mipira ya adhabu ndogo (free-kicks) na mikwaju ya penalti. Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS) lilimuweka Higuita katika nafasi ya nane ya makipa bora katika historia ya Amerika Kusini.

Hata hivyo, maisha yake binafsi wakati mwingine yaliathiri kwa kiasi fulani uwezo wa timu yake kucheza vizuri.


PIGO LA NGE (SCORPION KICK)

Higuita anaripotiwa kubuni pigo la nge (scorpion kick), mbinu inayohusisha kipa kuruka mbele, kunyanyua miguu juu kwa uwiano wa kichwa chake, na kisha kupiga mpira kwa visigino ili kuuondoa. Mojawapo ya matukio yake maarufu zaidi ya kutumia mbinu hiyo ilikuwa alipofanya hivyo kuondoa krosi ya Jamie Redknapp katika mechi ya kirafiki dhidi ya England kwenye Uwanja wa Wembley, England, Septemba 6, 1995, jambo lililompatia umaarufu mkubwa kwenye vyombo vya habari. Tukio hilo lilishika nafasi ya 94 katika orodha ya Channel 4 ya matukio 100 bora ya michezo 2002.

Pigo la nge, ambalo pia hujulikana kama mkasi wa nyuma (reverse bicycle kick), au pigo la nyuma la nyundo (back hammer kick), ni mbinu ya kimwili katika soka inayofanywa kwa kujirusha au kuutupa mwili mbele, kuweka mikono chini na kisha kusukuma visigino vya nyuma mbele ili kupiga mpira unaokuja.

Mwanahistoria wa michezo, Andreas Campomar anasifu mbinu hii kuwa ya kipekee, akibainisha kuwa, “inaonyesha kwamba kuna burudani nje ya soka lenyewe. Kwamba mchezo, licha ya upungufu wake mwingi, unaweza kutoa nyakati nzuri ambazo hazihusiani tu na ushindi au kushindwa.”

Akizungumzia mechi ya Septemba 6, 1995, beki wa zamani wa kati wa England, Steve Howey aliyekuwa amepewa jukumu na kocha wa Newcastle United wakati huo, Kevin Keegan, kutocheza mbali na mshambuliaji wa Colombia, Faustino Asprilla, alishangazwa na ‘scorpion kick’ aliyopiga Higuita, ambapo awali alidhani mchezo ulikuwa umesimama.

“Higuita hakuwa mtu wa kutegemewa sana golini, alikuwa anatoka nje (ya eneo la goli) na kuwadhibiti washambuliaji kwa kudribo na kushiriki mchezo. Alikuwa ‘kichaa’ kabisa. Kwa hiyo haikuwa ajabu sana kwa mtu kama yeye kufanya vile,” anasema Howey.

“(Wakati wa mchezo) kila mtu alidhani mwamuzi amepiga filimbi, lakini tuligundua haraka kuwa hakufanya hivyo. Kama mpira (alioupiga Higuita) ungeingia golini ungehesabiwa (kuwa ni bao).”

Ingawa Higuita mara nyingi hupewa sifa ya kueneza umaarufu wa mbinu hii, pigo la nge lilifanywa kwa mara ya kwanza na mshambuliaji wa Paraguay, Arsenio Erico, Agosti 12, 1934, alipoifungia bao timu ya Independiente de Avellaneda katika mechi dhidi ya Boca Juniors mbele ya watazamaji 50,000.

Baada ya krosi kutoka kwa Antonio Sastre, Erico alijaribu kupiga kichwa kwa kujirusha mbele, lakini aliposhindwa kuugonga mpira vizuri aliusukumiza kwa kisigino akiwa angani na kufunga bao lililowashangaza mashabiki.

Awali mbinu hiyo iliitwa “balancín”, yaani ‘bembea’ kwa Kiingereza, lakini baadaye ilihusishwa zaidi na Higuita baada ya kufanya hivyo katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Colombia na England 1995 kwenye Uwanja wa Wembley. Mbinu hiyo ilipata jina kutokana na mhusika anapofanya hivyo kuonekana mithili ya mkia wa nge wakati wa kuupiga.

