Roberto: Kibabu cha miaka 63 kinachoendelea kukipiga
Muktasari:
- Ni kama tu ule msemo wa avumaye baharini papa, lakini wengine wapo kwani unaambiwa kuna mwamba mmoja anayemfunika Miura kwa kuwa mchezaji mkongwe zaidi anayeendelea kukiwasha uwanjani.
MONTEVIDEO, URUGUAY: SIO mchezo. Licha ya mashabiki na wapenzi wengi wa soka kuamini Mjapan Kazuyoshi Miura ndiye mchezaji wa soka mwenye umri mkubwa zaidi, mambo sivyo yalivyo.
Ni kama tu ule msemo wa avumaye baharini papa, lakini wengine wapo kwani unaambiwa kuna mwamba mmoja anayemfunika Miura kwa kuwa mchezaji mkongwe zaidi anayeendelea kukiwasha uwanjani.
Ndiyo, mwamba anayeshikilia rekodi ya dunia iliyowekwa kwenye kitabu cha Guiness hadi sasa, ni Roberto Carmona raia wa Uruguay.
Carmona, kwa sasa ana umri wa miaka 63 akiwa amecheza zaidi ya mechi 2200 akiwa na timu 51 tangu mwaka 1980 hadi sasa.
Fundi huyu ambaye alizaliwa Aprili, 30, 1962 kwa sasa anaichezea Liffa Club inayoshiriki Ligi Daraja la nne huko Uruguay lakini kabla ya hapo, enzi za ujana wake amewahi kucheza timu mbalimbali za nchi kama Marekani, Canada, Hispania na Italia kwa nyakati tofauti tofauti pamoja na timu za Uruguay.
Haya hapa ni mahojiano yake, akielezea vitu vinavyomhusu ikiwemo lishe yake na siri ya kuendelea kucheza hadi sasa.
SIRI YA KUCHEZA HADI SASA
Robert anasema hadhani kama anaweza kuiita siri na badala yake anaona kama ameteuliwa tu na Mungu, wala siyo kwa uwezo wake.
“Imani yangu inanifanya nifikiri hakuna kinachotokea kwa bahati, kila kitu kina kusudio lake, mimi naona ni Mungu tu amenijaalia kuwa katika hali bora kimwili na kiakili hadi kuendelea kucheza soka la kiushindani kufikia sasa.”
Mbali ya kuamini ameteuliwa na Mungu, fundi huyu anasema pia amekuwa akifanya juhudi na kuzingatia mambo muhimu kama nidhamu, weledi, kujitoa, umakini, upendo na heshima si tu kwa klabu anayoitumikia, bali katika maisha kwa jumla.
“Hii ni pamoja na kukaa mbali na dawa za kulevya na pombe, kuishi kama mchezaji na kufuata lishe bora. Hakuna ‘siri’ iliyojicha katika soka au maisha yangu.”
LISHE YAKE IKOJE?
“Sifuatii mpangilio maalum wala sina na sijawahi kuwa na mtaalamu wa lishe. Najitunza mwenyewe, sili vyakula vya kukaanga wala vyenye mafuta yenye lehemu nyingi, sinywi soda, pombe au sigara na siweki chumvi wala sukari kwenye chakula changu na sili najitahidi sana kutokula vyakula ambavyo vina vitu hivyo kiasili,” alisema Carmona na kuongeza;
“Mbali ya mambo mengine, kwa asilimia kubwa naweza kusema utimamu wangu wa kimwili unachagiwa sana na lishe yangu.”
JE ANAFIKIRIA KUSTAAFU
Lejendi huyu anasema mara nyingi watu wamekuwa wakimuuliza kuhusu kustaafu, lakini anasisitiza hafikiri hilo kwa sasa.
“Siishi kwa kuangalia saa wala umri wangu, akili yangu haifikirii kuhusu kufanya hivyo na moyoni naamini bado nina nguvu na maadam nina nguvu na nipo hai nitaendelea kucheza hadi dakika ya mwisho.
Kustaafu si uamuzi wangu ni uamuzi utakaotoka kwa Mungu.”
CHANGAMOTO YA KUDHARAULIWA
Robert anafunguka baadhi ya wachezaji wa timu pinzani au hata mashabiki wao humdharau na kumtukana, lakini jambo hilo halimuathiri hata kidogo kwani ana ukomavu mkubwa wa kiakili.
