RISASI MUHIMU! Saini moja kwa kila timu ya Ligi Kuu England inayopasa kunasa Januari hii
Muktasari:
- Kutokana na hilo, makala haya yanahusu usajili mmoja unaopaswa kufanywa na kila timu iliyopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu katika dirisha hili la uhamisho wa Januari ili kumaliza msimu kwa kutimiza malengo ya msingi.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA la usajili la Januari bado lipo wazi na timu zinapambana kucheki maeneo ya kuboresha ili kumaliza msimu kibabe.
Kutokana na hilo, makala haya yanahusu usajili mmoja unaopaswa kufanywa na kila timu iliyopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu katika dirisha hili la uhamisho wa Januari ili kumaliza msimu kwa kutimiza malengo ya msingi.
Arsenal - straika
Kukosekana kwa Bukayo Saka uwanjani kumeifanya Arsenal kupungua nguvu kwenye idara yao ya ushambuliaji ikishindwa kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi. Kai Havertz ndiye kinara wa mabao wa Arsenal kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akiwa amefunga mara saba, lakini nafasi anazopoteza ni nyingi kwelikweli. Kutokana na hilo, Arsenal inahitaji Namba 9 mwingine ambaye atawapa nguvu kwenye vita yao ya kufukuzia ubingwa.
Aston Villa - winga wa kulia
Kocha Unai Emery anamhitaji Moussa Diaby mbadala wake ili kuja kumpa ushindani wa namba Leon Bailey kwenye wingi ya kulia. Bailey, bao lake alilofunga dhidi ya Leicester City lilikuwa la kwanza kwenye mechi 19 kwenye Ligi Kuu England na amehusika kwenye mabao matatu tu msimu huu. Jambo hilo linamfanya Morgan Rogers kuwa na mzigo mkubwa, hivyo miamba hiyo ya Villa Park inahitaji winga wa kulia kwenye dirisha hili.
Bournemouth - straika
Majeruhi ya Enes Unal na kuumia kwa Evanilson kumfanya kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola kutokuwa na Namba 9 wa maana kwenye kikosi chake. Washambuliaji bao ambao anawakosa wamehusika kwenye mabao saba, hivyo eneo la mshambuliaji wa kati ndilo analopaswa kuliboresha kwenye dirisha hili. Daniel Jebbison amerudishwa kwenye timu akitokea Watford alikokuwa kwa mkopo, lakini bado mchezaji huyo hawezi kumaliza tatizo lao la kuwa na mfungaji.
Brentford - beki wa kati
Brentford inaweza kuwa kwenye vita ya kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kama isingekuwa na beki inayoruhusu tu mabao hovyo. Majeraha ya Ethan Pinnock na Kristoffer Ajer yameifanya Brentford kuwa na udhaifu mkubwa kwenye beki yao huku Ben Mee naye mkataba wake ukienda kumalizika mwisho wa msimu, hivyo kocha Thomas Frank kipaumbele kikubwa kwenye dirisha hili ni kusajili beki wa kati. Timu imeruhusu mabao 35.
Brighton - straika
Kuna kundi kubwa la washambuliaji wenye vipaji vikubwa kwenye kikosi cha Fabian Hurzeler, lakini shida ni kwamba ina mawinga wenye kasi sana ambao wanapokimbia na mipira na kupiga krosi kunakuwa na shida ya washambuliaji wa kati kufunga mabao kutokana na kuzidiwa kasi.Danny Welbeck ndiye kinara wa mabao wa Brighton kwenye Ligi Kuu England, akiwa amefunga mara sita, lakini umri wa fowadi huyo ni miaka 34. Hivyo anahitajika straika kijana mwenye kasi.
Chelsea - beki wa kati
Safu ya ulinzi ya Chelsea inaonekana kuwa hovyo tangu Wesley Fofana alipoumia, hivyo kocha Enzo Maresca sasa ana kazi ya kusaka beki mpya wa kati wa kuja kuifanya timu hiyo kuwa na nguvu kubwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Chelsea ina wastani mkubwa wa kuruhusu mashuti ambayo yanawafanya wafungwe mabao huku pia mabeko wake wakishindwa kufanya vizuri kwa mipira ya juu. Hilo linaifanya Chelsea kuhitaji beki mpya wa kati.
