Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sauzi: Wazee wa vuvuzela wanaotua Marekani na somo la 2010

Muktasari:

  • Afrika Kusini ni sehemu muhimu ya historia ya kisiasa, kijamii na michezo ya Afrika. Taifa hilo limepitia vipindi vya maumivu, ubaguzi wa rangi, kufungiwa kwa miaka mingi na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), lakini likaibuka tena na kuwa moja ya nchi zenye ushawishi mkubwa zaidi katika soka la bara hili.

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI: IKITAJWA Afrika Kusini, moja kwa moja unaweza kukumbuka kelele za vuvuzela na namna zilivyounganisha Waafrika wote pamoja na dunia kwa ujumla kusherehekea fainali za Kombe la Dunia 2010 ambapo, kwa mara ya kwanza, zilifanyika katika ardhi ya Afrika.

Afrika Kusini ni sehemu muhimu ya historia ya kisiasa, kijamii na michezo ya Afrika. Taifa hilo limepitia vipindi vya maumivu, ubaguzi wa rangi, kufungiwa kwa miaka mingi na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), lakini likaibuka tena na kuwa moja ya nchi zenye ushawishi mkubwa zaidi katika soka la bara hili.

Kwa miaka 16 walikuwa wamefungiwa kushiriki mashindano ya FIFA kutokana na mfumo wa ‘apartheid’ uliokuwa ukiutenganisha watu kwa misingi ya rangi. Waliondolewa rasmi katika soka la dunia 1976.

Lakini waliporudi baada ya mfumo huo kuanguka, waliinuka haraka kuliko wengi walivyotarajia. Ndani ya muda mfupi wakajenga timu yenye ushindani mkubwa, wakaongeza uwekezaji kwenye soka na kuanza kurejesha heshima yao iliyopotea kwa miaka mingi.


HISTORIA ILIANZA KITAMBO

Soka liliingia Afrika Kusini mwishoni mwa karne ya 19 kupitia wanajeshi wa Kiingereza waliokuwa wakitawala eneo hilo. Kadri muda ulivyokwenda, mchezo huo ukaanza kupendwa zaidi katika jamii mbalimbali huku ukikua kwa kasi kwenye maeneo ya wafanyakazi, migodini pamoja na shuleni.

Mwaka 1906, Afrika Kusini walicheza mechi yao ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Argentina mjini Buenos Aires. Hilo linaifanya kuwa moja ya timu kongwe zaidi kuwahi kucheza soka la kimataifa nje ya bara la Ulaya.

Katika ziara hiyo ya Amerika Kusini mwaka 1906, walicheza mechi 12, wakashinda 11 na kufunga mabao 60 huku wakiruhusu saba pekee. Rekodi hiyo ilionyesha mapema kabisa kwamba taifa hilo lilikuwa na uwezo mkubwa wa kisoka hata kabla ya mataifa mengi ya Afrika kuanza rasmi kushiriki mashindano ya kimataifa.

Lakini kwa muda mrefu maendeleo yao yalikwamishwa na siasa za ubaguzi wa rangi zilizovuruga michezo yote nchini humo. Mfumo wa ‘apartheid’ uliigawa jamii kwa misingi ya rangi na hata katika mpira wa miguu kulikuwa na vyama tofauti kwa wazungu, watu weusi na jamii nyingine. CAF iliwafungia mwaka 1958 baada ya kukataa kuchezesha timu yenye wachezaji wa rangi tofauti katika AFCON ya 1957. FIFA nayo ikawasimamisha kabla ya kuwafungia rasmi mwaka 1976 kutokana na presha kutoka kwa mataifa mengi duniani yaliyokuwa yanapinga ubaguzi wa rangi.


WALIPORUDI WAKATISHA AFRIKA

Baada ya kurejea 1992, hakuna aliyedhani wangeweza kuwa na nguvu kubwa ya ushindi haraka kiasi hicho.

Lakini chini ya kocha Clive Barker, Afrika Kusini walijenga timu yenye nidhamu na morali ya hali ya juu. Wachezaji wao walicheza kwa moyo wakiamini wana nafasi ya kubadilisha historia ya taifa lao. Mwaka 1996 wakaandaa AFCON na kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kuifunga Tunisia mabao 2-0 fainali mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika Soccer City.

Neil Tovey aliliinua kombe hilo huku maelfu ya mashabiki wakilia kwa furaha ndani ya dimba hilo maarufu. Ilikuwa zaidi ya ushindi wa mpira wa miguu kwa sababu taifa lote lilikuwa limeungana nyuma ya timu yao.