Mbali na pigo la nge la kujirusha (diving scorpion kick), pia kuna aina nyingine ya pigo la nge la kusimama (standing scorpion kick), na pigo la nge la kuzunguka (spinning scorpion kick), ambazo siyo lazima zihusishe kuweka mikono chini. Mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic, alijulikana kwa kutumia sana pigo la nge la kusimama, huku beki mkongwe wa Italia, Giuseppe Biava, akijulikana kwa pigo la nge la kuzunguka.


SIKIA HII

Higuita anasema wazo la ‘scorpion kick’ lilimjia alipokuwa akirekodi tangazo la televisheni la kampuni moja ya vinywaji pamoja na watoto nchini Colombia 1993, ambapo mmojawao alipiga mpira juu angani kwa mtindo wa mkasi (bicycle kick) kuelekea kwa kipa, ambaye kwa hisia za haraka alirusha miguu yote miwili nyuma ya mgongo wake na kuupiga mpira mbali.

“Wananiita mcheshi kila mara na hapa ninathibitisha kuwa wako sahihi,”alisema Higuita wakati huo.

Anasema miaka miwili baadaye, baada ya kugeuza kuwa mbinu yake ya kuburudisha mazoezini kwa wachezaji wenzake na wakati wa kupasha mwili joto kabla ya mechi, aliamua kuwaburudisha mashabiki wachache waliokuwa Wembley katika mechi ya kirafiki inayotajwa kuwa haikuwa na msisimko.

Katika jaribio lililokosewa na kiungo wa England, Jamie Redknapp, lililokuwa likielekea taratibu kwa kipa huyo, aliutazama mpira ukipita juu ya kichwa chake kabla ya kujirusha mbele na kuupiga kwa visigino vyake mithili ya mkia wa nge.

“Ulikuwa mpira bora. Nilifikiri hakuna tatizo. Ulitoka kikamilifu (mbali na goli),”€  Higuita anakumbuka.

Martin Tyler, aliyekuwa mchambuzi wa soka wa Sky Sports, anasema: “Ulikuwa ni ubunifu wa ajabu wa kipa katika wakati mmoja uliomfanya mtangazaji (mechi) ashangae. Ni kama hadithi ya katuni. Ilikuwa kama kitu cha kubuni.”

“Kulikuwa na ukimya fulani mfupi, watu walijaribu kutafakari nini kimetokea,† anakumbuka mtangazaji wa BBC Radio Newcastle, Simon Pryde, aliyekuwa uwanjani. “Halafu kila mtu akapasuka kwa mchanganyiko wa kicheko cha ghafla na makofi.”€

Kwa wengi, wanadai Higuita alikuwa mcheshi na mburudishaji. Lakini, yote hayo yalitokana na ujasiri na uthubutu wa mtoto aliyempoteza mama yake akiwa mdogo, akilelewa na babu na bibi katika mtaa wa Medellín uliokumbwa na migogoro ya dawa za kulevya na matatizo ya kijamii.

Utotoni kwake alikuwa akiingia kisiri kwenye basi kwenda mazoezini, akicheza kama mshambuliaji na kufunga mabao katika viwanja vilivyojengwa na mfanyabiashara wa dawa za kulevya, Pablo Escobar, kabla ya kuvaa glovu baada ya mchezaji mwenzake kuumia.

Kuna video za zamani zinazoonyesha Higuita akiwanyang’anya washambuliaji mpira nje ya eneo lake, akishinda mipira ya juu kwa kichwa, akicheza pasi za haraka na kudribo kwa kasi akiwapita wachezaji karibu na mstari wa katikati ya viwanja vya vumbi vilivyojaa karatasi zilizotupwa kutoka majukwaani. Katika soka la leo, kugusa kwake mpira kungekuwa gumzo mitandaoni.

“Alikuwa mbele ya wakati wake,”€  anasema Jorge Campos, kipa maarufu wa Mexico wa kipindi hicho.

