Safari ya miaka 10 ya Guardiola Man City
Muktasari:
- Wiki hii kumekuwapo na habari nyingi juu kile kinachodaiwa kwamba ni uamuzi wa ghafla wa gwiji huyo wa Barcelona kuondoka, lakini kigugumizi kimeendelea kuwapo nyuma ya kuondoka kwake na hata mwenyewe amekuwa kuzungumzia hilo.
MANCHESTER, ENGLAND: WAKATI Arsenal tayari wameshabeba ubingwa wa Ligi Kuu England huku wakiwa na mchezo mmoja mkono wakihitimisha idadi ya timu zilizotwaa ndoo katika ligi tano bora Ulaya, habari nyingine kubwa inayojadiliwa kwa sasa ni juu ya kocha wa manchester City, Pep Guardiola anavyoondoka katika kikosi hicho baada ya kudumua kwa miaka 10.
Wiki hii kumekuwapo na habari nyingi juu kile kinachodaiwa kwamba ni uamuzi wa ghafla wa gwiji huyo wa Barcelona kuondoka, lakini kigugumizi kimeendelea kuwapo nyuma ya kuondoka kwake na hata mwenyewe amekuwa kuzungumzia hilo.
Mhispania huyo anatarajiwa kuondoka City baada ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa Jumapili ijayo, hatua ambayo itahitimisha moja ya vipindi vya mafanikio makubwa zaidi katika historia ya soka la England katika Uwanja wa Etihad unaomilikiwa na klabu hiyo.
Juzi mara baada ya mechi dhidi ya Bournemouth kumalizika alipoulizwa kuhusu mustakabali wake kufuatia sare ya 1-1 Guardiola aliwazungusha wanahabari na kuashiria kana kwamba bado yupoyupo sana.
“Naweza kusema nina mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wangu. Nimekuwa katika nafasi hii kwa miaka mingi sana. Kutokana na uzoefu wangu, kutangaza jambo kama hili wakati mashindano yanaendelea siyo jambo zuri,”€ alisema na kuongeza:
“Mtu wa kwanza ninayepaswa kuzungumza naye ni mwenyekiti wangu (wa klabu). Tutakapomaliza msimu tutaona na tutazungumza. Ni rahisi hivyo. Baada ya hapo tutafanya uamuzi. Sitawaambia hapa kwa sababu lazima kwanza nizungumze na mwenyekiti wangu, wachezaji wangu na benchi la ufundi.”€
Guardiola pia alisema: “Mimi ndiye mtu mwenye furaha zaidi duniani kuwa katika klabu hii. Klabu hii ni ya kipekee sana.”€
Na juzi hiyohiyo, Pep Guardiola aliondoka uwanjani huku timu ikiendelea kuwapongeza mashabiki waliokuwepo uwanjani, na kitendo hicho mara moja kilizua wasiwasi kuhusu mustakabali wake.
Picha zilimuonyesha Guardiola akielekea kwenye handaki la kuelekea vyumbani, katika tukio ambalo wengi walilitafsiri kama ishara au alama ya jambo linaloweza kutokea, hasa ikizingatiwa kuwa limetokea wakati ambao tetesi kuhusu kocha huyo Mhispania kuondoka mwishoni mwa msimu zinazidi kushika kasi.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 ametwaa mataji makubwa 17, na jumla ya mataji 20 tangu alipotua Man City 2016 yakiwemo sita ya Ligi Kuu England.
Pia aliiongoza kutwaa taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2023 baada ya kuifunga Inter Milan, na hivyo kupata taji lake la tatu la Ulaya akiwa kocha, baada ya kuwa na mafanikio mawili kama hayo akiwa na Barcelona. Taji lake la karibuni lilikuja wikiendi iliyopita wakati bao la Antoine Semenyo lilipoisaidia City kuifunga Chelsea kwa mabao 1-0 katika fainali ya FA.
Hata hivyo, kipindi chake Man City kimegubikwa pia na tuhuma za ukiukwaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England, ambapo 2023 walifunguliwa mashtaka zaidi ya 100 yanayohusiana na madai ya ukiukwaji wa sheria kati ya 2009 hadi 2018. Kesi hiyo ilisikilizwa na tume huru hadi Desemba 2024, huku uamuzi ukitarajiwa kutolewa mwaka huu.
Iwapo ataondoka, Guardiola anaweza kuchukua mapumziko kutoka kwenye soka, kama alivyofanya kati ya kuondoka Barcelona na kujiunga na Bayern Munich 2013. Ushindani wake mkubwa England umeonekana zaidi kupitia vita yake dhidi ya Liverpool na hasa kocha Jurgen Klopp. Miongoni mwa kumbukumbu kubwa ni ubingwa wa 2019 ambapo City walitwaa taji kwa tofauti ya pointi moja licha ya Liverpool kupata pointi 97.
Guardiola pia alivunja rekodi ya pointi 100 katika msimu wa 2018 na kuwa kocha wa kwanza katika historia ya soka la England kushinda mataji manne ya ligi kuu mfululizo.
Kabla ya fainali ya FA, alipoulizwa kama kipindi chake Man City kina ubora wa kipekee, Guardiola alisema: “Ndiyo, bila shaka. Mataji 19 ndani ya miaka 10 siyo mbaya. (Mashabiki) wanajua hawahitaji kusubiri mpaka niondoke ndipo watambue nimewafurahisha. Mataji 19, tukipigania la 20 ndani ya miaka 10 siyo mbaya, kwa kweli.”€
Kuondoka kwake kutaacha nafasi kubwa kuzibwa, huku City wakitajwa kuangalia makocha kadhaa akiwemo aliyewahi kuwa msaidizi wake Enzo Maresca. Pia kocha wa Bayern Munich, Vincent Kompany, ambaye ni gwiji wa City kama mchezaji chini ya Guardiola anatajwa miongoni mwa wanaoweza kupewa nafasi hiyo. Vilevile jina la kocha wa Bournemouth ambaye tayari keshaaga kwamba hatakuwapo kikosini msimu ujao, Andoni Iraola anatajwa kuwa katika orodha.