RIPOTI MAALUMU -2: Kwanini wanawake wanakata tamaa?

JANA tuliishia jinsi ambavyo wanariadha wanawake wanavyoshindwa kufanya vizuri hapa Tanzania huku zikitajwa sababu mbalimbali. Leo tutasikia kwa makocha na madaktari nini sababu za mkwamo wa Wanariadha wa kike. Kuna sehemu wanasema Wanawake wanapendelewa sana:
Kocha mzoefu wa wanariadha Tanzania, Anthony Mwingereza anasema ; “Tofauti kwa Wanawake ni kwamba wakipata majeraha kidogo wanaachana na riadha kwa kuwa wanakata tamaa mapema. Nchi za wenzetu wakiwemo Kenya wameweka msingi mzuri kwa wanariadha wao wakiwemo wanawake na kuwaandaa kuanzia wakiwa wadogo hii imekuwa kama sera ya nchi yao, mwanariadha mwanamke pale Kenya akishinda kwenye mashindano ya ndani huyu akienda Ulaya anashika nafasi ya kwanza kwa kuwa mashindano yao yapo siriazi tofauti na nchi nyingine.
“Kwetu mashindano ya kutafuta vipaji ni kama pikiniki fulani, lakini wenzetu wanakuwa na mchujo mkali na vipaji vinaonekana. Hapo nyuma, tulikuwa tunakwenda vijijini na kuwachukua watoto wengi wanawake wengi zaidi kuliko wanaume nia ilikuwa ni kuhakikisha wanakuwa wengi kwenye mashindano mbalimbali, lakini baadaye utaratibu huo uliisha na sijui kwanini.
“Kwangu mimi nina wanawake wanafanya mazoezi na timu yangu, unajua kwanini wanaweza ni kwa kuwa wanaenda kwenye mbio mbalimbali wanapata angalau kihela kidogo kinawafanya wanaamini kuwa huu mchezo una fedha, lakini vinginevyo wangeshindwa kuvumilia.”
Wanakimbia dakika nyingi:
“Hili wengine hawalifahamu, lakini wanawake hawawezi kukimbia dakika sawa na mwanaume, hii ni ngumu, kama mwanaume atashinda half marathoni kwa dakika 30, basi mwanamke atakimbia umbali huo kwa dakika 45.
“Kwenye viwango vya Olimpiki na mashindano mengine, muda wa kufuzu kwa mwanaume ni tofauti na mwanamke, sasa si unaona jinsi ambavyo dunia inawajali wanawake siyo kila kitu kipo sawa, ingawa kwenye mazoezi makocha tunawapa mazoezini sawa,” alisema Muingereza.
WANAKATA TAMAA SANA
“Kwa wasichana ni tofauti na wanaume, hawa wanaweza kukimba hadi miaka 39, lakini wakipata majeraha kidogo tu wanaachana na riadha, hii inazidi kuwarudisha nyuma, nafikiri wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha.
Huku kwenye taasisi kama za Jeshi na Polisi wanaweza kuendelea kucheza kwa kuwa wakitaka kuacha tunawasukuma kuendelea. Wanaume na wanawake wanatakiwa kuhakikisha wanakula vyakula vizuri, wale vyakula vya asili zaidi hii itawafanya wafike mbali zaidi,” alisema.
“Tatizo lingine kwa sasa ni kwamba wanariadha wengi hawapati kazi hii inazidi kuwarudisha nyuma, ndiyo maana wote wanataka kukimbia marathoni ili wapate fedha badala ya kutengeneza msingi wa baadaye kwenye mbio fupi.”
MILA KANDAMIZI
“Kuna makabila yanawazuia wanawake kuvaa vibukta, sasa hawa walikuwa wananipa wakati mgumu, huko Singida Karatu ni kazi sana kuwashawishi kuingia kwenye riadha ingawa kwa sasa wamebadilika kidogo. Ilikuwa inatubidi tuende huko kwa wazee na kuwaambia kuwa lazima tunakwenda kuwasomesha watoto wao, hii ilitusaidia kupata wanariadha wengi wa kike na hapa hupewi tu wanakuweka chini Baba na Mama na kukukabidhi alimalizia kocha huyo ambaye,” anasema Arusha na Manyara ni chimbuko la wanariadha wa mbio ndefu.
KUKIMBIA NA UJAUZITO INAWEZEKANA?
Daktari wa michezo Tanzania Magreth Isike(pichani kushoto), anasema amekuwa daktari wa wanamichezo tangu mwaka 1992 na yupo chini ya chama cha madaktari Tanzania (Tasma), kwa miaka zaidi ya 25 akiwa ni daktari wa michezo pekee.
Anasema amefanya kazi na wanariadha wote wakubwa wa mkoa wa Arusha wakiwemo Gabriel Geay, Filex Simbu, Failuna na wengine na anakiri kuwa kuna ugumu kwa wanawake kuliko wanaume.
“Nimefanya kazi hii mjini na vijijini hivyo naelewa changamoto nyingi kwa kuwa wengi wamekuwa wakinieleza mambo yao. Pamoja na mambo mengine lakini ni dhahiri kuwa kwa wanariadha ni ngumu kukimbia ukiwa na ujauzito, ingawa huwezi kuwazuia lakini kuna mambo ambayo unatakiwa kuyafanya kabla ya kukimbia.
“Natamani kungekuwa na mashi-ndano ya kutembea kwa kuwa mazoezi haya yanaruhusiwa kwa wajawazito, lakini kukimbia ni hatari, ingawa duniani wapo ambao wametwaa medali wakiwa wajawazito.
“Lakini hawa wanakuwa na ushauri wa daktari moja kwa moja ndiyo wanakwenda kukimbia sasa kama wewe utamuiga unaweza kwenda hospitali muda huohuo.”
“Mara nyingi nikiwashauri wanariadha huwa nawaambia wakiwa wajawazito waje kwangu tufanye kwanza vipimo, mwingine anaweza kuwa na kifafa kikampotezea uhai, lakini mwingine unaweza kumcheki ukaona yupo fiti, lakini hawawezi kufanana.
Hata baada ya kujifungua ni ngumu kurudi uwanjani haraka, inategemea amejifungua vipi, kuna wale wanafanyiwa upasuaji na wengine wanajifungua kawaida, hawa wana ushauri maalumu kabisa wa daktari kabla ya kuanza tena mazoezi, sijawahi kukutana na kesi hii lakini naamini lazima kuna ambao wamewahi kuacha riadha baada ya kujifungua,” anasema daktari huyo mzoefu.
Rekodi zinaonyesha, mwanariadha wa mbio fupi mita 800, Alysia Monteno raia wa Marekani(picha kubwa) ndiye ambaye anashikilia rekodi ya kutwaa medali kwenye mashindano makubwa ya USA Outdoor Track and Field Championships akiwa mjamzito wa miezi nane. Alitwaa medali hiyo mara sita, alikimbia akiwa mjamzito 2014. “Nilikuja hapa mwaka 2014, nikiwa na mimba ya miezi nane, nilipata vipimo na daktari wangu akaniambia niende hakuna madhara.” Daktari Christine Greves, anasema ni ngumu kwa mwanamke mjamzito kufanya vizuri akiwa na ujauzito wa zaidi ya miezi mitatu kwa kuwa mwili wake unaanza kupunguza nguvu na oksijeni, ”Christine Greves aliliambia jarida la Self la Marekani. Unajua nini wanariadha wenyewe wanawake wamesema kuhusiana na changamoto zao na jinsi walivyotusua?
Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation
Usikose kesho.