Prime
Baada ya timu kibao England, Sterling sasa anasukia wapi?
KAMA haujamsikia kwa muda mrefu Raheem Sterling, basi nakukumbusha tu kwamba yupo. Ndiyo, yupo. Juzi aliingia katika ofisi moja ya mabosi wa Chelsea pale Cobham wakakubaliana wachane mkataba wake.
Alibakisha mkataba wa miaka miwili London, lakini hajacheza mpira kwa miezi minane sasa. Kumbe hapa katikati alikuwa anakula mishahara ya bure tu Chelsea baada ya makocha kumuondoa katika mipango yao. Raheem ananifurahisha sana. Anajua kuzurura.
Natamani kujua kituo chake kinachofuata. Tayari ameshazurura miji yote mikubwa yenye timu kubwa England. Amecheza Liverpool, Manchester na London. Raheem kwanza kabisa alianzia London alikokuwa anacheza Queens Park Rangers (QPR).
Hauwezi kumlaumu wakati alipoamua kupanda basi kwenda zake Liverpool. Kwa kipaji chake cha wakati huo ilikuwa sahihi kwenda Liverpool. Timu kubwa. Akaenda zake Liverpool mwaka 2015. Alikuwa kinda sana lakini akafanya mambo makubwa na kucheza katika timu ya wakubwa.
Baadaye Raheem akawa staa mkubwa Liverpool. Hata hivyo aliwavuruga vichwa wakati pesa za Manchester City zilipoanza kuchanua. Akagomea mkataba mpya Anfield. Kumbe lengo lake lilikuwa kwenda Manchester City.
Liverpool wakachukia na wakanuna kweli. Wakati huo walikuwa wanajitafuta kujenga timu ya ushindani lakini pesa za City zikamvuruga Sterling. Siku za mwisho za maisha yake Anfield aligomea hata kufanya mazoezi na akaomba aachwe katika kikosi cha Liverpool kilichokuwa kinataka kwenda kufanya mazoezi barani Asia.
Kina Steven Gerrard na Jamie Carragher walilalamika kwelikweli kutokana na kitendo hicho cha Sterling. Mwishowe Liverpool waliamua kumuuza kwenda Manchester City ambako alicheza kwa mafanikio chini ya Pep Guardiola.
Baadaye akaenda zake Chelsea ambako hakucheza kwa mafanikio sana. Huko nako akaondolewa katika mipango ya kocha. Mwishowe akaenda Arsenal kwa mkopo. Katika timu ambayo inatengeneza nafasi nyingi kama Arsenal, Sterling hakufunga hata bao moja chini ya Mikel Arteta na aligeuka kuwa mchezaji wa ovyo.
Akarudi zake Chelsea ambako aliondolewa katika mipango ya msimu huu lakini sidhani kama alikuwa na haraka ya kucheza katika timu yoyote msimu huu. Na sasa amekubaliana na Chelsea kuchana mkataba wake.
Nimecheka baada ya kusikia kwamba Raheem anahusishwa na timu za Tottenham Hostspur, West Ham United na Crystal Palace. Anahusishwa pia kwenda nje ya England. Akibaki England, Raheem atakuwa mmoja kati ya wachezaji ambao wamevuruga klabu za Liverpool, Manchester na London. Sio wachezaji wengi ambao wamewahi kufanya hivyo.
Hapo England ni yeye na Nicolas Anelka tu ndio ambao wamewahi kucheza Liverpool, Arsenal, Chelsea na Manchester City. Yaani masela huwa hawahofii kujiunga na timu yoyote kubwa ya England bila kujali hisia walizoacha kwa mashabiki wa timu waliyoondoka.
Raheem ananikumbusha zamani namna ambavyo wachezaji wa Ligi Kuu Italia walikuwa hawahofii kuhama kutoka katika timu moja kubwa ya Italia kwenda katika timu nyingine. Kuna wachezaji wengi wa Italia ambao wamewahi kucheza AC Milan, Inter Milan na Juventus.
Hawa kina Andrea Pirlo, Zlatan Ibrahimovic, Christian Vieiri, Edgar Davids, Roberto Baggio na wengineo wengi wamecheza Inter Milan, AC Milan na Juventus. Sterling na Anelka wameongeza timu moja miongoni mwa timu kubwa za England.
Kule Hispania huwa hawana utaratibu kama wa Sterling. Watoto wa Barcelona huwa hawaendi kucheza Madrid na wala watoto wa Madrid huwa hawaendi kucheza Barcelona. Wana siasa zao za nje ya uwanja. Ukiona mchezaji anatoka Barcelona kwenda Real Madrid kama Luis Figo alivyofanya basi ujue huyo sio raia wa Hispania.
Ukiona mchezaji kama Antoine Griezman anahama kutoka Atletico Madrid kwenda Barcelona, basi ujue huyo sio Mhispaniola. England hawana siasa hizo na ndio maana Sterling huwa anazurura kadri anavyojisikia ingawa wachezaji wengi wameshindwa kufanya hivyo. Na ndio maana kando ya Anelka ambaye ni Mfaransa, yeye anabakia kuwa Mwingereza pekee kuchezea Liverpool, Manchester City, Chelsea na Arsenal.
Kwa Sterling ukimchunguza sana unakuja kugundua kwamba hawezi kutajwa kama ‘legend’ katika timu zote alizopita. Amekuwa na maisha ya soka ya nusu nusu tu katika timu hizi na walau Manchester City unaweza kudai kwamba alikuwa amefanya kitu cha maana kwa kutwaa mataji.
Hata hivyo, kutwaa kwake mataji kuliambatana na nyota yake kufunikwa na wachezaji wengi mastaa waliokuwa na ubora zaidi yake. Kina Kevin de Bruyne, Sergio Aguero, David Silva, Bernardo Silva na wengineo. Vinginevyo hauwezi kufikiria kujenga sanamu ya Sterling nje ya Uwanja wa Etihad.
Na sasa ana begi lake mgongoni. Anasaka kituo kinachofuata. Nilisoma mahala kwamba alikuwa anahusishwa na Manchester United. Sioni sana kama hilo likitokea, lakini kama likitokea basi atakuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kucheza Liverpool, Arsenal, Manchester United, Manchester City na Chelsea. Itafurahisha sana.
Hata hivyo hauwezi kujua. Ni mchezaji ambaye amezungukwa na nyota kali ya kucheza timu kubwa za England. Na endapo kama atahamia timu moja kati ya Spurs, West Ham au Crystal Palace, basi atakuwa mmoja kati ya wachezaji wachache kucheza timu nne za London.
Tayari ameshacheza klabu za Queen Park Rangers, Chelsea na Arsenal. Akiongeza moja atakuwa mmoja kati ya wachezaji wachache sana kucheza timu nne za London. Raheem hana baya. Wao tu wakijipendekeza ataenda zake kwa simu ya kwanza tu ambayo watampigia. Kuhamahama ndio maisha yake. Na wala huwa hasiti.