Kwa Waafrika Kusini wengi, huo ulikuwa ushahidi kuwa taifa lao jipya lilikuwa limeanza kuungana baada ya maumivu ya ubaguzi na migawanyiko ya miaka mingi. Miaka miwili baadaye, walifika tena fainali ya AFCON 1998 kabla ya kufungwa na Misri, jambo lililoonyesha wazi kuwa hawakuwa timu ya kuungaunga bali walikuwa wameanza kuwa moja ya mataifa makubwa zaidi Afrika.


KIZAZI CHA DHAHABU

Katika miaka yao bora zaidi, Afrika Kusini ilikuwa na mastaa waliotikisa Ulaya na kuifanya dunia iheshimu zaidi soka la taifa hilo.

Lucas Radebe alikuwa nahodha wa Leeds United ya England na mmoja wa mabeki waliotisha zaidi wakati huo. Uongozi wake, uwezo wake wa kusoma mchezo pamoja na nidhamu yake vilimfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaoheshimika zaidi katika historia ya Afrika Kusini.

Benni McCarthy akawa mshambuliaji bora zaidi kuwahi kutoka Afrika Kusini akiwa na mabao 31 ya kimataifa. Mwaka 2004 aliandika historia kubwa zaidi kwa kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Porto chini ya Jose Mourinho.

Kulikuwa pia na Shaun Bartlett, Doctor Khumalo, John Moshoeu, Mark Fish pamoja na Siphiwe Tshabalala ambaye bao lake dhidi ya Mexico  2010 bado linatajwa kuwa moja ya mabao bora kabisa katika historia ya Kombe la Dunia. Kizazi hicho kilifanya Bafana Bafana kuwa timu iliyokuwa ikipewa heshima kubwa Afrika na hata Ulaya kwa sababu walikuwa na wachezaji waliocheza katika ligi kubwa zaidi duniani.


WALIVYOIBADILI AFRIKA 2010

Hakuna taifa la Afrika litakalosahaulika katika historia ya Kombe la Dunia kama Afrika Kusini. Mwaka 2010 walipewa jukumu kubwa la kuandaa mashindano ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa karibu sana. Walikuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kuandaa michuano hiyo mikubwa zaidi duniani na walihakikisha wanaacha alama kubwa ambayo haitafutika kirahisi katika historia ya mchezo huo.

Kuanzia Johannesburg, Durban hadi Cape Town, dunia nzima ilielekeza macho yake Afrika. Viwanja vya kisasa vilijengwa, miundombinu ikaboreshwa huku mamilioni ya mashabiki kutoka kila kona ya dunia wakifika kushuhudia mashindano hayo.

Sauti za vuvuzela zikawa utambulisho wa mashindano hayo huku mabilioni ya watu wakishuhudia namna Waafrika walivyofanikiwa kuandaa tukio kubwa zaidi duniani kwa mafanikio makubwa.

Ingawa Bafana Bafana walitolewa katika hatua ya makundi, waliandika rekodi nyingine ambayo hawataisahau kirahisi kwa sababu walikuwa wenyeji wa kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kushindwa kuvuka hatua ya makundi. Hata hivyo, ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Ufaransa uliendelea kubaki sehemu muhimu ya kumbukumbu za mashabiki wao kutokana na namna walivyopambana mbele ya taifa kubwa la Ulaya.


HUGO BROOS AMEWAREJESHA

Baada ya miaka mingi ya kuyumba, kubadilisha makocha mara kwa mara na kukosa mashindano makubwa, ujio wa Hugo Broos umeleta uhai mpya ndani ya Bafana Bafana.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliyeipa Cameroon ubingwa wa AFCON 2017 ameijenga upya Afrika Kusini kwa kutumia nidhamu kubwa, mshikamano wa timu pamoja na mfumo wa kisasa wa kucheza mpira wa kasi.

Chini yake, Bafana Bafana walimaliza nafasi ya tatu AFCON 2023 na kuonyesha kuwa wanaweza tena kushindana na vigogo wa bara hili baada ya miaka mingi ya kupoteza mwelekeo. Kitu kinachowapa nguvu zaidi ni kwamba wengi wa wachezaji wao wanacheza pamoja katika klabu kubwa za ndani kama Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates, jambo ambalo limeongeza maelewano ndani ya kikosi.

Broos ameonekana kuwa kocha aliyerejesha imani ya mashabiki ambao kwa muda mrefu walikuwa wamekata tamaa kuhusu timu yao ya taifa.