Crystal Palace - wing-back wa kulia
Wing-back wa kulia, Daniel Munoz amekuwa akipewa sifa kubwa kutokana na mchango wake kwenye safu ya ushambuliaji, lakini kocha Oliver Glasner anapaswa kuongeza nguvu zaidi kwenye safu yake ya ulinzi kwa upande huo. Kutokana na idadi ya mashambulizi iliyoruhusu kupitia upande huo wa kulia ni zaidi ya asilimia 39 ya mashambulizi wote na hivyo kuwa eneo ambalo wapinzani wamekuwa wakilitumia kuwaadhibu Palace kwenye mikikimikiki ya ligi msimu huu.
Everton - straika
Everton ni kama vile imeacha kufunga mabao. Kwa ujumla wake imefunga mabao 15 tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ikishika namba mbili kwa timu zilizofunga mara chache. Timu hiyo ya Goodison Park imeshindwa kufunga mabao kwenye mechi 11 za Ligi Kuu England msimu huu, ikiwamo nne kati ya tano za mwisho na ilishindwa kupiga shuti hata moja lililolenga goli kwenye mechi mbili msimu huu. Straika Dominic Calvert-Lewin amechoka, anahitaji msaada.
Fulham - straika
Fulham imekuwa na msimu bora kabisa, ikiwa haijapoteza kwenye mechi nane na ipo pointi sita nyuma ya Chelsea kwenye nafasi ya sita na kwa timu zote za Ligi Kuu England yenyewe ndiyo inayohitaji maboresho kidogo sana kwenye dirisha hili. Lakini, eneo ambalo inahitaji kuliboresha ni kwenye safu ya mshambuliaji wa kati ili kuja kuongeza nguvu kwenye eneo hilo baada ya kutoka sare sita katika mechi nane zilizopita, ambazo hakika ilipaswa kushinda.
Ipswich Town - kiungo wa kati
Ipswich Town inajitafuta kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, lakini kikosi hicho cha kocha Kieran McKenna bado kimekuwa na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira kwenye mechi zake. Ilimsajili Kalvin Phillips kwa mkopo, lakini kiungo huyo ameanzishwa kwenye nusu ya mechi za ligi ilizocheza timu hiyo. Kutokana na mtindo wa uchezaji wao, Ipswich inahitaji kiungo wa kati mwingine ili kuja kuwaweka kwenye wakati mzuri wa kusambaza mipira na kucheza mtindo wao.
Leicester City - winga
Kukosekana kwa kasi kwenye safu ya ushambuliaji ya Leicester City ni tatizo kubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Ruud van Nistelrooy. Kabla ya kupata majeraha yanayomfanya awe nje kwa msimu mzima, Abdul Fatawu, alikuwa tegemeo kubwa kwa Leicester City kutokana na kasi yake. Lakini, sasa timu hiyo imekuwa dhaifu kwenye eneo hilo na haijafunga bao la shambulizi ya kushtukiza hata moja, hivyo winga mwenye kasi ni eneo ambalo Leicester inahitaji mtu.
Liverpool - kiungo wa kati
Baada ya kushindwa kunasa saini ya Martin Zubimendi kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, kocha Arne Slot bado anahitaji Namba 6 anayecheza kwa staili ya Rodri ili kuwa bora zaidi, licha ya Liverpool kuwa na utajiri mkubwa wa wachezaji wa eneo la katikati ya uwanja. Liverpool ya sasa inashambulia zaidi kuliko ile ya Jurgen Klopp katika msimu wa 2023/24, lakini bado kuna shida inamtegemea Ryan Gravenberch pekee, akiumia ni shida.
Man City - kiungo wa kati
Ushindi mara mbili mfululizo kwenye Ligi Kuu England umeirudisha Manchester City kwenye hali yake, lakini kocha Pep Guardiola bado anahitaji kufanya usajili hasa eneo la kiungo wa kati ili kuweka mambo sawa. Kwa sasa Man City inaonekana kuwa kwenye shida tangu Rodri alipoumia, hivyo ni eneo ambalo wanahitaji kulifanyia maboresho makubwa na matazamio ni makubwa kwa kocha Guardiola kufanya usajili huo kwenye dirisha hili la Januari.
