Prime
Kutoka Marc-vivien Foe mpaka Che Malone, Afrika inaanguka
ZIPO nyakati unakubali kuonekana kichaa. Ni kazi ngumu, lakini mwanadamu anapaswa kuifanya. Niliandika mahala katika mitandao ya kijamii kwamba Taifa Stars itapita katika kundi lake pale Morocco. Nilionekana mwehu kwa sababu pambano la mwisho la kundi Stars walikuwa wanacheza na Tunisia.
Ni kweli Stars wamemaliza kama ‘best looser’ katika kundi lao. Ni kweli wamemaliza bila kushinda mechi yoyote ile.
Kilichowakatisha watu tamaa wakati huo Stars wakiwa na pointi moja tu mkononi ni kwamba mechi ya mwisho walikuwa wanacheza na Tunisia. Binafsi nilianza ukichaa kwa kuamini kwamba Stars wangeweza kushinda mechi hiyo. Hata hivyo, waliishia kutoka sare ya bao 1-1.
Bado waliweza kupita. Kufikiria kwamba Stars ingeweza kushinda ilionekana kama ukichaa. Kufikiria kama wangeweza kukwepa kipigo ilionekana kama wendawazimu. Ni kwa sababu watu wamekariri majina makubwa ya nchi fulani za Afrika.
Watu wanaishi na majinamizi ambayo hayapo tena. Tunisia ya leo sio ile ya zamani wakati ule wakiwa na kina Hatem Trabelsi na Raidh Jaidi.
Niliwatazama mechi mbili dhidi ya Uganda kisha Nigeria na nikaiona nafasi ya Tanzania. Kuna mambo mawili hapa. Kwanza ni kwa sababu kuna namna Tanzania imeimarika.
Tuna wachezaji wengi waliopitia soka la vijana na hawaugopi mpira. Mpira unatembea. Pili tuna wachezaji wengi kadhaa wakiongozwa na Mbwana Samatta ambao wanacheza nje. Wamezoea mikikimikiki ya mechi kama hizi.
Tatu tuna wachezaji wa ndani wa ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika michuano ya CAF kupitia klabu zao. Lakini kikubwa zaidi mpira wa Afrika kwa namna fulani umeshuka. Haueleweki. Wakubwa wamekuwa kama wadogo na wadogo wamekuwa kama wakubwa. Comoro imekuwa kama Cameroon na Cameroon imekuwa kama Comoro.
Afrika ya leo pambano la Tunisia na Tanzania ni gumu. Afrika ya leo pambano la Madagascar na Ghana halitabiriki. Binafsi naamini kuna wakubwa wengi ambao wameanguka kimpira. Tunisia ni miongoni mwao. Cameroon ni miongoni mwao. Ghana ni miongoni mwao. Nigeria ni miongoni mwao. Ivory Coast ni miongoni mwao.
Utajiuliza kwanini nimeitaja nchi kama Ghana. Ndiyo, wao na Cape verde wamefuzu kwenda Kombe la Dunia. Sasa inawezekana vipi ukafuzu Kombe la dDunia halafu ukashindwa kufuzu kwenda Afcon? Kuna tatizo mahala. Ukosefu wa mwendelezo wa ubora au ubahatishaji. Hiki ni miongoni mwa viashiria kwamba mpira wa Afrika haueleweki kwa sasa.
Wakubwa wameanguka kwa kiasi kikubwa. Bila kumkosea heshima Che Malone Fondo. Beki wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa amekwenda kucheza soka lake Afrika Kaskazini. Sasa hivi anazima kama beki wa kati wa Cameroon. Anavaa jezi ya indomitable Lions kama beki wa kati. Sio mchezaji wa kiwango hicho.
Akiwa Tanzania Che Malone hajaacha hata alama katika klabu yake ya Simba. Hauwezi kumuweka katika kundi moja na Serge Wawa Pascal, Joash Onyango, Victor Costa, Boniface Pawassa, Joseph Owino na wengineo waliopita Simba ndani ya miaka 20 iliyopita. Leo, Che Malone anazima kama beki wa kati katika kikosi cha Cameroon.
Ndani ya miaka hii ishirini Cameroon ilikuwa na kina Marc-vivien Foe, Samuel Eto’o, Geremi Njitap, Raymond Kalla, Solomoni Olembe na wengineo. Wachezaji wote walikuwa wanacheza Ulaya.
