Salamba ataja kinachompa dili klabu za nje

BAADA ya mashabiki wa soka kujiuliza nani yupo nyuma ya dili za kupata timu nje kwa straika, Adam Salamba ambaye kwa sasa amejiunga na Ghaz El Mahalla ya Misri anayochezea Himid Mao, mchezaji huyo amefunguka.

Anasema hajawahi kujibweteka tangu alipoamua kuchagua soka kuwa chanzo chake cha mapato. Ndipo alipoamua kujitengenezea utaratibu wa kuhakikisha kwa siku anafanya mazoezi mara tatu, ili kuhakikisha mwili wake unakuwa fiti.

Anakiri kukutana na ujumbe kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, unaomzungumzia ana bahati ya kupata timu za nje, ila jambo pekee aliloamua kuwaambia Watanzania ni kwamba ofa anazozipata siyo kwa bahati mbaya, bali anawajibika na kusaka fursa.

“Niwe na timu nisiwe na timu natumia muda mwingi kufanya mazoezi kwa siku mara tatu. Inapotokea sehemu ya kwenda kufanya majaribio tayari mwili wangu unakuwa upo fiti na sijawahi kusaini moja kwa moja, makocha wa timu hizo wananiona kwenye mazoezi yao.

Anaongeza: “Pia nina mawakala mbalimbali ambao ndio wanakuwa wananiambia nienda nchi fulani nikafanye majaribio, nimefunguka hilo ili wachezaji wenzangu kama wana la kujifunza hapo wajifunze na huo ndio ukweli, maana siwezi kumjibu kila mtu kwamba ninafanya hiki na kile.”

Anafichua kilichomfanya aondoke Algeria ambako alisaini timu ya JS Saoura msimu wa 2021/22, ni kutofautiana na wakala wake aliyekuwa anataka amwongoze moja kwa moja, akitaka asaini mkataba ambao uliandikwa kwa Lugha ya Kifaransa.

“Huyo wakala ndiye aliyenipeleka kufanya majaribio katika JS Saoura, baada ya kucheza mechi kama nne akafukuzwa kocha niliyeanza naye kazi, akaja mwingine aliyeletwa na wakala huyohuyo, basi akaniambia kwa sababu umekataa kusaini mkataba hutacheza, nikaona isiwe tabu nikaondoka;

Anaongeza: “Wachezaji wengi wameumizwa kusaini mikataba kwa lugha wasizozijua, ndio maana aliponiletea Kifaransa nikaona siwezi kujiingiza kwenye vitu ambavyo vitaniletea shida baadaye.”


FAIDA ZA KUCHEZA NJE

Anasema maisha yake kiuchumi yamebadilika akiyatofautisha na kabla ya kuanza kucheza nje na akili yake inapanuka kutokana na mazingira ya aina tofauti anayokutana nayo.

“Soka limenifanya nipige hatua kubwa sana kimaisha, japokuwa siwezi kusema nimepata hiki na kile, hiyo ndio sababu inayonifanya nisiridhike, pia unapokutana na wachezaji mbalimbali unajifunza vitu vingi, jambo lingine linalonipa nguvu nikiwaona wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu najiuliza mimi nitashindwa nini,” anasema.

Tayari amecheza nchi tatu tofauti Algeria, Misri na Kuwait aliyoielezea ndio iliyomfunza na kumpa ujasiri wa jinsi ya kuishi mbali na Tanzania.

“Nilipata shida sana Kuwait kuzizoea tamaduni zao, hilo halikuwa rahisi kwangu, ingawa ikanifunza nakunifanya niwe najaribu kuchangamkia fursa za nchi mbalimbali,” anasema.

Salamba anasema kutokana na kuzunguka kwake ameanza kujifunza kuzungumza Kiarabu, ili kupata urahisi wa kuwasiliana na wachezaji wenzake.

“Nazungumza baadhi ya maneno, ila kwa asilimia kubwa nasikia kile kinachoongelewa.”

Jambo aliloweza kuwashauri wachezaji wenzake, anawataka wasiogope kwenda kujaribu kusaka maisha nje, ili kupanua wigo wa kufurahia matunda ya vipaji vyao, anaamini hilo liwajenga kujiamini zaidi.

“Mfano mzuri Tanzania wapo wachezaji wa kila aina, kama wao wanakuja nchini kwetu kwa nini sisi tusitoke, wasipuuze majaribio naamini kuna mabadiliko watayaona maishani mwao,”anasema.


ALIFIKIA KWA HIMID

Anasema kwa sasa yupo kwenye mchakato wa kuhamia kwenye nyumba waliomtafutia, baada ya kufikia kwa Himid Mao “Ndio maana nimesema kwamba sijajisikia mpweke, maana nimekaa na Himid na nitahamia nilikotafutiwa nyumba siyo muda mrefu.”

Anaongeza “Na kucheza bado nasubiri ITC kutoka JS Saoura, lakini hilo halijanizuia kufanya mazoezi na kuzingatia ratiba ya timu niliyopo.”

Kabla ya kuanza kucheza nje, timu za Tanzania za Ligi Kuu alizocheza Salamba ni Stand United kabla haijashuka daraja, Lipuli, Simba na Namungo FC.


SIMBA YAMFUNGULIA NJIA

“Nilianza kuonekana na timu za nje baada ya kuanza kuichezea Simba, nilipata ofa nyingi ndipo kwa mara ya kwanza nikaangukia Al Jahra ya Kuwait, pia huko ni kama kulinifunguliwa milango mingine zaidi;

Anaongeza “Kucheza Simba na Yanga ni fursa kubwa kwa wachezaji kujitambulisha nje, maana hizo klabu zina nafasi pana ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ambako zinakutana timu mbalimbali.”

Salamba ambaye kutua kwake Simba kulitokana na kiwango kikubwa alichokionyesha akiwa na Lipuli ya Iringa, anasema kila fursa anayokutana nayo kwenye maisha yake ya soka, anaitazama kwa jicho la hatma ya maisha yake.

“Pengine historia ya maisha yangu ya kushindwa kusoma baada ya wazazi wangu kufariki dunia ndio inayofanya niweke nguvu zaidi ninapoona sehemu kuna nafasi ya kucheza, ndio maana nawasisitiza wachezaji wenzangu wajifunze kuthubutu hakuna linaloshindikana,” anasema.


WALIYOWAHI KUKIPIGA NJE

Straika wa zamani wa Simba, Danny Mrwanda ambaye pia amecheza nje baadhi ya klabu ni Al Tadamon (2008/9) na Dong Tam Long An (2010-2012), anasema kuona fursa katika soka ni uwezo wa mchezaji mwenyewe.

“Kila mchezaji ana uwezo wake wa kutafsiri fursa zilizopo kwenye soka, namuona (Adam) Salamba anapambana na hakati tamaa katika kuhakikisha anakiishi kile anachoona ni ndoto yake.” anasema.