RONWEN, TAU NA KIZAZI KIPYA

Nahodha Ronwen Williams kwa sasa ni mmoja wa makipa bora kabisa Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuokoa michomo ya hatari, kupanga safu ya ulinzi pamoja na uzoefu wake mkubwa katika mashindano ya kimataifa. Ubora wake katika AFCON ulimfanya kuwa mmoja wa wachezaji waliovuta macho ya wengi huku akiisaidia Afrika Kusini kufanya vizuri zaidi ya matarajio ya watu wengi.

Mbele yao yupo Percy Tau ambaye bado ni sura kubwa ya Bafana Bafana kutokana na uzoefu wake Ulaya, ubora wake wa kutengeneza nafasi pamoja na uwezo wake wa kubeba presha ya mechi kubwa. Lakini tofauti na zamani ambapo walitegemea nyota wachache, sasa Afrika Kusini ina kizazi kipya chenye ushindani mkubwa na njaa ya mafanikio.

Teboho Mokoena amekuwa injini ya timu katikati ya uwanja huku Themba Zwane akiendelea kuwa chanzo kikubwa cha ubunifu na utulivu katika mechi muhimu. Mbele kuna Lyle Foster anayekipiga Burnley ya England, Evidence Makgopa pamoja na Relebohile Mofokeng ambaye anaonekana kuwa moja ya vipaji vikubwa zaidi vya Afrika Kusini kwa sasa kutokana na kasi yake, kujiamini pamoja na uwezo wake wa kutengeneza nafasi.


WALIVYOFUZU 2026

Safari yao ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 haikuwa rahisi hata kidogo kwa sababu walikutana na ushindani mkubwa kutoka Nigeria, Benin, Lesotho, Rwanda na Zimbabwe. Walipitia presha kubwa, malalamiko ya uamuzi pamoja na adhabu ya kupokwa pointi baada ya kumchezesha Teboho Mokoena katika mechi ambayo hakustahili kucheza kutokana na masuala ya kinidhamu.

Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa Afrika Kusini huku mashabiki wengi wakihoji namna kosa hilo lilivyoweza kutokea katika hatua muhimu kama hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia. Lakini pamoja na misukosuko yote hiyo, waliendelea kupambana kwa nguvu kubwa hadi kufanikiwa kufuzu mashindano hayo wakiwa kileleni mwa Kundi C na pointi 18, jambo lililorejesha furaha kwa mashabiki wao.

Kwa sasa, Afrika Kusini ipo nafasi ya 60 katika viwango vya FIFA huku ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri zaidi Amerika Kaskazini kutokana na maendeleo ya kikosi chao.


KUNDI LITAKALOWAPIMA

Katika Kombe la Dunia 2026, Afrika Kusini ipo Kundi A pamoja na Mexico, Jamhuri ya Czech na Korea Kusini katika kundi ambalo wengi wanaamini lina ushindani mkubwa lakini pia lina nafasi kwao kufanya vizuri.

Ratiba hiyo tayari imeanza kuwapa presha mashabiki wao kwa sababu watafungua michuano dhidi ya Mexico kwenye dimba la Estadio Azteca Juni 11, 2026 mbele ya maelfu ya wenyeji hao. Hii itakuwa mara ya pili kwa Bafana Bafana kucheza mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo mwaka 2010 dhidi ya Mexico pia, jambo ambalo limeongeza hisia kubwa kwa mashabiki wao.

Mchezo dhidi ya Czech unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na ubora wa timu hiyo ya Ulaya huku Korea Kusini nao wakitajwa kuwa moja ya timu tishio kutoka Asia. Hata hivyo, wengi wanaamini kundi hilo linaweza kuwapa nafasi ya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia yao ikiwa wataanza vizuri na kutumia uzoefu wa wachezaji wao.


WANACHOTAFUTA SASA

Kwa miaka mingi, Afrika Kusini imekuwa ikitafuta kurejea katika hadhi yao ya zamani baada ya kipindi kirefu cha kuyumba na kushindwa kufikia mafanikio makubwa kimataifa. Wameshawahi kuwa mabingwa wa Afrika, wamewahi kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia na wamewahi kuwa taifa lililoivutia dunia nzima kupitia mpira wa miguu.

Lakini bado kuna jambo moja kubwa ambalo hawajawahi kulifanya katika historia yao yote ya Kombe la Dunia. Hawajawahi kuvuka hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa zaidi duniani. Hiyo ndiyo ndoto kubwa ya Bafana Bafana 2026 na ndiyo sababu mashabiki wao wana matumaini makubwa kuhusu kizazi cha sasa.