Prime
Luca Zidane amekimbilia Afrika, wazungu sio wanafiki
KWAMBA nyoka anazaa nyoka? Nadhani ni msemo tu. Usiutilie sana maanani. Wakati mwingine nyoka anaweza kuzaa mjusi bila ya kujijua. Imetokea katika soka mara nyingi tu. Kitu kinachoitwa 'like father like son' huwa hakitimii kwa kiwango kile kile kinachotakikana. Wote wanaweza kuwa katika fani moja, lakini uwezo ukawa mbingu na ardhi.
Majuzi nilimwona Zinedine Zidane akiwa jukwaani pale Morocco akimtazama mwanae, Luca Zidane akiwa katika jezi ya timu ya taifa ya Algeria katika pambano dhidi ya Sudan. Niliendelea kujikumbusha jambo hili. Ni wanasoka wachache duniani ambao baba zao walikuwa wanacheza soka na wao wakafikia viwango vya baba zao.
Luca naye ameshindwa. Hayupo Morocco kwa bahati mbaya. Wazungu sio wanafiki. Luca angeweza kucheza katika timu za taifa za Ufaransa, Hispania au hii Algeria ambayo anachezea kwa sasa. Mama yake Veronique ni Mhispaniola. Baba yake Zidane ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria. Luca alikuwa na machaguo matatu.
Kama ingekuwa hiyari yake au kama angekuwa bora zaidi nadhani angechagua kucheza Ufaransa au Hispania. Kule kunakupa nafasi ya kukaribia kushinda fainali za Kombe la Dunia. Kunakupa nafasi ya kucheza pia Kombe la Dunia mara kwa mara. Hata hivyo, Luca alishindwa mapema.
Kitendo cha kuchagua kuwa kipa wakati baba yake alikuwa fundi ndani ni ishara tosha alijiona hatoshi katika nafasi za ndani tangu akiwa mdogo akakimbilia kuwa kipa.
Faida wanayoipata watoto wa mastaa ni nafasi wanazopewa kufanya mazoezi katika timu za vijana za baba zao. Asubuhi wanaamka pamoja na wanapanda Limousine moja kwenda mazoezini.
Wakati baba anafanya mazoezi katika timu ya wakubwa mtoto anakwenda katika timu ya watoto. Ni nafasi ambayo kijana wa Dakar, Douala, Bamako, Dar es Salaam hawezi kuipata. Inabidi apambane kweli kweli kufika Ulaya na kuonyesha kiwango chake.
Hata hivyo, wazungu sio wanafiki. Mbele ya safari hautafanikiwa kwa sababu ya jina la baba yako. Utafanikiwa kwa sababu ya uwezo wako. Ndiyo maana Luca amejikuta Morocco akiwa na jezi ya Algeria. Usidhani kama alipenda sana.
Na katika ngazi ya klabu anacheza Daraja la Kwanza katika klabu ya Granada. Siyo bahati mbaya. Angekuwa hodari wa kiasi hicho angeweza kuwa Real Madrid, Manchester City, Aston Villa au kwingineko.
Na imemchukua muda kukubali ukweli, lazima arudi kwa babu zake ndiyo apate nafasi ya kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa.
Mwanzoni mchezaji wa aina ya Luca huwa anapambana kweli kweli kusaka nafasi katika kikosi cha wakubwa. Ukiangalia katika Wikipedia unamuona namna alivyocheza katika timu za vijana za Hispania. Giza linapoanza kutanda ndipo wanapotafuta shuka.
Kwa sasa ana miaka 27 na mechi yake ya kwanza ya timu ya taifa amecheza mwaka jana tu dhidi ha Uganda.
Ina maana Algeria ni chaguo lake la pili, lakini muda wote alikuwa anasubiri kuona kama atafikia uwezo wa kucheza katika chaguo lake la kwanza Ufaransa.
Haikuwezekana. Ni kama ambavyo kuna wachezaji wanakuja kucheza Afrika kwa sababu hawatoshi katika timu za wazungu. Hawa ndio kina Aaron Wan Bissaka, Inaki Williams na wengineo.
Luca ana kaka yake anaitwa Enzo. Naye ni hivi hivi. Tena afadhali ya Luca kuliko Enzo. Enzo tulimsubiri zaidi kwa sababu alikuwa mtoto wa kwanza wa Zidane.