“Ndiyo, alifanya hatari nyingi lakini pia aliokoa nyingi. Watu hawatambui, alikuwa beki wa ziada. Rene ndiye aliyeanzisha staili ya sasa ya mashambulizi kuanzia kwa makipa. Alikuwa mfano kimataifa na hilo likawa mapinduzi.”€

Mchambuzi wa soka la Amerika Kusini, Tim Vickery, aliwahi kudai: “(Higuita) alikuwa mwanzilishi wa ustadi wa kucheza mpira kwa miguu na katika utayari wake kuchukua majukumu mita 40 kutoka langoni.”


STRAIKA HADI KIPA

Alipokuwa mdogo, Higuita alicheza soka kama mshambuliaji, na alikuja kuwa kipa baada ya kuchukua nafasi ya mchezaji aliyeumia katika timu ya utotoni ya Millonarios iliyopo Bogota, ambayo baadaye ilimpandisha kikosi cha wakubwa. Inaelezwa kwamba 1985, akiwa na kikosi hicho, alikihama na kutua Atletico Nacional, timu kutoka mji wake wa Medell’­n. Kocha wa Atletico Nacional na Colombia, Francisco Maturana, alimpa jina la utani ‘El Loco’  yaani Mwendawazimu.

Higuita alihimizwa kucheza nje ya eneo la kipa, na Maturana aliwahi kukaririwa enzi hizo akisema, “Rene akiwa kama msafishaji (sweeper) tunakuwa na wachezaji 11 wa uwanjani.”€  Higuita alidumu na timu hiyo kwa miaka 10, akiondoka tu alipokwenda kwa mkopo wa mwaka mmoja katika klabu ya Hispania, Real Valladolid, 1991. Akiwa Atletico Nacional, timu ilitwaa taji lake la kwanza la Copa Libertadores 1989 na kushinda Ligi Kuu Colombia mara mbili.

Enzi zake golini, alikuwa akipiga mipira mingi ya adhabu na ya kona, jambo lililomwezesha kufunga mabao 41. Mwaka 1997 alihamia Mexico katika timu ya Tiburones Rojos de Veracruz, lakini alirudi Colombia 1999. Baadaye alichezea timu mbalimbali za Colombia na kuondoka kwenda kucheza msimu mmoja S.D. Aucas huko Quito, Ecuador, 2004, kisha misimu miwili na timu ya Venezuela ya Guaros de Lara (2007-08). Alistaafu kwa muda mfupi 2006. Higuita alitoka kwenye ustaafu Julai 21, 2007 ili kusaini Guaros FC ya Venezuela. Januari 2008, akiwa na umri wa miaka 41, alisaini na timu ya daraja la pili ya Colombia ya Deportivo Rionegro. Ilipofika Juni 2008, alisaini na timu nyingine ya Colombia, Deportivo Pereira, na hatimaye alistaafu Januari 25, 2010. Kwa ujumla, alicheza timu tofauti 11.

Higuita alichezea Colombia kuanzia mwishoni mwa 1980 hadi 1990, akicheza mechi 68 na kufunga mabao matatu. Katika Kombe la Dunia 1990, alifanya kosa la ajabu uwanjani alipokuwa akijaribu kukokota mpira karibu na goli lake, ambapo alipokonywa mpira na Roger Milla wa Cameroon aliyeukwamisha wavuni kwenye dakika ya 108 ya muda wa nyongeza. Ikumbukwe kwamba kabla ya hapo timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, hivyo kuondolewa kwa kipigo cha mabao 2-1.

“Nilikuwa shujaa wa mchezo mpaka Milla alipotufunga,” Higuita alilalamika baadaye. Hata hivyo, yeye na wachezaji wenzake walipokewa kama mashujaa waliporudi nyumbani Colombia.


FIFA YAJA NA ‘SHERIA YA HIGUITA’

Kabla ya kukubaliwa kwa pasi ya nyuma kwa kipa katika Olimpiki Barcelona 1992, makipa waliruhusiwa kudaka mpira kwa mikono baada ya kurudishiwa na mchezaji mwenzao.

Higuita anaamini ni mtindo wake uliothibitisha kuwa makipa wanaweza kucheza vizuri kwa miguu na ndiyo ilikuwa sababu muhimu iliyolifanya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kubadili hilo na ikajulikana kama ‘Sheria ya Higuita.’€

“Wachezaji wakubwa kama Pele na Diego Maradona walikuwa bora sana, lakini hawajabadilisha sheria yoyote ya Fifa,”€  anasema Higuita.


