Sangawe: Ukitaka kutoboa kimaisha, cheza gofu

VIJANA wengi wanaocheza gofu wanapata fursa ya kukutana na viongozi wa serikali na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali na wengine wamesaidiwa kupata ajira na watu hao.”

Ndivyo anavyoanza kusema mchezaji wa klabu ya Lugalo, Laurent Sangawe (handcup 11, daraja B) anayeamini vijana wanafaidi pia maarifa na kuonyeshwa njia za mafanikio.

Anaeleza kukutana na watu tofauti kunamsaidia akili yake kuwaza makubwa kwani anapata maarifa kutoka kwao.

Kwenye mahojiano na Mzuka wa Gofu, anawashauri vijana walioko vyuoni, shuleni na mtaani kuzifuata fursa hizo kwani zitabadilisha maisha yao.

“Niwaondoe wasiwasi vijana wanaodhani mchezo huo ni wa matajiri, kuna vijana wengi wametoka familia za kipato cha chini, gofu imebadili maisha yao, hivyo wanapaswa kuthubutu na siyo kuogopa wakiwa mbali,” anasema.


ALIKOANZIA

“Tangu nianze gofu mwaka 2020 nimefikisha miaka minne, tayari nina mataji zaidi ya 10 ya ndani na nje, nina zawadi ya friji mbili, kubwa moja na ndogo pia niliwahi kupata simu,” anasema na kuongeza;

“Zawadi za mchezaji wa ridhaa, kwa asimilia kubwa zinakuwa ni vitu vya ndani na wengi wetu hatujatumia gharama kubwa kununua vitu vya ndani.”

Analojivunia kwenye gofu ni namna anavyopata elimu kutoka kwa viongozi mbalimbali, wanaompa njia za kujijenga kiuchumi, anakiri ameanza kuchukua hatua ya kuyafanyia kazi baadhi ya mambo na imani yake miaka ya baadaye atakuwa levo nyingine.

“Siwezi kutaja kiongozi mmoja baada ya mwingine, lakini huwa nikipata nafasi ya kuzungumza nao, wananielekeza vitu vya kufanya, nimegundua vijana wengi wanapotea kutokana na makundi na kukosa watu sahihi wa kuwashauri,” anasema.

Sangawe ambaye ni mwanajeshi (private), anasimulia namna gofu ilivyomjenga kuwa na nidhamu binafsi, umakini na afya vinavyomsaidia kutekeleza majukumu yake kirahisi.

“Gofu inaondoa msongo wa mawazo, tunakutana na watu wenye mitazamo tofauti, inayotusaidia kuvichukulia vitu kwa mapana yake ya kile unachokiona kinafanyika ama kinachoongelewa,” anasema na kuongeza;

“Ujue watu waliofanikiwa wana historia tofauti, wakisimulia zinasaidia kutokukata tamaa na kuamini kama leo ni ngumu, basi kesho itakuwa njema, mfano natarajia kufungua biashara baada ya kushauriwa na baadhi ya vigogo njia za kupita.”

Pia anasema anapambana kupunguza handcup na anatamani kuitumikia timu ya taifa ya gofu.

“Zamani nilikuwa nacheza soka, lakini baada ya kujifunza gofu ndio mchezo ninaoupenda zaidi, ndio maana natamani nipate nafasi ya  kulitumikia taifa langu.”


WATOA FURSA

Mchezaji wa gofu wa klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, Shabir Abji ambaye ni mkurugenzi wa New Africa Hotel, anasema kuna vijana alikutana nao kwenye gofu na akawashika mkono kupata kazi.

“Naamini katika vijana, kikubwa wanapaswa kusomea fani, ili iwe rahisi kusaidika, wawe waaminifu kwa sababu hawajui wanakutana na nani na kwa wakati gani maishani mwao. Gofu ni rahisi kupangilia muda, hivyo unaweza ukafanya shughuli zako na kucheza kama kawaida,” anasema.

Peter Fiwa ni mchezaji wa klabu ya Lugalo, fani yake ni rubani, anasema vijana wanaocheza gofu wanapata fursa ya kukutana na watu tofauti, wanaowapa koneksheni ya kupata kazi.

“Mfano makedi katika kupiga stori za hapa na pale, wanauliza kazini kwako, huwezi kutufanyia mpango, wapo ambao nimewatafutia kazi na wengine kuwaendeleza kimasomo,” anasema.


Imeandikwa na Olipa Assa, Nevumba Abubakar na Brown Msyani.