Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi zatikisa EPL 2025/26, Salah aandika historia mpya

SALAH Pict

Muktasari:

  • Achana na mastaa hao ambao walidumu Liverpool kwa misimu takriban minane, kuna mambo flani ambayo yameacha rekodi zitakazodumu kwenye vitabu vya kumbukumbu za ligi hiyo pendwa duniani yaliyotokea msimu huu wa 2025-26. Kwa msaada wa timu mahiri ya uchambuzi wa takwimu ya Opta nchini Uingereza, inaangazia baadhi ya takwimu bora zaidi zilizojitokeza.

LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England ilimalizika juzi, ikiondoka na utamu ambao mashabiki wa soka duniani waliushuhudia kwa takriban miezi 10, huku mastaa kibao wakiaga katika vikosi walivyovitumikia kwa misimu mingi iliyopita wakiwamo Andy Robertson na Mohamed Salah wa Liverpool.

Achana na mastaa hao ambao walidumu Liverpool kwa misimu takriban minane, kuna mambo flani ambayo yameacha rekodi zitakazodumu kwenye vitabu vya kumbukumbu za ligi hiyo pendwa duniani yaliyotokea msimu huu wa 2025-26. Kwa msaada wa timu mahiri ya uchambuzi wa takwimu ya Opta nchini Uingereza, inaangazia baadhi ya takwimu bora zaidi zilizojitokeza.


AGOSTI 2025

Mohamed Salah aliendeleza rekodi yake ya mabao katika siku ya ufunguzi wa msimu akiwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 10 katika mechi za kwanza kwenye historia ya ligi hiyo. Lakini, mchezaji mwenzake wa Liverpool, Hugo Ekitike alikuwa mchezaji wa pili kufunga na kutoa pasi ya bao katika mechi yake ya kwanza, baada ya Darwin Nunez kufanya hivyo dhidi ya Fulham 2022.

Kupitia Eliezer Mayenda, Dan Ballard na Wilson Isidor, Sunderland ikawa timu ya kwanza kuwa na wachezaji watatu kufunga katika mechi ya kwanza ya EPL tangu Reading 2006. Itakumbukwa Sunderland imerudi Ligi Kuu England msimu uliomalizika. Na kwa mara ya tatu katika historia ya ligi hiyo, timu mbili zilizopanda daraja yaani Leeds na Sunderland zilishinda katika mechi ya kwanza ya msimu.

Dhidi ya Spurs, kipa wa Burnley, Martin Dubravka akawa kipa wa kwanza kuadhibiwa kwa sheria mpya ya “sekunde nane” katika ligi hiyo. Ieleweke kwamba makipa hawatakiwi kuchelewa kuanzisha mpira zaidi ya muda huo.

Tijjani Reijnders akawa mchezaji wa pili kufunga na kutoa asisti katika mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo kwa Manchester City baada ya Sergio Aguero 2011. Tottenham Hotspur ikawa timu ya pili kushinda ugenini dhidi ya timu inayofundishwa na Pep Guardiola katika misimu miwili mfululizo na papo hapo kocha wa Spurs (wakati huo), Thomas Frank akawa wa tatu kumfunga Guardiola ugenini akiwa na klabu mbili tofauti.

Dhidi ya Leeds, Max Dowman (Arsenal) mwenye miaka 15 na siku 235 akawa mchezaji wa tatu kucheza EPL kabla ya kutimiza miaka 16, huku Rio Ngumoha akiwa mfungaji mdogo zaidi wa Liverpool katika mashindano hayo akiwa na miaka 16 na siku 361.

Iliman Ndiaye alikuwa mfungaji wa kwanza wa Everton katika Uwanja wa Hill Dickinson, ilhali ndiye aliyekuwa mfungaji wa mwisho wa klabu hiyo kwenye dimba la Goodison Park. Nayo penalti ya James Milner, 39, dhidi ya Man City ilimfanya kuwa mfungaji mkongwe zaidi wa penalti katika historia ya michuano hiyo.

Kwa upande mwingine Manchester United ilikuwa timu ya kwanza kuona mabao yake mawili ya kwanza ya msimu yakiwa ni ya kujifunga, huku

Crystal Palace ikiweka rekodi ya kutopoteza mechi 14 mfululizo katika mashindano yote, rekodi yao bora zaidi kama timu ya Ligi Kuu England.

SAL 01

SEPTEMBA 2025

Aston Villa ilishindwa kufunga katika mechi nne za kwanza za ligi kwa mara ya kwanza katika historia yake, huku Wolverhampton Wanderers wakianza msimu kwa kupoteza mechi nne mfululizo kwa mara ya kwanza, ilhali Liverpool wakiwa timu ya kwanza kushinda mechi nne mfululizo kwa mabao ya ushindi yaliyofungwa ndani ya dakika 10 za mwisho.

Nick Woltemade alikuwa Mjerumani wa tatu kufunga katika mechi yake ya kwanza, lakini Erling Haaland alifikisha mabao 50 ya nyumbani katika mechi yake ya 50 ya ligi hiyo akiwa Man City na Bruno Fernandes akifikisha mabao 100 akiwa Manchester United katika mashindano yote.

Kwa upande wake, Casemiro akawa mchezaji wa kwanza wa Man United kufunga na kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza cha mchezo wa ligi hiyo na Robert Sanchez alipata kadi nyekundu ya mapema zaidi kwa Chelsea katika ligi ndani ya dakika ya tano.


OKTOBA 2025

Mwezi huo, kocha Mikel Arteta alipata ushindi wake wa 177 katika mchezo wake wa 300 akiwa Arsenal na Arsenal walifikisha mechi 100 bila kuruhusu mabao matatu katika mashindano yote.