Katika nafasi ambayo leo Che Malone anacheza kulikuwa na wachezaji kibao kutoka Ulaya ambao walikuwa hawawezi hata kuitwa. Leo mchezaji anacheza USMA Alger anazima katika safu ya ulinzi ya Cameroon. Tanzania tumemuona. Hakuwa na maajabu makubwa.
Mtazame mchezaji anayeitwa Pacome Zouzoua. Ni fundi wa mpira hasa. Lakini katika kiwango hiki hiki alichonacho asingeweza kuitwa katika kikosi cha Ivory Coast ya miaka kadhaa iliyopita katika mechi za kirafiki ambazo aliitwa karibuni. Wakati ule wa kina Didier Zokora, Yaya Toure, Didier Drogba, Solomon Kalou na wengineo lukuki.
Bila kumkosea heshima Pacome. Licha ya uhodari wake, lakini nafasi yake ingezibwa na mastaa kutoka Ulaya au Asia. Mataifa ya Afrika Magharibi yamesheheni wachezaji wa Ulaya.
Kwao kumuita mchezaji anayecheza nje halafu Afrika Mashariki, halikuwa jambo lao. Waliokuwa wanapata bahati hizo ni makipa kwa sababu watu wa Afrika Magharibi hawajapeleka makipa wengi nje.
Kuna tatizo kule kwa wakubwa ndio maana sishangai sare ya Taifa Stars na Tunisia. Kwa mfano, zamani wachezaji wetu wakubwa wa Afrika walikuwa wamejaa katika timu kubwa za Ulaya.
Arsenal kulikuwa na Nwankwo Kanu, Laurent Etame Mayer na Kolo Toure. Leo Arsenal haina hata mchezaji mmoja kutoka Afrika.
Zamani Didier Droba, Solomon Kalou, Michael Essien na Obi Mikel walikuwa wanacheza Chelsea. Baada ya mechi za kalenda ya Fifa tajiri Roman Abramovich alikuwa anawatumia ndege yake binafsi kuwakusanya kutoka Afrika ili wawahi kurudi Stamford Bridge. Leo Chelsea kuna nani?
Barcelona ilikuwa na Samuel Etoo, Real Madrid ilikuwa na kina Geremi Njitap. Liverpool iliwahi kuwa na Salif Diao na El Hadji Diouf.
Baadaye imebebwa na Sadio Mane na Mo Salah. Lakini wakati huu Salah akiishia, leo kutakuwa na nani pale Liverpool? Afrika haina tena wachezaji wakubwa katika timu kubwa za wakoloni wetu.
Zamani kucheza Marseille, Napoli, Anderlecht au Porto kulikuwa hakukupi uhakika sana wa kuanza kama beki wa kati Cameroon, lakini leo Che Malone anaanza vizuri tu pale Cameroon. Kwanini mechi ya Cameroon na Madagascar isiwe ngumu? Kwanini Stars lazima ifungwe na Tunisia? Hakuna ulazima huo.
Kuna staa gani wa Tunisia ambaye anakipiga katika timu kubwa na ni gumzo kama vile ambavyo Mo Salah alikuwa gumzo pale Anfield? Hata hizi timu za kawaida hawapo sana. Ndio maana walinyanyasika wakati walipocheza na Nigeria ambayo walau ina kina Victor Osimhen, Alex Iwobi, Samuel Ezechukwu, Wilfred Ndidi na wengineo.
Nchi za Afrika ambazo unaweza kuzihofia na kuzitabiria makubwa ni Senegal na Morocco. Kule Senegal bado kuna wanaume. Kina Sadio Mane, Idrissa Gana Gueye, Khalidou Koulibaly, Eduardo Mendy na wengineo wengi ambao wanacheza Ulaya na kutamba. Wapo ambao wametamba katika klabu kubwa.
Morocco kuna watoto waliozaliwa Ulaya kina Achraf Hakimi lakini pia wana mfumo wa uzalishaji wa wachezaji ambao umewafanya watambe katika michuano mingi Afrika. Sio timu ya wakubwa tu, bali hata timu za vijana na wanawake. Moja kati ya Morocco au Senegal inaweza kuchukua taji hili moja kwa moja.
Lakini kwa timu ambayo imeanguka kutoka kwa Rigobert Song hadi Che Malone sidhani kama inaweza kuambulia chochote.
Timu iliyotoka kwa kina Marc-vivien Foe hadi Che Malone nadhani ina tatizo kubwa. Tatizo la msingi. Tatizo ambalo limesambaa Afrika na sasa Tanzania inaweza kutoka sare na Tunisia huku kipa wa Tanzania asiwe mchezaji bora wa mchezo.