“Mwishowe, wale waliokuwa wakinidharau kabla ya mechi, huishia kuomba kupiga picha nami au kunipongeza. Maisha yangu ya kila siku ni kama mtihani kwa sababu kitendo cha kushikilia rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi hakiishii pale Kiwanjani bali unapaswa kuwa mfano wa kuigwa hata nje ya Uwanja.”
VITU ANAVYOPENDA
“Ndiyo kuna vitu ninavyopenda nje ya soka. Nilipokuwa mdogo nilikuwa napenda kuendesha pikipiki na kusafiri kwa kutumia barabara, kwa sasa hilo pia ndiyo jambo ninalopenda ingawa nimekuwa zaidi nikiendesha magari yangu kwenda safari ndefu nikiwa na familia au peke yangu.”
Pia anasema anapenda kwenda sinema, kula chakula cha pamoja na familia, kutazama filamu nyumbani na kutumia muda mwingi na mke wake na watoto.
FAMILIA YAKE INASEMAJE?
Carmona anasema familia yake ndiyo nguzo yake kuu na mkewe pamoja na watoto na ndio wamekuwa wakimsaidia katika kumhudumia na kumpa ushauri wa mambo mbalimbali na hawataki kuona akistaafu.
“Hawataki niache soka. Badala yake, wananitia moyo na wamekuwa wakionyesha kuchanganyikiwa pale ninapopata majeraha. Kila siku wananiambia nijitahidi kuwa mwangalifu na yote kwa yote huwa wanafurahi kuona nacheza kwa sababu wanajua soka ndiyo kitu kinachonipa furaha.”
ALIKUTANA NA RAIS WA URUGUAY
“Nimekuwa nikishirikiana na viongozi katika kampeni na miradi mbalimbali na kutokana na mradi wangu wa ‘Un Gol a la Vida’, wenye lengo la kuweka usawa wa maadili, elimu, afya ya akili na kupunguza vurugu pamoja na matumizi ya pombe na dawa za kulevya, nilikutana na viongozi wengi wa serikali siyo tu hapa nyumbani Uruguay bali hata nje ya nchi.
“Kwa mfano, nilipata heshima ya kumkabidhi tuzo Naibu Waziri Mkuu wa Serbia, Ivica Dacic. Pia kukutana na Rais wa Uruguay ilikuwa ni jambo la kipekee zaidi na kuzungumza naye kwa dakika 15 hadi 20 pamoja na kumpa mpira, niliwahi pia kukutana naye akiwa Seneta.”
“Nilihisi msisimko na furaha isiyoelezeka. Alinipongeza, akanitia moyo wa kuendelea mbele na akaniambia mimi ni mfano kwa Uruguay na dunia.”
JE ANAONA SOKA LIMEBADILIKA KWA UKUBWA GANI?
Carmona anasema soka limebadilika sana kuanzia kwa mashabiki, klabu, wachezaji, viwanja, waamuzi, vyombo vya habari na fedha.
“Soka la leo ni la kasi zaidi, nguvu zaidi na tunakosa namba 10 wabunifu kama zamani, pia hata mtindo wa soka la tararibu kwa sasa haupo, vilevile kuna uhusiano mkubwa sana wa soka na biashara, kila kitu sasa ni pesa,” anasema na aliongeza soka la sasa halina uhalisia, teknelojia imefanya kuwa kama mchezo wa maroboti.
“Nadhani wachezaji wa leo wasingepata nafasi katika soka la zamani na wale wa zamani wengi wasingecheza soka la sasa. Kila zama zina changamoto zake. Soka la kisasa ni la kasi na nguvu nyingi, jambo ambalo si kila mtu anaweza kulicheza.”
MAREKANI NOMA
Fundi huyu ambaye amecheza soka la kulipwa katika zaidi timu 40 nchini kwao Uruguay, pia aliwahi kucheza soka katika nchi kama Canada, Marekani, Hispania na Italia.
Anasema kila nchi ilimpa uzoefu wa aina yake lakini miaka 10 aliyohudumu Marekani katika nyakati tofauti tofauti kwake ndio ilikuwa ya kipekee sana.
“Ilikuwa kipindi bora zaidi katika maisha yangu ya soka, nilicheza kwenye viwanja vya nyasi bandia na asilia, nilikuwa nahodha na mchezaji muhimu katika kila timu, nilifunga mabao mengi na nilipata pesa nyingi. Uzoefu huo ulinijenga na kunibadilishia maisha.