KAZI YA UKOCHA

Higuita aliwahi kuelezea kiu yake ya kufundisha timu ya taifa ya Colombia, na Desemba 2008 alipata kazi ya kuwa kocha wa makipa katika klabu yake ya zamani Real Valladolid nchini Hispania.

Alijiunga na Al Nassr nchini Saudi Arabia 2011, na alikuwa kocha wa makipa wa klabu hiyo kwa takribani miaka mitano hadi 2016. Alirejea Atletico Nacional ya Colombia, Juni 28, 2017, baada ya kupata kazi ya ukocha wa makipa. Aliporejea alisema,” doto ya maisha yangu ilikuwa kurudi Atletico Nacional.”€


MAISHA BINAFSI

Mke wa Higuita anaitwa Magnolia, na wana watoto wawili, Andres na Pamela. Pia ni baba wa Cindy Carolina, binti wa mkewe wa kwanza aliyefariki dunia. Mwamba huyo ni babu wa wasichana wawili na mvulana mmoja.

Higuita alikuwa rafiki wa Diego Maradona na alicheza katika mechi ya kumuaga mwanasoka huyo mwaka 2001.

Higuita alifungwa jela 1993 baada ya kuhusika katika tukio la utekaji nyara. Akiwa kama mpatanishi kati ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya Pablo Escobar na Carlos Molina, alihusika kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha binti wa Molina anaachiwa huru kwa kuwasilisha fedha za fidia.

Alilipwa Dola 64,000 kwa huduma zake, jambo lililokiuka sheria za Colombia kwani ni kosa kufaidika kutokana na utekaji nyara. Alikaa gerezani kwa miezi saba kabla ya kuachiwa bila mashtaka. Akizungumzia tukio hilo, alikaririwa akisema, “mimi ni mwanasoka, sikujua chochote kuhusu sheria za utekaji nyara. Nilifanya kwa sababu za kibinadamu. Kama ningehitajika tena kumsaidia mtu aachiwe huru, ningefanya bila kusita.”€

Katika makala ya ESPN ‘The Two Escobars’, Higuita alidai alikamatwa kwa kumtembelea Pablo akiwa gerezani kwa nia ya kumshukuru kujisalimisha, jambo lililosaidia kuleta utulivu nchini Colombia kwa muda mfupi. Alisisitiza kuwa wakati wa mahojiano aliulizwa tu kuhusu Pablo Escobar na siyo tukio la utekaji.

Kutokana na kifungo hicho, Higuita hakushiriki fainali za Kombe la Dunia 1994. Katika kashfa nyingine, Novemba 23, 2004, alipimwa na kukutwa akitumia dawa za kulevya aina ya cocaine alipokuwa akiichezea Aucas, klabu ya Ecuador.

Mwaka 2005, Higuita alishiriki katika kipindi cha televisheni cha uhalisia kiitwacho La Isla de Los Famosos: Una Aventura Pirata (Kisiwa cha Watu Maarufu: Safari ya Maharamia). Pia mwaka huo alifanyiwa upasuaji wa urembo kubadilisha kabisa mwonekano wake. Kwa sasa amekuwa akionyesha pia hamu ya kujihusisha zaidi na siasa nchini kwao Colombia.

Licha ya scorpion style kuanzishwa kitambo na Higuita na kubamba wakati wake, lakini kwa sasa ni kama imepotea. Hakuna makipa wanaotoa burudani hiyo, isipokuwa kilichobaki na kinachosisitizwa katika soka la kisasa ni kuchezesha timu kwa kuanzisha mashambulizi kuanzia golini na kupandisha juu kwa wapinzani wa timu. Vilevile makipa kucheza mpira mara kwa mara kwa miguu kama alivyokuwa akifanya Higuita.

Pamoja na yote hayo hata baada ya kustaafu, hadithi ya kipa huyo aliyefunga mabao, mwenye maonyesho ya kuvutia na pigo la nge imeendelea kuishi.