Samahani Pluijm, nina akina Zuttah 20 huku Mwananyamala
Muktasari:
Nyerere amenijengea tabia ya kurudia kusoma kitabu tena na tena, amenijengea tabia ya kuchunguza kitu zaidi ya mara moja. Bahati nzuri ukipata jibu lile lile basi gundua kuwa uko sahihi.
MWAKA fulani, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutuambia kuwa alikuwa amerudia kukisoma tena na tena na tena kitabu chake cha Azimio la Arusha na wala hakuwahi kuona kosa la azimio lile.
Nyerere amenijengea tabia ya kurudia kusoma kitabu tena na tena, amenijengea tabia ya kuchunguza kitu zaidi ya mara moja. Bahati nzuri ukipata jibu lile lile basi gundua kuwa uko sahihi.
Ni kama ambavyo nimeendelea kurudia kumtazama tena na tena beki wa kulia wa Yanga kutoka nchi kubwa kisoka ya Ghana, Joseph Zuttah. Mechi ya kwanza kumuona uwanjani niliamini alikuwa na uwezo wa kawaida.
Baadaye nikarudi kumtazama tena, kisha nikamtazama tena, halafu nikamtazama tena. Nikagundua kuwa nilikuwa sahihi. Ningekuwa nimemtazama mara moja ningekuwa nimekosea sana, baada ya hapo nimegundua mambo matatu.
Jambo la kwanza kabisa nimegundua kwa nini kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alikuwa anamkosoa sana kiungo aliyekuwa anajaribiwa, Lassana Kamara. Nilimtazama Kamara katika pambano la Yanga na Sports Club Villa wakati Kamara alipoamua kuchezea Villa.
Kamara alionekana kucheza soka la msingi. Aliziba njia zote. Hakuwa mtu wa mbwembwe sana lakini alifanya kazi ambayo kwa sasa Azam wanafanyiwa na kiungo wao Mnyarwanda, Jean-Baptiste Mugiraneza.
Lakini kumbe Pluijm anaonekana alikuwa hamtaki Kamara kwa sababu ya kumtafutia nafasi rafiki yake kutoka Ghana Joseph Zuttah. Nafasi za wachezaji wa kigeni zilikuwa chache na Pluijm akatumia undugu na urafiki.
Pluijm anaishi Ghana na amekaa katika nchi hiyo muda mrefu. Inavyoonekana yeye na Zuttah hawakujuana barabarani, walijuana muda mrefu uliopita nchini Ghana. Kuna namna ambavyo imefanyika.
Jambo la pili ambalo nimegundua ni kwamba Zuttah hafikii nusu ya uwezo wa beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul. Abdul ana kila kitu katika eneo la kulia. Anakaba, anasogeza timu kwa kasi na zaidi ya yote ni mpigaji mzuri wa krosi ambazo zina macho.
Kabla hata Pluijm hajafikiria kutuletea Zuttah hapa Tanzania alijiuliza kama anamleta beki ambaye ana uwezo juu ya Juma Abdul? Mchezaji wa kigeni hapaswi kuja kukaa benchi kwa mchezaji wa Tanzania.
Na si Abdul tu, Zuttah hafiki katika uwezo wa Shomari Kapombe, Hassan Kessy wala Michael Aidan. Kwa nini makocha wa kigeni wanatuchezea akili na bado Watanzania tunakubali?
Hata kama Zuttah angekuwa beki wa upande wa kushoto bado angekuwa hana sababu ya kupewa mkataba Tanzania. Upande wa kushoto kumejitokeza wachezaji wengi nchini ambao wana uwezo kuliko yeye.
Kuna yule Haji Mwinyi anaonekana kuwa fundi. Kuna mtaalamu wa nafasi hiyo kwa sasa, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anaonekana kuwa fundi zaidi, kuna David Luhende naye anaonekana kuwa fundi.
Kwa jinsi nilivyouchunguza mpira wa sasa wa Tanzania, ndani ya uwanja tunakabiliwa na matatizo mawili. Tunakabiliwa na ukosefu wa washambuliaji wenye uwezo mkubwa wa matumizi ya nguvu na akili.
Lakini pia tunakabiliwa na tatizo katika eneo la mabeki wa kati. Mabeki wa kati ni wafupi na kuna tatizo kubwa la matumizi ya nguvu. Hatuna walinzi kama Sergi Wawa Paschal na mchezaji wa aina yake anaponunuliwa hapa Tanzania huwa tunakubali kwamba anastahili kuchukua mshahara wetu.
Tanzania haijafika katika matatizo makubwa ya mabeki wa pembeni, mabeki hao na wachezaji wa eneo la kiungo bado wanajitahidi sana. Unapomleta mchezaji wa pembeni inabidi awe tofauti kidogo na wachezaji wa pembeni waliopo.
Bahati mbaya kwa Zuttah ni kwamba si tu kuwa hayupo sawa na kina Kapombe, lakini pia wachezaji hawa wanamzidi uwezo na wanaicheza nafasi yake kiufasaha zaidi.
Nadhani kinachombeba Pluijm katika uhamisho huu wa Zuttah ni mafanikio ambayo ameyapata na Yanga msimu uliopita.
Mashabiki na mabosi wa Yanga wanamuonea aibu, labda wanaogopa kumwambia kuwa usajili wa Zuttah ni matumizi mabaya ya pesa za usajili na mishahara kwa jumla.
Kuna kina Zuttah wengi ambao wanaweza kupatikana huku kwetu Mwananyamala Kisiwani. Wapo wengi kwelikweli. Wanatembea na mpira na kupiga krosi kuliko yeye.
Kitu cha mwisho ambacho naendelea kujifunza na sio kwamba nimegundua ni kwamba uzubaifu wa wachezaji wetu kwenda katika nchi za nje ndio unawafanya wachezaji hawa watuzoee na kuona kama hatujui mpira.
Hili ndio tatizo la wachezaji wetu kujificha, ukijumlisha na ukosefu wa mafanikio katika soka, basi kila mmoja anajiona anaweza kucheza Tanzania. Na hata makocha wetu wanaona wanaweza kutuuzia mbuzi katika gunia kwa urahisi.