Ni kipindi hichocho Jean-Philippe Mateta akawa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick nyumbani katika ligi bila kushinda tangu Andy Carroll  2016, huku Erling Haaland akifikisha mabao 10 ya msimu mapema zaidi katika historia ya ligi kwa mara ya tatu.

Nao Liverpool walipoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote kwa mara ya kwanza tangu 2014 ilhali Alex Iwobi (Fulham) akiwa Mnigeria wa kwanza kufikisha mechi 300 za Ligi Kuu England.

SAL 02

NOVEMBA 2025

Katika mwezi huu Mohamed Salah alikuwa mchezaji wa tatu katika historia ya Liverpool kufikisha mabao 250, lakini Eberechi Eze (Arsenal) akiwa mchezaji wa nne kufunga hat-trick katika mechi kati ya Arsenal na Tottenham Hotspur.

Ni kipindi hicho hicho Pep Guardiola aliiongoza Man City katika mchezo wake wa 1,000 kama kocha, na Idrissa Gueye (Everton) akawa mchezaji wa kwanza kutolewa nje kwa kupigana na mchezaji mwenzake katika mashindano hayo tangu 2008.


DESEMBA 2025

Erling Haaland alifunga bao lake la 100 la Ligi Kuu England akiwa Man City katika mechi yake ya 111 pekee ikiwa ni rekodi ya haraka zaidi katika mwezi ambao ulimshuhudia Mohamed Salah akivunja rekodi ya Wayne Rooney (Man United) kuhusika na mabao mengi kwa klabu moja katika ligi hiyo. Desemba vilevile Unai Emery akawa kocha mwenye ushindi mwingi zaidi wa Ligi Kuu England katika historia ya Aston Villa na

Tottenham Hotspur walipoteza mechi 11 za nyumbani ndani ya mwaka 2025 ikiwa ni rekodi mbaya zaidi ya klabu hiyo.


JANUARI 2026

Mwezi huo Enzo Maresca akawa kocha wa kwanza kuondoka kazini siku ya Mwaka Mpya katika historia ya Ligi Kuu England, lakini Liverpool walicheza sare yao ya kwanza ya suluhu (0-0) baada ya mechi 117 mfululizo.

Ni katika kipindi hicho Mateus Mane akawa mfungaji mdogo zaidi wa Wolves katika ligi hiyo, huku James Milner akiwa mchezaji wa tano  kucheza Ligi Kuu England akiwa na miaka 40 au zaidi na Declan Rice, 27, akawa mmoja wa wachezaji watano wenye umri mdogo zaidi kufikisha mechi 300 za michuano hiyo.

SAL 03

FEBRUARI 2026

Raul Jimenez (Fulham) aliweka rekodi ya kufunga penalti zote 12 alizopiga Ligi Kuu England bila kukosa na Cole Palmer akawa mchezaji wa kwanza katika historia ya mashindano hayo kufunga hat-trick tatu zote katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Ni mwezi huo ambao James Milner alivunja rekodi ya mechi nyingi zaidi za Ligi Kuu England akimpita Gareth Barry, ambapo alifikisha 653 dhidi ya 652, na Arsenal waliifunga Tottenham mabao 4-1 na kupata ushindi mkubwa zaidi ugenini dhidi ya wapinzani wao wa London Kaskazini tangu 1978.


MACHI 2026

Mechi zote nne za Ligi Kuu England zilizochezwa tarehe 1 Machi ziliisha kwa matokeo ya 2-1, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Ligi Kuu England, na Max Dowman akawa mfungaji mdogo zaidi katika historia ya ligi hiyo akiwa na miaka 16 na siku 73.

Ni mwezi pia uliokuwa wa Aaron Ramsdale (Newcastle United) akawa mchezaji wa kwanza kushinda Stamford Bridge dhidi ya Chelsea akiwa na klabu tatu tofauti zingine zikiwa ni Arsenal na Southampton. Naye Dominik Szoboszlai alifunga mabao manne ya moja kwa moja ya faulo, mengi zaidi kwa mchezaji wa Liverpool katika msimu mmoja wa mashindano hayo.


APRILI 2026

Katika mwezi huo Bournemouth iliweka rekodi bora zaidi ya kutopoteza katika ligi hiyo kwa mechi 12 mfululizo, lakini ulishuhudia Burnley wakishuka daraja kwa mara ya tano katika historia ya Ligi Kuu England.

Naye Virgil van Dijk (Liverpool) alifunga bao la sita la ushindi dakika ya 90 dhidi ya Everton ikiwa ni rekodi dhidi ya mpinzani mmoja, huku  Mohamed Salah akiifikia rekodi ya Steven Gerrard ya mabao mengi katika Dabi ya Merseyside.


MEI 2026

Mwezi huu, straika Viktor Gyokeres amekuwa mchezaji wa kwanza wa Arsenal kufunga mabao 20+ katika msimu wake wa kwanza tangu Alexis Sanchez  2014-15, lakini Bukayo Saka akawa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mabao 50+ na asisti 50+ katika Ligi Kuu England. Saka ana miaka 24. Pia ni mwezi ulioishuhudia Arsenal ikiwa timu ya kwanza katika historia ya ligi hiyo kutomaliza msimu bila kuruhusu penalti wala kupata kadi nyekundu.

Kwa upande mwingine, Bernardo Silva (Man City) akawa Mreno wa kwanza kufikisha mechi 300 za Ligi Kuu England na Mreno mwenzake Bruno Fernandes akimaliza msimu akiwa na asist 21 zikiwa ni nyingi zaidi kwa mchezaji yeyote katika msimu mmoja wa michuano hiyo. Na kwa mara ya kwanza katika taaluma yake ya ukocha, Pep Guardiola alishindwa kutwaa ubingwa wa ligi katika misimu miwili mfululizo.