Man United - wing-back wa kushoto
Uhitaji wa kocha Ruben Amorim kutumia fomesheni ya 3-4-3 inamfanya ahitaji kuwa na wing-back wenye kasi na ubora mkubwa wa kutawala kwenye eneo la pembeni kwa baada ya kusaidia ulinzi na kwenye kushambulia. Diogo Dalot alionyesha kiwango bora kwenye mechi dhidi ya Liverpool kwenye wing-back ya kushoto, lakini eneo hilo bado linahitaji mchezaji mwingine ili kuifanya Manchester United kuwa imara zaidi na kufanya matokeo kuwa bora uwanjani.
Newcastle United - winga wa kulia
Ni wazi Newcastle United inahitaji maboresho kwenye wingi yake ya kulia, mahali ambako kwa sasa anaanzishwa Jacob Murphy mbele ya Miguel Almiron. Murphy ameasisti mara saba msimu huu na kuliweka juu jina lake kwamba anastahili kuanzishwa. Lakini, ukweli kwenye kikosi wingi ya kulia ni eneo linalohitaji maboresho ili kwenda sawa na ule upande wa kulia, ambao yupo Anthony Gordon, anayeonyesha balaa kubwa.
Nottingham Forest - winga wa kulia
Anthony Elanga amefunga au kuasisti katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu England, jambo linalomfanya kocha Nuno Espirito Santo kufikiria mara mbili ishu ya kuleta winga mpya wa kulia. Lakini, Forest imekuwa na udhaifu kwenye eneo hilo, ambako Elanga na Callum Hudson-Odoi wamekuwa wachezaji wa kuchezeachezea tu mpira na kushindwa kuifanya timu hiyo kuwa na nguvu kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Straika Chris Wood anahitaji krosi nyingi.
Southampton - beki wa kati
Ni ngumu kuchagua eneo moja tu kwenye kikosi cha Southampton, ambayo kwa sasa inaburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini kwa kocha mpya Ivan Juric kwa kuanzia anahitaji kuweka kipaumbele kwenye kuboresha safu ya mabeki katika dirisha hili la Januari. Beki ya Southampton ni dhaifu sana, ambapo wikiendi iliyopita iliruhusu mabao 5-0 mbele ya Brentford, hivyo kupunguza aibu kama hizo, inahitaji beki mpya wa kati kuja kupunguza balaa.
Tottenham – beki wa kati
Kikosi cha kocha Ange Postecoglou kimekuwa na bahati mbaya kutokana na kuwa na majeruhi wengi hivyo kulazimika kuwatumia mabeki wa pembeni pamoja na viungo wa kati kwenye nafasi ya mabeki wa kati. Jambo hilo limefanya kuruhusu mabao mepesi na hivyo inahitaji kufanya usajili wa mabeki wa kati ili kufanya mambo kuwa mazuri na kuendelea kwenye harakatio za kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
West Ham United - straika
West Ham United haifungi sana mabao chini ya Julen Lopetegui, ambapo ilifunga mabao 24 katika mechi 20 za Ligi Kuu England, hivyo itahitaji kufanya maboresho makubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji wakati huu ikiwa chini ya kocha mpya, Graham Potter. Brighton ilikuwa na wastani wa kufunga bao moja katika kila mechi ya Ligi Kuu England walizocheza chini ya Potter, hivyo ni wazi atafanya usajili wa straika ili kuifanya West Ham kuwa ya mabao.
Wolves - beki wa kati
Hakuna mjadala kwamba Wolves inahitaji beki mpya wa kati ili kuifanya timu hiyo kuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye Ligi Kuu England na kuwapunguzia mabao wanayofungwa. Timu hiyo sasa imeruhusu mabao mawili au zaidi katika mechi saba kati ya nane za mwisho ilizocheza kwenye Ligi Kuu England ambapo hadi sasa nyavu zao zimeguswa mara 45 katika mechi 20 na hivyo kuthibitika kwamba beki wa kati anahitaji kwa nguvu zote kwenye kikosi hicho.