Safari ya Serengeti hadi Kombe la Dunia

New Content Item (1)
New Content Item (1)

TIMU ya Taifa ya Wanawake wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), imeandika historia baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake wa umri huo zitakazofanyika nchini India kuanzia Oktoba 11 hadi 30, mwaka huu.

Mwanaspoti linakuletea safari ya mabinti hawa na kile ambacho wanakwenda kukutana nacho kwenye michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya soka duniani.


SAFARI ILIVYOKUWA

Serengeti Girls ilianza harakati kwa kuifunga Botswana jumla ya mabao 11-0, kisha Burundi mabao 5-2 na hatua ya mwisho ikacheza dhidi ya Cameroon ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 ugenini kabla ya kumalizana nao kwenye mchezo wa mkondo wa pili wikiendi iliyopita iliposhinda kwa bao 1-0 katika Uwanja wa amaan, Zanzibar na kufuzu kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.


SOKONI

Kombe la Dunia ni miongoni mwa michuano inayoangalia na timu nyingi duniani na wachezaji wengi wa Afrika Magharibi wamekuwa wakifaidika nayo kama kupata nafasi ya kucheza soka barani Ulaya, hivyo ikiwa wataupiga mwingi na kuonyesha viwango bora kwenye michuano hii wengi wao wanaweza kupata nafasi ya kubadilisha maisha yao ya soka na kutimiza ndoto kwa kupata nafasi ya kucheza katika nchi mbalimbali zilizoendelea kisoka.


WAMEMALIZA KIHESHIMA

Serengeti Girls imemaliza huku ikiwa na heshima ya straika wao, Clara Luvanga kuwa mfungaji kinara wa michuano ya kufuzu kwani hadi sasa ana mabao 10, nyuma ya binti wa Kinigeria, Opeyemi Ajakaye aliyemaliza na mabao sita. Pia Neema Paul naye amemaliza michuano hii katika nafasi za juu za wafungaji bora kwa mabao matano akifuatiwa na Aisha Juma aliyefunga mabao matatu na akashindwa kuendelea kutupia zaidi kutokana na majeraha.KAMBI YA KIBABE

Moja kati ya mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangia hamasa ya mabinti hawa na viwango vyao uwanjani ni kambi walizoweka eneo la Karatu mkoani Arusha na Unguja kule Zanzibar.

Mazingira ya maeneo yote yaliakisi moja kwa moja kile nchi mbalimbali walizokwenda kucheza na kufanikiwa kutimiza lengo.

Mfano ni mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Cameroon ambapo kabla ya kusafiri kambi ilikuwa mkoani Arusha ambapo kulikuwa na mazingira ya baridi sawa na nchini Cameroon ambako kulikuwa na mazingira ya baridi pia na hadi siku waliyokwenda kucheza mechi.


WANAOKUTANA NAO

Tayari wawakilishi wa mabara yote washajulikana na timu zilizofuzu kwa ujumla zinafahamika na droo ya hatua ya makundi inatarajiwa kufanyika nchini Uswisi yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Juni, 24 jijini Zurich.UEFA

Hispania, Ufaransa na Ujerumani


OCENIA

New Zealand


CONMEBOL

Brazil, Chile, Colombia


CONCACAF

Canada, Mexico na Marekani


CAF

Tanzania, Nigeria na Morocco


AFC

India, China na Japan


WAENDAKO

Michuano hii mikubwa itafanyika kwenye miji mitatu nchini India na viwanja vitatu ambavyo ni Kalinga Stadium kilichopo jijini Odisha, Pandit Jawaharlal Nehru kilichopo Goa na DY Patil Stadium cha Navi Mumbai.


HISTORIA YA MICHUANO

Kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia kwa wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17, ilifanyika 2008 ambapo Korea Kaskazini ilifanikiwa kuibuka mabingwa kwa kuichapa Marekani katika mchezo wa fainali.

Korea Kusini iliibuka bingwa wa mashindano ya mara ya pili yaliyofanyika Trinidad and Tobago 2010 wakati Ufaransa ikichukua ubingwa kwenye michuano iliyofanyika Azerbaijan 2012.

Japan ilikuwa bingwa 2014 kwenye michuano ya Costa Rica, kisha 2016 Korea Kusini ikachukua ubingwa wa pili katika fainali zilizopigwa nchini Jordan na mwaka 2018 Hispania ambayo ndio bingwa mtetezi ikafanikiwa kuchukua taji hilo kwa mara kwanza kwenye michuano iliyopigwa nchini Uruguay.

Hivyo timu tishio zaidi kwenye michuano hii ambazo zimefuzu kutoka mabara mbalimbali ni Ufaransa, Hispania na Japan ambazo zote zimewahi kuchukua kombe hilo.