Prime
Mo Banka: Bangi zilikaribia kuua kipaji changu
UTASEMA nini kuhusu kiungo fundi wa boli, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ aliyewahi kuwika na timu mbalimbali ikiwamo Yanga na Taifa Stars kabla ya ghafla kuzimika na kuzua maswali kwa wadau wengi wa soka ndani na nje ya nchi.
Mwanaspoti liliamua kumsaka fundi huyo wa boli ili kujua kuliko juu ya ukimya wake wa karibu miaka miwili katika mahojiano maalumu ambayo bila hiyana mwenyewe amefunguka makubwa akieleza namna ujana na mambo ya kuiga yaliyotka kumponza.
Mo Banka amefunguka mambo mazito ikiwamo kuhusishwa na dawa za kusisimuwa misuli, kukumbwa na ugonjwa wa ajabu uliomfanya akae kimya ili kupata tiba akiwa na hali ya utulivu.
Licha ya kuona baadhi ya kejeli na taarifa mitandaoni, Mo Banka anasema alijipa moyo mgumu na wa kijasiri kuacha upepo mbaya upite, huku akisubiri muda sahihi ya kueleza kipi kilimsibu.
“Kuna nyakati zingine hapaswi kushindana na kila jambo, ndiyo maana katika akaunti zangu naishia tu kuangalia vitu vinavyokwenda lakini siposti chochote, kwa sababu nilichagua kujipa utulivu na nimefanikiwa katika hilo,” anasema Banka.
AKIRI KUTUMIA BANGI
Unakumbuka tukio la kufungiwa na Kamati ya Kupambana na Kuzuia Dawa zisizoruhusiwa michezoni Afrika (RADO) kwa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Banka mwenyewe amefunguka akikiri kutumia bangi.
Banka alifanyiwa vipimo hivyo Disemba 9, 2017 na majibu kuonyesha anatumia dawa za kulevya aina ya bangi ambayo hairuhusiwi michezoni na mwenyewe akizungumza na Mwanaspoti amethibitisha ni kweli alikuwa anatumia bangi na sio dawa za kulevya kama wengi walivyokuwa wakiripoti.
“Maisha yangu ya mpira yalikuwa yapotee mapema sana, nakumbuka kipindi nikiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes wakati nacheza mashindano ya Kombe la Chalenji la Cecafa pale Kenya, kutokana na uwezo mkubwa niliouonyesha tulitajwa na wenzangu wengine wanne ili tupimwe kwa madai tunatumia dawa za kusisimua misuli,” anasema na kuongeza;
“Nilishaitwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nitoe ushauri kwa wachezaji wa timu za Ligi Kuu kuwaambia waachane na matumizi ya bangi kwa sababu ni mbaya. Sitaki kuweka wazi jina la kiongozi huyo aliyenishauri hivyo, lakini nilimuuliza ningekuwa mwanao ungenifanyia hivyo, alijibu kama sitaki basi siwezi kusamehewa na mimi nilikubali kutokusamehewa.”
Banka anasema kutokana na majibu hayo hana maelewano mazuri na huyo kiongozi kwani hata akipata nafasi ya kuwa mgeni rasmi kwenye usimamizi wa mechi suala la kupeana mikono kwao ni tatizo wanakuwa kama hawafahamiani.
“Ishu ya Kenya nakiri ilikuwa ni ya kutengeneza kwa sababu kama walitaka kujua, basi tungekamatwa wawili kwani kati ya wanne tuliopimwa, mimi ndiyo nilitajwa, ingawa nakumbuka tulikuwa tumetoka kutumia wote,” anasema na kuongeza:
“Huyo ambaye kipindi hicho tulikuwa tunatumia wote bangi siku wanatuita kutupima walituambia tunaenda kupimwa kama tunatumia dawa za kusisimua misuli na kwa kuwa hatukuwa tunafanya hivyo tulikubali na kwa kuamini hakuna mtu anatumia lakini baadae majibu ndio kama mlivyosikia.”
SIKU YA KWANZA KUVUTA BANGI
“Ni vishawishi tu lakini pia mtaa niliokulia umechangia mimi kuingia kwenye shida ya kuvuta bangi. Mimi Zanzibar nimekulia mtaa unaitwa Mbolibolini uliza sifa zake utaambiwa sio mtaa mzuri,” anasema na kuongeza:
“Ni mtaa ambao vizazi vingi vimeharibika, pia maisha ya mpira yalikuwa yananichanganya unaenda mazoezi unapata elfu mbili. Nakumbuka kipindi hicho pia nilikuwa nafuga ng’ombe hivyo nikachagua njia sahihi ya kufuga. Huko ndiko nilikokuwa nakutana na watu wa aina tofauti.
