SADIO MANE... Alivyogeuka shujaa wa Senegal AFCON 2025
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich alitwaa taji lake la pili la Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Jumapili, baada ya Simba wa Teranga kuifunga nchi mwenyeji Morocco bao 1-0 katika fainali iliyojaa utata.
RABAT, MOROCCO: SADIO Mane amekuwa shujaa wa Senegal kwa mara nyingine tena, lakini si kwa sababu ambazo wengi wangezitarajia.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich alitwaa taji lake la pili la Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Jumapili, baada ya Simba wa Teranga kuifunga nchi mwenyeji Morocco bao 1-0 katika fainali iliyojaa utata.
Katika dakika za majeruhi, kocha mkuu wa Senegal, Pape Thiaw alijaribu kuwaongoza wachezaji wake waondoke uwanjani baada ya Morocco kupewa penalti katika dakika ya 98, pale beki El Hadji Malick Diouf alipomwangusha Brahim Diaz ndani ya boksi.
Wachezaji wa Senegal walipokuwa tayari wamerudi vyumbani, Mane alionekana akiingia humo kwa kukimbia na kisha kuwaongoza kurejea uwanjani, akisaidiwa na kipa Edouard Mendy. Takribani dakika 16 baada ya penalti kuamuliwa, penalti ya Panenka ya Díaz ilidakwa kwa urahisi na Mendy katika tukio la kusikitisha kwa mmoja wa nyota wa mashindano.
Mchezo ulipokuwa 0-0, ulienda muda wa ziada. Pape Gueye alipiga shuti kali lililozaa bao la ushindi na kuhakikisha taji linakwenda Senegal kwa namna ya kusisimua. Mane, ambaye amesema Afcon hii itakuwa ya mwisho kwake, alimaliza kama kiongozi baada ya kuvikwa kitambaa cha unahodha na wachezaji wenzake kabla ya kuinua kombe.
Alisema: “Soka ni kitu cha kipekee. Dunia ilikuwa inatazama, dunia inapenda soka na soka ni furaha, hivyo tunapaswa kutoa taswira nzuri ya mchezo huu.
Ingekuwa ni wazimu kuacha kucheza mechi hii kwa sababu tu refa ametoa penalti. Hilo lingekuwa jambo baya sana, hasa kwa soka la Afrika. Ningependelea kupoteza kuliko kuona jambo kama hilo likitokea kwenye soka letu.
Ni jambo baya sana. Soka halipaswi kusimama hata kwa dakika kumi, lakini tufanye nini? Cha muhimu ni kwamba tulirudi, tukacheza na kilichotokea kikatokea.”
Mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi, alisema: “Mane alijitolea zaidi kuhakikisha timu yake inarudi uwanjani, na hilo limewaletea mafanikio.
Ni balozi wa kweli wa soka. Tunajua alivyo nje ya uwanja, na anajua maana halisi ya soka.”
Mchezaji wa zamani wa Morocco, Hassan Kachloul, alisema: “Soka la Afrika na soka la dunia vilikuwa vinapoteza, hadi Mane alipoingilia kati.
Aliliambia E4: “Kile nilichokipenda zaidi ni mchezaji pekee wa Senegal alikuwa Sadio Mane. Hilo linaonyesha ukubwa wa mtu alivyo. Alirudi vyumbani na akawaleta wachezaji wote uwanjani. Mane ndiye aliyewarejesha.”
Mahali ilipoanzia hadithi ya Senegal
Kwa Mane, yote yalianzia Bambali. Ni kusini-magharibi mwa Senegal ambako alianza kucheza soka kwenye mitaa yenye udongo mwekundu na viwanja vya mchanga na ambako akiwa na umri wa miaka 13 alitazama comeback maarufu ya Liverpool dhidi ya AC Milan kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2005.
Tangu wakati huo ameendelea kushinda Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu ya England akiwa na Liverpool, pamoja na mataji mawili ya Afcon akiwa na Simba wa Teranga. Mane alifunga penalti ya ushindi dhidi ya Misri kwenye fainali ya Afcon 2021 na akaielezea kama: “Siku bora zaidi ya maisha yangu na taji bora zaidi maishani mwangu.”
Uwanja uliopewa jina lake ulijengwa katika mji wa Sedhiou, chini ya kilomita 20 kutoka alikozaliwa, kama heshima kwa mafanikio yake. Sasa akiwa bingwa mara mbili na mwenye umri wa miaka 33, Mane amehitimisha safari yake ya Afcon kwa kilele cha mafanikio.
Lakini Gueye anasema kikosi kinapanga kumshawishi Mane, ambaye alimwita “gwiji wa Senegal”, abadili mawazo yake na abaki hadi Afcon 2027 itakayofanyika Kenya, Tanzania na Uganda.
“Tutajaribu kumbakiza nasi kwa muda mrefu zaidi, kwa sababu bado ana miaka mizuri ya kutoa,” alisema mchezaji wa Villarreal mwenye umri wa miaka 26 akiiambia BBC Afrique.
Mtu mnyenyekevu na mwenye moyo wa kutoa
Mane, ambaye sasa anacheza soka Saudi Arabia katika klabu ya Al-Nassr, ana mafanikio mengi lakini hajawahi kusahau alikotoka.
Amejipatia heshima kubwa Bambali kwa kujitolea kujenga hospitali na shule, kuchangia ujenzi wa misikiti, kusaidia mapambano dhidi ya uviko 19, na kutuma jezi 300 za Liverpool kijijini kwake kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa 2018.
“Akija hapa, anajituma kama mtu wa kawaida kabisa,” alisema Fode Boucar Dahaba, rais wa ligi ya kanda na kuongeza: “Hapendi kujionyesha. Kijiji kinamrudishia mapenzi hayo.”
Familia yake inamuelezea kama mtu “anayefanya kazi kwa ajili ya kila mtu” na “Mwislamu mwema.”
Hilo lilionekana England aliposaidia kusafisha vyoo katika msikiti wa Toxteth baada ya ushindi wa Liverpool.
“Hakufanya kwa ajili ya umaarufu,” alisema imam Abu Usamah Al-Tahabi.
“Hana majivuno.”
Senegal wanatarajia mchango wake
Mane ana zaidi ya mechi 120 za kimataifa na ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Senegal akiwa na mabao 53.
Atacheza Kombe la Dunia 2026, na anaendelea kuwa nguvu muhimu, hasa ubunifu wake. Bao lake la dakika ya 78 dhidi ya Misri liliipeleka Senegal fainali.
“Hicho ndicho tunachotarajia kutoka kwake,” alisema Idrissa Gana Gueye.
“Ni mchezaji mkubwa na lazima aonyeshe ubora wake kwenye mechi kubwa.”
Ingawa si nahodha rasmi, Mane anapozungumza wenzake humsikiliza.
“Hotuba yake kabla ya mechi ilituhamasisha sana,” alisema Pape Gueye.
“Ana uzoefu wa mechi kubwa na anajua kututuliza.”
Kocha Pape Thiaw alisema: “Nadhani uamuzi wake aliutoa kwa hisia. Taifa halikubaliani, na mimi kama kocha sikubaliani kabisa. Tunataka abaki nasi kwa muda mrefu iwezekanavyo.”