Tulidhani angeweza kufikia walau robo ya uwezo wa baba yake, lakini haikuwezekana. Alikuwa ovyo tu na akaishia kucheza timu za madaraja ya chini. Sasa hivi ana miaka 30 lakini hana timu. Mpira umemshinda.
Wako wapi watoto wa David Beckham? Kina Brooklyn walinyoosha mikono juu. Walipata nafasi ya kucheza katika timu za vijana za Real Madrid, LA Galaxy, Arsenal na kwingineko lakini haikuwezekana. Wazungu sio wanafiki. Hawawezi kukupeleka katika kiwango cha baba yako kama haujawahi kufika huko.
Kwa sasa pia tunamsubiri Kai Wayne Rooney. Amefikisha miaka 16. Ambacho kinatushtua kidogo ni kwamba baba yake akiwa na umri wa miaka 16 alishaanza kuishika Ligi Kuu England akiwa na jezi ya Everton.
Yeye hadi sasa hivi hajaanza kufanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha Manchester United. Tumemwona mtoto wa Darren Fletcher, Jack Fletcher akicheza pambano lake la kwanza jezi ya United, lakini Kai bado.
Wakati mwingine watoto wenyewe wamedai presha inakuwa kubwa sana kwao kwa sababu mashabiki wamekuwa wakitazamia wao wafanye mambo ambayo baba zao walikuwa wakifanya uwanjani.
Wakati mwingine pia kadri unavyojaribu kujipambanua wewe mwenyewe bado unaishia kuonekana 'mtoto wa Rooney' kuliko kutambulika wewe kama wewe.
Mfano ni kama Luca akiwa Algeria au popote anapokwenda. Anatambulika zaidi kama 'mtoto wa Zidane' kuliko kutambulika kama kipa wa Algeria.
Hata katika michuano hii atatambulika zaidi kama 'mtoto wa Zidane' kuliko ubora ambao atajaribu kuuonyesha katika lango la Algeria. Kisaikolojia hili nalo ni tatizo kubwa kwao.
Hata hivyo, kuna mastaa wa zamani ambao watoto wao wamekuwa wakali kuliko wao. Hizi kesi si nyingi na unatazama nyuma na kugundua hata ubora wa baba zao haukuwa kama huu wa kina Zidane.
Mfano mmojawapo ni Erling Haaland. Baba yake, Erling Haaland alikuwa mchezaji mzuri Leeds na Manchester City lakini sio kiwango cha kuimbwa kama kina Beckham. Hata hivyo, mtoto wake amekuwa mkubwa zaidi kuliko yeye.
Wengine huenda hawajawa wakubwa zaidi lakini wanabebwa zaidi na ubora wao. Mfano ni mtoto wa Diego Simeone, Giuliano Simeone.
Ni mtaalamu haswa na haonekani kama anabebwa na jina la baba yake. Yupo Atletico Madrid na baba yake, lakini haonekani kama anatembelea nyota ya baba yake. Uwezo wake uwanjani umekuwa ukijipambanua wenyewe na amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Atletico.
Wazungu sio wanafiki. Kama angekuwa hatoshi wangemwambia Diego Simeone aachane na mwanae. Kuna idara nyingi zinazofanikisha uhamisho wa mchezaji.
Kuna kiasi kikubwa cha pesa za uhamisho na mshahara wa mchezaji. Hauwezi kumpendelea mwanao na watu wakakutazama tu.
Hii 'like father like son' imeshindwa kufanya kazi hata katika michezo mingine. Mfano ni mtoto wa bingwa wa zamani wa mbio za magari, Michael Schumacher, Mick Schumacher. Hajawahi kufika ubora wa baba yake ambaye alisumbua vilivyo katika mbio za magari. Yeye amekuwa wa kawaida tu.
Pale katika mchezo wa kikapu Marekani, rafiki yetu LeBron James amelazimisha kadri alivyoweza ili acheze na mwanae, Bronny James lakini ni wazi kwamba LeBron amelazimisha tu kwa ajili ya kuweka historia ya kwamba alicheza na mwanae katika timu moja. Kiwango cha Broony kimeonekana kuwa cha kawaida tu kwa watu wanaoufahamu mchezo wa kikapu.