“Wakabaji wa wanawake na pombe, starehe kibao, hivyo nikajikuta naingia kwenye uvutaji wa bangi.
“Siku ya kwanza kuvuta hakuna mtu aligundua ila ulaji wangu ndio ulimshtua mama kwani nilikula sana hadi mama alihoji nikamwambia nilikuwa na njaa sana,” anasema Banka na kuongeza dirisha dogo ndio atafungua mlango wa kurudi ligi kuu.
ULIKUWA NI MPANGO TU
Licha ya kukubali kuwa alikuwa anatumia bangi kiungo huyo ameendelea kufunguka juu ya sakata hilo, akilihusisha na moja ya timu ambayo hakutaka kuitaja ndio waliomzushia sakata hilo baada ya kugoma kusaini timu yao.
“Nakumbuka sakata hilo lilitokea kipindi ambacho tayari kulikuwa na mchakato wa mimi kuwaniwa na baadhi ya timu ambazo kila moja kati ya hizo zilikuja na dau lake lakini moja ilikuwa inaonyesha nia ya kunihitaji zaidi nikawa naipa shida ilikuja hadi Kenya kipindi hicho na kwenda hadi kwa baba yangu kumshawishi ili nisaini mkataba,” anasema na kuongeza;
“Ushawishi wao waliingiza hadi hadhithi za kuninunulia gari na baba yangu akawa anashawishika kwa kuniomba nisaini mkataba lakini niligoma,” anasema na kuongeza, aliposaini Yanga ndipo majibu ya bangi yakatoka.
Banka anasema licha ya kumalizana na Yanga akitokea Mtibwa Sugar, ilionyeshwa bado ni mchezaji wa Mtibwa ingawa wao wenyewe walikana si mchezaji wao, hata hivyo ililazimishwa ni mchezaji wa timu hiyo.
AZAM PIA ILIMTAKA
Anasema hata tangu akiwa Mtibwa Sugar, Azam FC ilikuwa inamuwinda imsajili lakini mkataba ulimbana, na alipoenda Yanga na kumalizana nao, alijua kituo kinachofuata ni Azam lakini haikuwa hivyo.
“Kwenye usajili kuna mengi, niliongea na Abdulkarim Amin ‘Popat’ na timu hiyo ilianza kunitafuta tangu nikiwa Mtibwa Sugar, lakini mkataba ulinifunga hivyo baada ya kujiunga Yanga na mkataba kuishia nikaamini naenda Azam FC lakini hadi dirisha linaelekea ukingoni sikutafutwa ndio nikajiunga na Ruvu Shooting kwa mkataba wa miezi sita baada ya hapo nikaenda Namungo.”
Anasema aliitumikia Yanga kwa miaka yote miwili na mara baada ya kumaliza mkataba zikiwa zimebaki mechi sita aliigomea timu bila sababu akivimbia ofa kutoka Azam FC, huku akizikataa zimu mbalimbali lakini mwisho wa siku dili lilikufa na kujikuta akiangukia Ruvu Shooting.
MILIONI 40 YA YANGA
Anasema sakata la dawa za kusisimua misuli ikiwa ni siku chache baada ya kusaini na kutambulishwa Yanga lilimvuruga, kwani lilisababisha asipate mshahara wa miezi mitatu na kuhofia kurudisha pesa ya usajili wa miaka miwili kwa Sh40 milioni.
“Namshukuru sana kocha Mwinyi Zahera kipindi hicho alisisitiza bado ananitaka na anajua nitamsaidia. Akaongea na viongozi kwa miezi mitatu ambayo nilikuwa natumikia adhabu nisilipwe mshahara,” anasema na kuongeza:
“Mwezi mmoja nilikuwa nje na Yanga na miezi mingine miwili nilianza mazoezi na timu na baada ya adhabu kuisha nikaanza kulipwa mishahara yangu. Haikuwa rahisi,” anasema kiungo huyo ambaye ameziita timu kumsajili.
UGONJWA USIOJULIKANA
“Nakumbuka nilikuwa nimelala usiku kama sijakosea ilikuwa saa nane, nilisikia kama misuli inakaza kama napigwa shoti, nilikuwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ nikamshirikisha kuna kitu kama kinaingia mwilini mwangu akaniambia nilale itakuwa ni misuli tu,” anasema na kuongeza:
“Asubuhi kulivyokucha tulikuwa na ratiba ya mazoezi kama kawaida niliibuka mazoezini katika harakati za kutafuta pumzi kukimbia nilishtushwa na hali ya kusikia uvimbe kwenye kigimbi uvimbe huo ukawa unahama mara kwenye paja mara karibu na mgongo.”
Banka anasema alikaa chini na cha kushangaza akirudi kambini anakuwa mzima kabisa kesho akiamka akigusa tena uwanja shida inakuwa ile ile ya kuvimba kigimbi, paja na sehemu ya juu ya karibu na mgongo. Baada ya kuona shida hiyo ndipo ulifanyika uamuzi wa kupelekwa hospitali na uongozi wa timu ya Polisi Tanzania.
“Nilipelekwa hospital kufanyiwa X ray lakini hakuna kitu kilichoonekana walisema hawaoni tatizo lolote, nilipewa dawa za kuchua misuli na kuambiwa huenda ikanisaidia,” anasema na kuongeza:
“Uongozi wa Polisi nahisi na wao walikuwa wanajua nadanganya, wakanisafirisha na kunileta Dar es Salaam ambapo pia walinipiga X ray lakini hawakuona tatizo, walinipa daktari wa misuri ambaye alikuwa ananiangalia kila muda na akibaini naendelea vizuri alikuwa ananiambia nirudi kambini, lakini nikirudi mambo ni yale yale.”
Anasema baada ya kuhangaika sana alifanya jitihada za kumtafuta hadi daktari wa Taifa Stars, Gilbert Kigadye ambaye pia alishindwa kuona tatizo.
MIAKA MIWILI BILA SOKA
Anasema ugonjwa huo ulimtesa miaka miwili na alikuwa ameshaingia kwenye mfumo, hata hivyo, balaa hilo lilimfanya ashindwe na hata mazoezini hakuweza.
“Ilifika muda nilikuwa nalazimisha kwenda mazoezi lakini nikigusa tu mpira ilikuwa inaniwia ugumu zaidi naumia.
“Ugonjwa huo ulikuwa unachukia hadi nguo za mazoezi kwani nilikuwa nikivaa pia napata shida nikitoa tu narudi kwenye hali ya kawaida.”
Anasema bila kuvuliwa nguo anajikuta analia muda wote bila kujua ugonjwa huo upo mguu gani kwani kulikuwa na mabadiliko mara mguu wa kushoto mara wa kulia, kuna muda alikuwa anasikia maumivu kwenye vidole muda wingine mkono unapinda.
SHEIKH AOKOA KIPAJI
“Baada ya kuona mambo magumu katika hospitali licha ya kufanya vipimo vyote niliamua kuanza kuhangaika nje ya tiba ya hospitali na nashukuru Mungu katika hangaika zangu nilikutana na Shekhe ambaye siwezi kuweka jina wazi kwani sifahamu ni nani kati ya wengi nilio wafuata aliyenitibu,” anasema na kuongeza:
“Sitaki kuweka bayana pia nini niliambiwa na shekhe kuhusu shida yangu ninachoshukuru ni nipo salama na hali ya kutoeleweka iliyokuwa inanitokea sasa naendelea vizuri na natarajia kurudi tena uwanjani.”
Banka anasema mpango wake ni kuona anatafuta timu dirisha dogo ili arudi na kuendeleza kipaji chake huku akibainisha anaomba apate timu itakayomwamini kwa miezi sita tu kabla ya kuingia makubaliano ya muda mrefu.
“Shida niliyoipata kwa namna moja ama nyingine imenirudisha kwenye ibada kwa sababu nimepitia changamoto nyingi nikaona bora kurudi kwa Mwenyezi Mungu kweli amenijibu,” anasema kiungo huyo ambaye yuko tayari kurudi uwanjani.
ALIVYOPOKEA TAARIFA YA KUFUNGIWA
“Nakumbuka siku ya kwanza najiunga na kambi ya Yanga nilifanya mazoezi siku ya kwanza na siku ya pili naingia mazoezi meneja wa Yanga Saleh Hafidh aliniambia siruhusiwi kufanya mazoezi natakiwa kwenda TFF,” anasema na kuongeza:
“Nilihoji kwa ajili ya nini ndiyo aliniuliza unakumbuka shida uliyoipitia Kenya, nikasema ndiyo, akasema inasemekana Kenya umepimwa umegundulika unatumia dawa nikasema twende huko TFF.”
Anasema alivyofika TFF akaambiwa majibu yamerudishwa amethibitika anatumia bangi akaangua kilio akiamini ndoto zake za kucheza zinapotea lakini Hafidh hakukubaliana na hilo.
“Huwezi amini nimeenda TFF wananihukumu kwa hilo nilikuwa nimetoka kucheza mechi nikiwa na Taifa Stars dhidi ya Congo na viongozi wa shirikisho walinisifia sana siku tatu naitwa na kupewa majibu hayo baada ya hapo nikatoka nalia.”
Banka alimtaja Baraka Kizuguto alitumia muda mwingi sana kumshauri na kumsisitiza aombe msamaha kwa TFF.
Anasema sakata hilo lilimtoa mchezoni kabisa ni kipindi ambacho alikuwa anapokea simu nyingi sana za waandishi huku akikiri mengi yaliongelewa mazuri na mabaya ya ukweli na uongo.
MILIONI 10 ZA POLISI
Anasema alisaini mkataba wa miezi sita Polisi Tanzabia kwa Sh10 milioni akitokea Namungo lakini hakuitumikia hata mechi moja.
“Naushukuru uongozi wa Polisi Tanzania ulinigharimikia sana baada ya tatizo na nafikiri ata wao walijua nafanya utapeli kwa kuigiza kuumwa nikiwa tayari nimechukua mamilioni yao. Baada ya kuona sichezi nilisitisha kulipwa mshahara maana nilikuwa siitumikii timu,” anasema na kuongeza:
“Walinifanyia uungwana sana maana nilikuwa sielewi nitatoa wapi pesa ya kuwarudishia baada ya hali yangu kutokukubali kucheza tena mpira, lakini haikuwa hivyo, nilikula pesa ya mkataba bila kuitumikia timu.”
Anasema anakumbuka kipindi anasajiliwa na Polisi Tanzania ilikuwa inatafuta pointi sita isishuke daraja, hivyo walimwamini na kumpa mkataba wa miezi sita.
Banka anasema alitamani kulipa fadhira siku moja lakini ndio hivyo timu imeshuka daraja na anahofia kucheza daraja la kwanza ambalo licha ya kuto kuwahi kucheza anahofia ni ligi ngumu.
ALIPOTEZA MARAFIKI
“Huwezi kuamini kwa miaka miwili na nusu niliyokaa nje ya uwanja hakuna mchezaji wala rafiki yangu yeyote aliyenikumbuka zaidi ya mke wangu na ndugu zangu,” anasema na kuongeza:
“Hakuna wachezaji ambao nawasiliana nao licha ya urafiki tuliokuwa nao kipindi nacheza na simu zilikuwa zinaita mtu anakupigia ulicheza poa mechi iliyopita au nipo Zanzibar uko wapi tuonane.
“Kiufupi sina mtu yeyote wa mpira ambaye nawasiliana naye na hata ukiwauliza sina hakika kama wanafahamu nilipo, mawasiliano yamekufa kabisa. Ndiyo maisha lakini.”
Alipoulizwa ni mchezaji gani wa kigeni aliyewahi kucheza naye anawasiliana naye anasema hakuna hata mmoja na hajawahi kuwa na namba zao kwani yeye lugha ya kiingereza ni mtihani kipo mbali sana.
MECHI YA MWISHO
“Mechi yangu ya mwisho ya kiushindani kabla ya kuachana na soka kutokana na changamoto ilikuwa ni dhidi ya Singida mchezo ulichezwa uwanja wa Liti.”
“Baada ya hapo mkataba wangu ukawa umeisha nikapata ofa Mtibwa Sugar, Mbeya City na Polisi Tanzania ambayo ndio nikasajili mkataba wa miezi sita,” anasema Banka.
Kiungo huyo anasema kabla ya kwenda Polisi Tanzania alikuwa na mkataba wa miezi sita na Namungo lakini alikuwa anaidai hela hivyo aliomba kuondoka na lengo lake ni kurudi kucheza Mtibwa Sugar lakini mambo yakaenda tofauti.
“Nakumbuka Aboubakar Swabri alinishawishi nijiunge na Mtibwa nikamwambia nina mkataba wa miezi sita, akahofia siwezi kuachiwa na bosi nikamwambia hilo aniachie mimi kweli nikampigia nataka kuondoka alihoji kwa nini nikamjibu nimeamua tu,” anasema na kuongeza:
“Baadae akaniuliza au kwa sababu sijakumalizia fedha zako nikaingia kwa gia hiyo mimi si nimebakiza miezi sita hiyo hela nasamehe sitakuja kuidai wala kuzungumza popote kama nawadai naomba uniachie tulikubaliana. Mtibwa Sugar nawapigia wanasema tutakutafuta sikulaza damu nilipata ofa Mbeya City wao Sh10 milioni, walitaka nisaini mwaka nikaachana nao na ndipo nilipotua Polisi Tanzania,” anasema Banka.
Itaendelea kesho